Monday, 4 March 2019

RAIS MAGUFULI AWACHANA POLISI SAKATA LA KUTEKWA MO DEWJI....."POLISI WAELEWE WATANZANIA SIYO WAJINGA SANA"

...
Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema suala la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ limeacha maswali mengi kwa wananchi ambayo yanahitaji majibu hivyo jeshi la polisi liwaeleze Watanzania kwani si wajinga sana.

Mo alitekwa Oktoba 11, 2018 saa 11 alfajiri eneo la Hotel ya Colosseum iliyopo barabara ya Haile Selassie, Oysterbay jijini Dar es Salaam ambako alikwenda kufanya mazoezi na akapatikana Oktoba 20 eneo la Gymkhana jijini Dar es salaam.

Leo Jumatatu Machi 4,2019 mara baada ya kuwaapisha mawaziri wapya wa katiba na sheria, Balozi Agustine Mahiga na wa mambo ya nje ya ushirikiano wa Afrika mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, Rais Magufuli amesema ana imani kubwa na jeshi la polisi lakini kuna dosari zinazopaswa kufanyiwa kazi huku akitolea mfano wa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo.

Amesema Watanzania wanajua kuchambua mambo na lilipotokea tukio la kutekwa kwa Mo zilikuja habari nyingi kwamba waliohusika na utekaji ni Wazungu wa aina fulani lakini suala hilo lilipomalizika liliacha maswali mengi zaidi.

“Jeshi la Polisi linatakiwa kuelewa kuwa Watanzania sio wajinga, kama suala la kutekwa kwa Mo Dewji linaacha maswali. Tuliambiwa alitekwa na wazungu lakini lilipoisha haikueleweka, mwishoni aliyetekwa alionekana akinywa chai na Mambosasa.

“Baada ya siku chache tukaambiwa nyumba aliyokuwa katekwa Mo Dewij hii hapa na dereva aliyekuwa anawabeba watekaji huyu hapa, tukahisi atapelekwa mahakamani akatoe maelezo, baadaye kimya mpaka leo miezi imepita, hakuna aliyepelekwa Mahakamani, ile inatoa maswali mengi ambayo hayana majibu. Hata kama Watanzania watanyamaza lakini mioyo yao haitakuwa ‘clear’. 

“Mambo haya yanalitia doa Jeshi la Polisi. Lazima tujenge taswira ya Jeshi la Polisi kama lilivyoasisiwa na Mwalimu Nyerere. Kama kuna maafisa wa Jeshi la Polisi wanaofanya vibaya leta taarifa ili hata nyota zao zipunguzwe na wanaoshindwa wasipelekwe Makao Makuu.

“Wale Askari wadogo wanaofanya kazi vizuri msiwakatishe tamaa, anamkamata Mtu mnamwambia amwachie. Msisite kuleta mapendekezo kwa wale wanaofanya vizuri. Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri kama majeshi mengine lakini hizi dosari lazima zirekebishwe,” amesema Rais Magufuli.

“Mtu aliyetekwa alikutwa Gymkhana usiku lakini watu wanajiuliza Mmhh aliendaje pale, lakini alipowekwa pale na bunduki zikaachwa pale, unajiuliza huyu mtekaji aliamua kuziacha je angekutana na polisi wanaotafuta njiani?” Amehoji Magufuli.

Amesema walijaribu kulichoma moto gari lakini baadaye aliyetekwa akaonekana anakunywa chai na kamanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

“Baada ya siku chache tukaambiwa nyumba ya alimokuwa ametekwa ni hii hapa na aliyekuwa anawabeba wale watekaji ni huyu hapa, Watanzania tukawa tunasubiri kwamba huyu sasa ndio atakuwa kielelezo cha kupelekwa mahakamani tusikie kitakachotokea lakini kimya mpaka leo miezi imepita,” amesema.

Amesema jambo hilo linaaacha maswali mengi ambayo hayana majibu, mtu aliyekuwa akiwasafirisha angewataja na Watanzania walitaka kuona huyo mmiliki wa nyumba angalau akajibu.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger