Sunday, 29 June 2025
Saturday, 28 June 2025
FRED ROMANUS AJITOSA KUWANIA UBUNGE JIMBO JIPYA LA ITWANGI
Kijana na mwanazuoni Fred Romanus kutoka Kijiji cha Mendo, Kata ya Ilola, ametangaza nia ya kugombea Ubunge katika Jimbo jipya la Itwangi, mkoani Shinyanga.
Fred Romanus amesema amekuwa na ndoto ya muda mrefu ya kuwatumikia wananchi kupitia nafasi ya Ubunge, akilenga kuwaletea maendeleo jumuishi na endelevu kwa makundi yote katika jamii.
“Ndoto yangu ni kuona kila mwananchi ananufaika na matunda ya uongozi bora. Naamini kupitia nafasi hii ya Ubunge, nitaweza kusukuma gurudumu la maendeleo kwa vitendo,” amesema Fred Romanus.
Kwa sasa, amesema sera na mikakati yake ya maendeleo itawasilishwa kwa wananchi katika siku zijazo wakati wa kampeni rasmi endapo chama kitampa ridhaa ya kugombea Ubunge.
Friday, 27 June 2025
SERIKALI YAJENGA VITUO 472 VYA POLISI HADI NGAZI YA KATA
Na Emmanuel Mbatilo
SERIKALI imeendelea kuliimarisha jeshi la polisi kwa kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza miundombinu, ambapo vituo vya polisi 472 vimejengwa hadi ngazi ya kata na shehia.
Ameyasema hayo leo Juni 27, 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akitoa hotuba ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 Jijini Dodoma.
"Tumeboresha makazi ya askari na kununua vitendea kazi, ikiwemo magari na pikipiki, kwa ajili ya kazi za utawala na operesheni. Aidha, askari wapya 16,009 wameajiriwa, huku Maofisa,Wakaguzi na Askari 10,363 wakipandishwa vyeo". Amesema Rais Samia
Aidha ametoa pongezi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwa kuzuia uhalifu.
"Kasi ya kuwabaini na kuwakamata wahalifu, na kuwafikisha Mahakamani imeongezeka. Jambo ambalo bado hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani. Lazima nazo tuendelee kuzitafutia muarobaini wake.
WATUMISHI WA MAGEREZA MANYARA WAPATIWA MAJIKO YA GESI

📌Mifumo ya uzalishaji wa bayogesi 126 mbioni kuanza
📌REA, Jeshi la Magereza kununua mashine 61 za mkaa mbadala
📌REA kuwajengea uwezo magereza uendelezaji miradi ya nishati safi
Serikali imewapatia watumishi wa Jeshi la Magereza mitungi ya gesi na majiko ya gesi ya kupikia ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi na wananchi iliyolenga kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Hayo yamebaibishwa leo Juni 26, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu wakati wa uzinduzi wa kugawa majiko ya gesi kwa watumishi wa magereza iliyofanyika gereza la Babati mkoani Manyara.
Amesema kuwa, katika mkoa wa Manyara tayari Serikali imegawa mitungi ya gesi na majiko ya gesi yapatayo 330 kwa watumishi wa jeshi la magereza na katika gereza la Babati jumla ya majiko na mitungi 150 wamegawiwa watumishi hao wa magereza.
Amesema kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia makubaliano na Jeshi la Magereza ya kuwawezesha magereza kuhama kutoka katika matumizi ya nishati isiyo salama kwenda katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika magereza yote nchini.
"Kuanzia mwanzoni wa mwezi januari 2025 jeshi la magereza walishaingia kwenye matumizi ya nishati safi na salama na tayari wameachana na nishati isiyo salama na chafu kwa afya na mbaya kwa mazingira yetu, " Ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amewataka watumishi wa jeshi la magereza kuibeba ajenda ya Mhe. Rais Samia ya kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia hapa nchini.
Katika hatua nyingine Mha. Saidy ameeleza kuwa, mifumo ya uzalishaji wa bayogesi ipatayo 126 tayari ipo mbioni kuanza kwa kushirikiana na jeshi la magereza ambayo itawezesha ununuzi wa mashine za kutengeneza mkaa mbadala 61, vile vile kuwajengea uwezo watumishi wa jeshi la magereza ya kuendeleza miradi hiyo ya nishati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza mkoa wa Manyara ACP Solomon Mwambingu amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia watumishi wa magereza majiko ya gesi na mitungi ya gesi na kusisitiza kuwa wataendelea kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia katika jamii yote inayowazunguka.

















































