Saturday 19 September 2020

TUICO SHINYANGA YAPATA VIONGOZI WAPYA...MENDE AMWANGUSHA MLINDOKO



Mwenyekiti mpya wa Chama Cha wafanyakazi wa Viwanda Biashara, Fedha Huduma na Ushauri TUICO mkoa wa Shinyanga Ebenezer Mende akiwashukuru wanachama kwa kumchagua na kuahidi kutatia changamoto zote zilizopo. Picha na Suzy Luhende.

Sehemu ya wanachama wa TUICO wakiwa ukumbini

Wanachama wa TUICO wakiwa katika picha ya pamoja.

Wanachama wa TUICO wakiwa katika picha ya pamoja.


Na Suzy Luhende, Shinyanga
CHAMA Cha Wafanyakazi wa Viwanda Biashara, Fedha Huduma na Ushauri (TUICO) mkoa wa Shinyanga kimefanya uchaguzi na kupata viongozi wapya ambao watafanya kazi kwa muda wa miaka mitano kwa ajili ya kushughulikia migogoro mbalimbali ya kikazi.

Akisimamia uchaguzi huo leo Ijumaa uliofanyika mjini Shinyanga, Katibu wa TUICO mkoa wa Shinyanga Fabian Samkumbi,  amesema wamefanya uchaguzi huo kwa kufuata utaratibu na kanuni za Sheria baada ya viongozi waliokuwepo kumaliza muda wao wa miaka mitano.

"Nategemea kuona nyote mliochaguliwa kimkoa matawini na sehemu za kazi, wawakilishi mtakiongoza chama chetu kwa ufanisi mkubwa ili kukivusha katika kipindi kingine Cha miaka mitano 2020 mpaka 2025",amesema Samkumbi.

Samkumbi amebainisha kuwa viongozi waliomaliza muda wao walichaguliwa mwaka 2015 mpaka 2020, hivyo wamemaliza muda wao na kuchagua uongozi mwingine unaoongozwa na Mwenyekiti mpya Ebenezer Mende.

"Chama chetu hapa kwa kushirikiana na wanachama waliochaguliwa leo, tutahakikisha wanachama wetu wanazielewa vyema sheria za kazi na tutaendelea kuingiza wanachama wapya na kuimalisha matawi aliyopo", ameeleza Samkumbi.

Aidha Samkumbi amemtaka Mwenyekiti aliyechaguliwa na uongozi wake kusimamia ipasavyo wafanyakazi wote kwani bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili , kwani baadhi ya waajili wamekuwa na kawaida ya kuwazuia wafanyakazi wao kujiunga na chama hicho.

Mwenyekiti ambaye amemaliza muda wake Fue Mlindoko ambaye kura zake hazikutosha amemshauri Mwenyekiti aliyechaguliwa Ebenezer Mende kusimamia vizuri wafanyakazi ili waweze kutendewa haki katika sehemu za kazi zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti aliyechaguliwa kukisimamia chama hicho Ebenezer Mende amesema changamoto zinazowahusu wafanyakazi ni nyingi hivyo atahakikisha anawatembelea wafanyakazi na kujua kero zao ili aweze kuzitatua kwa wakati.

"Nitatakiwa kuwa na mawasiliano ya karibu baina ya waajili na wafanyakazi ili kutatua changamoto mbali mbali kwa kufuata kanuni na kuhakikisha sitahiki za wafanyakazi zinapatikana kwa wakati na kuhakikisha amani inakuwepo katika sehemu ya kazi",amesema Mende.

"Natarajia kuleta muungano kwa waajili na wafanyakazi kwani mfanyakazi anatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu ili aweze kulipwa sitahiki zake kwa wakati na mwajili amlipe mfanyakazi wake sitahiki zake kwa wakati unaotakiwa ili kuondoa migogoro makazini",amesema Ebeneza.

Baadhi ya wafanyakazi waliohudhuria mkutano huo wa uchaguzi akiwemo Neema Wilson na Husna Waziri wamesema uchaguzi umefanyika kwa amani na ulikuwa wa haki, hivyo wanawaamini viongozi waliochaguliwa ni wachapa kazi.

