Monday, 4 March 2019

KAULI YA MBOWE LOWASSA KUREJEA CCM

...

Edward Lowassa akiwa na Freeman Mbowe.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amemtakia maisha mema aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Edward Lowassa baadaya kurejea CCM.

Mbowe ambaye yupo gereza la Segerea ambapo anatumikia adhabu yake ya kukiuka masharti ya dhamana kutokana na kesi yake inayomkabili, amesema kuwa safari ya mabadiliko lazima ipite katika vikwazo vingi na si wote watakaofika mwisho wa safari hivyo wapo watakaoishia njiani.

"Julai 2015, tulimpokea Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa katika chama chetu, na baadae kupitishwa na vikao vya chama kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Machi 01, 2019 Mhe. Lowassa ametangaza kurudi katika chama chake cha zamani Chama Cha Mapinduzi (CCM)".

Ujumbe wa Mbowe umeendelea kusema kuwa, "Wana-CHADEMA tunapotofakari jambo hili rejeeni kauli yangu ya wakati wote inayobeba falsafa yetu ya mabadiliko kwamba safari ya kusaka mabadiliko ni sawa na safari ya treni kutoka Dar es salaam kuelekea Kigoma, wapo wanaoanza na safari mwanzo wa safari na wapo wanaonzia katikati, pia wapo wanaoteremka njiani na wapo wanaoendelea na safari hadi mwisho, wote hao ni abiria, cha msingi kwetu hapa ni kuhakikisha safari yetu inaendelea, na ni imani yangu na matumaini yangu kwamba mtakubaliana na mimi kuwa safari yetu inaendelea".

"Aidha, kurejea kwa Mhe. Lowassa CCM, kunatupa pia fursa ya kuzidi kutafakari kama chama juu ya hamia ya wana-CCM katika chama chetu nyakati za uchaguzi na maamuzi yetu na namna tunavyowapokea, hatuna budi kutulia na kumtakia maisha mema nyumbani alikorejea, sisi tuendelee na safari yetu yakuelekea Kigoma", amemalizia Mbowe.

Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu juzi Ijumaa Machi mosi alitangaza kurejea CCM na kudai kuwa aliondoka kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger