Tuesday, 27 January 2026

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE JANUARI 27,2026

 Magazeti

       

Share:

Sunday, 25 January 2026

WAKULIMA TABORA WALALAMIKIA UPUNGUFU WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA LICHA YA AHADI ZA COP30



Na Hadija Omary Mazezele 

Katika Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliofanyika nchini Brazil, Tanzania ilisimama kidete si tu kama mshiriki, bali pia kama kiongozi wa msimamo wa Afrika.

Ikiwa Mwenyekiti wa Kikundi cha Majadiliano cha Afrika (AGN), Tanzania ilisisitiza umuhimu wa huduma za hali ya hewa, sera jumuishi na mifumo ya chakula endelevu kama nguzo kuu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima.

Msimamo wa Tanzania, kama mwakilishi wa bara la Afrika, ni kwamba huduma za hali ya hewa ni muhimu kwa kuwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi kuhusu kilimo, hasa katika mazingira ya sasa yanayobadilika kwa kasi.

Kauli ya Tanzania, iliyotolewa na Dkt. Richard Mayungi Mshauri wa Rais kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi na mwenyekiti wa AGN, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, wakati wa COP30, ilisisitiza umuhimu wa huduma za hali ya hewa kuwafikia wakulima wadogo ambao ndio walio hatarini zaidi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wakulima wadogo nchini wakiwemo wa mkoa wa Tabora hupoteza mapato, usalama wa chakula na ustawi wa kijamii kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa taarifa sahihi za hali ya hewa. 

Tafiti zinaonyesha kupungua kwa mavuno kwa zaidi ya asilimia 30–50, kushuka kwa kipato cha kaya kwa asilimia 60–80, na kuongezeka kwa hatari ya umasikini na uhamaji wa kijamii.

Ripoti ya Taasisi ya utafiti na uchambuzi wa sera za kiuchumi na kijamii nchini (ESRF) kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima wadogo ya mwaka 2013 ilibainisha kuwa, wakulima wadogo hupoteza sehemu kubwa ya mavuno kutokana na ukame na mvua zisizotabirika, hali inayosababisha upungufu wa chakula na kipato vijijini.

Ripoti ya Benki ya Duinia (WB) kuhusu athari za kicuhumi zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ya mwaka 2024, ilionyesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha watu milioni 13 kuhamishwa ndani ya nchi kutokana na ukame na mafuriko barani Afrika.

Kulingana na Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2023, ilionyesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yameongeza migogoro kati ya wakulima na wafugaji, na kuathiri haki za kijamii na kiuchumi, huku shirika la IIrish Aid katika ripoti yake ya mwaka 2018 ilibainisha kuwa kupungua kwa mavuno husababisha lishe duni, hususan kwa watoto na wanawake.

Kutamatika kwa mkutano wa COP30 kumeendelea kuibua maswali na mijadala kwa wakulima wa mkoa wa Tabora na nchini kwa jumla, kuhusu huduma za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), hususan taarifa zinazohusu mienendo ya mvua na ukame.

Kwa mujibu wa Kidumila Mtandi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chang’ombe katika wilaya ya Tabora mkoa wa Tabora, mavuno yake yameshuka kutoka gunia 80 hadi gunia tano.

Hii ni taswira ya athari binafsi, huku tafiti za kitaifa zikionyesha upungufu wa mavuno kwa asilimia 30–50 na kukiosekana kwa taarifa sahihi za hali ya ewa kumechangia hali hiyo.

Anasema huwa anasikia taarifa za hali ya hewa zikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) kupitia redio, lakini mara anashindwa kuelewa kutokana na lugha inayotumika jambo linalomfanya mtandi na wakulima wrngine wa Tabora kulima kwa mazoea hivyo kupata hasara kwenye mavuno.

“Wapo wananchi hapa kijijini hawana redio wala simu janja, hivyo kushindwa kufuatilia taarifa hizo. Hali hii imekuwa kikwazo kwa wakulima wengi kufikia malengo yao ya kilimo kutokana kukosa taarifa sahihi za hali ya hew ana kukabiliana na  mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Ameongeza kuwa, miaka sita iliyopita alikuwa na uwezo wa kupata hadi gunia 80 za mahindi na gunia 100 za mpunga pamoja na mazao mengine, lakini kwa sasa hupata gunia tano za mahindi na gunia nane za mpunga. 

Kwa upande wake, Asha Masoud ambaye pia ni mkulima wa Kijiji cha Chang'ombe ameiomba TMA iwe na mpango madhubuti wa kuwasilisha taarifa za hali ya hewa kwa wakulima kwa lugha rahisi na inayoeleweka.

“Kufanya hivyo kutasaidia wakulima kupata taarifa sahihi kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata na vijiji kuhusu mwelekeo wa mvua,” amesema.

Naye Eliud John, mkulima wa mazao ya chakula, amesisitiza na kuomba maafisa ugani wapate nafasi ya kuwatembelea wakulima na kutoa ufafanuzi badala ya kukaa ofisini. 
Amesema kufanya hivyo kutawasaidia wakulima kuamua aina ya mazao ya kulima na kuepuka hasara.

Hata hivyo, mjadala wa COP30 umefungua ukurasa mpya kwa Tanzania katika kuimarisha juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan katika sekta ya kilimo inayogusa maisha ya wananchi wengi vijijini.

Kupitia msimamo wa Tanzania kama kinara wa masuala ya Afrika, imebainika wazi kuwa huduma za hali ya hewa zilizo sahihi, za wakati na zinazoeleweka kwa wakulima ni nguzo muhimu za kujenga kilimo chenye ustahimilivu.

Changamoto zinazowakumba wakulima wa mkoa wa Tabora, ikiwemo kukosekana kwa taarifa za uhakika za hali ya hewa na mifumo hafifu ya mawasiliano, zinaakisi uhalisia unaohitaji hatua za haraka na za kimkakati.

COP30 imeweka msingi wa uwajibikaji kwa serikali, taasisi za hali ya hewa na wadau wa maendeleo kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinawafikia wakulima wote kwa lugha rahisi na njia zinazowafikia.

Hatua hizi si tu zitapunguza hasara ya mazao, bali pia zitachangia kuongeza uzalishaji, usalama wa chakula na ustawi wa wananchi. 

Msimamo wa Tanzania katika COP30 unagusa moja kwa moja wakulima wadogo kama wa Tabora, ambao wanakabiliana na changamoto hizi kila siku.
Kwa wakulima kama Kidumila, taarifa sahihi za hali ya hewa zinaweza kubadilisha maamuzi shambani na kuleta mavuno bora.
Share:

RAIS SAMIA AMEIMARISHA UCHUMI GEITA KUPITIA UJENZI WA BARABARA YA KASAMWA-GAMASHI - PROF. SHEMDOE

Na OWM - TAMISEMI, Geita

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha Shilingi 1,035,047,200/= za ujenzi wa dharura wa barabara ya Kasamwa- Gamashi yenye urefu wa kilomita 18, iliyoimarisha shughuli za kiuchumi kupitia Sekta ya Usafiri na Usafirishaji kati ya Wilaya ya Nyang’hwale na Makao Makuu ya Mkoa wa Geita.

Prof. Shemdoe amesema barabara hiyo ina umuhimu kiuchumi kwa wananchi wa Nyang’hwale na Geita ambao wanategemea shughuli za kilimo na  ufugaji, hivyo uzalishaji unaofanyika Nyang’hwale ulikuwa hauwezi kufika makao makuu ya mkoa kutokana na changamoto iliyokuwepo ya ubovu wa miundombinu ya barabara ya  Kasamwa- Gamashi.

“Ujenzi wa barabara hii ni muhimu sana kiuchumi, hivyo tunapaswa kumshukuru Mhe. Rais kwa kuidhinisha fedha zilizowezesha barabara kujengwa ili kuendeleza shughuli za wananchi kiuchumi,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amempongeza Mshauri Elekezi kampuni ya Norplan Tanzania Ltd kwa usimamizi mzuri wa mradi huo  akiwa ni mwakilishi wa mshitiri, na kuongeza kuwa Washauri Elekezi wote wangetekeleza wajibu wao kama alivyotekeleza Norplan Tanzania Limited, kusingekuwa na malalamiko wala changamoto ya miradi kusuasua.

Aidha, Prof. Shemdoe amempongeza Mkandarasi wa mradi huo kampuni ya Madata Investment Ltd kwa utekelezaji mzuri wa mradi huo uliofikia asilimia 82 kwa kutumia fedha yake mwenyewe, na kuanisha kwamba wakandarasi wa aina ya Madata Investment wakipatikana kutakuwa hakuna miradi mingi inayosuasua.  

“Nakupongeza sana mkandarasi kwa kazi nzuri uliyoifanya katika mradi huu, na ninakuhakikishia kuwa fedha ya kukulipa ipo, wewe lete maombi ulipwe lakini nakuomba uzingatie Februari 27, 2026 unapaswa kukabidhi mradi huu,” ameeleza Prof. Shemdoe.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita, Mhandisi Bahati Subeya amesema mradi huo wa ujenzi wa dharura katika barabara ya Kasamwa- Gamashi ulianza rasmi Agosti 25, 2025 na unatarajiwa kukamilika Februari 27, 2026.

Mhandisi Subeya amefafanua kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutaboresha sekta ya usafiri na usafirishaji pamoja na shughuli za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii zikiwemo za afya na elimu.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Grace Kingalame amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa barabara ya Kasamwa- Gamashi ambayo itaondoa changamoto ya mawasiliano kati ya wilaya yake na makao makuu ya mkoa, na kuongeza kuwa wananchi wa Nyang’wale na Geita wanafurahishwa na dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya kuwaletea maendeleo kupitia ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Mradi huo wa Barabara ya Kasamwa- Gamashi, ni miongoni mwa miradi tisa (9) yenye thamani ya Shilingi 4,015,469,549/= inayotekelezwa na TARURA mkoa wa Geita kupitia Mradi wa CERC (Contingency Emergency Response Component) - DMDP II unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ambao unatokana na barabara  zilizoathiriwa na mvua za Elnino mwaka 2023.

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI JANUARI 25,2026

Magazeti



 
Share:

Saturday, 24 January 2026

MV NEW MWANZA: MKOMBOZI WA UCHUMI NA BIASHARA KANDA YA ZIWA

Kukamilika na kuzinduliwa kwa meli ya kisasa ya MV New Mwanza, kumeleta matumaini mapya ya kiuchumi kwa mamilioni ya wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafirishaji wa bidhaa na abiria kati ya majiji ya Mwanza na Bukoba.

Meli hiyo, ambayo sasa ndiyo mfalme wa maji katika Ukanda wa Maziwa Makuu, si chombo cha usafiri tu, bali ni kiunganishi kikuu cha biashara kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Uganda na Kenya.

Uwezo wa Kipekee

Kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu cha "ukame" wa vyombo vikubwa, MV New Mwanza inakuja na uwezo mkubwa wa kubeba abiria na mizigo. Ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 inapunguza msongamano na gharama kubwa za usafiri wa barabara.

Kwenye suala la mizigo ambapo ndipo penye moyo wa biashara, meli hii ina uwezo wa kubeba tani 400 za bidhaa kwa wakati mmoja, jambo ambalo litaleta mapinduzi ya bei za bidhaa sokoni. Aidha ina uwezo wa kubeba magari madogo 20 na makubwa (malori) 3 .

Manufaa ya Kiuchumi

Kukosekana kwa meli ya uhakika kwa miaka mingi kuliathiri vibaya mabadilishano ya bidhaa. Sasa, kwa safari ya saa 6 hadi 7 pekee wakulima wa kahawa, ndizi, na mazao mengine ya chakula kutoka mkoani Kagera sasa wanakuwa na soko la uhakika jijini Mwanza na mikoa mingine. Bidhaa hizi zitafika zikiwa bado mbichi na kwa gharama nafuu ya usafirishaji.Wakati huo huo wafanyabiashara wa Mwanza sasa wanaweza kusafirisha bidhaa za viwandani, vifaa vya ujenzi, na samaki kwenda Bukoba na maeneo ya pembezoni mwa ziwa kwa urahisi zaidi.

Ongezeko la uwezo wa kubeba mizigo mikubwa kutaondoa gharama za ziada za usafirishaji zinazosababishwa na malori, hivyo kupelekea bei za bidhaa kupungua kwa mlaji wa mwisho.

Usalama na Utimamu wa Biashara 

Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO, Eric Hamisi, amebainisha kuwa meli hiyo imetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa inayohakikisha usalama wa watu na mali zao. Uwepo wa madaraja mbalimbali, ikiwemo daraja la biashara na VIP, unatoa fursa kwa wafanyabiashara kufanya safari zao kwa faraja huku wakiratibu mipango yao ya kibiashara.

Kwa wakazi wa kandoni mwa Ziwa Victoria, MV New Mwanza si tu fahari ya kitaifa, bali ni injini ya kukuza kipato, kutoa ajira, na kufungua fursa za kitalii ambazo zilikuwa zimefifia. Huu ni mwanzo wa zama mpya ambapo biashara itashamiri na uchumi wa kaya utaimarika kupitia maji ya ziwa hilo kuu.

Share:

BILIONI 67 ZIMETUMIKA KUJENGA BARABARA NA MASOKO MWANZA - PROF. SHEMDOE



Na OWM – TAMISEMI, Mwanza

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali kupitia Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) imetumia kiasi cha bilioni 67 kujenga Barabara na Masoko ili kuwahudumia wananchi wa Mwanza.

Prof. Shemdoe ametoa taarifa hiyo leo jijini Mwanza wakati alipopewa nafasi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ya kuzungumza na wananchi wa mwanza waliojitokeza kumsikiliza Waziri Mkuu mara baada ya Waziri Mkuu kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzindua meri ya New MV Mwanza.

Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, fedha hizo zinatumika kujenga barabara ya Nyamaghani yenye urefu wa kilomita 14 yenye thamani ya bilioni 22, barabara ya Ilemela yenye urefu wa kilomita 12 yenye thamani ya bilioni 24, Soko la Samaki Mkuyuni Nyamaghana lenye thamani ya bilioni 7 pamoja na soko la mazao mchanganyiko Ilemela lenye thamani ya bilioni 14.

Akizungumzia hatua ya ujenzi wa barabara hizo, Prof. Shemdoe amesema zimekamilika na ziko kwenye hatua ya kuweka taa za barabarani ili wananchi waweze kuzitumia nyakati za usiku huku wakiwa salama. 

“Mhe. Waziri Mkuu ikikupendeza pindi barabara zikikamilika, tutakuomba uje kuzizindua rasmi kwa ajili ya kuanza kutumiwa na wananchi wa Mwanza na watanzania wote watakao kuja jijini Mwanza kwa shughuli mbalimbali,” Prof. Shemdoe amewasilisha ombi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemhakikishia Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa, ofisi yake itaisimamia vema TARURA ili miradi yote ya Barabara, Soko la Samaki na Soko la Mazao mchanganyiko ikaamilike kwa wakati, na hatimaye wanachi waanze kunufaika na uwepo wa miradi hiyo.




Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger