Monday 10 August 2020

MGANGA MKUU WA SERIKALI AWAAGIZA WAGANGA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KUONGEZA JITIHADA KATIKA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

NA WAMJW- KILIMANJARO

MGANGA Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ameagiza ndani ya miezi sita (6) Waganga Wakuu wote wa mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya na Waganga wafawidhi wa hospitali zote nchini kuongeza kasi katika kupunguza zaidi vifo vya mama na mtoto kwa kuboresha huduma na usimamizi katika maeneo yao.


Mganga Mkuu wa Serikali ametoa agizo hilo jana wakati wakati akiongea na Watumishi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi-Kilimanjaro kwenye ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma na ujenzi wa miundombinu ya afya katika Mkoa huo.

“Waganga Wakuu wote wa Mikoa, Wilaya pamoja na Waganga wafawidhi wa Hospitali zote mlifanyie kazi hili suala la kupunguza zaidi vifo vya akina mama wajawazito, nawapa miezi mitatu hadi sita, nione hali ya vifo vinakushuka zaidi kila mkoa, na Wilaya, na pamoja na Waganga wafawidhi wa Hospitali zote za kanda na Wilaya, itakavyofika miezi sita nitafanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na TAMISEMI, Kiongozi ataeshindwa tutafanya mabadiliko” alisema

Prof. Makubi amesema kuwa, vifo vya akina mama wajawazito na mtoto vinaweza kuisha kabisa nchini kama kutakuwa na uwajibikaji na kujitoa kwa kila mtu kwa nafasi yake, ikiwemo uratibu mzuri baina ya watoa huduma za afya ili kuondoa ucheleweshaji wa kupata huduma kwa mama wajawazito, huku akisisitiza kuzitumia Hospitali za kanda kubadilishana ujuzi na hospitali za ngazi ya chini, na utambuzi wa viashiria vibaya kwa mjamzito wakati wa mahudhurio kliniki.

“Kuna njia nyingi mnaweza kutumia ili kushinda hili, ikiwemo kuwawezesha Wataalamu ngazi za chini kuwa na uwezo wa kuzuia hiyo shida, kutoa mafunzo kwa kutumia hospitali za kanda tulizonazo, utambuzi wa viashiria vibaya ambavyo anakuwa navyo mjamzito wakati wa kliniki na uratibu mzuri ili kuondoa ucheleweshaji” alisema Prof. Makubi

Prof. Makubi aliendelea kwa kusisitiza kuwa, katika kuelekea zoezi hili, ni muhimu kuhakikisha utoaji takwimu zilizo sahihi zitakazosaidia kuleta mabadiliko kwa kufanya maboresho katika maeneo mbali mbali ya utoaji huduma.

Mbali na hayo, Prof. Makubi ametoa wito kwa viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro – Mawenzi kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa huo kumalizia mradi wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali hiyo, jambo litalosaidia kurahisisha utoaji huduma, hivyo kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Mradi huo wa jengo la mama na mtoto haujamalizika, Serikali inatoa wito mradi huo umalizike kwa wakati, sisi kama Serikali tutafanya kwa upande wetu, ili kuweza kuhakikisha jengo hilo linaweza kukamilika na linaanza kutoa huduma mara moja ” alisema


Share:

Mkutano Wa 40 Wa SADC Kufanyika Jijini Dodoma

Mkutano wa 40 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 Agosti, 2020 kwa njia ya mtandao (video conference) Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.
 
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge amesema mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na vikao vya Kamati ya kudumu ya Maafisa Waandamizi/Makatibu Wakuu na Mkutano wa Baraza la Mawaziri itakayoanza kufanyika tarehe 10 -13 Agosti, 2020 jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao (video conference).

"Kulingana na taratibu na miongozo ya uendeshaji wa SADC, nafasi ya uenyekiti hushikiliwa na nchi wanachama kwa kupokezana kwa kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Tanzania imekuwa Mwenyekiti tangu Mwezi Agosti, 2019 na inatarajwa kukabidhi Uenyekiti kwa Jamhuri ya Msumbiji katika Mkutano huo. Aidha, itakumbukwa kuwa mara ya mwisho Tanzania ilishika nafasi hii mwaka 2003," Amesema Balozi Ibuge.

Ameongeza kuwa, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa sasa wa SADC,  atakabidhi Uenyekiti kwa Mheshimiwa Philipe Jacinto Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji tarehe 17 Agosti 2020 jijini Dodoma kwa njia ya Video Conference.

Balozi Ibuge ameongeza kuwa, kwa kuwa kwa sasa Kiswahili ni moja kati ya lugha rasmi za mikutano ya SADC, lugha hiyo itatumika katika ngazi ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri na ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali.

Aidha, Katibu Mkuu, Balozi Ibuge amesema kuwa, kutokana na janga la COVID-19 na  mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya kufanya mikutano ya ana kwa ana, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania italazimika kukabidhi uenyekiti kwa njia ya mtandao ambapo Balozi wa Msumbiji hapa nchini atakabidhiwa uenyekiti kwa niaba ya nchi yake. Hali kadhalika, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji atakabidhi Uenyekiti kwa Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika hatua nyingine, Balozi Ibuge amesema kuwa mkutano huo utaongozwa na kauli mbiu ambayo ni “Miaka 40 ya Kuimarisha Amani na Usalama, Kukuza Maendeleo na kuhimili Changamoto zinazoikabili Dunia” ambapo kauli mbiu hiyo inatakiwa kutekelezwa na nchi zote Wanachama.

Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 16 wanachama wa SADC wakiwa katika nchi zao. Nchi hizo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ufalme wa Eswatini, Ufalme wa Lesotho, Jamhuri ya Namibia, Jamhuri ya Visiwa vya Shelisheli, Jamhuri ya Afrika Kusini, Jamhuri ya Malawi, Jamhuri ya Msumbiji, Jamhuri ya Mauritius, Jamhuri ya Madagascar na Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Zimbabwe.


Share:

MAKALA - HESLB WALIVYOFAFANUA HOJA NA MASWALI YA WAOMBAJI MIKOPO WA ELIMU YA JUU MIKOA YA KIGOMA NA GEITA

Na Ismail Ngayonga-HESLB

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) hivi karibuni imefungua dirisha la maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ya Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa  masomo 2020/2021.


Kufunguliwa kwa dirisha hilo kunatoa fursa kwa Wanafunzi mbalimbali waliohitimu masomo ya kidato cha sita na ngazi ya stashahada kutoka katika vyuo mbalimbali nchini kutuma maombi ya mikopo ya elimu ya juu ili kuwezeshwa na serikali katika gharama za ada, chakula na malazi pindi wawapo masomoni.

Katika kuhakikisha kuwa kila wanafunzi wote wa Kitanzania wenye sifa stahiki wananufaika na mikopo hiyo, HESLB imetoa mwongozo wa uombaji wa mikopo unaoanisha hatua muhimu na za msingi zinazopaswa kuzingatiwa na waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021.

Itakumbukwa kuwa katika kila mwaka wa masomo pindi unapotaraji kuanza, Serikali kupitia HESLB imekuwa ikitoa mwongozo kwa waombaji mikopo, ikiwa ni mojawapo ya hatua mahsusi iliyolenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wanufaika wanapata fursa ya kufahamu vigezo na sifa mbalimbali vinavyotumika katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu.

Aidha pamoja na kutoa miongozo hiyo, utafiti uliofanywa na HESLB umebaini kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakishindwa kupata mikopo ya elimu ya juu kutokana na kufanya makosa mbalimbali wakati wa kujaza fomu za maombi ya mikopo kama inavyoelekezwa katika mwongozo wa mwaka husika.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia HESLB kuanzia mwaka wa masomo 2019/2020 imekuwa ikiendesha programu mafunzo ya elimu kwa umma kwa wanafunzi wanaotaraji kujiunga na masomo ya elimu ya juu kwa kutembelea mikoa mbalimbali nchini ili kutoa ufafanuzi na hatua mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa katika kujaza fomu za maombi ya mikopo ya elimu ya juu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru anasema katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga fedha za mkopo kiasi cha Tsh. Bilioni 464 zinazotarajia kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 145,000 wakiwemo wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 91,000 wanaoendelea na masomo.

Anaongeza kuwa bajeti ya Tsh. Bilioni 464 kwa mwaka 2020/2021 imeongezeka kutoka Tsh. Bilioni 450 mwaka 2019/2020 ambazo ziliwanufaisha jumla ya wanafunzi 132,119, ambapo  ongezeko hilo la bajeti inatokana na adhma ya serikali ya kupanua wigo wa elimu ya juu hususani kwa wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi.

Hivi karibuni HESLB iliendesha mafunzo ya programu ya elimu kwa umma katika mikoa 14 nchini yakiwa na lengo la kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali kutoa kwa wadau wa elimu nchini ikiwemo wanafunzi, watendaji wa serikali na watoa huduma za mtandao katika ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini.

Mikoa hiyo ni pamoja na Rukwa, Mbeya, Katavi, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Geita, Kigoma pamoja na Zanzibar Unguja (Mjini Magharibi, Unguja Kaskazini, Unguja Kusini, Pemba Kaskazini, Pemba Kusini), ambapo Maofisa Mikopo wa HESLB waliweza kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wakati wa uombaji wa mikopo ya elimu ya juu unaofanyika kwa njia ya mtandao.

Wakati wa mafunzo hayo, katika Mikoa ya Geita na Kigoma Maofisa wa HESLB waliweza kufanya jumla ya mikutano 7 katika Halmashauri za Wilaya ya Geita, Chato, Bukombe, Mbogwe (Mkoa wa Geita) pamoja na Wilaya za Kasulu, Kibondo na Manispaa ya Kigoma Ujiji (Mkoa wa Kigoma) ambapo waliweza kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa maswali 159 kutoka kwa wanafunzi 3500 waliohitimu kidato cha sita na masomo ya stashahada katika Mikoa hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo Mkoani Geita, Meneja Mikopo wa HESLB Kanda ya Ziwa, Usama Choka anasema pamoja na nia njema iliyowekwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini wananufaika na mikopo hiyo, bado miongoni mwao wamejikuta wakikosa fursa hiyo kutokana na kufanya mbalimbali wakati wa kujaza fomu za maombi.

Anaongeza kuwa utafiti uliofanywa na HESLB umebaini kuwa wanafunzi wengi hususani wanaotoka katika kaya maskini wamejikuta wakikosa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kutokana na kukiuka maelekezo yanayotolewa katika mwongozo wakati wa kujaza fomu za maombi mtandaoni.

‘’Wanafunzi wengi wanaotoka katika kaya maskini hususani waliopo katika Mikoa ya pembezoni, wamekuwa wakishindwa kukamilisha baadhi ya maelekezo yanayotolewa wakati wa kujaza fomu za maombi ya mikopo ya elimu ya juu kupitia mtandao, hivyo HESLB tumeamua kuanzisha programu ya elimu ya mafunzo ya jinsi ya kujaza fomu hizo ili kuongeza wigo wa wanufaika wa mikopo hii’’ alisema Choka.

