Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amefungua maonesho ya viwanda ya nchi za Jumuiya ya SADC, yaliyofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki hiyo, Rais Magufuli amezitaka nchi hizo kupeana fursa wenyewe kwa wenyewe hasa linapofikia suala la biashara, ambapo ameziomba nchi hizo, kuangalia namna ya kushirikiana kwa manufaa ya uchumi wa viwanda.
"Tuweke kipaumbele kwenye utumiaji wa teknolojia ya viwanda kwenye Jumuiya yetu kabla ya kwenda mbali, tuuziane bidhaa kabla ya kwenda kwingine, kama Namibia wanahitaji mahindi tuwapelekee mahindi, hili soko la watu Mil. 300 wa SADC litakuza uchumi wetu." amesema Magufuli.
"Sekta ya viwanda imeanza kuleta mafanikio kwa nchi za SADC, hamasa ya ujenzi wa viwanda umeongezeka, kwa sisi Tanzania tumeweka mkazo wa kutumia malighafi zinazozalishwa hapa, kwa miaka 3 zaidi ya viwanda 4000 vimeanzishwa." Amesema Rais Magufuli.
Maonesho hayo ya viwanda yanatarajia kufanyika kwa wiki nzima kuanzia leo, Julai 05, ambapo mara baada ya kukamilika kwa maonesho hayo, utaanza mkutano wa Marais 19 wa nchi za Jumuiya ya SADC ambapo Rais Magufuli ni Mwenyekiti.
0 comments:
Post a Comment