
Thursday, 29 May 2025
NDOA YANGU ILIKARIBIA KUVUNJIKA, HIVI NDIVYO NILIVYOIOKOA!

Wednesday, 28 May 2025
DIWANI AWAWASHIA MOTO WANAOMKASHIFU NA KUMTUKANA RAIS SAMIA,
Na Woinde Shizza ,moshi
Diwani wa kata ya Boma Mbuzi Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Juma Rahibu, amewajia juu baadhi ya Watanzania wanaomkashifu na kumtukana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akisema ni ishara ya kuporomoka kwa maadili katika jamii na kudhalilisha heshima ya taifa.
Akizungumza kwa hisia kali katika sherehe za uzinduzi wa kikundi cha mtetezi wa mama , Rahibu alisema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya watu wakitumia majukwaa ya mitandao ya kijamii na mikusanyiko ya watu kumvunjia heshima kiongozi mkuu wa nchi ambaye, kwa mujibu wake, amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa bidii na mafanikio makubwa.
“Huu si ustaarabu Rais Samia anajitahidi kutuletea maendeleo kama barabara, afya, elimu halafu mtu anajitokeza tu na kuanza kumtukana? Tunataka vyombo vya dola viwajibike,” alisema Rahibu.
Diwani huyo alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuenzi maadili ya taifa, hasa heshima kwa viongozi walioko madarakani, huku akionya kuwa uhuru wa kutoa maoni haupaswi kuwa kisingizio cha matusi, kashfa na propaganda zisizojengwa kwenye hoja za msingi.
Katika hatua nyingine, Rahibu alielekeza lawama kwa baadhi ya raia kutoka mataifa jirani ya Kenya na Uganda kwa kile alichokieleza kuwa ni tabia ya kudhalilisha na kumsema vibaya Rais Samia kwenye mitandao ya kijamii.
“Sasa imefika hatua hata baadhi ya Wakenya na Waganda wanathubutu kumtukana Rais wetu? Hii ni dharau ya hali ya juu ,Tanzania si uwanja wa mazoezi wa siasa za kejeli,” alisema kwa msisitizo.
Alisema Tanzania imekuwa nchi ya mfano wa heshima na ustaarabu kwa viongozi wa mataifa jirani, hivyo si haki kuona baadhi ya watu kutoka nje ya nchi wakitumia vibaya uhuru wa mitandao kwa maneno ya matusi dhidi ya kiongozi wa Tanzania.
“Tunawaheshimu viongozi wao, hatujawahi kusikia Watanzania wakimtukana Rais wa Kenya au wa Uganda ,Na wao wajifunze kutufanyia heshima hiyo hiyo,” aliongeza.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wakazi wa Moshi wameonyesha kuguswa na kauli hiyo, wakisema kuwa ni kweli kuwa maadili yanaporomoka na watu kutumia mitandao ya kijamii vibaya.
Esther Kilave, mkazi wa Pasua, alisema:
“Mitandao inatumika kama sehemu ya matusi sasa huu si utamaduni wetu ,Rais Samia anastahili kuheshimiwa kwa kazi anayoifanya.”
John Mlay, fundi umeme mjini Moshi, alisema:
“Tunaona mabadiliko mengi nchini Watu wanapaswa kutoa hoja za maana, si kejeli na matusi na niseme Wanapotukana Rais, wanatudhalilisha sisi sote. Acheni siasa za matusi.”
Rais Samia ameendelea kupokea pongezi kutoka kwa wananchi wa makundi mbalimbali nchini, kufuatia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na msimamo wake wa kudumisha amani, umoja wa kitaifa na usawa wa kijinsia.
JUMUIYA YA WANADIPLOMASIA YAKARIBISHWA NCHINI
WAZIRI DKT. GWAJIMA AANISHA VIPAUMBELE VITANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII 2025/2026


Na WMJJWM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii. Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameainisha vipaumbele vya Wizara vikubwa vitano katika utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mhe. Dkt. Gwajima ameainisha hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka husika wa Fedha leo Mei 27, 2025 Bungeni jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa Wizara kupitia Idara na Taasisi zilizo chini yake zitatekeleza vipaumbele hivyo ambavyo ni kukuza ari ya Jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ngazi ya msingi, kuratibu na kuimarisha utoaji wa huduma za ustawi wa maendeleo ya jamii, kutambua pamoja na kuratibu maendeleo ya ustawi kwa Makundi Maalum.
Mhe. Dkt. Gwajima ameongeza kuwa vipaumbele vingine ni pamoja kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika Taasisi na Vyuo vya Ustawi na Maendeleo ya Jamii na kuimarisha mazingira ya ushiriki na mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa.
Amesema Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo katika Ngazi ya Msingi (2022/23 – 2025/26) ambao unalenga kuwawezesha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo na kuchochea mageuzi ya kifikra, mtazamo na kiutendaji kwa timu ya wataalam ngazi ya msingi ili kuboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika kuhakikisha Watoto wanalindwa na ukatili Waziri Dkt. Gwajima amesema Wizara imeratibu na kusimamia Kampeni ya Taifa ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni (Child Online Protection - COP) katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara. Kampeni ilikuwa na lengo la kuelimisha Wazazi au Walezi na Watoto wenyewe kuhusu Usalama wa Mtoto anapokuwa anatumia mitandao.
Aidha Mhe. Dkt. Gwajima amefafanua kuwa Wafanyabiashara ndogondogo 601 (Me 274; Ke 327) wamekopeshwa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1,101,650,000 na zoezi hilo linaendelea. Vilevile maombi 2,092 yanaendelea kuchakatwa yenye thamani ya Shilingi Bilioni 3,590,477,000.
"Wizara kwa kushirikiana na OR - TAMISEMI imeendelea kuratibu na kufuatilia maendeleo ya ya Ujenzi wa Ofisi za wafanyabiashara ndogondogo katika ngazi ya mikoa ambapo hadi kufikia Aprili 2025 mikoa 17 kati ya mikoa 26 imekamilisha ujenzi wa Ofisi hizo" ameeleza Mhe. Dkt Gwajima.
Akichangia hoja, Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Dkt. Thea Ntara amesizitiza Serikali kuchukua hatua na kusimamia maadili nchini, kutokana na kuwepo kwa matukio mengi ya uvunjifu wa maadili.
Naye Mbunge wa kuteuliwa Dkt. Shukurani Manya ameshauri kuongezeka kwa juhudi za kuelimisha Jamii kuhusu elimu ya malezi ili kuepusha kutelekezwa kwa watoto ili waweze kupata malezi ya baba na mama.





