Thursday, 2 July 2026

TEMESA YAONESHA MAGEUZI MAKUBWA,WAZIRI KAPINGA ATOA PONGEZI





Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, leo Julai 1, ametembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza bandani hapo, Mhe. Kapinga ameipongeza TEMESA kwa kasi ya mabadiliko inayoenda nayo katika matengenezo ya magari na mabadiliko ya mifumo ya utoaji huduma.



“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnazozifanya katika matengenezo ya magari na pia matumizi yenu ya mifumo katika utoaji huduma. Hongareni sana.” Amesema Mhe. Kapinga.

Waziri wa Viwanda na Biashara alipotembelea banda la TEMESA alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na TEMESA, ikiwemo huduma za vivuko, umeme na elektroniki, matengenezo ya magari na mitambo, ushauri wa kihandisi pamoja na mifumo ya kidijitali na ubunifu unaolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.



Maonesho hayo ya biashara yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Hii ni Kubwa Kuliko” na yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya ijumaa tarehe 3 Juni, 2026



TEMESA inaendelea kuwakaribisha wananchi, wadau na wageni wote kutembelea banda lake ili kujifunza kuhusu huduma zake, kupata ushauri wa kitaalamu na kufahamu mchango wa Wakala katika maendeleo ya sekta ya ufundi na umeme nchini.





Share:

Wednesday, 1 July 2026

BIMA YA AFYA ZA WEZESHWA KWA WANAGENZI


-IKUJUMUISHWA NA POSHO YA USAFIRI

Na Mwandishi OWM-KAM, Mara

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kuboresha mazingira ya mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi kwa kuwapatia wanagenzi 5,746 bima ya afya na posho ya usafiri ya shilingi 100,000 kwa mwezi kwa kipindi cha mafunzo ya vitendo sehemu za kazi. Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanagenzi kuendelea na mafunzo katika mazingira salama na kuongeza ufanisi wa programu ya taifa ya kukuza ujuzi.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Wilbard Munisi, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi katika Chuo cha Ufundi Stadi St. Anthony, Musoma mkoani Mara, Juni 30, 2026.

Alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya vijana ili kujenga nguvukazi yenye ujuzi, maarifa na ushindani unaohitajika katika soko la ajira la ndani na kimataifa.

Dkt. Munisi alisema maboresho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, inayolenga kuongeza idadi ya Watanzania wenye ujuzi stahiki wa kujiajiri na kuajiriwa huku ikipunguza pengo la ujuzi katika soko la ajira.

Aidha, Naibu Waziri alisisitiza kuwa Serikali inatarajia kuona wahitimu wanaotumia ujuzi walioupata kuibua suluhisho bunifu kwa changamoto za uzalishaji na utoaji huduma nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bi. Alana Nchimbi, alisema kuwa mfumo wa uanagenzi umeendelea kuwa njia bora ya kuziba pengo la ujuzi kwa kuunganisha mafunzo ya darasani na uzoefu wa moja kwa moja mahali pa kazi.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi St. Anthony Fr. Dkt. Constatine Changwe alisema chuo hicho kimepokea wanagenzi 186 wanaofadhiliwa kikamilifu na Serikali katika awamu ya nane ya programu hiyo, huku chuo kikiongeza nafasi kwa wanagenzi wengine 25 kwa ufadhili wa Kanisa Katoliki kutokana na mahitaji makubwa ya vijana waliotuma maombi. Alibainisha kuwa mafunzo yanatolewa katika fani sita zenye mahitaji makubwa katika soko la ajira.

Kwa niaba ya wanagenzi, Neema Abeli aliishukuru Serikali kwa kugharamia ada za mafunzo kwa asilimia 100, kutoa bima ya afya na kuweka utaratibu wa posho ya usafiri kwa kipindi cha mafunzo ya vitendo. Alisema hatua hizo zimeondoa changamoto za kifedha na kuwapa vijana nafasi ya kuzingatia masomo na kujenga ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu, huku akiomba Serikali iendelee kupanua programu hiyo ili vijana wengi zaidi wanufaike.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO JULAI 1,2026



Magazeti













Share:

Tuesday, 30 June 2026

NAIBU WAZIRI MAHUNDI AHIMIZA WANAWAKE KUTUMIA MIKOPO KUINUA UCHUMI



Na Jackline Minja, Mtwara

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Maryprisca Mahundi, amezindua rasmi Mfuko wa Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika Jimbo la Mtwara Mjini (UWEZO Program) na kusema Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za uwezeshaji wa wanawake.

Akizungumza katika hafla hiyo Juni 30, 2026, Naibu Waziri Mahundi amesema Serikali inaamini kuwa maendeleo ya Taifa hayawezi kupatikana bila kuyawezeaha makundi maalum wakiwemo wanawake na vijana.

Amesema ushiriki wa makundi maalum katika shughuli za kiuchumi ni hatua ya kujivunia na kuongeza kuwa mafanikio yatapatikana kwa makundi hayo kupatiwa mafunzo stahiki.

"Serikali inaamini kuwa maendeleo ya Taifa hayawezi kupatikana bila wananchi wake kuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na hii ndiyo sababu kuwndelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake na vijana kupata fursa za kiuchumi kupitia sera na programu mbalimbali," alisema Naibu Waziri Mahundi.

Aidha, ameeleza kuvutiwa kwake na Programu ya UWEZO kwa kuanza kutoa mikopo na kuwajengea wanawake uwezo kupitia mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu za biashara na uundaji wa vikundi, akieleza kuwa msingi huo utasaidia kuhakikisha mikopo inazalisha matokeo chanya na kuongeza maendeleo ya wanawake pamoja na familia zao.

Awali akitoa maelezo kuhusu Programu ya UWEZO, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesema wazo la kuanzisha mfuko huo limetokana na ahadi aliyoitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Amesema kupitia mfuko huo wenye mtaji wa shilingi milioni 150, wanawake zaidi ya 5,000 walitambuliwa kutoka kata zote 18 za jimbo hilo, wanawake 300 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na wanawake 81 wamekabidhiwa mikopo katika awamu ya kwanza.

"Mikopo hiii haina riba kutokana na ushirikiano kati ya Joel Nanauka Foundation na Benki ya Ushirika (Coop Bank), sababu lengo la programu hii si kutoa fedha pekee bali kujenga wanawake wajasiriamali wenye uwezo wa kujitegemea, kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mtwara Mjini na Taifa kwa ujumla". alisema

Nao baadhi ya wanufaika wa Mkopo huo wameipongeza Serikali na kumpongeza Waziri Nanauka kwa maono na kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni zake ambapo kwa sasa wataweza kujiendesha kiuchumi na kupunguza makali ya ugumu wa maisha na kuingizia taifa mapato.






Share:

WALIMU DODOMA WAELEKEA KOREA KUSINI KWA ZIARA YA KIMASOMO


Na Mwandishi Wetu

UJUMBE wa walimu na viongozi wa elimu kutoka Mkoa wa Dodoma wapatao 40 umeondoka kwenda Korea Kusini kujifunza, namna ya kufundisha, kusimamia shule na kutumia teknolojia katika elimu.

Ujumbe huo unatarajiwa kushiriki programu ya mafunzo na ziara ya kielimu ya siku nne kamili nchini Korea Kusini, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa walimu walioonesha utendaji bora na kufanikisha ongezeko la ufaulu wa wanafunzi katika Mkoa wa Dodoma.

Mratibu wa safari hiyo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Molle alisema walimu hao waliondoka juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Juni 27, 2026, kuelekea Seoul, Korea Kusini, kupitia Doha, Qatar.

Alisema ziara hiyo ya kimasomo itafanyika kwa siku nne, ambapo walimu na viongozi wa elimu wanatarajiwa kushiriki katika mafunzo, kubadilishana uzoefu na kujifunza kuhusu matumizi ya teknolojia, ubunifu, uongozi wa shule na mbinu za kisasa za ufundishaji.

Alisema katika ziara hiyo ya siku nne, ujumbe unatarajiwa kujifunza namna Korea Kusini inavyotumia teknolojia, ubunifu, nidhamu na usimamizi bora katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.

Alisema walimu wanatarajiwa kupata uzoefu kuhusu matumizi ya vifaa na mifumo ya kidijitali darasani, maandalizi ya masomo, ushirikishwaji wa wanafunzi na ufuatiliaji wa maendeleo yao ya kitaaluma.

Alisema kabla ya safari hiyo, walimu na viongozi wa elimu waliomo katika ujumbe walipatiwa mafunzo maalumu ya maandalizi ambapo walielezwa kuhusu mazingira ya Korea Kusini, utamaduni wa nchi hiyo, nidhamu, utunzaji wa muda na wajibu wao kama wawakilishi wa Mkoa wa Dodoma na Tanzania.

Alisema mbali na kushiriki katika udhamini, taasisi ya Global Education Link imeratibu maandalizi mbalimbali ya ujumbe na kutoa mwongozo muhimu kwa washiriki kabla ya kuondoka nchini.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mollel aliwataka washiriki kutumia safari hiyo kama fursa ya kujifunza na kurejea na maarifa yatakayoweza kuleta mabadiliko yanayoonekana katika shule za Mkoa wa Dodoma.

Alisisitiza kuwa lengo la safari si kufika na kutembelea Korea Kusini pekee, bali kupata uzoefu wa kimataifa kuhusu matumizi ya teknolojia katika elimu, mbinu za kisasa za ufundishaji, usimamizi wa shule na mikakati ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Katika mafunzo hayo, washiriki walipatiwa maelezo kuhusu jiografia, uchumi, maendeleo ya teknolojia, hali ya hewa, utamaduni, mila na mfumo wa elimu wa Korea Kusini.

Pia walielekezwa kujiandaa kisaikolojia na kimwili, kuheshimu muda, kufuata ratiba rasmi na kuzingatia sheria na utamaduni wa nchi watakayotembelea.

Mollel alisema safari hiyo ni matokeo ya jitihada za Mkoa wa Dodoma za kutambua, kuthamini na kuwapa motisha walimu walioonesha utendaji mzuri katika kutekeleza majukumu yao na kuwasaidia wanafunzi kupata matokeo bora.

Alisema mpango huo ulitokana na Mkutano wa Wadau wa Elimu wa Mkoa wa Dodoma uliofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mollel alisema mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa Serikali, walimu, maofisa elimu, viongozi wa shule, taasisi za umma, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo ya elimu.

Molle alisema katika mkutano huo, walimu, wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya kitaaluma zilitambuliwa na kupongezwa kutokana na mchango wao katika kuinua kiwango cha elimu mkoani Dodoma.

Alisema mpango wa kuwapeleka walimu Korea Kusini ulianzishwa kama sehemu ya kutoa motisha kwa walimu walioonesha kujituma, nidhamu, uwajibikaji na mafanikio katika kufundisha na kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri.

Alisema safari hiyo imefanikishwa kupitia ushirikiano wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma na wadau mbalimbali wa elimu, wakiwamo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Benki ya NMB na Global Education Link.

Alisema ushirikiano huo unaonesha namna Serikali na wadau wanavyoweza kuunganisha nguvu katika kutambua utendaji bora na kutoa fursa za maendeleo ya kitaaluma kwa walimu.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger