Thursday 31 December 2020

Waziri wa Mambo ya Nje wa China kufanya ziara Tanzania


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema mtazamo wa Tanzania kwa Bara la Afrika ni kuona linajitegemea kwa kutumia rasilimali zake kufanya maendeleo.
 
Waziri Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na Waandishi wa habari, ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia ujio wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi Januari 7 mwaka 2021.

Ziara ya siku mbili ya Wang Yi hapa nchini, ni muendelezo wa uhusiano wa muda mrefu baina ya Tanzania na China.


Share:

Vanessa Mdee avalishwa pete ya Uchumba na Mpenzi wake Rotimi


MWANAMUZIKI wa Tanzania, Vanessa Mdee, amevalishwa pete ya uchumba na mpenzi wake Rotimi ambaye ni msanii wa filamu ambapo wote kwa sasa wanaishi nchini Marekani.

‘Videos clips’ ambazo zimepostiwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha Rotimi akiwa amepiga magoti mbele ya Vanessa huku akimvalisha pete hiyo ya uchumba, kisha wakakumbatiana na kuanza kupigana mabusu.
 
Vanessa amethibitisha hilo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo ameweka video mbili moja ikionesha pete aliyovishwa huku nyingine ikiwa ni kipande cha video ya mahojiano aliyowahi kufanya na moja ya vyombo vya habari na kusema ilimgharimu siku mbili tu kujua kwamba Rotimi ndiye atakayekuja kuwa mume wake.

“Mwaka mmoja na nusu uliopita dunia ilicheka niliposema kuwa nilijua kuwa wewe utakuja kuwa mume wangu muda mfupi baada ya kukufahamu, sikuwalaumu kwani hisia unayoipata pale unapokutana na mpenzi wa maisha yako si ya kawaida na haiwezi kuelezeka lakini pia wao walikuwa wakimfahamu Vanessa ambaye hakuwa na mpango wa kuolewa kwa wakati huo,” ameandika Vanessa.

Rotimi naye kupitia ukurasa wake wa Instagrama ameweka video fupi ya pete aliyomvalisha Vanessa akiambatanisha na ujumbe unaoelezea namna anavyompenda mrembo huyo.

“Unanifanya niwe mwanaume bora. Nina deni kwa Mungu kwa kunipa wewe na nitamlipa kwa kukupenda na kukupa kila kitu unachostahili, nakupenda,” ameandika Rotimi.

Uhusiano wa wawili hao ulianza mwaka 2019 baada ya Vanessa kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, mwanamuziki wa Tanzania, Jux.

Kwa sasa Vanessa ambaye mwezi Juni alitangaza kuachana na shughuli za muziki anaishi Marekani pamoja na mwanume huyo na mara kadhaa amekaririwa akimsifia kuwa ni mwanaume aliyefanya aitambue thamani ya maisha yake.

Mwanzoni mwa mwezi wa kumi mwaka 2020, Vanessa  na Rotimi walishea picha mitandaoni zikiwaonyesha wamechorana ‘tattoo’ zenye majina yao kwenye miili yao.



Share:

KARIBU EJOS STATIONARY & GENERAL SUPPY ...TUNAPATIKANA KAMBARAGE SHINYANGA MJINI

 

Share:

REA na TANESCO wapewa miezi mitatu kuunganishia wateja Umeme


 Na Mwandishi Wetu,
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijjini (REA), kuhakikisha wanawaunganishia umeme wateja wote waliolipia ankara za umeme jijini Mwanza na maeneo ya vijijini ndani ya miezi mitatu kuanzia tarehe 30 Desemba, 2020.

Waziri Kalemani ameyasema hayo, tarehe 29 Desemba, 2020, alipokuwa akizungumza na Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kikao kazi cha pamoja kilichofanyika kwenye ukumbi wa  Benki Kuu jijini Mwanza.

Pamoja na agizo hilo la kuwaunganishia umeme wateja hao ndani ya miezi mitatu, Waziri Kalemani, amewaelekeza watendaji hao kuhakikisha wateja wote walioko katika maeneo ya vijijini na kando kando ya miji, wanaunganishiwa umeme kwa gharama ya Shilingi 27,000 bila kujali umbali wa mita 30 kwani ni wajibu wa TANESCO kuwafikishia wananchi nguzo za umeme ili kuwafikia wateja hao.

“Mnataka kila mwananchi awe mita 30 ndipo muwafikishie umeme? Ni kazi yenu kupeleka nguzo hadi muwafikie wananchi hao. Nisisikie mtu anaongelea suala la mita 30.” amesema Kalemani

Vilevile, Waziri Kalemani, ameitaka TANESCO  kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja ili kuhakikisha wateja wanapatiwa huduma bora na kwa wakati ili kuwaondolea adha ya kufuatilia maombi ya kuunganishiwa umeme kwenye Ofisi  za TANESCO wilayani.

Amewataka watendaji wa TANESCO kuwafuata wateja mahali walipo na kuepuka kutumia lugha ya kukatisha tamaa kwa wateja ili kujenga mahusiano mazuri na wateja  jambo litakalopelekea kupanua wigo wa wateja na kuongeza mapato kwa Shirika.

” Masurveyor ndio wanaolalamikiwa sana kwa kutoa lugha zinazokatisha tama, ninawasihi mbadilike kuanzia sasa, atakayebainika anatumia lugha mbaya kwa mteja, huyo tutaachana naye na atachukuliwa hatua za kinidhamu. Wateja wote wahudumiwe bila kubaguliwa, tunataka wateja wote wapate umeme bila kubaguliwa.”Amesema Dkt. Kalemani

Aidha,  Dkt. Kalemani, amewapongeza watumishi wa TANESCO kwa utendaji mzuri na kueleza kuwa kwa zaidi ya asilimia 80 utendaji wa TANESCO ni wa Kuridhisha.

Waziri Kalemani pia ameelekeza watumishi walioajiriwa kwa muda, wanaohusika na kazi za kupimia wananchi  maeneo ya kuunganisha umeme, wanunuliwe pikipiki zitakazowawezesha kuwafikia wateja kwa urahisi.

Vilevile, Waziri Kalemani amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na kwa usahihi na amewataka watumishi wa TANESCO na REA kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi hicho, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, amewataka watumishi wote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Kalemani, na kueleza kuwa atahakikisha anasimamia na kufuatilia utekelezaji wake kwa ukamilifu.

Kikao kazi baina ya Waziri  Kalemani na watumishi wa TANESCO na REA, ni kikao kazi cha pili baada ya kufanya  kikao na wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Geita wiki iliyopita. Lengo la vikao hivyo ni kuweka misingi ya pamoja ya utendaji kazi unaolenga kuleta matokeo chanya na ya haraka katika Sekta ya Nishati.


Share:

Taarifa Kwa Umma Kuhusu Kusitisha Makongamano Au Mikutano Ya Mkesha Katika Maeneo Ya Wazi Siku Ya Tarehe 31 Desemba, 2020.



Share:

TAWA Yatoa Ufafanuzi Kwa Wanao Sambaza Taarifa Za Uzushi Kuhusu Simba Aliye Uawa Songwe.


Kufuatia taarifa zinazo sambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu askari wa  mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania TAWA kumuua Simba katika kijiji cha Ngwala wilayani Songwe ili kunusuru maisha ya watu na kuonekana kuwa wamekiuka haki za wanyama na kuleta mjadala katika mitandao ya kijamii mamlaka hiyo imetoa ufafanuzi kwamba ilikuwa inatekeleza majukumu yake.
 
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari afisa wanyamapori mwandamizi udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu TAWA Wilbright Munuo, amesema mamlaka inakemea vikali taarifa za opotoshaji zinazo sambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.


Amesema jamii inatakiwa kufahamu kuwa kazi zinazofanywa na wataalam wa TAWA zinafanywa kwa kuzingatia sheria ya uhufadhi ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, hivyo hazipaswi kubezwa kwani kufanya hivyo ni kuingilia majukumu ya mamlaka.
 
Aidha amesema sheria ya uhifadhi wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 inatambua umuhimu wa kulinda maisha ya watu na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu, licha ya mamlaka kutumia mbinu  mbalimbali za kuthibiti wanyamapori hao katika vijiji ikiwemo kutishia kwa risasi.


Pia amesema njia nyingine zinazotumika ni kuwapeleka wanyama wakali na waharibifu katika bustani na ranchi za wanayapori kwa kuzingatia mahitaji Ili kuepusha taharuki kwa wananchi.
 
Amesema mamlaka katika kuhimarisha usalama wa maisha ya watu na mali zao imekuwa ikihamisha wanyamapori waliokuwa wakivamia maeneo ya wananchi na kuwarudisha katika maeneo ya hifadhi.

‘‘Mwezi mei,2017 Tembo wanne walivamii maeneo ya chuo kikuu cha dodoma waliwarudisha hifadhini bila ya kuleta madhara kwa wananchi,pia mwezi February 2020 TAWA kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania TAWILI tuliwahamisha Simba 36 ambao waliua ng`ombe zaidi ya 100 katika Vijiji cha Kwitete,makundusi,iharara,robanda,pakinyigoti,nichoka na maeneo ya hifadhi ’’Alisema Wilbright Munuo.
 
Vilevile Munuo ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa  2020 pekee jumla ya matukio 993 ya wanyamapori kuvamia maeneo ya wananchi yaliripotiwa katika vituo vya TAWA ambapo wanyamapori hao walirudishwa kwenye maeneo ya hifadhi.



Share:

Jeshi La Polisi Latoa Onyo Kwa Watakaovunja Sheria Siku Ya Sherehe Za Mwaka Mpya



Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi Disemba 31



Share:

Wednesday 30 December 2020

Watoto Watatu Wafariki Dunia Kigoma Baada ya Nyumba Kuteketea Kwa Moto


Wototo wawili wa familia moja wamefariki dunia katika kijiji cha Nyarugisu wilayani Kasulu mkoani Kigoma, baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kigoma, -James Manyama amewataja watoto hao kuwa ni Yumwema Festo na Enifa Festo ambao ni raia kutoka nchi jirani.

Kamanda Manyama amesema kuwa, Jeshi la polisi mkoani Kigoma linaendelea kuwatafuta wazazi wa watoto hao wanaodaiwa kukimbia baada ya tukio hilo, kwa hofu ya kukamatwa kwa kosa la kuishi nchini kinyume cha sheria.

Pia amethibitisha kufariki dunia katika ajali ya moto mtoto mwingine katika kijiji cha Mpeta wilayani uvinza, baada ya nyumba alimokuwa akiishi na Wazazi wake kuungua moto.

Kufuatia matukio hayo, Kamanda Manyama amewataka Wazazi na Walezi mkoani humo kuacha utamaduni wa kuwaacha watoto nyumbani bila uangalizi.

Katika hatua nyingine Jeshi la polisi mkoani Kigoma limewataka Wakazi wa mkoa huo kusherekea sikukuu ya mwaka mpya kwa amani na kuepuka kujihusisha na vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani.


Share:

TECNO Kuwazawadia Wateja Wa Camon 16 Na Spark 5Pro Nchi 55 Ya TV


TECNO inaendelea kuwapa furaha wateja wake hii ni baada ya kukabidhi zawadi kwa Bwana Ramadhani Salim aliyejishindia mashine yakufulia, Jacquline Kaseja vocha ya manunuzi yenye thamani ya sh.500,000 na mshindi wa TECNO Spark 5pro Zee la Vyeti aliyepatikana kupitia challenge ya iliyofanyika twitter. 


Zawadi bado zipo nyingi na TECNO inawakumbusha wateja wake kutembelea maduka yote ya simu ili kuendelea kufurahiya zawadi mbalimbali kutoka TECNO kama vile rice cooker, blender, cattle na gift package pindi ununua apo simu yoyote ya TECNO lakini pia endapo ukinunua camon 16 na Spark 5 pro moja kwa moja utaingizwa katika droo kubwa na washindi kuondoka na Smart TV ya nchi 55, droo hii kubwa itachezeshwa live trh 15/1/2021 kupitia @tecnomobiletanzania.

TECNO camon 16 na Spark 5pro ni matoleo mapya kwa kampuni hii nah ii imepelekea simu hizi kuwa muonekano wenye kuvutia na uimara katika utumiaji. Camon 16 ni simu yenye kamera kali kuzidi simu zote za TECNO nyuma ikiwa na MP 48 na selfie ni MP 16, ukubwa wa memory ni 128GB+4GB RAM na battery lenye kudumu na chaji wa muda mrefu la mAh 5000.


Spark 5 pro ni simu yenye kioo kipana cha nch 6.6, Spark 5pro inakupa nafasi ya kuchukua picha kwa ukubwa zaidi kutoka na kuwa na wigo mpana wa kioo vilevile ina MP16 nyuma na selfie MP 8, memory kubwa GB 64+GB 3 RAM na battery lenye kudumu na chaji kwa muda mrefu mAh5000.


Tembelea https://www.tecno-mobile.com/tz/home/#/ 


 




Share:

Dkt. Ndugulile Aipa Siku 90 Shirika La Posta Kuboresha Utendaji Na Ufanisi Wake


Na Prisca Ulomi, WMTH
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ameipa siku 90 Shirika la Posta Tanzania (TPC) kuboresha utendaji kazi na ufanisi katika kuhudumia wateja na wananchi kwa ujumla katika shughuli za kila siku za uendeshaji wa Shirika hilo

Dkt.Ndugulile ameyasema hayo kwa Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wakati wa ziara yake ya kutembelea Shirika hilo, Dar es Salaam ambapo aliambatana na Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo A. Mathew, Katibu Mkuu, Dkt. Zainab Chaula na Menejimenti ya Wizara hiyo kwa lengo la kufahamu utendaji kazi wa Shirika ili kuhakikisha kuwa linahudumia vema wananchi

Ameongeza kuwa TPC ipitie mikataba yake ambayo haina maslahi kwa Shirika na isimamie vizuri rasilimali zake ikiwemo viwanja, ofisi na magari kwa kuwa rasilimali ni mtaji na mtaji sio fedha ili rasilimali hizo zitumike kuongeza mapato ya Shirika

Vile vile ameiagiza  Wizara yake kushirikiana na TPC kufanya mapitio ya sera na sheria ya posta ili ziweke kuendana na wakati kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi

Pia, amewakumbusha kuwa na mahusiano mazuri baina ya viongozi, wafanyakazi, menejimenti na wajumbe wa bodi katika mazingira ya mahali pa kazi ili kuboresha na kuongeza utendaji kazi wa Shirika

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew amelipongeza TPC kwa kutengeneza Mfumo wa Taarifa wa Posta ambao unasimamia na kufuatilia uendeshaji wa Shirika; malipo na ukusanyaji wa mapato; na taarifa za watumishi

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula, ameueleza uongozi wa TPC kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nao ili kufanikisha utendaji kazi wa Shirika katika kuhudumia wateja

Mwenyekiti wa Bodi wa TPC, Kanali mstaafu, Dkt. Haruni Kondo na Posta Masta Mkuu wake, Hassan Mwang’ombe wamemshukuru Dkt. Ndugulile kwa ziara yake na kulitaka Shirika liboreshe utendaji kazi wake na wako tayari kufanyia kazi yaliyoelekezwa


Share:

Askari shujaa Koplo Denis Minja aokoa mtoto mwingine chooni


Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Koplo Denis Minja, ambaye mwezi Mei alimwokoa mtoto mchanga akiwa hai ndani ya shimo la choo wilayani Ngara mkoani Kagera, amemwokoa tena mtoto mwingine wa kiume mwenye umri wa miaka 2, kutoka katika shimo la choo, eneo la Kayanga wilayani Karagwe.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Hamis Dawa, amesema kuwa walipata taarifa za mtoto kutumbukia katika choo cha shimo wakati akimfuata mama yake aliyekuwa bafuni akioga na kwenda kumuokoa na kufanikiwa kumtoa akiwa hai na kwa sasa anaendelea vizuri.

Amesema Askari huyo Koplo Minja, ambaye alishirikiana na Askari wenzake na kuingia katika shimo hilo kumwokoa mtoto huyo, kituo chake cha kazi ni wilaya ya Ngara lakini yuko wilayani Karagwe kumuuguza mke wake.

Dawa amesema kuwa tukio hilo limetokea Desemba 28 mwaka huu, saa 10:00 jioni, na kutaja Askari wengine wa zimamoto walioshiriki kuokoa maisha ya mtoto huyo kuwa ni Norbert Saka, Eliad Batanyangwa na James Lucas.

Aidha Mkuu huyo wa Zimamoto na Uokoaji ametumia fursa hiyo kuwaasa wazazi kuacha tabia ya kwenda na watoto wadogo katika maeneo hatarishi ikiwamo chooni na mtoni, ili kuepusha majanga kama hayo na kuwa uchunguzi wa kina unaendelea.




Share:

Jafo: Natamani kuona Halmashauri zinajitegemea


Na. Angela Msimbira TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe, Selemani Jafo amesema ndani ya miaka mitatu ijayo matamanio yake ni kuona Halmashauri zinajitegemea zenyewe kupitia mapato ya ndani na kwamba ifike muda ziwe zinalipa watumishi wake mishahara.

Waziri Jafo ameonyesha matamanio hayo leo wakati alipotembelea ujenzi wa mradi wa Government City Complex katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba unaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 59.3 hadi kukamilika kwake ambapo ametumia nafasi hiyo kulipongeza jiji la Dodoma kwa kutekeleza kwa kutumia mapato yake ya ndani na si fedha za serikali.

Amesema hakuna halmshauri yoyote iliyofanya uwekezaji mkubwa nchini kama uliofanyika katika Jiji la Dodoma huku akieleza kuwa sasa analiona jiji hilo kupitia viongozi wake kuwa wapo kwenye sura hiyo anayoitamani.

“Hakuna halmashauri yoyote iliyofanya uwekezaji mkubwa kama huu hivyo nawapongeza jiji la Dodoma, nataka jengo hili liwe kielelezo na kama nilivyosema mimi matamanio yangu nataka nione halmashauri zinazoweza kujitegeme zenyewe ifike muda halmashauri iseme hata nikiwa na watumishi wangu nitawalipa mimi mwenyewe natamani itokee ndani ya miaka mitatu ijayo,” amesema Waziri Jafo.

Ameendelea kufafanua kuwa analiona Jiji la Dodoma lipo kwenye sura hiyo kupitia hoteli hiyo kubwa ya mikutano iliyojengwa katika Mji wa Serikali.

“Nikiangalia hoteli kubwa ilivyo kuwa mjini ya ghorofa 11 nikiangalia soko lenu la Dodoma nikiangalia eneo la maegesho ya magari Nala, eneo la mapumziko na michezo Chinangali, Stendi ya Dodoma, ninapata uhakika kwamba halmashauri ya jiji la Dodoma inaenda kujitegemea,”amesisitiza Waziri Jafo.

Ameuagiza uongozi wa jiji la Dodoma kuhakikisha wanakwenda kusimamia kazi hiyo kwa kiwango cha juu ili iwe nzuri ambapo mtu akija ajifunze na kumtaka mkandarasi kutulia na kufanyakazi kwa uangalifu mkubwa.

Amesema anahitaji jengo hilo kuwa kielelezo na kama nilivyosema mimi matamanio yangu ni kuona halmashauri zinazoweza kujitegemea zenyewe na ifike wakati ziwe zinalipa wafanyakazi wake kupitia fedha za ndani”

Amemuagiza mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ikiwa ni pamoja na mshauri wa mradi huo anayehusika na kazi ya michoro kuhakikisha ifikapo siku ya jumatatu awe amekamilisha kazi na asiwe kikwazo cha kuchelewesha mradi.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Jiji Joseph Mafuru amesema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 59.3 ambapo kwa awamu mbili ambapo ya kwanza ni ujenzi wa jengo la Tower B lenye ghorofa tano na kumbi za mikutano tano zenye uwezo wa kuchukua watu 1297.


Share:

Wachimbaji Wadogo Watakiwa Kuwa Na Sehemu Ya Pamoja Kuchenjua Dhahabu Mkoani Geita


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mwita Waitara amewataka wachimbaji wadogo kuwa na sehemu ya pamoja na kuchenjua dhahabu ili kudhibiti kusambaa kwa mabaki ya zebaki.

Waitara alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wachimbaji wadogo kwenye mgodi mdogo wa Blue Leaf uliopo mkoani Geita alipofanya ziara ya kikazi.

Naibu waziri huyo alisema wachimbaji wanapaswa kuwa na sehemu moja kwa shughuli za uchenjuaji hatua itakayosaidia kudhibiti maji yasisambae kwenye mazingira hivyo kuathiri binadamu, wanyama na mimea.

“Lengo la Serikali sio kuwakwamisha wachimbaji wadogo lakini pia wanapaswa kutekeleza kanuni na taratibu hivyo wana nafasi ya kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kupanda miti maeneo wanayokatwa kwa kuwa wanatumia sehemu kubwa ya miti katika shughuli zao,” alilisitiza.

Pamoja na mambo mengine katika ziara hiyo Waitara alipanda mti kuhamasisha wachimbaji wengine wafanye hivyo kwa kuwa wanatumia sehemu kubwa kuikata. Pia alimpongeza mwenyekiti wa mgodi huo, Christopher Kadio kwa kuzingatia kanuni za mazingira zikiwemo kupanda miti katika maeneo hayo.

Aidha, akizungumza katika kikao na maafisa mazingira kutoka halmashauri za Mkoa wa Geita alizitaka halmashauri hizo kujenga madampo ya kisasa kwa ajili ya taka ngumu ili kutunza mazingira.

Waitara alisema pia zinapaswa kuweka mfumo unaoeleweka wa maji taka na taka ngumu ili wananchi wajue taka hizo zinatupwa wapi na kushirikiana na wanaozalisha taka hizo hususan za plastiki kuzilejeza.a agizo hilo jana

Naibu Waziri Waitara amefanya ziara mkoani Geita kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu juhudi za Serikali katika kulinda hifadhi ya mazingira, kuhamasiaha usafi wa mazingira, upandaji miti pamoja na kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Hifadhi ya Mazingira ya mwaka 2004.


Share:

Wafugaji Watakiwa Kuwa Na Mifugo Bora, Kuboresha Maisha Na Kukidhi Mahitaji Ya Viwanda

 Na. Edward Kondela
Wafugaji wametakiwa kuanza kufikiria kuwa na ng’ombe bora badala ya kuwa na ng’ombe wengi wasio na ubora ambao hawakidhi tija katika maisha yao kwa kutotoa mazao bora ambayo hayawezi kutoa kipato cha kuridhisha.

Akizungumza jana (29.12.2020) katika Kijiji cha Kinango kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wakati akishuhudia zoezi la uogeshaji mifugo dhidi ya magonjwa mbalimbali wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema mifugo mingi wakiwemo ng’ombe ni njia mojawapo ya kutunza fedha ambayo imekuwa ikitumiwa na wafugaji hivyo ni muhimu wafugaji hao kuhakikisha mifugo yao inakuwa bora kwa kuipatia huduma muhimu ikiwemo ya kuiogesha.

“Nchi yetu tuna ng’ombe wengi sana, lakini wengi siyo bora kama inavyotakiwa sasa tunatakiwa kutoka kuwa na ng’ombe wengi tu bali tuwe na ng’ombe walio bora, tukiwa na ng’ombe wengi wasio bora hawatusaidii sana katika maisha yetu, kwa sababu lengo la kuwa na ng’ombe atupe nyama, atupe maziwa na atupe kipato sasa tufikirie kuwa na ng’ombe bora na moja ya njia ya kuwa na ng’ombe bora ni hii ya kuwaogesha.” Amesema Mhe. Ndaki

Mhe. Ndaki ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa fedha 2020/2021 imetenga bajeti ya kukarabati majosho kadhaa yaliyopo maeneo mbalimbali nchini na kuahidi kuwa wizara itakarabati majosho matano yaliyopo katika Wilaya ya Magu ili mifugo mingi iweze kuogeshwa na kuwa bora.

Pia, Mhe. Ndaki akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul katika ziara hiyo amesema njia nyingine ya kuwa na ng’ombe bora ni wafugaji kuhakikisha mifugo yao inapata malisho bora ambayo yatafanya mifugo hiyo kuwa na afya bora lakini kwa sasa wafugaji wamekuwa wakichunga katika maeneo machache hali inayofanya mifugo kutokula chakula kinachotakiwa.

Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikishughulikia sana suala la malisho ambalo ni moja ya tatizo kubwa kwa wafugaji pamoja na maji na kutumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kutokana na kuruhusu wafugaji wachunge kwenye baadhi ya maeneo yaliyokuwa ya hifadhi na mengine kuzuiliwa hali iliyotoa ahueni kwa wizara kupata maeneo ya kulisha mifugo ili iwe na ubora.

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Nchini (TMB) Bw. Iman Sichalwe amewaeleza wafugaji kuwa suala la kuogesha mifugo dhidi ya magonjwa ni muhimu kwa kuwa limekuwa likizuia Tanzania kuuza nyama katika nchi mbalimbali kutokana na viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama kutopata mifugo bora.

Amefafanua kuwa uogeshaji unaboresha afya ya mfugo ikiwemo ya nyama na ngozi hivyo kuvifanya viwanda kufanya kazi na kuwaongezea vipato wananchi kwa kupata masoko ya kuuza mifugo yao, serikali kupata fedha kupitia tozo mbalimbali, upatikanaji wa fedha za kigeni na kwamba hali hiyo haitawezekana endapo mifugo haitadhibitiwa na magonjwa ili kupata nyama bora na kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi bora.

Katika ziara hiyo ya siku mbili Mkoani Mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametembelea pia kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama cha Alpha Choice kilichopo wilayani Magu na kuzungumza na baadhi ya wafugaji waliofika kiwandani hapo kwa kuwataka waanze kubadilisha ubora wa mifugo yao kwa kuwachanja, kuwaogesha, kuwapatia maji na malisho yanayotosheleza na kuacha kuwachunga katika maeneo marefu ili mifugo hiyo iwe na afya nzuri ambayo mfugaji atauza kwa bei nzuri na mwenye kiwanda kupata mfugo wenye mazao bora.

Mhe. Ndaki amesisitiza hilo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wawekezaji kwenye viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama kutopata ng’ombe bora ambao wanaweza kukidhi katika soko la kimataifa hali ambayo wakati mwingine nyama kukataliwa na baadhi ya nchi kutokana na mifugo kuwa na magonjwa na nyama kutokuwa na ubora unaotakiwa.   

“Nawaombeni sana tuanze kuboresha ng’ombe wetu ili tupate faida ya kuwa na kiwanda hapa na kingine nimekiona kule wilayani Misungwi na chenyewe wanapata ng’ombe kidogo sababu ni hiyo hiyo ng’ombe wetu hawajawa bora sana, sasa wawekezaji hawa wamelazimika wawe wananununa ng’ombe wanawafuga mahali kwanza wanawalisha ili wabadilike sura na afya waliyotoka nayo kwa wafugaji ambao  ni sisi.” Amefafanua Mhe. Ndaki

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul na Katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah pamoja na wataalam wengine kutoka wizarani, amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Mwanza ambapo amejionea mambo mbalimbali yanayohusu sekta za mifugo na uvuvi.



Share:

Bashungwa:Tutaendelea Kusimamia Maadili katika Sanaa kumuenzi Mngereza


Na Shamimu Nyaki -WHUSM

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia vyema Maadili na Utamaduni wa Taifa kupitia Sanaa ili kumuenzi aliyekua Katibu Mtendaji Marehemu Godfrey  Mngereza.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo Desemba 29, 2020 Jijini Dar es Salaam katika tukio la kuaga mwili wa aliyekua Katibu Mtendaji Marehemu Godfrey Mngereza ambapo amesema  Serikali itaweka mazingira mazuri kwa nchi rafiki kwa ajili ya kupata  soko la kuuza  kazi za sanaa.

“Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 inaelekeza kusimamia vyema Sekta ya Sanaa na Michezo ambazo zinakua kwa kasi hapa nchini, na sisi kama viongozi tutaisimamia kikamilifu” Waziri Mhe. Bashungwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali  Dkt. Hassan Abbasi  amesema kuwa wizara  imepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo,  huku akieleza kuwa marehemu Mngereza alikua anasimamia Sheria pamoja kutenda haki kwa wadau wake. Na ni mtu ambaye waliheshimiana na kutaniana sana.

Naye waziri Mstaafu wa wizara hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe ameleeza kuwa marehemu Mngereza alikua anaisimamia vizuri BASATA, hasa kukuza sanaa, kulinda utamaduni wa Taifa letu na kusimamia Sheria na taratibu za kufanya kazi ya Sanaa.

Aidha, Mbunge na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Humfrey Polepole amesema kuwa mazuri aliyoacha Marehemu Mngereza  ni vizuri kuyaenzi na aliyoanzisha kuyaendeleze.

Vile vile, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abubakari Kunenge alieleza masikitiko yake kwa kusema msiba hauzoeleki, huku akieleza kuwa jamii na wadau wa Sanaa wanapaswa kuendelea kumuenzi kwa kufanya mazuri kwakua kufanya hivyo atakua anaishi mioyoni mwao.

Halikadhalika, Msanii wa Kizazi Kipya Nasib Abdul (DiamondPlatnumz) alieleza kuwa marehemu Mngereza alikua mlezi mzuri kwa wasanii kupitia ushauri aliokua anatoa na pale palipohitaji ukali alitumia busara katika kufanya maamuzi.

Marehemu Godfrey Mngereza alifariki Desemba 24, katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na atazikwa Desemba 30, 2020 kijijini kwao Suji Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro.


Share:

Waziri Mhagama: Waajiri Msiogope Uwepo Wa Vyama Vya Wafanyakazi Kwenye Maeneo Ya Kazi

 


Na: Mwandishi Wetu, Morogoro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka waajiri nchini kutoogopa uwepo wa Vyama vya Wafanyakazi katika sehemu za kazi kwa kuwa ndio fursa ya pekee ya kutatua changamoto zinazojitokeza katika sehemu za kazi.

Ametoa kauli hiyo jana Disemba 29, 2020 alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa sita (6) wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliyopo katika Hoteli ya Edema, Mkoani Morogoro.

Waziri Mhagama alieleza kuwa Vyama vya wafanyakazi vimekuwa tegemeo kwa wafanyakazi hususan katika kulinda na kutetea maslahi na haki za wafanyakazi waliopo nchini, hivyo wajibu wa waajiri kutambua uwepo wa vyama vya wafanyakazi ili kuleta tija katika sehemu za kazi.

“Uwepo wa Vyama Vya Wafanyakazi imekuwa ni nyenzo muhimu ambayo imeongeza tija na kujenga hali ya msukumo katika utendaji wa kazi wa wafanyakazi waliopo katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini,” alieleza Mhagama

Alifafanua kuwa, vyama vya wafanyakazi ni umoja wa hiari na wa kidemokrasia ambao wafanyakazi wamekuwa wakitumia kulinda na kupeleka mbele mahitaji na matakwa ya pamoja kwa waajiri wao.

“Tumeshuhudia namna baadhi ya vyama vya wafanyakazi vimekuwa chachu katika kuhamasisha majadiliano baina ya waajiri na wafanyakazi katika kufunga mikataba ya hali bora ya kazi ambayo imekuwa ikiwanufaisha wanachama,” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa, vyama vya wafanyakazi vijenge utaratibu wa kuandaa mpango kazi wa muda mrefu na wa muda mfupi ili kutimiza malengo ya vyama hivyo vinavyowawakilisha wafanyakazi kwa wakati. Pia amehimiza suala la utoaji wa elimu kwa wanachama wa vyama vya wafanyakazi ili kuwapa wanachama wao uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama vyao.

“Mkiwaelimisha wanachama mtajenga uthubutu wa kusimamia masuala mbalimbali na mtawajengea ujasiri wanachama wenu kwa kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi,” alisema

Sambamba na hayo amevitaka vyama vya wafanyakazi kusimamia misingi ya sheria, maudhui ya uwepo wa taasisi zao na sekta zao badala ya kuanzisha migogoro isiyokuwa na sababu ambayo itapelekea waajiri kuogopa uwepo wa vyama vinavyowawakilisha katika maeneo ya kazi.

“Matumaini yangu vyama vya wafanyakazi vitajenga mahusiano mazuri baina ya wafanyakazi na waajiri ili kupunguza migogoro iliyopo katika sehemu za kazi,” alisema Mhagama

Pia, Waziri Mhagama amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi vilivyopo nchini kujenga utaratibu wa kukumbushana wajibu wao kama viongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao sawasawa katika maeneo wanayoyawakilisha.

Aidha, pongezi nyingi zilitolewa kwa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) na Mheshimiwa Mhagama ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo kutokana na namna chama hicho kimekuwa kikiratibu shughuli zake, pamoja na kuwatakia uchaguzi wenye amani na utulivu ambao ulifuata baada ya ufunguzi wa mkutano huo.

Kwa Upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Ndg. Tumaini Nyamuhokya alieleza Serikali imekuwa msatri wa mbele katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi nchini akitolea mfano suala la punguzo la kodi “Pay as You Earn” ambalo limewanufaisha wafanyakazi waliopo katika sekta binafsi na sekta ya umma.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), Bw. Paul Sangeze alifafanua kuwa TUICO ni miongoni mwa Vyama huru kumi na moja vya wafanyakazi nchini ambavyo vitaendelea kuboresha hali ya wanachama na wafanyakazi wakati wote wakiwa makazini.

“Tunaahidi kuendelea kushirikiana na serikali pale tutakapoona kuna haja ya kutunga sheria sahihi za kazi na kuandaa sera nzuri za kuendeleza uchumi na manufaa kwa wafanyakazi,” alieleza Sangeze

Pia, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Karubelo alieleza kuwa tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani kumekuwa na mshikamo mkubwa na amani miongoni mwa waajiri na wafanyakazi ambayo imepelekea wafanyakazi kupata heshima kubwa na tunashuhudia wafanyakazi wakishiriki kwenye miradi mkubwa ambayo inatekelezwa hapa nchini.

Naye, Kaimu Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Pendo Berege alisema kuwa mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa katiba na ndio sehemu pekee ya kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu chama.

“Ofisi ya Msajili inategemea kuona vyama vya wafanyakazi nchini vinaendelea kutekeleza katiba za vyama vyao, kutambua mipaka ya kiutendaji na kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachama,” alisema Berege

Mkutano huo Mkuu wa wa sita (6) wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) uliofanyika Mkoani Morogoro ilikuwa ni sehemu mmoja wapo ya utekelezaji wa mikutano kwa mujibu wa katiba ya Chama ambapo tukio hilo lilihusisha na uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger