NA TIGANYA VINCENT
SERIKALI imesema katika bajeti yamwaka huu wa fedha imetenga bilioni 40 kwa ajili ya kujenga Vyuo ha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi (VETA) vipya katika wilaya 25 nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Elimu , Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa uzindizi wa Chuo cha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi wilayani Urambo.
Alisema lengo la ujenzi wa vyuo hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali iliyopo madarakani ya kuhakikisha kuwa inajenga walau Chuo cha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi (VETA) katika wilaya zote ambazo hazina.
Profesa Ndalichako alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha vijana wengi wapate elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya kuwawezesha kushiriki katika uchumi wa viwanda hapa nchini badala ya kuwa watazamaji.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema chuo hicho kimegharimu milioni 217.2 ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Alisema kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi milioni 198.8 zilitolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kiasi kilichobaki cha milioni 18.3 zimechangiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Dkt Bujulu alisema ili kukamilisha huduma za msingi Chuoni, VETA pia imekusudia kujenga bwalo kwa ajili ya mikutano na wanafunzi kulia chakula kwa gharama ya Shilingi Milioni 20.
Alisema kwa kuanzia Chuo kitaanza kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kozi ndefu katika fani za ushonaji nguo, umeme wa majumbani, uashi na uhazili na komputya.
Kozi za muda mfupi ni matumizi ya komputya, uhazili, ushonaji nguo, uashi, umeme wa majumbani na udereva wa awali wa magari.
Mwenyekiti wa Bodi ya VETA Peter Maduki aliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kuwaongezea eneo lilibaki ambalo lilikuwa likitumiwa na Mkandarasi ili waweze kuongeza fani nyingi ambazo zinalingana na sifa za Chuo cha VETA ngazi ya wilaya.
Alisema kuwa eneo la sasa ni dogo na linaruhusu kozi nne na hivyo kuongezwa kwa eneo kutawawezesha kutoa fani sita hadi saba kwa mwaka.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey aliwataka wakazi wa Urambo kuhakikisha wanatumia Chuo hicho kama fursa ya kuwapatia watoto wao elimu ili waweze kushiriki vema katika ujenzi wa Taifa badala ya kuwa Watazamaji.
Alisema wasipotumia Chuo hicho vizuri nafasi za ajira zitawapita kwa sababu ya kukosa ujuzi unaostahili kuajirika.
Naye mbunge wa Jimbo la Urambo Margaret Sitta ameahidi kusomesha watoto 62 kutoka Vijiji 62 vya Wilaya ya Urambo kwa gharama za shilingi 60,000/- kila mmoja.
Alisema lengo ni kuwahamasisha wazazi wengi wa eneo hilo kuhakikisha wanatoa fursa kwa watoto wao wanaomaliza elimu ya msingi na wale wa sekondari kujiunga na fani mbalimbali
0 comments:
Post a Comment