Aidha Choka anazitaja baadhi ya changamoto ni pamoja na waombaji wengi kusahau kupiga mihuri fomu, uwekaji wa saini ya mwombaji pamoja na mdhamini pamoja na kuacha kudhibiti cheti cha kuzaliwa katika mamlaka za serikali ikiwemo Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufulisi (RITA), na hivyo kufanya maombi yao kutofanyiwa kazi wakati wa zoezi la upangaji wa mikopo.

Kwa mujibu wa Choka anasema kutokana na kutambua ukubwa wa tatizo hilo, pamoja na kuendesha kampeni ya elimu kwa umma kuhusu utaratibu wa kujaza fomu za maombi ya mikopo ya elimu ya juu nchini, HESLB pia imefungua Ofisi za Kanda katika Mikoa 6 nchini ikiwemo Arusha, Mbeya, Dodoma, Mwanza, Mtwara pamoja na Zanzibar.

‘’Tumefungua ofisi kwa malengo mahsusi ya kusaidia waombaji wa mikopo hii ambao idadi yao imekuwa ikiongezeka siku hadi siku, kujaza fomu zao kwa usahihi pamoja na kuwasaidia pale wanapopata changamoto mbalimbali wakati wa kuwasilisha kudhibitisha nyaraka zao katika mamlaka mbalimbali za Serikali’’.

Akifafanua zaidi, Choka anasema HESLB pamoja na kutoa mwongozo kwa waombaji wa mikopo hiyo, katika mwaka huu wa masomo 2020/2021 HESLB pia imetoa mwongozo kwa watoa huduma za mtandao (internet) unaoanisha hatua mbalimbali muhimu zinazopaswa kuzingatiwa na watoa huduma za mtandao kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaotuma maombi ya mikopo ya elimu ya juu.

Kwa upande wake, Afisa Mikopo wa HESLB Jonathan Nkwabi aliwataka wanafunzi wanaotuma maombi ya mikopo kwa mwaka 2020/2021 kujihadhari na kundi la matapeli ambao mara kadhaa wamekuwa wakiwadanganya kuwa ni mawakala waliotumwa na Ofisi hiyo huku wakidai kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wakati wa kutuma maombi yao.

‘’Uzoefu unaonyesha kuwa katika kipindi kunaibuka wimbi la matapeli wanaoanzisha makundi ya mtandaoni ikiwemo whatsapp na kuanza kuwadai kuchangisha pesa ili kuwasaidia kujaza fomu, ukweli ni kuwa HESLB haina wakala yoyote hivyo watu hao ni matapeli, tunawashauri kusoma mwongozo wetu na iwapo kutatokea changamoto zozote pigeni simu zetu zilizotolewa katika mwongozo wa maombi’’ alisema Nkwabi.

Nkwabi anasema Serikali imetoa kipaumbele cha mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wote hususani wanaotoka katika kaya maskini na kusisitiza kuwa hakuna upendeleo unaotumika wakati wa upangaji mikopo hiyo na badala yake wanafunzi wahitaji wanatakiwa kujaza fomu kwa usahihi na kuambatanisha nyaraka zote muhimu ikiwemo vyeti vya vifo iwapo mwombaji amepoteza mzazi/wazazi.

Akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo, Grace Selestine ambaye ni mhitimu wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Udizungwa iliyopo Mkoani Iringa ameipongeza Serikali kupitia HESLB kwa kutoa mikopo ya elimu ya juu nchini kwani imekuwa faraja kubwa kwa wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini.

Anasema utaratibu wa utoaji mikopo ni mzuri kwa kuwa unaongeza fursa na wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu kwa usawa pasipo na ubaguzi, kwani silaha ya kujikwamua na umaskini wa fikra na kipato katika ngazi ya kaya ni pamoja na uhakika wa elimu bora.

‘’Tunaoipongeza HESLB kwa kuweka utaratibu wa mafunzo elekezi kuhusu namna ya kujaza fomu za maombi ya mikopo tunaomba utaratibu huu uwe endelevu ili uweze kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu hususani kwa wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini’’ alisema Grace.

Naye Erick Bukuru, mhitimu wa Kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Ilboru Mkoani Arusha alisema mafunzo ya mwongozo wa uombaji mikopo yamewasaidia kupata ufafanuzi kuhusu vigezo na sifa zinazotumika katika upangaji wa kiwango cha mikopo baina ya mwombaji mmoja na mwingine kwani awali suala hilo lilikuwa likiwachanganya wanafunzi wengi.

Bukuru aliipongeza HESLB kwa kutoa mwongozo wa uombaji mikopo katika kila mwaka wa masomo, kwani umewawezesha waombaji wengi kufahamu kipaumbele kinachopangwa na Serikali katika uhitaji wa mikopo ya elimu ya juu na utofauti uliopo baina ya mwombaji mmoja na mwingine na kutokana na sifa na vigezo vilivyoanishwa.

Aidha Jeremiah Deus mhitimu wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Umbwe iliyopo Mkoani Kilimanjaro alisema mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na HESLB tangu mwaka 2005 imekuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi yaliyofikiwa na Tanzania ikiwemo kufikia nchi ya kipato cha kati kabla ya muda wa malengo yaliyowekwa katika dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025.

‘’Elimu ndio mhimili wa maendeleo ya nchi, kupitia mikopo ya elimu inayotolewa na HESLB imesaidia kuzalisha wataalamu wa kada mbalimbali za kiuchumi, na kuwa chachu ya kufikia nchi ya kipato cha kati, nashauri kila mwaka Serikali iendelee kuongeza bajeti ili Wanafunzi wengi hususani wanaotoka katika familia za kaya maskini waweze kunufaika’’ alisema Jeremiah.

Programu ya mafunzo ya elimu kwa umma kupitia kampeni ya WeweNdoFuture iliyoanza kutolewa na HESLB hivi karibuni kuhusu taratibu za uombaji mikopo wa wanafunzi wa elimu ya juu nchini, ni mojawapo ya mikakati inayotumika katika kuhakikisha kuwa wanafunzi waombaji wanajaza fomu zao kwa usahihi ili kuepuka makosa yanayoweza kuwakosesha sifa za kupata mikopo ya elimu ya juu.

Kupitia utaratibu huo, HESLB imefanikiwa kufanya mikutano na kutembelea wadau wake mbalimbali ikiwemo wanafunzi, watoa huduma za mtandao (internet) pamoja na watendaji wa mamlaka za mitaa ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sifa na vigezo vinavyotumika katika upangaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

MWISHO.



Share:

Waziri Mkuu Atoa Wiki Moja Kwa Wizara Ya Elimu

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa muda wa wiki moja kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kukutana na Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini ili kubaini vyuo ambavyo vimeshindwa kuwasilisha michango ya wanafunzi katika Mfuko wa Taifa Bima ya Afya (NHIF) licha ya wanafunzi kulipa fedha hizo.

“Katibu Mkuu Wizara ya Elimu kashughulikie jambo hili tujue mifumo wanayotumia, pia nataka kujua ni wanafunzi wangapi ambao wamelipa na hawajapewa vitambulisho na kwa nini na nani amesababisha haya na hatua alizochukuliwa. Taarifa hiyo nataka niipate tarehe 16 mwezi huu, wiki moja inakutosha.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumapili, Agosti 9, 2020) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza kwa mwaka 2019/2020 wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania(TAHLISO) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi hao yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa TAHLISO, Bw. Peter Niboye ambaye alisema kwamba kumekuwepo na ucheleweshaji wa vitambulisho vya bima ya afya unaotokana na baadhi ya vyuo kuchelewa kufikisha fedha NHIF.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziagiza Menejimenti zote za vyuo vikuu nchini ziendelee kushirikiana kwa karibu na Serikali za Wanafunzi kwenye vyuo vyao ili waweze kushughulikia changamoto za wanafunzi kwa wakati.

Akizungumzia kuhusu wabunifu pamoja na wanafunzi bora, Waziri Mkuu amesema “Naiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia isimamie utambuzi wa masuala mbalimbali ya kitaaluma iwe ni kwenye teknolojia, afya na hawa wabunifu watambuliwe na waendelezwe. Tuwe na benki ya wabunifu waliobuni kazi ambazo zinaweza kusaidia jamii.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa taarifa ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia inaeleza kuwa tangu kufunguliwa kwa vyuo nchini tarehe 01 Juni, 2020 wanafunzi wote walioripoti wapo salama na wanaendelea vema na masomo yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAHLISO, Bw. Niboye  amesema wanajivunia kufanya kazi kwa karibu na Bodi ya Mikopo na Mfuko wa Bima ya Afya na imechangia kutokuwepo kwa migomo ya wanafunzi.

Akitoa tamko la jumuia hiyo katika kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu, amesema TAHLISO inamuunga mkono mlezi wao na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika uchaguzi huo na watahakikisha  anashinda kwa kishindo.

Mwenyekiti huyo amesema TAHLISO imefanya uamuzi huo baada ya kuridhishwa na utendajikazi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama ya elimu, umeme, maji, miundombinu na afya.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Share:

MWANAFUNZI WA SEKONDARI AANDAA MAONESHO YA WATU WA TANZANIA ILI KUKUZA UTALII, SERIKALI YAMPONGEZA


MWANAFUNZI wa sekondari Rania Nasser (17) ameandaa maonesho ya picha maarufu kama –WATU WA TANZANIA yatakayofanyika ukumbi wa Alliance Francie jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 7 hadi Agosti 12 mwaka huu.

Maonesho hayo yamedhaminiwa na Ubalozi wa Ufaransa kwa siku tano lengo ikiwa ni kusaidia kukuza utalii nchini kutokana na picha hizo kubeba maudhui yanayoonesha shughuli mbalimbali za kiuchumi pamoja na maisha halisi ya mtanzania yaliyojaa simulizi na historia za Taifa letu

Akizindua maonesho hayo rasmi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dk.Damas Ndumbaro kwa niaba ya Serikali ya Tanzania aliahidi kuendelea kuimarisha mahusiano ya Kidemokrasia na kiuchumi kati yake na Serikali ya Ufaransa ikiwa ni pamoja na kutumia mahusiano hayo katika kuitangaza Sekta ya utalii iliyopo nchini ili sekta hiyo iweze kutangazika zaidi katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Amesema “Tanzania na Ufaransa tunamahusiano mazuri kwa muda mrefu hali ambayo kwa kiasi kikubwa inatunufaisha nchi zote kwenye nyanja mbalimbali hivyo ni wajibu wetu kama nchi kuyatunza mahusiano haya ili yaendelee kutunufaisha”.

Baada ya kuzindua Maonesho hayo Dk.Ndumbaro alipongeza mwanafunzi Rania Nasser kwa jinsi alivyojitoa muda wake na kupiga picha nzuri zinazoonesha uhalisia na jinsi watanzania tunavyoishi kwa upendo Amani na kuamua kuzitoa bure picha zote kwa Bodi ya Utalii Tanzania ili zitumike kukuza utalii nchni.


“Hongera Rania kwa niaba ya watanzania wote ninakushukuru” amesema Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje,Dk. Damas Ndumbaro.

Kwa upande wa Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier, kwa nafasi yake pamoja na mambo mengine ameahidi kuendelea kuzitangaza fursa za utalii zilizopo Tanzania ili sekta hizo ziendeleee kuiamrika na hatimaye kukuza uchumi wa Taifa.

“Sisi Ufaransa tutaendelea kushirikiana na Tanzania ili kila ubunifu unaolenga kuimarisha utalii uweze kuleta maendeleo nchini.” amesema Balozi wa Ufaransa,Frederic Clavier.

Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania TTB Bi Devotha Mdachi akiahidi kuziweka picha hizo katika vivutio vya utalii nchini na kubanisha kuwa sanaa hii ya picha ambayo imepewa jina la Watu wa TANZANIA wataiendeleza kwa kuwa itasaidia mataifa mengi ulimwenguni kufahamu uhalisia wa maisha ya watanzania vyema na kukuza Utalii.
Naibu Waziri wa Mambo ya nje Dkt Damas Ndumbaro akiwa na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier, pamoja na Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania TTB Bi Devotha Mdachi wakishirikiana na Mwanafunzi wa sekondari umri wa miaka 17 Rania Nasser kukata utepe ikiwa ni ishara ya kufungua maonesho ya picha maarufu kama –WATU WA TANZANIA yaliyoandaliwa na mwanafunzi huyo. Meonesho hayo ya Picha Maarufu kama watu wa Tanzania yatakayofanyika kwa udhamini wa Ubalozi wa ufaransa katika ukumbi wa Alliance Francie kwa siku tano mfululizo kuanzi tareh 7 hadi 12.
Mwanafunzi wa sekondari umri wa miaka 17 Rania Nasser akimuonesha baadhi ya picha Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier
Mwanafunzi wa sekondari umri wa miaka 17 Rania Nasser akiongea mbele ya wakati wa kuzindua onesho lake la picha alilolipa jina la –WATU WA TANZANIA linalofanyika katika ukumbi wa Alliance Francie kwa siku tano mfululizo kuanzi tareh 7 hadi 12.
Naibu Waziri wa Mambo ya nje Dkt Damas Ndumbaro akizungumza kwenye uzinduzi wa maonesho ya picha yaliyopewa jina la –WATU WA TANZANIA yaliyoandaliwa na mwanafunzi Rania Nasser yatakayofanyika katika ukumbi wa Alliance Francie kwa siku tano mfululizo kuanzi tareh 7 hadi 12.
Naibu Waziri wa Mambo ya nje Dkt Damas Ndumbaro akipokea moja kati ya picha zilizopo kwenye maonesho ya picha yaliyopewa jina la –WATU WA TANZANIA yaliyoandaliwa na mwanafunzi Rania Nasser yatakayofanyika kwa udhamini wa Ubalozi wa ufaransa katika ukumbi wa Alliance Francie kwa siku tano mfululizo kuanzi tareh 7 hadi 12. Watatu kulia ni Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier, na Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania TTB Bi Devotha Mdachi.
Naibu Waziri wa Mambo ya nje Dkt Damas Ndumbaro akipokea moja kati ya picha zilizopo kwenye maonesho ya picha yaliyopewa jina la –WATU WA TANZANIA yaliyoandaliwa na mwanafunzi Rania Nasser.
Share:

WAFANYABIASHARA WADOGO MWANZA WANUFAIKA NA MIKOPO NBC

Mfanya biashara wa jijini Mwanza Grace Meshaki maarufu kama Mama Kweka (katikati) akitoa ushuhuda mbele ya Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (Kulia) akieleza namna Benki ya NBC ilivyompatia mkopo mpaka sasa anamtaji wa Zaidi ya milioni 250 kutoka milioni 17 katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kutoa mikopo kwa wafanya biashara wadogo na kati iliyofanyika Gold Crest jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Meneja wa Tawi la NBC Mwanza, Rodgers Masolwa.

Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya taifa ya NBC hapa nchini Theobard Sabi akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa benki ya NBC Mkoa wa Mwanza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi kutoa mikopo nafuu kwa wafanya biashara wadogo na wakati jijini Mwanza
**
MFANYABIASHARA wa jijini Mwanza, Grace Kweka, ambaye amenufaika kupitia Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) amewataka watanzania kutoogopa kwenda kukopa benki kwa sababu taasisi hizo zimeanzishwa kwa ajili ya wananchi kukuza uchumi wao.

Akizungumza jijini hapa jana katika hafla maluum iliyoandaliwa na NBC na kukutanisha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kutoka mikoa ya kanda ya ziwa ambao ni wanufaika wa benki hiyo, Kweka alisema alianza na mkopo wa Sh milioni 17 mwaka 2005 sasa amefikia kiwango cha Sh milioni 300.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara hasa wanawake wamekuwa wakiogopa kukopa katika taasisi za kifedha hivyo kujikuta wanashindwa kukuza mitaji yao wakati ipo benki maalum iliyolenga kuwainua wafanyabiashara wa ngazi zote.

“NBC ni benki yetu wafanyabiashara tuitumie vizuri ili tunufaike nayo riba zake ni rafiki, mimi nilianza nikiwa mjasiriamali lakini sasa ni mfanyabiashara wa kati, kikubwa ambacho nawasihi wafanyabiashara wenzangu ni uaminifu na kufanya biashara kwa kujituma ili kuweza kurejesha mkopo kwa wakati,”alisema na kuongeza.

“NBC ni benki inayosikiliza wateja wake, binafsi nimenufaika sana kupitia benki hii, hata kipindi cha corona niliwafuata nikawaeleza kwamba sasa sijaagiza mzigo kutoka nje tukazungumza wakanipunguzia riba kitendo hiki kinaonyesha kweli wamedhamiria kutuinua wafanyabiashara,”alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema lengo la benki hiyo ni kuhakikisha sekta binafsi inaendelea kupata sapoti ya kifedha kama mikopo na huduma za kibenki ili kuongeza uwezo wao wa kiuchumi na kukuza shughuli zao za uzalishaji hivyo kuwezesha uchumi wa nchi kuwa wa ushindani na kulifanya taifa kufikia uchumi wa kati.

Mkurugenzi wa Kitengo cha biashara kwa wateja wadogo na wakati kutoka NBC, Elvis Ndunguru, alisema lengo lakukutana na wafanyabiashara hao ni kuzungumza nao kuhusu bidhaa za kibenki ambazo benki hiyo inazitoa ili kuwawezesha wajasiriamali kukuza shughuli zao za kiuchumi.

“Leo tutawaeleza wafanyabiashara kuhusu bidhaa za mikopo tunazozitoa ambazo zimeondolewa dhamana kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara na makampuni makubwa,” alisema.
Share:

Waziri Wa Kilimo Aanza Ziara Ya Ukaguzi Wa Msimu Wa Ununuzi Wa Pamba Simiyu Na Shinyanga

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Baada ya kumalizikia kwa Sherehe za Wakulima (NANENANE) Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga leo Tarehe 9 Agosti 2020 ameanza ziara ya kikazi katika Mikoa ya Simiyu na Shinyanga ambapo pamoja na mambo mengine atakagua msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka 2020/2021.

Ktiaka ziara hiyo Waziri Hasunga amemuagiza Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt Benson Ndiege kwa kusaidiana na Warajis wasaidizi wa Ushirika wa mikoa kuhakikisha kuwa wanatoa elimu ya kutosha kwa wanachama wa vyama vya Ushirika ili kuwa na elimu ya kutosha kuhusu usimamizi wa mali za ushirika, kadhalika umuhimu Ushrika.

Kutokana na Wakulima kulalamikia mfumo wa kuwalipa fedha wakulima wa Pamba kupitia kwenye Account za Benki, Waziri wa Kilimo amemuagiza Mrajis Msaidizi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Simiyu Ndg Ibrahim Kadudu kuzielekeza kampuni zinazonunua Pamba kuwalipa fedha taslimu wakulima wenye kiasi kidogo cha Pamba.

Agizo hilo limetokana na malalamiko ya viongozi wa vyama vya Ushirika alivyotembelea na kukagua msimu wa ununuzi wa Pamba ambavyo ni Maendeleo AMCOS na Ngolomamali AMCOS za Wilayani Itilima pamoja na Malita AMCOS kilichopo Wilayani Maswa.

Waziri Hasunga amesema kuwa Wizara yake imejipanga kufanya mazungumzo na Benki mbalimbali nchini pamoja na kampuni za simu ili kujadili uwezekano wa kupunguza bei za makato ya wakulima. “Dhamira yetu sisi kama serikali tunataka mkulima apate kiasi anachostahili kutokana na jasho lake makato makato sio sawa” Alisema

Pia, Waziri Hasunga amewataka wakulima wa Pamba nchini ambao hawajalipwa fedha zao kuwa wavumilivu wakati huu ambapo serikali inaendelea kulitafutia ufumbuzi jambo hilo ili kulitatua.

Katika Mkoa wa Simiyu wakulima wanadai Bilioni 2.9 ambapo tayari imeshawalipa wakulima kiasi cha takribani Bilioni 414.4 kati ya Bilioni 419 zilizokuwa zinadaiwa na wakulima wa Pamba kote nchini.

MWISHO


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatatu August 10





















Share:

Sunday 9 August 2020

WAZIRI MKUU MAJALIWA AVUTIWA NA MFUMO WA KUHAKIKI PEMBEJEO 'T-HAKIKI' WA TTCL

Waziri Mkuu, Mh. Kassim Majaliwa akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Waziri Kindamba kikombe cha Mshindi wa Kwanza kipengele cha watoa huduma za Mawasiliano nchini katika hafla ya ufungaji maonesho ya Nanenane kitaifa yaliyofanyika mkoani Simiyu Viwanja vya Nyakabindi. 
Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Waziri Kindamba jana kikombe cha mshindi wa tatu wa jumla Maonesho ya Nanenane kitaifa yaliyofanyika kitaifa mkoani Simiyu Viwanja vya Nyakabindi. 
Waziri Mkuu, Mh. Kassim Majaliwa akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Waziri Kindamba (katikati) alipotembelea Banda la TTCL kwenye maonesho ya Nanenane kitaifa yaliyofanyika mkoani Simiyu Viwanja vya Nyakabindi. 
Wafanyakazi wa TTCL pamoja na Mkurugenzi Mkuu wao, Bw. Waziri Waziri Kindamba wakishangilia na vikombe walivyovitwaa kwenye maonesho ya Nanenane kitaifa yaliyofanyika mkoani Simiyu Viwanja vya Nyakabindi. 

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Kassim Majaliwa amefuraishwa na mfumo maalum wa kuhakiki pembejeo za wakulima unaojulikana kama 'T-Hakiki' uliozinduliwa hivi karibuni na Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL) kuwasaidia wakulima kutambua ubora wa pembejeo kabla ya kuzitumia.

Waziri Mkuu amevutiwa na mfumo huo alipotembelea Banda la TTCL kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa aliyoyafunga rasmi jana katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoa wa Simiyu. Alisema mfumo huo ni mzuri endapo utatumika vizuri kwa wakulima na unaweza kuwasaidia kupambana na pembejeo feki.

Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Waziri Kindamba alisema mfumo huo umetokana na ubunifu wa Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL), Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Tropiki (TPRI/TAPHPA), wakilenga kumsaidia mkulima kutambua pembejeo feki, ikiwemo madawa, mbegu na mbolea wanazotumia.

Mkurugenzi Kindamba alisema ubunifu huo umeenda sambamba na malengo ya Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo. "..Uuzaji wa pembejeo bandia za kilimo una athari kubwa kiuchumi na kijamii. 

Kwa sasa huduma hii itamsaidia mkulima kufahamu matumizi sahihi ya pembejeo hizo kupitia simu ya mkononi. Alisema; "..T-Hakiki ni mfumo wa njia ya SMS ambapo mkulima atatakiwa kubofya *148*52# na kuingiza namba ya siri iliyopo kwenye vifungashio vya mbegu, mbolea au kwenye chupa za vifungashio vya mbegu, mbolea au kwenye chupa za viuatilifu ili kuthibitisha uhalisi wa pembejeo,"

Katika hatua nyingine TTCL imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha watoa huduma za Mawasiliano nchini na vile vile TTCL imechukua ushindi wa tatu wa jumla katika maonesho ya NaneNane Kitaifa mwaka huu na kukabidhiwa vikombe vya ushindi huo jana kwenye sherehe za kuhitimisha maonesho hayo.

TTCL imekabidhiwa kikombe cha mshindi wa kwanza katika kipengele cha watoa huduma za Mawasiliano nchini jana na Waziri Mkuu Majaliwa huku kile cha ushindi wa tatu wa jumla kikikabidhiwa na Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga kwenye hafla za ufugaji wa maonesho hayo.


Share:

Head of Retail Banking at KCB Bank Tanzania Limited

Job Title Head of Retail Banking Location TANZANIA Organization Name KCB Bank Tanzania Ltd Department Description To develop and implement growth of Retail business, sales and improve customer service strategies and plans to drive revenue growth for KCBT. To manage operational risk in Retail Business while ensuring staff performance and development. Brief Description To develop and implement growth […]

The post Head of Retail Banking at KCB Bank Tanzania Limited appeared first on Udahiliportal.com.

Share:

Marketing Manager at KCB Bank Tanzania Limited

Job Title Marketing Manager  Location TANZANIA  Organization Name KCB Bank Tanzania Ltd  Department Description Marketing & Corporate Affairs department is responsible for developing and implementing long-term plans/strategies in digital/traditional marketing, internal and external communications, public relations, events management, corporate social investment/responsibility through 2jiajiri initiative, products and tariff /management, pushing of the sustainability agenda for the bank. All these […]

The post Marketing Manager at KCB Bank Tanzania Limited appeared first on Udahiliportal.com.

Share:

Sales and Marketing Assistant at Pyxus Agriculture Tanzania Limited

Pyxus Agriculture Tanzania Limited Sales and Marketing Assistant Company: Pyxus International, of which Pyxus Agriculture Tanzania Limited (PAT) is a subsidiary, is a global agricultural company united behind a common purpose – to transform people’s lives so that together we can grow a better world. With 145 years’ experience delivering value-added products and services to […]

The post Sales and Marketing Assistant at Pyxus Agriculture Tanzania Limited appeared first on Udahiliportal.com.

Share:

Chief of Party, Tanzania Marine Biodiversity Project at Winrock International

Chief of Party, Tanzania Marine Biodiversity Project  PROGRAM SUMMARY: Winrock is seeking Chief of Party candidates for the anticipated USAID-funded Tanzania Marine Biodiversity project. The anticipated contract will incorporate a series of interventions that support and strengthen capacity for biodiversity conservation in a manner that i) reduces the use of illegal and unsustainable fishing; ii) […]

The post Chief of Party, Tanzania Marine Biodiversity Project at Winrock International appeared first on Udahiliportal.com.

Share:

Human Resources Manager at Tanzania Youth Alliance (TAYOA)

Human Resources Manager Position Overview: Job Title: Human Resource Officer (1 Post) Department: HR and Outreach Reporting to: Deputy CEO Working Location: Dar es salaam The human resource officer will serve as an active member of the human resource team and will be responsible for providing support for operations and outreach team (as up to 40% of fieldwork […]

The post Human Resources Manager at Tanzania Youth Alliance (TAYOA) appeared first on Udahiliportal.com.

Share:

SERIKALI YAISHUKURU SUA KWA KUSAIDIA UPIMAJI SAMPULI ZA WASHUKIWA WA COVID 19

Kaimu Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Prof. Maulid Mwatawala (Kulia) Akimkabidhi Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Wapili kutoka kulia) kapu lililojaa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa Chuoni hapo.

Na Calvin Gwabara, Morogoro

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya jamii Jinsia wazee na watoto Mhe. Umma Mwalimu Amelia huku tu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na Wataalamu wake kwa msaada Mkubwa waliotoa katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa COVID 19.

Mhe. Mwalimu ameyasema hayo alipotembelea Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwenye maonesho ya Wakulima nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika Mkoani Morogoro kabla ya kufunga rasmi maonesho hayo Kikanda.

“Nitumie nafasi hii kuushukuru Uongozi mzima wa SUA na Watafiti wake kwa msaada Mkubwa mliotoa wakati wa mapambano ya COVID 19 Kwa kusaidia kwenye upimaji wa sampuli mbalimbali za wagonjwa kwa ubora mkubwa, Hakika Tina kila sababu ya kuwashukuru kwa jitihada hizi kubwa mlizozifanya” Alisisitiza Mhe. Umma Mwalimu.

Aliongeza “Wakati tunahangaika na zoezi la upimaji wa sampuli zilizokuwa zinakuja kwenye Maabara kuu kutoka nchi nzima mlitusaidia sana kupunguza mzigo wa upimaji sampuli zile baada ya nyinyi pia kuthibitika kuwa mnaweza kufanya kazi hii katika viwango vinavyokubalika”.

Waziri huyo wa Afya ametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho na kujionea teknolojia na mbinu mbalimbali za Kilimo,Mifugo na Uvuvi kabla ya kufunga rasmi maonesho hayo ya Wakulima nanenane Kanda ya Mashariki.

Akiwa kwenye banda la SUA alijionea vifaa mbalimbali vya maabara na wataalamu ambao walishiriki kwenye zoezi hilo na Upimaji wa sampuli za washukiwa na Ugonjwa wa COVID 19 sambamba na Hospitali pekee Taifa ya Rufaa ya wanyama iliyopo  chuoni hapo.

Waziri huyo wa Afya pia amepata nafasi ya kujionea Wataalamu na wajasiliamali wa masuala ya Lishe kutoka SUA ambao wanazalisha bidhaa mbalimbali kutokana na mazao lishe na kuwataka kuanza kufungasha bidhaa zao kwaajili ya wanunuzi wadogo kwa bei nafuu ili hata watoto waweze kununua kwa hela ndogo.

Maonesho hayo ya Wakulima nanenane yamefanyika kwenye Kanda mbalimbali na yalianza tarehe 1/8/2020 na kufikia kilele tarehe 8/8/2020 lakini Serikali imeongeza siku mbili ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kujifunza na pia waonyeshaji kufanya biashara zao.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kama Mdau Mkubwa wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi kimeshiriki kwenye maonesho hayo Kitaifa Mkoani Simiyu na Kikanda kwenye Kanda ya Mashariki Mkoani Morogogoro.

Maonesho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi chagua viongozi Bora Mwaka 2020”.
Share:

LORI LA MAFUTA LALIPUKA NA KUZUA TAHARUKI KAHAMA MJINI..LAJERUHI NA KUHARIBU MALI


Muonekano wa tanki la mafuta baada ya mfuniko wake kuripuka gari likitengenezwa Kahama Mjini.

Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog Kahama
Kijana ambaye jina lake halijafahamika mara moja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25-30 amenusurika kifo kwa kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya mfuniko wa tenki la mafuta la gari lenye namba za usajili namba T 393 BEZ kulipuka katika eneo la Bijampola Mjini Kahama likifanyiwa matengenezo.

Wakizungumza na Malunde 1 Blog baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, Baraka John amesema kuwa akiwa katika eneo lake la kazi majira ya saa tatu asubuhi leo Jumapili Agosti 9,2020 wakati mafundi wa kuchomelea magari wakiwa wanalifanyia matengenezo gari hilo ghafla lililipuka na kusababisha madhara mbalimbali.

Amesema Mafundi waliokuwa wanatengeneza gari hilo hawakuchukua tahadhari ili kujiridhisha kama kuna mafuta yaliyosalia kabla ya kuanza kulichomelea hali iliyosababisha kujitokeza kwa mlipuko huo ambao umesababisha majeruhi mmoja na kuharibu mali mbalimbali katika eneo hilo ikiwemo vibanda na nyumba.

“Magari kama haya yanayobeba vimiminika vinavyolipuka ni bora yakazuiwa kufanyiwa matengenezo katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu au kwenye makazi ya watu,serikali ipige marufuku uchomeleaji wa magari haya mitaani kwani ni hatari kwa usalama,”amesema John.

Naye Joyce Paulo anayejihusisha na shughuli ya kuuza vyakula 'Mamalishe' katika eneo la Bijampola amesema kuwa tukio hilo limezua taharuki kubwa kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo kwani mlipuko huo ulikuwa ni mkubwa na baadhi ya vyuma vilikuwa vinaruka katika maeneo mbalimbali huku moshi mkubwa ukiwa unasambaa kwa kasi katika makazi ya watu.

“Tulidhani ni bomu limelipuka katika eneo letu kwani nyumba ya jirani yetu imeharibiwa sana na baadhi ya vyuma vilivyokuwa vinajitokeza baada ya kulipuka,tunaiomba serikali idhibiti uegeshaji ovyo wa magari yenye mafuta katika eneo hili,”amesema Joyce.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, Dk Lucas David amethibitisha kupokea majeruhi mmoja ambaye ametokana na ajali ya kulipuka kwa tanki la Mafuta iliyotokea leo katika eneo la Bijampola ambaye amepata majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake na anaendelea kupatiwa matibabu.

“Kwa sasa amepelekewa katika chumba cha X-ray kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi,anaonekana amepata mivunjiko katika maeneo mbalimbali ya mwili wake",amesema Dk. David.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amethibitisha kutokea kwa tukio na kwamba atatoa taarifa rasmi.
Muonekano wa tanki la mafuta baada ya mfuniko wake kuripuka gari likitengenezwa
Nyumba ikiwa imeharibika baada ya mfuko wa tanki la mafuta kuripuka gari likitengenezwa
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger