Friday 30 August 2019

Rais Magufuli Atoa wito kwa Mataifa ya Afrika kutafsiri vizuri dhana ya uhuru na kujiepusha na masalia ya fikra za kikoloni

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Mataifa ya Afrika kutafsiri vizuri dhana ya uhuru na kujiepusha na masalia ya fikra za kikoloni za kuamini kuwa watawala wa zamani wa Mataifa ya Afrika ndio wenye uwezo wa kusaidia kusimamia na kuendeleza rasilimali zilipo katika Bara la Afrika.

Rais Magufuli ametoa wito huo jana Ikulu alipohutubia Mkutano wa 6 wa Jukwaa la Uongozi Afrika unaohudhuriwa na Marais Wastaafu Benjamin William Mkapa (Tanzania), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (Tanzania), Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Hassan Mohamud (Somalia), Hery Rajaonarimampianina (Madagascar), Mabalozi, Wawakilishi wa Kimataifa na washiriki wa Jukwaa la Uongozi Afrika.

“Maana hasa ya kupigania uhuru ilikuwa ni kurejesha rasilimali na hasa maliasili zetu lakini pia kuwa na maamuzi kamili kuhusu namna ya kuzisimamia na kuzitumia kwa manufaa yetu ili kuleta ukombozi wa kiuchumi, na hii ndio maana pekee ya kulinda uhuru wa kisiasa” Rais Magufuli

Tusijidanganye watawala wetu wa zamani hawawezi kugeuka kwa usiku mmoja na kuwa wajomba zetu au wakombozi wetu kiuchumi, utegemezi huu ndio umeimarisha mizizi na misingi ya ukoloni mamboleo, ni lazima tuamke” Rais Magufuli.


Share:

TETESI ZA SOKA LEO IJUMAA AGOSTI 30,2019

Mchezaji wa kiungo cha kati wa Manchester United na timu ya taifa ya Ufaransa Paul Pogba, mwenye umri wa miaka 26, hatosaini kuongeza mkataba wake hivi sasa na anataka kujiunga na Real Madrid haraka iwezekanavyo. (Marca)

Paris St-Germain inamtaka kiungo wa kati wa Tottenham Christian Eriksen mwenye umri wa miaka 27, kama mchezaji atakayeichukua nafasi ya mchezaji wa timu ya taifa ya Brazil Neymar, anayekaribia kurudi Barcelona. (Le Parisien)

Bayer Leverkusen inataka kumsaini beki wa kati wa Tottenham na timu ya taifa ya Ubelgiji Jan Vertonghen, aliye na miaka 32, kabla ya kuwadia Jumatatu muda wa mwisho wa dirisha la uhamisho Ulaya. (Kicker)

Beki kamili wa Manchester United na timu ya taifa ya Italia Matteo Darmian, mwenye umri wa miaka 29, yupo katika majadiliano kurudi katika ligi ya Serie A na klabu ya Parma. (La Gazzetta dello Sport kupitia Football Italia)

Mchezaji wa kiungo cha kati wa Arsenal na timu ya taifa ya Misri Mohamed Elneny, aliye na miaka 27, yupo katika mazungumzo na timu ya Uturuki Besiktas kuhusu uhamisho wa msimu mzima kwa mkopo (Sky Sports)
Meneja wa Gunners Unai Emery anasema beki kamili mwenye umri wa miaka 33 Nacho Monreal, aliyehusishwa na uhamisho kwenda Real Sociedad, huenda akaondoka katika klabu hiyo kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho Ulaya. (Mirror)

Bosi wa Tottenham Mauricio Pochettino anasua sua kumuita mlinzi wa timu ya taifa ya Ivory Coast Serge Aurier kwa Derby ya London kaskazini siku ya Jumapili huko Arsenal wakati mchezaji huyo wa miaka 26 akiwa anaweza kuondoka kabla ya kufungwa dirisha la uhamisho Ulaya Jumatatu. (Evening Standard)

Manchester United ilijitoa katika mkataba wa msimu wa joto ya mshambuliaji wa Juventus Paulo Dybala, mwenye umri wa miaka 25, kutokana na matakwa ya malipo ya mchezaji huyo wa Argentina ya thamani ya £18m kwa mwaka. (Mail)

Aliyekuwa mshambuliaji wa Manchester United Romelu Lukaku, mwenye umri wa miaka 26, amepunguza uzito wa mwili baada ya kufuata muongozo wa lishe chini ya meneja Antonio Conte tangu raia huyo wa Ubelgiji kujiunga na Inter Milan. (Mail)

Mlinzi wa Barcelona Gerard Pique anatumai kuwa Harry Maguire ataweza kuisaidia klabu yake ya zamani Manchester United kushinda taji la ligi kuu ya England. (Express)
Mchezaji wa kiungo cha kati wa Aston Villa Aaron Tshibola amejiunga na timu ya Ubelgiji Waasland-Beveren kwa mkataba wa miaka mitatu. (Birmingham Mail)

Arsenal dhidi ya Tottenham inajitayarisha kuipiku Liverpool dhidi ya Everton katika mchezo mkali wa Derby katika ligi kuu ya England. (Sun)

Kipa wa Paris St-Germain Alphonse Areola, mwenye umri wa miaka 26, amekubali kujiunga na Real Madrid. (RMC Sport)

Mchezaji wa kiungo cha mbele wa Chile Alexis Sanchez, mwenye umri wa miaka 30, ametuma ujumbe kwa wachezaji wenzake wa Manchester United katika Instagram kabla ya kujiunga na Inter Milan kwa mkopo. (Manchester Evening News)
Meneja wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer yupo tayari kusubiri hadi msimu ujao w ajoto kushinikiza kiungo cha ushambilizi , huku mchezaji wa kiungo cha mbele wa Borussia Dortmund Jadon Sancho, mwenye umri wa miaka 19, akisalia kuwa mchezaji anayemlenga pakuu. (Evening Standard)

Barcelona na Paris St-Germain zimekubali malipo ya uhamisho wa mchezaji wa miaka 27 wa timu ya taifa ya Brazil Neymar, lakini majadiliano yanaendelea kuhusu makubaliano ya mkataba huo. PSG inataka mchezaji wa kiungo cha mbele wa Ufaransa Ousmane Dembele, mwenye umri wa miaka 22, kuwa sehemu ya mpangilio huo. (Mirror)

Hatahivyo, Ajenti wa Dembele anasema mchezaji huyo hatoondoka Nou Camp, hatua ambayo huenda ikachangia kupromoka kwa pendekezo la uhamisho wa Neymar kwenda Barcelona. (Daily Mail)

Mchezaji wa kiungo cha kati wa Chelsea raia wa Ufaransa Tiemoue Bakayoko, mwenye umri wa miaka 25, amekubali makubaliano ya kujiunga upya na Monaco kwa mkopo - huku kukipangiwa malipo ya £31.8m ka mkataba wa kudumu.(RMC Sport, kupitia Sun)
Mlinzi wa Arsenal Nacho Monreal, mwenye umri wa miaka 33, c huenda akarudi katika klabu alikotoka Uhispania kaba ya kufungwa dirisha la uhamisho Ulaya Jumatatu, huku Real Sociedad ikiwa na hamu kubwa ya kumsajili mchezaji huyo wa zamani wa Osasuna na Malaga. (Evening Standard)

Mshambuliaji wa Arsenal na timu ya taifa ya England Sam Greenwood, mwenye umri wa miaka 17, ametambuliwa na timu bingwa ya Italia AC Milan na Juventus kama mchezaji anayelengwa baada ya kuridhisha maajenti katika mshindano ya ubingwa wa Ulaya wa timu za wachezaji walio chini ya umri wamiaka 17 mapema msimu huu wa joto. (Sun)
Chanzo - BBC
Share:

MAREHEMU ALIYEZIKWA NA TAI,VIATU AZUA BALAA.....'ANATAKA AZIKWE UPYA'

Huenda familia moja kutoka eneo la Ikolomani, kaunti ya Kakamega nchini Kenya ikafukua maiti ya jamaa wao waliyemzika kufuatia ripoti kwamba alikuwa anawahangaisha kwa kutozingatia utaratibu wakati wa mazishi yake.

 Inasemekana marehemu Pius Shipanda Shitsukane, ambaye alihudumu kama naibu wa chifu katika mtaa wa Shiseso na aliyezikwa hizi majuzi, amekuwa akiwahangaisha jamaa zake na kutaka mwili wake ufukuliwe. 

Inaelezwa kuwa Mkewe Shipanda amekuwa akiugua tangu kuzikwa kwa mumewe na wazee wa jamii wamedai maradhi yanayomkumba yamesababishwa na gadhabu ya mumewe.

Pius Shipanda alidaiwa kuzikwa akiwa amevishwa viatu na tai kinyume na mila na desturi za jamii ambapo baadhi ya jamaa wa familia hiyo walidai wamekuwa wakikumbwa na masaibu katika nyumba yao tangu jamaa huyo azikwe.

Duru zinaarifu kwamba, marehemu alivishwa viatu na tai na kisha rungu ambayo alipenda kutembea nayo haswa wakati akihudhuria vikao vya wanaume wa kikatoliki ikatiwa katika sanduku lake kabla ya kuzikwa.

 Pindi tu baada ya mazishi yake katika boma lake kijijini Ikhumbula-Ibukhubi, mkewe alianza kuugua na kulazwa hospitalini.

 Hata hivyo, wakazi wanaamini chifu huyo ndiye chanzo cha mkewe kuugua kwa kuwa alikuwa hajafurahishwa na mazishi yake. 

 "Ni kinyume na mila za jamii ya Luhya kumzika marehemu na bidhaa kama vile tai, saa, pesa, shanga, chupi au soski," Lawrence Alusiola ambaye ni mzee wa jamii alisema.

 Alisema wale wote ambao wamekiuka tamaduni hiyo wamepokea adhabu na kulazimika kuufukua mwili ili kuondoa vifaa alivyozikwa navyo marehemu. 

 "Tumeshuhudia visa kama hivyo kwa miaka ya hapo awali. Unapata familia inakiuka desturi zetu na kusisitiza kuwazika wapendwa wao jinsi wanavyotaka kisha wanajuta baadaye wakati wanapotatizwa na marehemu," Elias Khwani mzee mwingine kutoka jamii hiyo alisema.

 Inadaiwa, marehemu Shipanda amekuwa akiwatatatiza jamaa wa familia yake haswa nyakati za usiku akitaka tai, viatu na rungu aliyozikwa navyo ziondolewe.

"Maradhia ambayo yamemkumba mkewe ghafla yanahusikana na marehemu kwa kuwa baadhi ya wanachama wa kikundi cha wanaume wa kikatoliki walikataa kusikiza ushauri wa wazee na kumzika marehemu na bidhaa zisizostahili. Ni sharti waufukue mwili au familia itazidi kuhangaika," mzee mwingine wa jamii alitoa tahadhari. 
Via Tuko
Share:

JUMUIYA YA MADAKTARI WATANZANIA WALIOSOMA CHINA (DCAT) YATOA HUDUMA YA AFYA BURE KISARAWE, PWANI


WAKAZI wa Kisarawe wamenufaika na kambi ya kwanza ya kampeni ya uchunguzi na matibabu dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza inayotolewa na madaktari bingwa wa Jumuiya ya Madaktari  Watanzania waliosoma China (DCAT).

Awali akifungua kambi hiyo wiki hii katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo amewahamasisha kujitokeza kwa wingi ili kujua hali zao.

Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe ametumia fursa hiyo kuwasilisha ombi lake kwa Mwambata wa Ubalozi wa China, anayeshughulikia masuala ya utamaduni na elimu, Gao Wei, ambaye alimwakilisha Balozi wa China, kwamba waijengee Hospitali hiyo jengo la kisasa la matibabu.

"Tunashukuru wataalamu wetu wameona katika kampeni hii, Kisarawe iwe ya kwanza kisha watakwenda maeneo mengine ya nchi, Rais Dk. John Magufuli anatujengea jengo la kisasa la OPD (wagonjwa wa nje) hapa Kisarawe.

"Nitumie fursa hii kuuomba ubalozi wa China, ikizingatiwa pia kwamba Wilaya hii ina historia hasa katika ujenzi wa reli ya Tazara, Wachina walikaa hapa na wakazi wa Kisarawe walishiriki kuijenga.

"Ukiacha mahusiano yale ya ujenzi wa reli ya Tazara, leo hii wigo umepanuka mpaka kwenye elimu, afya na sekta nyinginezo," amesema.

Ameongeza "Nawasihi wakazi wa Kisarawe kuitumia fursa hii ya uchunguzi vizuri, hata yule mwenye mgonjwa aliyepo nyumbani amlete, hapa Wapo madaktari wabobezi watachunguzwa na watagundua tatizo linalomsumbua.

Kuhusu ombi hilo la Waziri Jafo, Mwambata huyo wa Ubalozi amesema amelipokea na kuridhia kwamba wapo tayari kujenga jengo la kisasa kwa Hospitali hiyo.

Awali, amesema ushirikiano wa China na Tanzania ni wa miaka mingi na imekuwa ikitoa ufadhili kwa watanzania kwenda kusoma nchini humo elimu mbalimbali .

Amesema wanafurahi kuona kwamba wataalamu waliopata ufadhili wa masomo China sasa wanasaidia nchi katika mambo mbalimbali.

Mwenyekiti wa DCAT, Dk. Liggyle Vumilia amesema katika siku hizo tatu wanatarajia kuwachunguza afya watu kati ya 600 hadi 1000 ambapo watachunguzwa magonjwa ya saratani, moyo, kisukari na mengineyo.

"Kampeni yetu ina kauli mbiu 'Jali Afya yako, Fanya uchunguzi mapema', tunalenga wananchi wa kawaida kabisa, kuwahamasisha wajenge tabia ya kuchunguza afya zao, itawasaidia kujua mapema kama wanakabiliwa na matatizo au la!

"Wale tutakaowakuta na matatizo madogo tutawatibu kupitia mfuko tulioandaa, tunawapa na elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa haya," amesema.

Amesema wanatarajia pia kwenda hivi karibuni mkoani Tanga ambako watafanya kampeni hiyo na baadae nchi nzima.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Jokate Mwegelo amesema utoaji wa huduma bora za afya ni miongoni kwa vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli na kwamba msisitizo zaidi ni katika utoaji wa huduma za kinga.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo  akiwashukuru wanajumuiya ya Watanzania walioishi nchini China (DCAT) kwa kujitolea kuwapa huduma ya afya bure kwa wakazi wa wila ya Kisarawe, Pwani. 
Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo (kushoto) akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo  kutoa hotuba yake.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amesema utoaji wa huduma bora za afya ni miongoni kwa vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli na kwamba msisitizo zaidi ni katika utoaji wa huduma za kinga.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Watanzania waliosoma nchini China Dkt. Liggyle Vumilia akielezea kwa ufasaha huduma hiyo ya afya bure.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Utamaduni wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, Bwana Gao Wei akisoma hotuba yake.
Mtaalam wa Tiba ya jadi ya Kichina Dkt Paul Mhame akitoa ushauri kwa jamii.


Wananchi wa wilaya ya Kisarawe, Pwani na vitongoji vyake wakipima uzito na urefu ili kuweza kupatiwa matibabu ya bure kutoka kwa Jumuiya ya Madaktari  Bingwa Watanzania waliosoma nchini China (DCAT) waliopiga kambi kwa muda wa siku tatu. Jumuiya hiyo imejipanga kuendelea na zoezi la kutoa huduma katika mkoa wa Tanga na maeneo mengine ya Tanzania. Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Dokta Bingwa wa Magonjwa ya Saratani, Dkt Heri Tungaraza akitoa maelekezo kwa wagonjwa.

Wagonjwa wakipimwa presha.
Wagonjwa wakipimwa ugonjwa wa Kisukari.
Mtatibu wa zoezi la upimaji wa Afya Bure, Bi. Linas akigawa maji kwa wagonjwa.

Wananchi wakisubiri huduma.
Wazee wakipatiwa ushauri kabla ya kuingia kuwaona Madaktari bingwa waliojitolea kufanya zoezi la kutoa huduma ya Afya Bure kwa wananchi wa Jumuiya ya Madaktari  Bingwa Watanzania waliosoma nchini China (DCAT).
Kila mmoja alijitahidi kumleta mgonjwa wake ili apatiwe huduma ya afya bure.
Wananchi wa wilaya ya Kisarawe, Pwani na vitongoji vyake wakipimwa presha ili kuweza kupatiwa matibabu ya bure kutoka kwa Jumuiya ya Madaktari  Bingwa Watanzania waliosoma nchini China (DCAT) waliopiga kambi kwa muda wa siku tatu.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Watanzania waliosoma nchini China Dkt. Liggyle Vumilia (aliyevaa tai) akitoa ushari kwa wagonjwa walifika kupatiwa huduma ya Afya bure iliyofannyika wilaya ya Kisarawe, Pwani.

Wananchi wa wilaya ya Kisarawe wakiwa wamepanga foleni kuoatiwa huduma ya Afya Bure.
Watoa huduma wakiendelea kutoa ushari kwa wagonjwa waliofika kupatiwa huduma ya Afya bure.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Watanzania waliosoma nchini China Dkt. Liggyle Vumilia akigawa maji kwa wagonjwa aliojitokeza kupatiwa huduma ya Afya Bure.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger