Tuesday, 20 January 2026

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE JANUARI 20,2026

Magazeti



 
Share:

Monday, 19 January 2026

HUWEZI KUISHIWA PAWA UKIPANDA MLIMA LOLMALASIN


Wakati anamsifia mpenzi wake Msanii Mbosso aliimba “ Kamusi namaliza kurasa kukusifia” ,na akahitimisha kwa kusema anaishiwa pawa kwa kuwa penzi la huyo ampendaye ni mizani nzito.

Mbosso angepata fursa ya kupanda mlima Lolmalasin uliopo Ngorongoro kamwe asingeishiwa pawa, badala yake angeongeza maneno katika kamusi kuusifia mlima huu unaopatikana katika kivutio namba moja cha utalii barani Afrika.

Angeusifia mlima huu kwa kuwa ni mlima mrefu zaidi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na mlima wa tatu kwa urefu Tanzania, ukiwa na kimo cha mita 3,700 kutoka juu ya usawa wa bahari.

Angepanda mlima huu asingeweza kuishiwa pawa kutokana na mandhari yaliyopambwa na maua, miti, ndege, wanyama huku akishuhudia Kreta ya Olmoti kwa mbali ikitiririsha maji yake kwenda Kreta ya Ngorongoro kupitia mto Munge.

Mlima huu si mzuri tu kupanda laah hasha, unakusaidia kupiga jaramba na kunyoosha misuli hasa kwa wanaojiandaa kukwea Milima mirefu kama Meru na Kilimanjaro.

Ukipanda mlima huu si tu unajenga afya na kupanua mawanda ya upeo wa macho na akili yako, bali utahisi upo peponi na kusahau changamoto zote ikiwemo Stress za ada za januari, vikoba, kazi na hata mapenzi.

Na kama Mbosso alisema kwamba yeye ni Mjusi anaparamia ukuta wa plasta basi hata watalii kutoka maeneo mbalimbali wanaweza kuupanda mlima huu bila kuuparamia na wala hawataishiwa Pawa kamwe.

Karibuni wageni kupanda mlima Lolmalsin, Ngorongoro inawahakikishia kutoishiwa pawa na badala yake pawa zitaongezeka maradufu.

Tuishie hapa kwa methali isemayo " Kinywa ni Jumba la Maneno " kesho kutoka Ngorongoro tutakuletea maneno ya kivutio kingine cha utalii kwa kuwa "Jungu kuu halikosi ukoko"

Maajabu ya Ngorongoro yanakuita,

Uzoefu usiosahaulika,

Tumerithishwa, Tuwarithishe.

Share:

SIMBA WA TERANGA WANG’ARA MOROCCO, WANYAKUA UBINGWA WA AFCON 2025


Timu ya Taifa ya Senegal, maarufu kama Lions of Teranga 'Simba wa Teranga', imeandika historia mpya baada ya kutwaa ubingwa wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika fainali kali iliyochezwa usiku wa Januari 18, 2026 nchini Morocco.

Mchezo huo uliwakutanisha wababe wawili wa soka barani Afrika, huku kila timu ikionesha kiwango cha juu, nidhamu ya kiufundi na mapambano ya hali ya juu. 

Dakika 90 za kawaida ziliisha bila mshindi kutokana na uimara wa safu za ulinzi na makipa wa pande zote mbili, hali iliyosababisha kuchezwa kwa dakika 30 za muda wa nyongeza.

Dakika ya 107, mashabiki wa Senegal walilipuka kwa furaha baada ya mshambuliaji Pape Alassane Gueye kufunga bao la ushindi, bao lililodumu hadi filimbi ya mwisho na kuipa Senegal taji lao la pili la AFCON katika historia ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Kwa mafanikio hayo, Senegal imejinyakulia zawadi ya Dola za Kimarekani Milioni 10 (sawa na takriban Shilingi Bilioni 24.7 za Kitanzania), ikiwa ni ongezeko kubwa la fedha za zawadi ikilinganishwa na AFCON 2023, hatua inayolenga kuinua ushindani na hadhi ya mashindano hayo.

Kwa upande wao, wenyeji Morocco walioshindwa katika fainali hiyo wamepokea Dola Milioni 4, kama ilivyotangazwa na Rais wa CAF Patrice Motsepe, ikiwa ni sehemu ya mpango wa CAF kuongeza motisha kwa timu zinazofika hatua za juu.

Matokeo hayo yanaifanya Morocco kupoteza fainali ya pili ya AFCON katika historia yao, baada ya mara ya kwanza kufanya hivyo mwaka 2004 walipopoteza dhidi ya Tunisia.

Senegal sasa inajiweka kwenye ramani ya mataifa makubwa ya soka Afrika, ikithibitisha uimara na ubora wake katika anga la soka la bara hilo.


Share:

WANA SANTA RC BUNJU WAPIGWA MSASA MATUMIZI SAHIHI YA MITANDAO



Wanakwaya wa Mt. Joseph, Parokia ya Mlima Karmeli Bunju, Jimbo la Bagamoyo wakiwa Zanzibar kushiriki moja ya matamasha makubwa nchini kwa mwaliko.

**
Wanakwaya wa Mt. Joseph, Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmel Bunju, jimbo la Bagamoyo wameaswa kutumia vema mitandao ya kijamii kutangaza kwaya yao na ujasiriamali ili kujiongezea kipato.

Wito huo umetolewa Januari 18,2026 Parokiani hapo na Msemaji wa kwaya hiyo Bi. Rose Ngunangwa wakati wa mafunzo kwa wanakwaya hao ambapo amesisitiza pia umuhimu wa kuwa na nidhamu na kuheshimu utu mitandaoni.

“Kama vijana wa kikatoliki na wanakwaya ninawaasa kuheshimu utu wa watu mitandaoni na kutochangia kutweza, kudhalilisha au kutusi mtu. Tumieni mitandao kunadi kazi zenu ili kuongeza kipato. Naomba msiwe watumwa wa historia hata kama hukubahatika kufanya vema kwenye masomo tumia karama ulizonazo kutengeneza kipato,” amesisitiza.

Katika miaka ya hivi karibuni, kwaya ya Mt. Joseph Bunju imejipatia umaarufu mkubwa katika uimbaji huku baadhi wakiita Tanzania 2 kutokana na uimbaji wenye sauti zilizopangiliwa.

Kwa sasa kwaya hiyo inatamba na nyimbo zake mpya kama Ishara ya Msalaba na Nia Yangu, nyimbo ambazo zinafanya vema kwenye majukwaa mbalimbali ya kidijitali.

Kwaya hiyo imeweza kushiriki matamasha makubwa ya kitaifa kama Mkatoliki Concert, Tamasha la Yesu ni Mwema na lile la Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu  wa Mhashamu Augustine Shao wa Zanzibar ambapo ilijizolea mashabiki lukuki visiwani humo.
Share:

Sunday, 18 January 2026

SAUTI ZA WANANCHI: AMANI NDIO MSINGI WA MAENDELEO NA JIBU KWA MIHEMKO YA KISIASA NCHINI

Watanzania wamehimizwa kulinda amani, umoja, na mshikamano wa taifa kwa wivu mkubwa kama msingi pekee wa kujiletea maendeleo ya kweli, huku wakionywa kuwa pasipo utulivu hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana. 

Kauli hizi zimetolewa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, akiwemo Athumani Mkongota, mkazi wa Kibaha Mjini, ambaye amesisitiza kuwa mshikamano ndio nguzo inayolishikilia taifa. 

Mwelekeo huu wa kizalendo unakuja wakati ambapo mijadala ya kijamii imeongezeka kuhusu namna ya kudai haki bila kuhatarisha usalama, huku wananchi wakitakiwa kurudi katika kujitafakari na kuona ni kwa kiasi gani maisha yanaweza kubadilika na kuwa katika taharuki kubwa pindi amani inapotoweka.

Katika kile kinachoonekana kama funzo kutokana na matukio ya hivi karibuni, Daudi Inuka, mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, ametoa mwito wa kutafuta njia mbadala na bora za kudai haki badala ya kukimbilia vurugu ambazo mara nyingi huacha majeraha kwa jamii.

Maoni haya yanaungwa mkono na Musa Mseti ambaye amebainisha kuwa amani ndiyo kila kitu kwa sababu shughuli zote za kiuchumi na kijamii zinafanyika kwa ufanisi pale tu ambapo utulivu umetawala. Wananchi hao wamebainisha kuwa kushuhudia taharuki inayoweza kutokea kupitia vurugu kumejenga ufahamu mpya kuwa amani si jambo la kuchukulia mzaha, bali ni fursa muhimu inayopaswa kulindwa dhidi ya yeyote anayejaribu kuivuruga.

Mjadala huu umepata mwangwi mpana pia katika mitandao ya kijamii ambapo Watanzania wengi wameanza kuhoji nia ya mataifa ya nje, kama Marekani, wakiamini kuwa mataifa hayo mara nyingi huchochea vurugu nje ya ardhi yao huku yakilinda usalama wa ndani. 

Baadhi ya wachangiaji wamebainisha kuwa Tanzania ina akili nyingi na busara kuliko mataifa mengine mengi ya Afrika, na kwamba mabadiliko ya kweli yanapatikana kupitia maridhiano na njia za amani badala ya kufuata mikumbo ya vurugu. Hoja imekuwa ni kwamba, ingawa kuna madai ya haki au changamoto za kimaisha , njia ya kuivuruga nchi haijawahi kuwa suluhu ya kudumu, bali ni mtego unaoweza kumrudisha mwananchi nyuma kimaendeleo.

Hisia za wananchi zimejikita katika ukweli kuwa kufuata mikumbo ya kisiasa bila kutafakari kunaweza kuleta madhara makubwa kwa mtu mmoja mmoja. Watu wengi sasa wamechagua amani kama njia sahihi, wakiamini kuwa haki inaweza kupatikana bila kumwaga damu au kuharibu mali. Mwito uliotolewa kwa Watanzania wote ni kuendelea kuwa na uelewa mpana wa kijiopolitiki na kutambua kuwa kazi na utu ndizo silaha za kusonga mbele. Katika kipindi hiki cha mabadiliko, busara imeshinda mihemko, huku wananchi wakiazimia kusimama kidete kukataa ajenda zozote zinazolenga kuingiza taifa kwenye machafuko, wakitambua kuwa ukombozi wa kweli unajengwa juu ya misingi ya utulivu na siyo mabaki ya nchi iliyovurugika.

Share:

WAZIRI AWESO ATAKA KAZI ZIFANYIKE USIKU NA MCHANA KUKAMILISHA MRADI WA MAJI MKINGA

 

Na Oscar Assenga, MKINGA

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Maji Mkinga – Horohoro kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana kuukamilisha kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Aweso aliyasema hayo leo wakati wa halfa ya Mapokezi ya Vitendea kazi (Mabomba) vitakavyotumika katika utekelezaji wa Mradi wa Maji Mkinga-Horohoro ambao unagharimu kiasi cha Bilioni 35.



Halfa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tanga Uwasa,Dkt Ally Fungo,Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Geofrey Hilly,Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo pamoja na watumishi wa Tanga Uwasa,Ruwasa,Viongozi wa CCM na wananchi wa eneo la Manza.

Alisema kutokana na kwamba mradi huo ni muhimu kwa wananchi ambao wanakabiliwa na changamoto ya maji hivyo wahakikishe unakamalika kwa wakati na ujenzi wake uwe tofauti uende na maji katika maeneo yanayolazwa mabomba nao wapate maji.



“Tunajua tuna miradi mingi sana lakini nikuombe Katibu Mkuu utoe fedha ili mradi huo ukamilike kwa wakati ili wana Mkinga waweze kupata huduma ya maji safi na salama”Alisema



“Kama mnakumbuka tulimleta Rais Dkt Samia Suluhu aliweke kuweka jiwe la msingi kukamilika kwake tumuombe Rais aje kuzindua mradi huu wa Mkinga sababu ndio muasisi na ndio aliyweka jiwe la msingi”Alisema

Waziri Aweso aliwataka wafanye kazi hiyo kwa uadilifu na uaminifu ili kuhakikisha hiyo kazi inakamilika na wana Mkinga waweze kupata maji safi na salama



Hata hivyo Waziri huyo alimuahidi Mbunge wa Jimbo la Mkinga Twaha Mwakiojakwamba watafanya kazi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kutokana na kwamba wapo baadhi ya watumishi wanaishi Tanga kutokana na changamoto ya maji wakikamilisha mradi huo watapata maendeleo makubwa.


Alisema maendeleo hayo yatapatikana kwa wana Mkinga na wawekezaji mbalimbali watakwenda kuwekeza hiyo kazi wameibeba na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika.


Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Gilbert Kailima alisema wanaishukuru Serikali kutokana na kwamba mradi huo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya ya Mkinga na utaondoa adha kubwa ya Maji.


Alisema wanamshukuru Rais kwa kutoa kipaumbele sana katika mradi huo na ndio maana alikuja kuweka jiwe la Msingi katika mradi huo na kuhaidi watajitahidi kusimamia mradi huo kwa karibu kwa kushirikiana na Tanga Uwasa ili utekelezwe kwa wakati ili uanze kufanya kazi kama Rais anavyotamani iwe pamoja nawe.

Aidha alisema katika wilaya hiyo wana miradi mengine mikubwa iliyopo wilayani humo ikiwemo wa Gombero, Mapatano, Muhinduro na Bamba Mwarongo yote ni mikubwa ambayo Serikali chini ya Wizara ya Maji inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wake na ipo katika hatua mbalimbali.


“Kutokana na kwamba umefika leo tunaomba nayo hii miradi waone namna gani inaweza kuisha kwa wakati kama ambavyo wananchi wa Mkinga wanatamani iwe tunaimani sana na utendaji wako na katibu mkuu wa wizara ya Maji “Alisema.


Alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa mkaandarasi ambaye atatoa huduma ya usambazaji wa maji katika mradi huo na kuhakikisha vifaa vyake havihujumiwi badala yake wawe walinzi ili kufanya kazi yake vizuri.

Naye kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mkinga (CCM) Twaha Mwakioja alisema kwamba katika taifiti iliyofanywa changamoto kubnwa inawakabili zaidi ya wananchi asilimia 80 wamelalamikia hali ya upatikanaji wa maji.



Alisema kwamba mradi huo kabla ya kuanza kutekelezwa wastani wa upatikanaji wa maji katika wilaya ya Mkinga ni asilimia 60 mpaka 69 hivyo wana imani mradi huo utakapokamilika upatinaji wa maji utafika zaidi ya asilimia 88 mradi huo ni mkombozi mkubwa kwao.

Aidha alisema kwamba mradi huo utakakamilika zaidi ya vijiji 37 vinakwenda kupata maji safi na salama ya uhakika na Serikali imeweka fedha nyingi ili kuhakikisha unakamilika ili wananchi waweze kuondokana na adha ya maji.

“Mhe Waziri tunaomba mradi huu kwa maana umesuasua kwa mude mrefu kama unavyotambua upo nyuma zaidi ya miaka miwili na ifikapo julai mradi uwe umekamilika hivyo tunashukuru na wananchi wana mategemeo makubwa sana “Alisema

Mwisho

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger