Sunday, 4 May 2025

MBUNGE IDDI KASSIM AWAONESHA NJIA – AWAKABIDHI BAISKELI WENYEVITI WA VIJIJI 92 KUFUATILIA MIRADI

Na Mwandishi Wetu, Malunde 1 blog

Mbunge wa Jimbo la Msalala mkoani Shinyanga, Mhe. Iddi Kassim, ametoa baiskeli 92 kwa wenyeviti wa vijiji vyote vya Halmashauri ya Msalala kwa lengo la kuwawezesha kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Baiskeli hizo zenye thamani ya shilingi milioni 23 zimekabidhiwa rasmi katika hafla iliyofanyika leo katika kata ya Bugarama zikiwa ni kwa ajili ya wenyeviti wa vijiji katika jimbo zima la Msalala kwa lengo la kurahisisha usafiri wa viongozi hao kuzungukia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Zoezi hilo la ugawaji wa baiskeli limefanyika leo Mei 4,2025 likiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Mohammed Ali Kawaida, ambaye pia amehutubia wananchi na kuwahimiza kuhakikisha miradi ya maendeleo inalindwa na kutunzwa kwa manufaa ya wote.

“Ni jambo la kuigwa. Mbunge amewawezesha viongozi wa msingi kufanikisha usimamizi wa maendeleo ya wananchi. Nawasihi wenyeviti kutumia baiskeli hizi kwa shughuli zilizokusudiwa,” amesema Kawaida na kupongeza hatua hiyo aliyoitaja kuwa ya kipekee katika ziara yake ya siku 10 nchini.

"Naomba mkazitunze hizi baiskeli ili ziwasaidie katika kuzungukia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na ilani ya Chama cha mapinduzi (CCM)", amesema.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge Iddi amesema kuwa wenyeviti wa vitongoji na vijiji wanafanya kazi kubwa bila kuwa na mshahara na kwamba jimbo la msalala lina utajiri mkubwa unaoweza kuwapa posho wenyeviti hao kupitia mapato ya ndani.

Ameeleza kuwa kila baiskeli imegharimu shilingi 250,000, na kwamba hatua hiyo inalenga kuwawezesha wenyeviti kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuhakikisha changamoto zinagunduliwa mapema na kutafutiwa ufumbuzi.

Aidha Mheshimiwa Iddi amewataka viongozi kuwatumikia wananchi kwa kusimamia kwa uaminifu miradi ya maendeleo ili kuinua Uchumi wa taifa na Uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Katika vijiji vyetu, kuna miradi mingi inayoendelea na inahitaji usimamizi wa karibu. Nitashirikiana na viongozi hawa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo ya kweli,” ameongeza.

Wakizungumza mara baada ya kupokea baiskeli hizo baadhi ya wenyeviti wamemshukuru Mbunge Iddi na kwamba baiskeli hizo zitawasaidia katika majukumu yao.

Katika tukio hilo, wanachama tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka Wilaya ya Kahama, wakiongozwa na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Tendaji ya wilaya hiyo, Samson Thomas, wamehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupokelewa rasmi na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Thomas amesema wameamua kuunga mkono juhudi za serikali ya CCM katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, na kuahidi kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na uongozi, huku akiahidi kuwa mtiifu kwa chama hicho.



Share:

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUEPUKA SIASA NA UCHOCHEZI


Na Mwandishi Wetu

VIONGOZI wa dini katika madhebu mbalimbali nchini wameshauriwa wasiwe wanasiasa na wala kuwa sehemu ya kuwa wachochezi kwani wao ni sehemu ya kimbilio pale ambapo nchi itakuwa na changamoto huku wakikumbushwa wajibu wa kuliombea Taifa la Tanzania hasa katika mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu.

Pia kwa waumini wa dini mbalimbali ambao ni wanasiasa wamekumbushwa na kuhimizwa kufanya kampeni za kistaarabu lakini wawe wenye kujishusha na kusamehe kwani kila mmoja wetu analojukumu la kuhakikisha amani,umoja na mshikamano unaendelea kuwepo.

Hayo yameelezwa na Wachungaji kutoka Tanzania na Kenya wa Kanisa la Wadventista Wasabato walipokuwa wakihitimisha Wiki ya Uamsho iliyokuwa na maombi mbalimbali yakiwemo ya kuliombea amani ,umoja na mshikamano Taifa la Tanzania ambalo Oktoba mwaka huu linatatajia kufanya uchaguzi Mkuu .

Wiki ya Uamsho imeandaliwa na Kwaya ya Gethsemane Group Kinondoni (GGK) kutokea Kanisa la Wadventista Wasabato Kinondoni Jijini Dar es Salaam ambapo katika maombi hayo pia wamewaalika wachungaji wa Kanisa hilo kutoka nchini Kenya.

Akizungumza baada ya kufanyika kwa maombi ya kuliombea Taifa, Katibu wa Jimbo la Mashariki Kati mwa Tanzania wa Kanisa la Waadvestita Wasabato Tanzania Mchungaji Shashi Musa Wanna amesema walikuwa na maombi katika juma zima ambapo wametumia nafasi hiyo kuwa na mahubiri pamoja na maombi.

“Tulikuwa na wiki ya Uamsho wa kiroho katika Kanisa letu lakini pia kuliombea Taifa letu na Wachungaji wenzetu kutoka Kenya ambao tulikuwa nao wenzetu wanauzoefu mkubwa mambo ya siasa yanayoendelea Kenya.Tumehimiza maombi na umuhimu wa amani katika nchi yetu.

Aidha amesema pia wanawashauri viongozi wengine wa dini wasiwe wanasiasa kwani viongozi wa dini ni sehemu ya kimbilio pale ambapo nchi itakuwa na shida hivyo wanawajibu wa kuombea Taifa lakini wanakazi ya kufanya usuluhishi kwa maana ya waumini wao pia ni sehemu ya wanasiasa.

Pia amesema wanawaambia waumini wawe ni wenye kusamehe na kujishusha huku akiendelea kutoa rai kwa viongozi wengine wa dini nchini kuliombea Taifa letu.”Tusiwe sehemu ya uchochezi bali tuwe sehemu ya kuleta amani kwa maombi na ushauri.”

Kwa upande wake Mhubiri kutoka nchini Kenya Mchungaji Patrick Muthee amesema katika zama hizi ambazo Dunia imeharibika wakati mwingine makanisa na waumini wake wanajaribiwa huku akieleza Kanisa linapoongia katika siasa kunakuwa na changamoto kwasababu ile roho ya Mungu inaondoka

“Kazi ya Kanisa ni kuleta watu pamoja na tunatambua viongozi Mungu ndio huchagua sisi kama waumini Mungu anatutumia katika hali ile ya kupiga kura lakini Mungu anajua njia iliyobora.Hivyo kama Kanisa viongozi,wachungaji , na masheikh tuzungumze na waumini wetu ….

“Kuwaambia jukumu kubwa la kuchagua viongozi ni la Mungu hivyo tumtangulize Mungu, wawe na imani Mungu ndiye anatuchagulia viongozi hatutakuwa na mashindano ,hatutakuwa na vurugu.

Wakati huo huo Mchungaji Haruni Muturi wa Kanisa la Wadventista Wasabato kutoka nchini Kenya amesema katika wiki hiyo ya uamsho wametumia nafasi hiyo kujihoji miyoni mwao na kujitoa upya kwa Yesu Kristo kwasababu wanajua kuna majaribu.

“Na kwasababu ya majaribu hayo Mungu aweze kusikia watu wake ,kuwarejesha katika upendo wake na jinsi tulivyokuwa tumekuja kuombea nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hilo nalo ni jambo tumelizingatia sana.

“Kwasababu tunataka waumini wasiwe na vita na Serikali ,wafahamu jinsi ya kufanya kampeni za kuchagua viongozi kwa ustaarabu na wawe watii na kuweka Serikali katika Maombi badala ya vita ,ni jukumu letu pia kuendelea kuomba mpaka uchaguzi utakapokwisha Oktoba mwaka huu.

Awali Mchungaji wa Kanisa la Waadvestita Wasabato Kinondoni Victor Geofrey amesema wamekuwa katika wiki ya Uamsho iliyokuwa na lengo la kukumbushana mambo muhimu katika maisha ya Kikristo na kusimama kama Kristo alivyofundisha na hasa wakijua wako siku za mwisho naye anakaribia kuja upesi .

“Lakini katika wiki ya Uamusho pia tumeomba kwa mambo mbalimbali kwa ajili ya maisha ya kiroho lakini pia kwa ajili ya mambo ya taifa letu la Tanzania kwani tuko katika wakati uliomakini ambao kila Mtanzania anatakiwa kuchukua jambo hilo kwa umakini wake.

“Tumeliombea Taifa amani na mshikamano na tumehitimisha siku ya ya Sabato, siku ya ibada kwa pamoja na tumekutana kumshukuru kwa kuwa ametusikia kwa wiki nzima na maombi haya yatakuwa endelevu kwasababu tumeamshwa maombi ni maisha ya kila siku ya wale ambao wanatazamia maisha ya kiroho.
Share:

SHY WOMEN’S DAY OUT YATIKISA TENA SHINYANGA! WANAWAKE WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI, UONGOZI UCHAGUZI MKUU 2025

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

SHEREHE ya Wanawake Shy Women’s day Out imefana, huku wanawake wakitakiwa kupendana,kushikamana pamoja na kuchangamkia fursa za kiuchumi na uongozi.

Sherehe hiyo iliyoandaliwa na Kikundi cha Women For Change,imefanyika jana katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga,ambapo mgeni rasmi ni Naibu Spika Baraza la Wawakilishu Zanzibar Mgeni Hassan Juma, huku mshereheshaji akiwa ni Dk. Kumbuka.

Awali akisoma taarifa ya Kikundi cha Women For Change Mwenyekiti wa Kikundi hicho Sara Sawe, amesema kuwa sherehe hiyo ya Women’s Day Out imefikisha miaka Sita sasa,ikiwa na lengo la kuwakutanisha wanawake sehemu moja,kufurahi,kutengeneza mtandao,pamoja na kupeana fursa za kiuchumi.

Amesema kwenye sherehe hiyo huwa zinatolewa mada mbalimbali ambazo zinawajengea wanawake maarifa yakiwamo ya kiuchumi,kijamii na kisiasa kutoka kwa watalaamu mbalimbali ambao wamebobea kwenye masuala hayo.

“Kikundi chetu cha Women For Change tulikianzisha mwaka 2013, kwa lengo la kusaidiana,kuinuana kiuchumi,kushirikiana huduma za kijamii pamoja kusaidia watu wenye uhitaji,”amesema Sara.

“Baadaye ndipo tukaja na wazo la kuwa tunafanya sherehe ya kuwatoa “out” wanawake wa Shinyanga “Shy Women’s Day Out”ili kuwakutanisha pamoja,kufurahi,kubadishana mawazo,kutengeneza “Connection” na kupeana fursa za kiuchumi na sasa sherehe hii imefikisha miaka 6,”ameongeza Sara.

Aidha,amesema kikundi hicho ni mdau mkubwa wa Serikali katika kuchagiza maendeleo, na kwamba wamekuwa wakitoa Madawati shuleni,kusomesha wanafunzi hadi vyuo vikuu,wameshakarabati bweni katika Kituo cha kulea watoto wenye Ualbino.
Ametaja misaada mingine ni kuwapatia mitaji Wajasiriamali wadogo na kwamba mipango yao ya mwaka huu 2025 ni kufanya pia ukarabati wa Jengo la Magereza ya Shinyanga kwa ajili ya wafungwa kulitumia kwa chakula na kazi hiyo walishaianza na imefikia asilimia 85.

Amesema mipango mingine ni kuwa na Taasisi kubwa ya kifedha kwa ajili ya kusaidia wanawake,pia kujenga ukumbi mkubwa na hata kutumika kwa mikutano ya kitaifa.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi,akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha kwenye sherehe hiyo, amekipongeza kikundi hicho cha Women For Change kwa kuwakutanisha wanawake wenzao na kupeana maarifa mbalimbali.

Mgeni rasmi Naibu Spika Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma, amewashukuru Women For Change kwa kumheshimisha, huku akiwasihi wanawake waishi kwa kupendana,kushikamana ili wapate kunyanyuka kwa pamoja.
Amesema matatizo ya wanawake karibia yote yanafanana hivyo kupitia sherehe hiyo,kila mmoja abadilike sasa na kuishi kama ndugu,kushikana mikono na kuinuana kiuchumi.

Amewataka pia wanawake watumie fursa zilizopo za kiuchumi na kwamba sheria inawapatia wanawake kipaumbele katika kupata Zabuni,pamoja na kuchangamkia mikopo ya halmashauri asilimia 10.
Katika hatua nyingine amewataka wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi mkuu 2025 kwa nafasi ya Udiwani na Ubunge, sababu nafasi ya Rais yupo Dk. Samia kwa upande wa Tanzania na Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi.

Pia,amewataka wananchi katika kuelekea kwenye uchaguzi huo waendelee kudumisha amani na utulivu, pamoja na kuendelea kuuenzi Muungano.


TAZAMA PICHA👇👇
Naibu Spika Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi akizungumza.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Women For Change Sara Sawe akizungumza.
Mwenyekiti wa Sherehe ya Women's Day Out 2025 Faustina Kivambe akizungumza.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo akizungumza.
MC Dk.Kumbuka akisherehesha.
Naibu Spika Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma (kulia)akiwa na Mwenyekiti wa Women For Change Sara Sawe.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi (kushoto)akiwa na Mwenyekiti wa Sherehe ya Women's Day Out Faustina Kivambe.
Mr Black akitoa somo la uchumi.
Sherehe ya Women's Day Out ikiendelea.








Utoaji wa vyeti vya shukrani kwa wadhamini wa sherehe hiyo ukiendelea.
Picha za pamoja zikipigwa.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger