Friday, 17 January 2025
TUME YA RAIS YA MABORESHO YA KODI YAKUTANA NA WADAU WA KODI MKOA WA SHINYANGA KUKUSANYA MAONI
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mkutano huo umefanyika leo, Ijumaa, Januari 17, 2025, katika ukumbi wa Lyakale Mjini Shinyanga, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi.
Akifungua mkutano huo, Wakili Mtatiro amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau katika michakato ya kuboresha mifumo ya kodi, akisema kuwa michango na maoni yao ni muhimu na yatatumika kama sehemu ya mikakati ya kuleta mageuzi ya kimsingi katika sekta hiyo.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mwanamapinduzi wa kweli, anayehamasisha na kusikiliza maoni ya wananchi. Anachukua hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa maoni ya wananchi yanatekelezwa kwa manufaa ya wengi. Tume hii ya Rais haiachi jambo lolote nyuma, inazingatia taaluma na weledi wa hali ya juu katika kufanya tathmini ya mifumo ya kodi. Hivyo, michango yenu leo itachukuliwa kama maoni muhimu kwa kuboresha mifumo ya kodi na itafanyiwa kazi,” amesema Wakili Mtatiro.
Wakili Mtatiro amesema changamoto za kodi ni changamoto za kitaifa na kuahidi kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kujitahidi kuboresha mifumo ili kuhakikisha kuwa masuala ya kodi yanakuwa endelevu na yanahusisha pande zote kwa faida ya nchi nzima.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, CPA Leonard Mususa, ameeleza kuwa tume hiyo inaendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu mifumo ya kodi, mapato, na tozo mbalimbali zinazohusiana na sekta ya kodi.
Amesema kazi hii inaimarisha juhudi za Serikali katika kuhakikisha kuwa mfumo wa kodi unakuwa rafiki kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, na kwamba tume inashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa kodi zinakusanywa kwa njia bora na yenye haki, huku ikifanya mabadiliko ili kutoa kero na malalamiko ambayo yamekuwa yakichochea malumbano.
“Tume ya Rais inatekeleza majukumu yake kwa umakini mkubwa ili kuondoa kero za kodi na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Tumelenga kuvutia mitaji ya ndani na nje ya nchi na kwa upande mwingine, tunafanya tathmini ya kina ili kuona ni hatua zipi zinapaswa kuchukuliwa ili kuboresha mifumo ya kodi nchini,” ameeleza CPA Mususa.
Mkutano huo umetoa fursa kwa wadau muhimu wa masuala ya kodi kutoka Mkoa wa Shinyanga kutoa maoni yao kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika masuala ya kodi.
Wadau hao pia wamependekeza njia mbalimbali za kutatua changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu katika ukusanyaji wa kodi, kuboresha mawasiliano kati ya serikali na wafanyabiashara na kuongeza ufanisi katika utendaji wa mifumo ya kodi.
Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi kukusanya maoni ya wadau kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ili kuwezesha mabadiliko ya mifumo ya kodi kwa namna itakayowafaidi wananchi na nchi kwa ujumla.