Saturday 29 October 2022
Friday 28 October 2022
MAENEO YALIYOMEGWA KWENYE HIFADHI YAPANGIWE MPANGO WA MATUMIZI YA ARDHI
MADEREVA WA MALORI WAIGOMEA TICTS BANDARINI
***
* Tanzania yanusurika kupata aibu kubwa mbele ya Rais wa Congo
* Ni kutokana na huduma mbovu za upakuaji wa makontena
Na Mwandishi Wetu - Dar es salaam
MADEREVA malori wameigomea kampuni ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania katika bandari ya Dar es Salaam (TICTS) kutokana ucheleweshaji mkubwa wa huduma ya kupakua makontena unaofanywa na kampuni hiyo.
Mgomo huo wa madereva wa malori ulianza usiku wa Ijumaa Oktoba 21, siku ambayo Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi, aliwasili nchini kwa ziara.
"TICTS ni wazembe sana. Utendaji kazi wao ni mbovu, kuanzia asubuhi hadi sasa hivi saa sita ya usiku tumekwama hapa bandarini kutokana na ucheleweshaji wa huduma ya upakiaji wa makontena," alisema Mohammed Abdallah, dereva wa lori la makontena, usiku wa mgomo ulipoanza.
Madereva hao, ambao wamekuwa wakigoma mara kwa mara kutokana na huduma mbovu za TICTS, wamesema miundombinu ya eneo la Kitopeni bandarini lililo chini ya TICTS ni mibovu, ikiwemo uhaba wa vyoo.
"Licha ya kucheleweshewa huduma za makontena kwa visingizio vya kreni kuharibika mara kwa mara na msongamano wa malori, kuna matundu ya vyoo mawili tu ambayo yanahudumia mamia ya madereva," alisema Abdallah.
Siku ambayo madereva malori wameanza mgomo wao mpya, Rais Tshisekedi, ambaye nchi yake ya DRC ndiyo mteja mkubwa kuliko wote wa bandari ya Dar es Salaam, aliwasili Zanzibar kwa mapumziko binafsi kabla ya kuanza ziara rasmi ya kikazi nchini Tanzania Oktoba 23.
Moja ya shughuli ambayo Rais wa Congo alipangiwa kufanya wakati wa ziara yake nchini ni kutembelea bandari ya Dar es Salaam.
"Tunashukuru kuwa Rais Tshisekedi alipata udhuru akalazimika kukatisha ziara yake nchini, hivyo hakwenda tena bandarini Dar es Salaam. Maana kama angeenda bandarini angekutana na mgomo wa madereva malori kutokana na huduma mbovu ya TICTS na hii ingekuwa ni fedheha kubwa kwa taifa," alisema Juma Hafidh, mdau wa bandari ya Dar es Salaam.
Hivi karibuni, wafanyakazi wa TICTS walilaumiwa kwa kudondosha makontena kwenye bahari na kufanya meli zishindwe kupita kwenda kupakua mafuta eneo la Kurasini KOJ kwa siku kadhaa na kuisababishia taifa hasara.
Kumekuwa na mlolongo wa tuhuma za uzembe na ukosefu wa ufanisi wa TICTS ambayo imekuwa ikisimamia eneo la makontena la bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 20 bila tija.
Serikali ya Tanzania kwa sasa iko kwenye majadiliano na TICTS kuhusu kuongeza au kutoongeza mkataba wake, huku kampuni hiyo ikilaumiwa na wadau wa biashara na usafirishaji kwa kukosa ufanisi.
Wadau wa sekta za biashara na usafirishaji wameitaka serikali kutoipa kampuni ya TICTS mkataba mpya wa kuendesha eneo la kontena la bandari ya Dar es Salaam kwa kushindwa kufikia lengo la kuongeza wingi wa mzigo kwa asilimia 37 kwa mwaka na kuwa na ufanisi mdogo.
MWANAFUNZI DARASA LA TANO SHINYANGA AJINYONGA BAADA YA KUMALIZA KUNYWA CHAI
Na Halima Khoya, SHINYANGA
WANAFUNZI wa darasa la tano shule ya msingi Ndala ‘A’ Manispaa ya Shinyanga Brayton Daniel (11) amekutwa amejinyonga kwa kamba nyuma ya mlango nyumbani kwao.
Tukio hilo limetokea Oktoba 26 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi, nyumbani kwao Mtaa wa Mwabundu Kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga.
Akielezea tukio hilo jana mama mkubwa wa marehemu Joyce Kalulu, amesema mtoto huyo hakuwa hana tatizo lolote, lakini siku hiyo walipomaliza kunywa chai, yeye aliondoka kwenye mihangaiko yake ya maisha na aliporudi nyumbani majira ya saa 8 mchana akakuta mlango umefungwa kwa ndani, walipovunja wakamkuta kijana wao amejinyonga.
“Asubuhi nimeamka na kufanya kazi zote nikawa nimewaacha kijana wangu na bibi yake, nimerudi saa 8 kutoka kazini nikamkuta mama anahangaika kumuita Brayton afungue mlango, ndipo tulipoamua kwenda kumuita Mwenyekiti ambaye alifanikiwa kutoboa nyavu za dirisha na kumuona Brayton akiwa amening’inia mlangoni,”amesema Kalulu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwabundu Pili Masanja amesema taarifa za tukio hilo alizipata majira ya saa 9 mchana, na alipofika kwenye familia hiyo ikabidi watoboe nyavu ya dirisha alipochungulia akamuona mtoto huyo akiwa amejinyonga nyuma ya mlango.
“Majira ya saa 9 nilikuja kuitwa na Joyce Kalulu ili nikawasaidie kufungua mlango ambapo nilizunguka nyuma yumba ili kutoboa dirisha lakini tulichokiona baada ya kutoboa dirisha ni Brayton akiwa amejinyonga na kamba nyeusi kwenye mlango, ndipo nikapiga simu Polisi,”amesema Masanja.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa Shinyanga Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akibainisha kuwa Jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.
MABUSHI ACHAGULIWA KUWA ASKOFU MKUU WA MAKANISA YA IEAGT TANZANIA
Akizungumza mara baada ya zoezi la upigaji kura kwenye uchaguzi huo Mwenyekiti Mtendaji bodi ya wadhamini Kanisa la IEAGT ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi huo Lucas Lugwila, amesema uchaguzi huo umefanywa na wajumbe wapatao 71, wa dhehebu la IEAGT kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
Mara baada ya zoezi la upigaji kura kumalizika msimamizi wa uchaguzi Lucas Lugwila amemtangaza Askofu David Mabushi kuwa ndiye Askofu Mkuu wa Umoja wa Kanisa la INTERNATIONAL EVANGELICAL ASSEMBLIES OF GOD TANZANIA (IEAGT), kwa kupata kura 68 kati ya kura 71 zilizopigwa.
“Nafasi ya Askofu Mkuu, David Mabushi ameibuka mshindi kwa kupata 68, nafasi ya Makamu Askofu Mkuu mshindi ni Simon Laizer amepata kura 58, nafasi ya Katibu Mkuu mshindi ni Flagson Ndibwa kwa kura 46 na nafasi ya Mwekahazina mshindi ni Timoth Mwantake ambaye amepata kura 58”, amesema Lugwila.
Mara baada ya uchaguzi huo kumalizika Askofu Mkuu David Mabushi akizungumza mbele ya baraza hilo, ameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi hao na kuitumikia vyema nafasi hiyo aliyochagulia kwa kusimamia miongozo, Katiba na Misingi iliyowekwa na umoja huo.
Aidha Makamu Mwenyekiti kutoka CPCT taifa, Bartholomeo Sheggah amewapongeza viongozi hao waliochaguliwa, na kuwataka kutumikia vizuri nafasi hizo ili kuendelea kujenga umoja wa kanisa hilo katika msingi mzuri.
Nao baadhi ya Wajumbe wa baraza hilo akiwemo Mchungaji Joseph Jackson amesema wanaimani na viongozi waliowachagua watakwenda kutumika vyema kwenye nafasi zao.