Katika uchaguzi huo waliojiteza kuwania nafasi ya Mwenyekiti walikuwa watatu kwa mara ya kwanza,ambao ni Rajabu Maulid ,Ebenezer Mende na Fue Mlindoko lakini kutokana na sheria na kanuni ya chama hicho mshindi hakufikisha idadi ya kura zinazotakiwa ambazo ni nusu ya wanachama waliopiga kura, hivyo uchaguzi ulirudiwa kwa watu wawili waliofuatana ambao ni Fue Mlindoko na Ebenezer Mende.

Fue Mlindoko na Ebenezer Mende walipigiwa kura Mlindoko alipata Kura 22 na Mende alipata kura 33 ambaye ndiye aliibuka kuwa mshindi na kuwa mwenyekiti wa TUICO mkoa wa Shinyanga.

Waliochaguliwa katika kamati tendaji sekta ya biashara ni Husna Waziri kutoka kutoka Shirika la umeme Tanesco Shinyanga, na Wolfgan Kalikawe kutoka Tanesco Maswa, sekta ya fedha walichaguliwa Fatuma Masha na Godfrey Hamba.

Katika sekta ya huduma na ushauri alichaguliwa Grace Kilenga kutoka Kahama na Twaiba Kweka kutoka Islamic Kahama, pia mjumbe wa mkutano mkuu Kanda ni Samson Sita, Sekta ya biashara ni Wolfgan Kalikawe, sekta ya fedha ni Godfley Hamba. 


Pia sekta ya huduma na ushauri Kanda alichaguliwa Rajabu Maulid, na mkutano mkuu Taifa sekta ya viwanda alichaguliwa Kondo Diharibika kutoka Kahama, sekta ya biashara Maria Mazelengwe, sekta ya fedha Fatuma Masha, huduma na ushauri Twaiba Kweka na wawakilishi wa vijana ambao wataingia mkutano mkuu Taifa ni Tawfiq Omary na Salama Mhajin
Share:

Friday 18 September 2020

CHEGE AAHIDI MAJI, KUFUFUA MICHEZO, AIRO, OCHELE,WATIA NIA WAMUOMBEA KURA UBUNGE JIMBO LA RORYA


Mgombea Ubunge jimbo la Rorya Jafari Chege akiwaomba kura wananchi wa Kata ya Roche wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea Udiwani.
Aliyekuwa mbunge wa Rorya Lameck Airo akimuombea Kura Jafari Chege katika uzinduzi wa kampeni za Mgombea Udiwani kata ya Roche
Mgombea ubunge kupitia CCM jimbo la Rorya Jafari Chege akifurahi wakati wa mkutano wa kampeni kata ya Roche
***
Na Dinna Maningo,Rorya 
Mgombea UbungeJimbo la Rorya kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jafari Chege amesema kuwa akichaguliwa kuwa mbunge kazi yake kubwa itakuwa ni kwenda kujenga hoja bungeni pamoja na kukumbusha utekelezaji wa yale yaliyopo kwenye Ilani ya CCM ikiwemo ya Zahanati kila Kijiji.

Akizungumza  leo kwenye uzinduzi wa kampeni za mgombea Udiwani kata ya Roche Ally Juma,mgombea huyo alisema kuwa  kazi kubwa ya mbunge ni kujenga hoja na kuzisimamia ili zifanyiwe utekelezaji  lakini piawenuatua kero mbalimbali zilizopo ndani ya jimbo.

"Rorya ina changamoto kubwa ya maji mimi nitajikita kuzungumzia sera na siyo kumzungumzia mtu,kwakuwa wananchi wanahitaji kuona mgombea wao anawaaeleza nini na kufahamu Sera zake,mimi ni kijana mwenye nguvu ambaye nitashughulikia kero kwa wakati.

"Wananchi wanahitaji kiongozi wa kuwaunganisha pamoja na siyo kiongozi anayewagawa,mkishatengana hakuna maendeleo, ukabila ulisemwa sana Rorya lakini nawashukuru wananchi mnajitahidi kuupinga ukabila na mimi naupinga na ndiyo maana nikawiwa kugombea ubunge ili tuungane katika kuleta maendeleo" alisema Chege.

Akizungumzia kero ya maji alisema kuwa vijiji vingi havina maji kikiwemo kijiji cha Migeko ambacho wananchi wanatembea km 20 kufata maji ziwa Victoria nakwamba atahakikisha kijiji hicho anakipa kipaumbele ili kisima kichimbwe wakati huo michakato mingine ya utatuzi wa maji ikiendelea.

"Nikiwa mbunge nitapitia miradi yote ya barabara kujua yenye changamoto  na kuhakikisha inaingizwa kwenye mipango na inakarabatiwa,nitahakikisha naondoa masharti magumu ya mipoko inayowakabili wanawake na vijana ikiwemo namna ya kuandika katiba na suala la uanzishaji wa akaunti",alisema Chege.

Mgombea huyo aliongeza kuwa kupitia Sera ya chama atamuomba Rais na chama chake kuwa na vyuo wiwili vya ufundi Rorya ili kurahisisha shughuli za wananchi lakini pia kukuza kipato cha wananchi wakiwemo vijana.

Kwa upande wa michezo alisema kuwa  lazima michezo irejeshwe Rorya kwakuwa ni sehemu ya kuzalisha vipaji na kuunganisha ushirikianao kwa wananchi na nakwamba inaleta hamasa kubwa kwa wananchi.

Mbunge wa jimbo la Rorya Lameck Airo anaemalizia muda wake wa ubunge ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni za mgombea Udiwani aliwaomba wananchi wakiwemo na wa vyama vya upinzani kumpigia kura Chege.

"Chagueni CCM,mimi sijawahi kuwabagua wapinzani nyie ni mashahidi kuna kata zilizokiwa na Madiwani wa Chadema nimechangia maendeleo ikiwemo kata ya Ikoma tumejenga shule 4 ,Kitembe nimeungana nao kupambana na wizi na michango mbalimbali mchagueni Rais Magufuli,mchagueni Chege na Diwani Juma, mnafahamu hata  Mwenyekiti wangu wa CCM Ochele akiwa Diwani hapa tumefanya mengi",alisema

"Hata nikiwa nje ya ubunge nitashirikiana nanyi,mkiniita kwenye shughuli zenu ziwe za mbunge au Diwani nitakuja msiwe na wasiwasi,nawashukuru wana Roche kwa miaka 10 sijawahi kupigiwa simu ya watu kuibiwa mifugo,naombeni tufanye uchaguzi kwa uungwana tusikilize sera za wagombea,sisi wana CCM hatuna nguvu za kupigana wala kuhamasisha kukatana mapanga kazi yetu ni kuwaombeni kura", alisema Airo.

Mgombea Udiwani kata ya Roche Ally  Juma aliwaomba wananchi kumpigia kura nakueleza kuwa kabla ya kuchukua fomu alifanya utafiti na kugundua changamoto mbalimbali ikiwemo ya adha wanayoipata wananchi juu ya ukosefu wa kituo cha kutolea huduma ya afya.

"Kilichonihamasisha ni kuhusu vituo vya avya,kuna zahanati ya Osiri na Ng'ope zilijengwa na wananchi lakini zimekuwa magofu watu wanaenda kutibiwa Kenya,nitakapokuwa kwenye vikao vya halmashauri nitalazimisha ili haya majengo yaweze kukamilika kwa wakati,lakini kwa mambo yatakayoshindikana  nitamweleza mbunge nae atayawasilisha bungeni", alisema Juma.

Mwananchi wa kijiji cha Roche Godwin Johson alimtaka mgombea ubunge na Udiwani kama wakishinda watatue kero ya maji na kujenga lambo la maji la kunyweshea mifugo,maji safi na salama kwa wananchi pamoja na zahanati ya afya huku waliotiania kugombea Udiwani wakiahidi kutoa ushirikiano.

Godfrey Obonyo ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Ilala-Dar es Salaam alisema dhamira ya kuzunguka vijijini ni kuitafutia kura CCM.

Waliotia nia kugombea ubunge viti maalumu Irine Makongoro na Stella Odatt waliwaomba wananchi hususani  wanawake kuipigia CCM kwakuwa ndiyo chama kitakachowaletea maendeleo.

Walio tiania kugombea Ubunge jimbo hilo akiwemo Wambura Sasi na Leonard Otuoma walisema kuwa wataendelea kumuunga mkono Chege kuhakikisha anashinda.

Daud Wembe alisema "Tumekuja kuzungumza mambo ya misingi,aliyepewa kusimamia rasilimali za Taifa ni Rais wetu Magufuli na yeye ndiye kamsimamisha Chege awe mbunge wetu najua kampeni bado zinaendelea tutasema mengi",alisema Wembe.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi  (CCM)wilaya ya Rorya Charles Ochele aliwaomba wana Roche kuwapigia kura viongozi wa CCM bila kumsahau Chege na kwamba chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinashinda.

Katika uzinduzi huo wanachama 6 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) walimkabidi Ochele kadi za chama hicho na kujiunga na CCM kwa madai kuwa Serikali inayoongozwa na John Magufuli imefanya mengi ambayo yamewavutia na hivyo kujiunga na CCM.
Kushoto ni mwenyekiti wa CCM wilaya ya Rorya Charles Ochele wakiwa kwenye mkutano Kata ya Roche
Kikundi cha akina mama wa kata ya Roche wakiimba wakati wa kampeni za CCM
David Wembe aliyetiania ya Ubunge Rorya akizungumza na wananchi wa kata ya Roche
Aliyekuwa Mtia nia Ubunge Leonard Otuoma  akizungumza na wananchi wa Roche

Irene Makongoro aliyekuwa mtiania ubunge viti maalumu akizungumza
Mwananchi wa Roche Godwin Jonson akizungumza
Aliyekuwa Mtia nia ubunge viti maalumu mkoa wa Mara Stella Odatt
Mgombea Udiwani kata ya Roche Ally Juma akiomba kura

Godfrey Obonyo mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Ilala-Dar es Salaam akizungumza kwenye mkutano wa kampeni

Wanachama wa CHADEMA wakikabidhi kadi zao baada ya kuhamia CCM
Share:

MWALIMU DELPHINA KUPITIA CUF AANIKA VIPAUMBELE VYAKE AKICHAGULIWA KUWA MBUNGE JIMBO LA SINGIDA KASKAZINI

Mgombea wa nafasi ya ubunge Jimbo la Singida Kaskazini Mkoani Singida Mwl Delphina Frank kupitia Chama cha Wananchi CUF akiomba kura kwa wananchi.
  Mgombea Ubunge akicheza za wananchi wa Kata ya Kinyagigi akicheza za wananchi wa Kata ya Kinyagigi
Wananchi wakimsikiliza mgombea Ubunge wa chama cha Wananchi CUF


Na Ismail Luhamba, Singida.
Mgombea wa nafasi ya ubunge Jimbo la Singida Kaskazini Mkoani Singida Mwl Delphina Frank kupitia Chama cha Wananchi CUF amesema akichaguliwa kuwa Mbunge atahakikisha anaimarisha sekta ya Afya, Elimu,Maji na Nishati katika Jimbo hilo.

Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Kinyagigi kwenye mwendelezo wa kampeni zake za kunadi sera za chama hicho,mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mwl Delphina Frank ametaja vipaumbele vinne ambavyo atavitekeleza endapo atachaguliwa kuwa Mbunge.

“Wananchi mnaonisikiliza hapa napenda kuwaambia kwamba nina mambo makubwa manne ya kuwafanyia nyinyi katika kipindi cha miaka 5, endapo mtanipa ridhaa ya kuwaongoza nitaanza na Sekta ya Afya, Elimu, Mifugo na Maji”, alisema Delphina.

Akizungumzia suala la Afya amesema atahakikisha kila Zahanati iliyojengwa na Serikali inakuwa na vifaa tofauti na sasa,kwani kwa sasa  kuna majengo tu huku kukiwa na ukosefu wa vifaa ndani ya hayo majengo.

“Ifikapo tarehe  28 Oktoba Jumatano mjitokeze kwa wingi kupiga kura ili kuhakikisha tunakiweka chama madarakani kutimiza ahadi tulizoziahidi”, alisema Delphina.

Delphina alisema kama CUF watapata ridhaa ya kuongoza katika Jimbo la Singida Kaskazini ndani ya miaka hiyo 5 watahakikisha wanasimamia vyema masuala yote yanayowahusu wafugaji na wakulima, kutunga na kutengeneza sera bora ili kuwa na ufugaji wenye tija na kilimo kwa ujumla.

“Hakika nawaambia wananchi wangu chagueni chama cha wananchi ili kiende kushirikiana na wataalamu wa kilimo, Maafisa mifugo tufuge na tulime kisasa ili tuondokane na umaskini tulionao,sasa tar 28 msifanye makosa kwa mgombea urais wetu Prof. Ibrahim Lipumba  na mimi”, alisema Delphina

Akifunga mkutano huo wa kampeni Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya Shabani Jumanne, aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera za mgombea Ubunge,na anaamini wamemuelewa na tar 28 watakwenda kufanya maamuzi ya haki kukipatia kura chama chicho.

"Nimefurahi sana tumefanya mkutano wetu kwa amani ila napenda kuwaambia tusifanye siasa za mazoea twendeni tukafanye mabadiliko sasa tumetawaliwa kwa muda mrefu sana bila maendeleo yeyote, hebu tazameni hatuna umeme, maji safi na salama, barabara mbovu chagueni Chama cha Wananchi  CUF kikaisimamie Serikali na kuhakikisha maendeleo haya yanapatikana katika Jimbo letu." alisema Jumanne.


Share:

CHADEMA WATIKISA KISESA WAKIZINDUA RASMI KAMPENI...GIMBI MASABA, KISHABI WANADI SERA


Makamu Mwenyekiti Chadema Kanda ya Serengeti Gimbi Masaba akiwaombea kura wagombea wa CHADEMA

Na Mwandishi wetu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo kimetikisa Jimbo la Kisesa, Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu, wakati wa uzinduzi kampeni za Mgombea Ubunge Jimbo la Kisesa Francis Kishabi.

Akihutubia wananchi waliohudhuria mkutano huo leo, Maka Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Gimbi Masaba, amewaomba wananchi wa Kisesa kuwachagua wagombea wote wa CHADEMA ngazi ya Ubunge, urais na udiwani.

"CHADEMA tukishinda tutaondoa kero zinazowakabili wananchi wa Kisesa, ikiwamo ya kuvamiwa wanyamapori- tembo", amesema.

Mgombea Ubunge Jimbo la Kisesa, Francis Kishabi, akihutubia mkutanoni hapo ameahidi kushughulikia tatizo la maji, afya na kuboresha sekta ya kilimo na elimu zinazowatatiza wananchi wa eneo hilo.

Kulingana na mgombea Kishabi, ataweka mazingira rafiki ya elimu iwapo ataaminiwa kwenda kuwawakilisha bungeni. 

"Hakutakuwa na makosa katika uongozi wangu. Naomba nitumeni nikawatetee bungeni na kuwaletea maendeleo ya kisekta," Kishabi amesema.
Mgombea Ubunge Jimbo la Kisesa ni Francis Kishabi akiomba kura kwa wananchi wa Kisesa
Share:

Kazi Imekamilika : NEC YAFANYA UAMUZI WA RUFAA 616 ZILIZOWASILISHWA NA WAGOMBEA UBUNGE NA UDIWANI


Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania, Dkt. Wilson Charles 
Share:

MGOMBEA UBUNGE CCM MANYONI MASHARIKI DKT.PIUS CHAYA AKICHAGULIWA KUVUTIA WAWEKEZAJI


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki mkoani Singida kupitia  tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Pius Chaya, akihutubia wananchi na wana CCM katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni ulioandaliwa na CCM wilayani hapa jana.


Katibu wa Umoja wa Vijana CCM Wilaya ya Manyoni, Wambura Igembya akizungumza kwenye mkutano huo. 

Mgombea Udiwani wa Viti Maalumu wa Tarafa ya Kintinku, Joyce Kalikawe, akizungumza kwenye mkutano huo.


Mgombea Udiwani wa Viti Maalumu wa Tarafa ya Kintinku, Sara Diria, akizungumza kwenye mkutano huo.



Dotto Mwaibale na  Alinikisya Humbo, Manyoni

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki mkoani Singida kupitia  tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Pius Chaya amesema iwapo wananchi watampa ridhaa ya kumchagua kazi kubwa atakayoanza nayo ni kuwavuta wawekezaji.

Chaya aliyasema hayo jana wakati akihutubia wananchi na wana CCM katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika stendi ya shimoni ulioandaliwa na CCM wilayani hapa.

" Mkinichagua kuongoza jimbo ili ahadi yangu kubwa kwenu nitahakikisha nawavutia wawekezaji waje kuwekeza kwa kuanzisha viwanda na kutafuta masoko ili kukuza wa wana Manyoni na Taifa kwa ujumla. 

Alisema Serikali yetu imejikita zaidi katika uchumi wa viwanda hivyo kwa kushirikiana kwa pamoja na wana CCM wenzake atahakikisha wanaitekeleza ilani ya chama hicho ya 2020-2025 kwa vitendo kwa kuwavuta wawekezaji" alisema Chaya huku akishangiliwa.  

Akizungumzia suala la kilimo na ufugaji, Dkt, Chaya alisema kuna haja ya kujenga mabwawa yatakayo tumika kuvuna maji kwa ajili ya kunywesha mifugo na kulima kilimo cha umwagiliaji jambo ambalo litapunguza changamoto ya ajira kwa vijana na kuongeza pato kwa Taifa.

Aidha kuhusu changamoto ya mawasiliano ya barabara inayounganisha wilaya ya Chemba na Manyoni kupitia Kata ya Makanda kwenda kata ya Kintinku ambayo imekuwa ikikata mawasiliano nyakati za mvua,  Chaya ameahidi kutafuta utatuzi wake mara moja baada ya kuchaguliwa.

Dkt. Chaya alitaja vipaumbele vyake vingine kuwa ni pamoja na maboresho ya huduma ya afya, huduma ya maji, elimu na sekta ya kilimo ambayo ndio uti wa mgongo kwa watanzania.

Aliongeza kuwa endapo watampa ridhaa atahakikisha anasimamia kikamilifu nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa mustakabali wa maendeleo ya jimbo hilo na taifa kwa ujumla.

Alisema atahakikisha anasimamia vyema fedha katika ukamilishaji wa miradi ya maji iliyopo kuondoa kero hiyo, sanjari na kupigania kuwa na hospitali mpya ya kisasa ya wilaya, huku katika kukuza sekta ya kilimo na mifugo bila kusahau suala la elimu na michezo, ameahidi kuipa kipaumbele.

Mgombea Udiwani wa  CCM kata ya Manyoni, Simon Mapunda ametaja vipaumbele vyake kwa kata hiyo mara atakakapochaguliwa  kuwa ni kuongoza kata hiyo  kuwa ni pamoja  Afya, elimu na maji. 

Alisema kwa ushirikiano wa wananchi na halmashauri atahakikisha wanaboresha miundo mbinu mbali mbali ambayo ni pamoja na  suala la ujenzi wa soko jipya la kisasa, afya pamoja na elimu ili kuleta heshima na hadhi ya mji wa Manyoni ikizingatiwa upo karibu na makao makuu ya nchi.

Juu ya ushirikiano katika kipindi cha kampeni kwa wagombea walioshindwa kwenye kinyang'anyiro cha kura za maoni, John Madindilo na Moses Ntandu wameahidi ushirikiano.

Kwa upande wake aliyekuwa diwani wa kata hiyo Magembe Machibula mbali ya kueleza aliyofanya kipindi chake kwa ushirikiano mwema na wananchi na serikali katika sekta mbalimbali ambayo ni pamoja na uboreshaji elimu, afya, maji na ardhi, alisema pamoja na juhudi hizo lakini bado kuna changamoto ambazo zinahitaji kutatuliwa.

Ameongeza kuwa juu ya suala la kuongeza maeneo ya utawala kwenye Kata ya Manyoni yenye kadirio la wakazi 60,000 na kuunda kata nyingine, Machibula akimnadi mgombea huyo amemuomba kubeba jambo hilo, huku akiahidi ushirikiano.

Kwa niaba ya madiwani wote wa jimbo la Manyoni mashariki, Joyce Kalikawe ambaye ni mteule wa udiwani viti maalumu kutoka CCM, akiomba kura kwa Rais, Wabunge na Madiwani wa chama hicho, amewasihi wanawake wenzake kukiamini Chama Cha Mapinduzi.

Kwa upande wake Munde Tambwe Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora na Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida alimkabidhi Dkt, Pius Chaya ilani ya chama hicho ya 2020-2025 itakayotekelezwa kwa miaka mitano ijayo nakuwaomba wananchi kumpa kura nyingi Mgombea urais kupitia CCM, Dkt. John Magufuli na Wabunge na Madiwani.
Share:

RC Tabora Ataka Mwekezaji Wa Kiwanda Cha Nyuzi Achukuliwe Hatua Stahiki Kwa Kushindwa Kukiendesha Kwa Faida


 NA TIGANYA VINCENT
MAMLAKA zinazosimamia  viwanda zimeombwa kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua na kufanya maumuzi yanazostahili kwa Mwekezaji wa Kiwanda cha  Nyuzi Tabora kwa kushindwa kukiendesha kulingana na mkataba wake wa ununuzi ili kiwezo kuongeza uzalishaji wa kuleta tija kwa Taifa na Mkoa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati baada ya kutembelea Kiwanda hicho ili kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji wa nyuzi ya pamba kwa ajili ya masoko mbalimbali na kutoridhishwa na utendaji kazi wake.

Alisema Mwekezaji aliponunua Kiwanda hicho alitoa ahadi za kukifanyia ukarabati ili kiwe cha kisasa na kisaidie kuleta mapinduzi ya viwanda hapa nchini lakini hajatekekeza jambo hilo.

Dkt. Sengati alisema kuwa licha ya Mwekezaji huyo kukukopa fedha nyingi katika Taasisi mbalimbali kama vile kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 6.1 na fedha za kitanzania shilingi bilioni 1 hazikuwekezwa katika Kiwanda ili kionekana kinafanya kazi kwa tija.

Alisema fedha hizo zingewekeza katika Kiwanda zingeondoa matatizo mbalimbali ikiwemo uchakavu wa mitambo kwa kuleta teknolojia ya kisasa.

Dkt. Sengati aliongeza kuwa Mwekezaji huyo pia amekiuka lengo la Kiwanda la kuzalisha nyuzi kwa ajili ya kutengenezea nguo kwenye Viwanda vya nguo vya hapa nchni bali ameanza kutengeneza Kamba za kufungia mazao na vitambaa.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa Mwekezaji huyo pia ameuza mali za Kiwanda ikiwemo nyumba mbili za ghorofa na nyumba nyingine tano kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6 ambapo fedha hizo hazionyesha kuboresha Kiwanda.

Alisema wakati bado kiwanda kinamilikiwa na Serikali kilikuwa na waajiriwa zaidi ya 1,000 lakini baada ya kukibinafisisha wamepungua na kubaki 100.

Dkt. Sengati alisema kutokana na mwenendo wa utendaji wa Kiwanda hicho hivi sasa inaonekana kinaendeshwa kwa hasara ni kubwa kuliko faida ambayo Serikali ilitarajia kuiona baada ya ubinafsishaji.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Tabora alisema ni jukumu la Mmiliki wa Kiwanda kupitia Idara ya Masoko kutafuta masoko na sio Serikali kama wao wanavyoomba wasaidiwe.

Awali Katibu wa Kiwanda hicho Jotham Pascal alisema baada ya kukinunua kiwanda hicho Viwanda vya nguzo ambavyo ndio walikuwa wateja wao wakubwa wa nyuzi zao walianza kuagiza toka nje na kuwadhofisha.

Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo waliamua kubadilika na kuanza kutengeneza kamba na vitambua kwa ajili ya ufungaji tumbaku na kuhifdha pamba iliyochambuliwa.

Pascal aliwaambia Mkuu huyo wa Mkoa alisema uwezo wa kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali wanao ikiwa watahakikishiwa na kutafutiwa soko la uhakika.

Mwisho


Share:

GGML MDHAMINI MKUU WA MAONYESHO YA TATU YA TEKNOLOJIA ZA UCHIMBAJI MADINI GEITA


 Kushoto ni baadhi ya wafanyakazi wa GGML wakizungumza na wageni wanaotembelea banda la kampuni hiyo lililopo katika maonesho ya teknolojia ya madini mjini Geita
Kulia ni baadhi ya wafanyakazi wa GGML wakizungumza na wageni wanaotembelea banda la kampuni hiyo lililopo katika maonesho ya teknolojia ya madini mjini Geita

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ndiye mdhamini mkuu wa Maonyesho ya Tatu ya Teknolojia za uchimbaji madini mkoani Geita yatakayofanyika kati ya tarehe 17 hadi 27 Septemba 2020. Mwaka huu, Kampuni ya GGML imetoa udhamini wa kiasi kinachozidi Shilingi Milioni 200 za Kitanzania unaohusisha gharama za kusawazisha eneo la maonyesho pamoja na kugharamia mabanda 100 pamoja na umeme wa dharura (jenereta na mafuta yake) katika kipindi chote cha maonyesho hayo.

Maonyesho hayo ambayo yanafanyika katika viwanja vya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Mjini Geita ambalo pia limejengwa na Kampuni ya GGML kupitia mpango wake wa huduma kwa jamii kwa gharama za Shilingi Milioni 800.

“GGML inajivunia kudhamini maonyesho haya kwa mwaka wa tatu mfululizo. Mwaka huu tunakusudia kutoa uzoefu wetu wa matumizi ya vifaa mbalimbali vya uchimbaji kwa makampuni mengine lakini pia kwa wachimbaji wadogo. Ni jambo zuri pia kwamba tumetoa udhamini huu tukiwa tunaadhimisha miaka 20 ya uwekezaji wetu mkoani Geita na Tanzania. Tunajivunia kuendeleza ushirikiano na jamii inayotuzunguka kunufaisha wafanyabiashara wa ndani wanaokusudia kufanya kazi na sisi,” alisema Bw Simon Shayo, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu.

Tunafarijika sana kuona ndoto ya kuwa na kituo cha Uwekezaji na biashara ya nje hapa Geita inatimia na GGML inakuwa sehemu ya mafanikio hayo kupitia mpango wake wa kusaidia jamii.

Pamoja na tunu yake kuu ya kuisaidia jamii ya Geita kuwa na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ambayo yatabakia hata baada ya shughuli za uchimbaji kumalizika, Kampuni ya GGML pia imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Geita ikiwemo uwekezaji wa mradi wa Kituo cha Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Mjini Geita uliotumia bajeti ya Shilingi Milioni 800 za Kitanzania.

Maonyesho haya yatakutanisha kampuni za uchimbaji madini, wachimbaji wadogo na wa kati, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na nchi nyingine kwa ajili ya kuonyesha teknolojia zinazotumika katika sekta ya uchimbaji madini na fursa za uwekezaji na biashara kwenye sekta hiyo.

Mwaka 2019, Kamati ya Maandalizi ya Maonyesho ya Teknolojia za Uchimbaji Madini, iliitunukia GGML tuzo ya mshindi wa kwanza aliyetoa elimu na mafunzo ya teknolojia muhimu kwa wachimbaji wadogo sanjari na mifumo ya usalama na uokoaji inayopaswa kutumika migodini.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger