Monday, 30 January 2023

UWT SHINYANGA WAADHIMISHA MIAKA 46 YA CCM KISHAPU, WAWAJULIA HALI VIJANA WALIOSHAMBULIWA NA FISI



Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Helen Bugoye (kulia) akimjulia hali mmoja wa wakazi wa Kishapu waliojeruhiwa kwa kushambuliwa na fisi ambapo sasa wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya  Jakaya Mrisho Kikwete ya Wilaya ya Kishapu. UWT Mkoa wa Shinyanga wametembelea hospitali hiyo na kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM
Na Halima Khoya - Shinyanga

Jumuiya ya Umoja wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Shinyanga imeadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kishapu kwa kupanda miti, kutembelea na kuwapa zawadi wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya  Jakaya Mrisho Kikwete ya Wilaya ya Kishapu.

UWT wakiongozwa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Helen Bugoye
pia wamewajulia hali watu wanne wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Mwalata Mkoani Shinyanga waliojeruhiwa kwa kushambuliwa na fisi sehemu mbalimbali za miili yao.


Tukio hilo la kushambuliwa na fisi limetokea Januari 30,2023 majira ya saa 7 usiku katika kijiji cha Mwalata Kata ya Ndololeji Halmashauri ya wilaya Kishapu Mkoani humo.


Akieleza juu ya tukio hilo, mama mzazi wa majeruhi wawili (Jishansa Kija mwenye miaka 18 na Lazaro Emmanuel anayesoma darasa la 5), Bi. Mbuko Jishanga amesema kuwa majira ya saa saba usiku alisikia kelele nje ya nyumba yake ndipo alipotoka na kumkuta mwanae Jishansa akiwa amejeruhiwa usoni pamoja na Emmanuel akiwa amejeruhiwa kichwani.


Jishanga amesema kuwa mara baada ya kukuta hali hiyo alimuagiza panga Mkwilima wake Malambi Mayara,ambaye baada ya kumjeruhi fisi huyo kichwani alimrukia kijana huyo ambapo aling'ata shingoni na kufanikiwa kumuua akiwa ameng'ang'ania kwenye mwili wa Mkwilima huyo.


"Majira ya saa 7 usiku nilisikia kelele nje,nilipotoka niliwakuta wanangu wakiwa wamejeruhiwa na fisi ikabidi nimuagize mtoto panga nikawa namvizia  fisi huyo atoke nje na alipotoka tu alikutana na panga la kichwa akaanguka,alipoamka tena nikamkata mara ya pili huku nikiwa napiga kelele,watu walijaa wakanisaidia kumuua vizuri pamoja na kuwaleta watoto hospitali", amesema Jishanga.


Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya Kishapu,Dr Mohamed Mkumbwa, amesema majira ya saa 10 alfajiri tarehe 30,2023 amepokea wanaume 4 wakiwa wamejeruhiwa maeneo mbalimbali ya miili yao ambao walipatiwa huduma za kimatibabu na kufikia sasa hivi hali zao ni nzuri.


Akizungumza baada ya kutembelea Hospitali ya  Jakaya Mrisho Kikwete ya Wilaya ya Kishapu, Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Helen Bugoye ameeleza kusikitishwa na tukio hilo huku akiwataka wakazi wa Kishapu kushirikiana na Mamlaka zinazohusika kudhibiti wanyama wakali kuwawinda  wanyama hao.

"Wanawake tunaweza,kwani mzazi mwenzetu amewapambania watoto wake ambao walikuwa wamevamiwa na fisi, inatakiwa mamlaka ya maliasili wafike kwenye kijiji hiki ili kuwawinda wanyama hatarishi", amesema Bugoye.
Share:

DKT MABULA ATAKA MAFUNZO YA MAADILI KWA MADALALI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika yanayofanyika kwenye Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam tarehe 30 Januari 2023.

Sehemu ya washiriki wa ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika (MADALALI) yanayofanyika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam tarehe 30 Januari 2023.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Baishara (CBE) Profesa Edda Lwoga akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika yanayofanyika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam tarehe 30 Januari 2023.

Washiriki wa ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika (MADALALI) yanayofanyika katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula tarehe 30 Januari 2023.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na viongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) alipowasili katika ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika tarehe 30 Januari 2023.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa tatu kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) alipokwenda kufungua mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika tarehe 30 Januari 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

*****************************

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameataka kutolewa mafunzo ya maadili kwa Mawakala wa Mali Zisizohamishika (MADALALI)

Dkt Mabula amesema hayo leo tarehe 30 Januari 2023 wakati akifungua Mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika (MADALALI) yanayoendeshwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa kushirikiana na Chama cha Mawakala wa Mali Zisizohamishika (AREA) yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema, pamoja na mafunzo yanayotolewa kuwa ya kitaalamu zaidi lakini upo umuhimu mkubwa wa kutolewa mafunzo yanayohusu maadili kwa kuwa eneo hilo limekuwa likisababisha malalamiko mengi kwa jamii.

Alitolea mfano wa Mawakala kuchukua kamisheni toka pande zote zinazohusika kwenye mauziano au upangaji nyumba na kubainisha kuwa suala hilo limekuwa kichocheo cha kupanda bei au kodi za nyumba na kuzidi viwango vya soko lengo likiwa kujipatia kamisheni kubwa na hivyo kuvuruga mwenendo wa soko la milki nchini.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, wapo Madalali wanaolalamikiwa kufanya vitendo vya utapeli ambapo huwadanganya wateja na kusababisha wateja hao kununua viwanja huku wakijua fika kuwa viwanja hivyo ni mali ya watu wengine na mwisho wa siku hujipatia fedha isivyo halali.

‘’Mafunzo kuhusu maadili ni muhimu sana kwa kuwa utendaji kazi unaozingatia suala hili la maadili utawezesha kujijengea heshima, kuaminika, kutoa huduma bora na hivyo kuwezesha kukua biashara na kujenga uaminifu kwa jamii waayoihudumia’’. Alisema Dkt Mabula

Alibainisha kuwa, katika baadhi ya nchi zikiwemo Kenya na Afrika kusini fani ya madalali inaheshimika na kuthaminiwa kwa kuwa imewekewa utaratibu wa usimamaizi na hivyo masuala ya uadilifu na weledi yanazingatiwa na kusimamiwa ipasavyo.

Alisema, Kenya inayo sheria ya usajili wa mawakala inayojulikana kama Estate Agents Act ya mwaka 1984 iliyorekebishwa mwaka 2012 huku Afirika Kusini ikiwa na sheria ya Property Prractitioners Act ya mwaka 2019 iliyounda mamlaka ya usimamaizi wa wataalamu wa masuala ya milki wakiwemo mawakala wa usimamizi wa mali zisizohamishika.

Alikipongeza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) pamoja na Chama cha Mawakala wa Mali Zisizohamishika (AREA) kwa kubuni mpango wa mafunzo unaoelenga kuhakikisha kuwa fani ya uwakala wa mali zisizohamishika inaendeshwa kitaalamu.

‘’Hatua hii mliyoichukua kuwafundisha vijana wajasiriamali wanaojishughulisha na shughuli zisizo rasmi ili kuingia katika utaratibu rasmi wa kufanya shughuli zao itawasaidia siyo tu kuwajengea uwezo wa kitaalamu bali pia kuwajengea kuajimini na kuaminiwa na jamii.

Amesema wizara yake iatatoa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha fani ya mwakala inaboreshwa ili shughuli za mawakala wa mali zisizohamishika ziweze kuanyuka kwa ufanisi na tija.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Mali Zisizohamishika (AREA) Erick Rweikiza amesema dhamira ya chama chake ni kuweka mazingira bora ya kuelimisha wanachama juu ya taaluma na kujenga umoja wa kibiashara pamoja na kutetea maslahi ya wanachama ili kuweka mazingira bora kwa wapangishaji, wauzaji na wanunuzi aliowaeleza kuwa ndiyo waajiri wa mawakala.

‘’Nia ni kuwafundisha wasio na ajira kujiajiri kupitia taaluma ya mawakala wa mali zisizohamishika’’ alisema Rweikiza.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Bishara (CBE) Prof Edda Lwoga alisema, elimu inayotolewa na chuo chake kwa mawakala inatolewa chini ya mpango kabambe wa kuwafikia vijana wa kitanzania na kurasimisha shughuli zisizo rasmi zinazofanywa na jamii kubwa ya watanzania.

‘’Katika kutambua juhudi za serikali kwenye mpango wa kurasimisha taaluma ikiwa ni pamoja na kusajili mawakala sisi kama chuo tumejidhatiti na tuko tayari kushirikiana na serikali kwenye mchakato ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhakikisha watendaji wana viwango vinavyokubalika kabla ya kuajiriwa’’. Alisema Profesa Edda Lwoga.
Share:

VIJANA WANNE WA FAMILIA MOJA WANUSURIKA KUFA KWA KUSHAMBULIWA NA FISI KISHAPU,... MAMA MWENYE PANGA ATISHA

Mnyama Fisi

Na Sumai Salum - Kishapu
Wanaume wanne wa familia moja katika kijiji cha Mwalata Kata ya Shagihilu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao kwa kushambuliwa na mnyama Fisi wakiwa wanalinda mbuzi na ng'ombe nyumbani kwao. 


Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Kishapu Bw. Mohamed Mkumbwa amesema waliwapokea majeruhi majira ya saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia leo Jumatatu Januari 30,2023 wakiwa na hali mbaya  na baada ya kuwapa huduma sasa wanaendelea vizuri.


"Ni kweli tumewapokea majeruhi wanne alfajiri ya leo wakiwa na hali si nzuri ,kuna aliyejeruhiwa kwa kung'atwa chini ya pua mwingine kichwani mwingine mapajani na mwingine sehemu ya kichwani kuelekea shingoni na sasa tunamshukuru Mungu wanaendelea vizuri", ameeleza Dkt. Mkumbwa.


Waliojeruhiwa ni Jishanga Izengo (18) aliyejeruhiwa sehemu ya chini pua, Kanizio Joseph mwanafunzi anayesoma darasa la 4 shule ya msingi Mwalata aliyejeruhiwa maeneo ya mapajani, Lazaro Emmanuel anayesoma darasa la 5 shule ya msingi Mwalata aliyejeruhiwa maeneo ya kichwani na mikononi pamoja na Malambi Mayala ambaye amejeruhiwa sehemu ya kichwani kuelekea shingoni na wote wameshonwa majeraha yao.


Akisimulia kuhusu tukio hilo, mama mzazi wa watoto hao, bi.Mbuke Jishanga Izengo amesema kuwa mnamo majira ya saa 7 usiku wa kuamkia leo tarehe 30 alimsikia kijana wake Jishanga akipiga kelele hivyo alivyotoka nje akakuta wameshambuliwa na fisi ambaye baadaye alichukua panga na kuanza kupambana naye huku akipiga kelele majirani zake wakaja kumsaidia.


"Yaani huyu fisi angeniulia watoto wangu sisi kwetu huwa tuna desturi ya watoto wa kiume kulinda mifugo ikiwemo mbuzi na ng'ombe hivyo wakati wamelala ndipo akaja fisi kuanza kuwashambulia kwa kweli nikaona nichukue panga nianze kupambana nae nikamkata eneo la kichwa akaenda kujibamiza ukutani mwa nyumba akapanga mipango ya kunirudia na mimi nikaweka panga vizuri akaja, nikamkata tena akalala na watu wakaja tunamalizia. Nashukuru Mungu amewasaidia na sasa wanaendelea vizuri", amesema Mbuke.

Kijana mkubwa wa familia hiyo anayejulikana kwa jina la Joseph Shija amesema kuwa fisi huyo wanamhusisha na imani za kishirikina.
Share:

WAKANDARASI WA REA SHINYANGA WAPEWA MWEZI MMOJA KUKAMILISHA MIRADI YA UMEME

 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Joseph Modest Mkude akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga.


Na Mwandishi Wetu - Shinyanga

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Joseph Modest Mkude ametoa muda wa mwezi mmoja na nusu kwa wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza umeme vijijini kukamilisha kazi waliyopewa na Serikali ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya nishati ya umeme.


Mhe. Mkude ambaye ni Mkuu wa wilya ya Kishapu ametoa agizo hilo leo Jumatatu Januari 30,2023 kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini kilichofanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.


Mkude amewataka wakandarasi hao kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa miradi hiyo kila wiki kwa wakuu wa wilaya zote na Ofisi ya Mkuu Mkoa.

"Utekelezaji wa miradi unasuasua sana na mkoa hauridhishwi na kasi yenu, endapo hamtajirekebisha Serikali haitasita kusitisha mikataba yenu", amesisitiza.

Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Masoko na Teknolojia wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rural Energy Agency – REA)Mhandisi Advera Mwijage amesema hakutakuwa na muda wa nyongeza kwa wakandarasi na kuwataka wazingatie mikataba yao.

Mhandisi Mwijage amewataka wakandarasi kushirikisha viongozi wa ngazi zote kuanzia vijiji, wilaya na mikoa pamoja na wananchi wakati wa utekelezaji wa mradi ili kuweza kuondoa changamoto za malalamiko ya wananchi.


Kwa upande wao, Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo, wameahidi kurekebisha kasoro zilizojitokeza na kuahidi kukamilisha miradi kwa mujibu wa mikataba waliyoingia na Serikali.

Mkurugenzi wa SUMA JKT Electric Co. Ltd ambao wanatekeleza Mradi katika wilaya ya Shinyanga Kishapu, Meja Simon Mhame amesema wameongeza vibarua na wameshaagiza vifaa vya kutosha kukamikisha Mradi hivyo watatimiza na kutii maagizo ya Serikali.


Mkurugenzi Mtendani wa Kampuni ya Ukandarasi ya Tontan Project Technology Co. Ltd, bw. Zheng Pengtao wanaotekeleza mradi wa umeme wilayani Kahama amesema watahakikisha wanakamilisha usambazaji wa umeme kwa wakati katika vijiji vyote kwa mujibu wa mkataba waliosaini na serikali.


Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili utanufaisha vijiji 216 mkoani Shinyanga kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 56 ambapo Wakandarasi wanaosimamia mradi wa usambazaji umeme wilayani Kahama, Shinyanga na Kishapu kuwa ni Suma JKT na Tontan Project Technology Co. Ltd.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Joseph Modest Mkude akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Joseph Modest Mkude akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga
 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Joseph Modest Mkude akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga
Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Masoko na Teknolojia wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Advera Mwijage akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga
Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Masoko na Teknolojia wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Advera Mwijage akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga

Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Masoko na Teknolojia wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Advera Mwijage (wa pili kushoto) akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga
Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Masoko na Teknolojia wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Advera Mwijage (wa pili kushoto) akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga
  Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Joseph Modest Mkude akiwa kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga
Mkurugenzi wa SUMA JKT Electric Co. Ltd , Meja Simon Mhame akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga
Mkurugenzi Mtendani wa Kampuni ya Ukandarasi ya Tontan Project Technology Co. Ltd, bw. Zheng Pengtao akielezea jitihada wanazofanya kuhakikisha wanakamilisha usambazaji wa umeme kwa wakati kwenye vijiji kwa mujibu wa mkataba waliosaini na serikali.
Wadau wakiwa kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga
 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Joseph Modest Mkude akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Shinyanga.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Share:

EFTA KUWEZESHA WAKULIMA ZAIDI YA 200 KUPATA MIKOPO YA MATREKTA BILA DHAMANA


Wakulima nchini wametakiwa kuchangamkia fursa za upatikanaji wa mikopo ya mashine za kilimo inayotolewa bila dhamana na kampuni ya Equity for Tanzania Limited (EFTA), Hatua ambayo imeelezwa kuwa itasaidia katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo pamoja na pato la taifa.

Wito huo umetolewa kwa wakulima baada ya kampuni ya EFTA kununua matrekta zaidi ya mia mbili aina ya New Holand TT75 4WD, kwa lengo la kuzikopesha kwa wakulima nchini bila dhamana, hatua ambayo inatajwa kuwa itasaidia kuongeza matumizi ya mashine katika kilimo na hivyo kupelekea Kuongeza kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo, na pato la taifa.

Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya EFTA bw. Nicomed Bohay amesema kupatikana kwa matrekta hayo mia mbili kutaongeza chachu kwa wakulima katika kuongeza uzalishaji.


“Matumaini yetu ni kuwa kadri wakulima wanavyoweza kumiliki mashine mbalimbali za kilimo ndivyo uzalishaji utakavyoongezeka, Hata hivyo changamoto kubwa ni kuwa wakulima wengi hawakopesheki kutokana na masharti mbalimbali yaliyowekwa na taasisi za kifedha na hivyo kundi kubwa la wakulima kuachwa wakiangaika na kilimo cha jembe la mkono”, amesema.

Baada ya kuiona changamoto hiyo, Bohay anasema ndio maana EFTA kwa kushirikiana na Taasisi zingine kama vile New Holand Agriculture, Hughes Agriculture Tanzania Ltd (HAT) na CRBD Benki wameingia makubaliano yatakayowezesha wakulima nchini kupata mikopo ya matrekta bila dhamana kupitia EFTA hatua ambayo amesema itaongeza idadi ya wakulima nchini watakaoweza kumiliki matrekta bila masharti magumu.


“Kwa wastani kwa Mwaka Matrekta yanayouzwa nchini ni 1800 idadi ambayo bado ni ndogo sana, na katika idadi hii EFTA pekee imetoa matrekta 530 sawa na asilimia 23%. Tamanio leo ni kuona masharti magumu kwa kundi hili tunayaondoa ili idadi ya wakulima wanaotumia mashine bora za kilimo inaongezeka”, amesema Bohay.


Bohay ameongeza kuwa EFTA kupitia makubaliano hayo sasa EFTA itaongeza idadi ya wakulima ambao watakopeshwa matrekta na hivyo kuwa na idadi kubwa ya wakulima wanaotumia matrekta katika kufanya shughuli zao za kilimo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc nchini, Bw. Abdulmajid Nsekela amesema ushirikiano ambao taasisi yake imeuingia na EFTA umelenga kusaidia katika kuwafikia wakulima wadogo nchini kuweza kupata mikopo ya mashine za kilimo kwa masharti nafuu nchi nzima.


"Ushirikiano huu na EFTA umelenga kusaidia wakulima wadogo na wakati nchini kupata mikopo kwa urahisi zaidi bila kuwa na masharti magumu ambayo wakulima wengi hawawezi kuyatimiza”, amesema Nsekela.


“Lengo la Benki yetu ni kuona wakulima nchini wanatumia mashine bora za kilimo maana tunatambua kwa kuwa na wakulima wengi wanaolima kisasa pato la taifa litaongezeka kutokana na uzalishaji utakaofanyika", ameongeza Nsekela.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya New Holand Agriculture Bw. Stuart Leishman, amesema aina ya trekta ambazo kampuni ya EFTA imezinunua ni imara na kuwa zinaweza kufanya kazi katika maeneo yote ya nchi.


“Trekta hizi ni muhimu na zitasaidia kuyafikia malengo ya nchi ya muda mrefu ya kuwa na uhakika wa chakula, na tunajivunia kushiriki katika mchakato wa Kuongeza idadi ya wakulima watakaomiliki trekta na hivyo kuwa na mavuno bora na yaliyoongezeka” amesema Stuart Leishman.


Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Makampuni ya EFAfrica, ambao ndio wamiliki wa Kampuni ya EFTA Bw. Michiel Timmerman amesema amefurahishwa na mpango huu, ambao umelenga kujibu njozi ya kuanzishwa kwa makampuni ya EFAfrica ya kuwasaidia wakulima wadogo na wale wa kati kuweza kumiliki mashine mbalimbali za kilimo bila dhamana hivyo kuchochea ongezeko la matumizi ya mashine katika kilimo.
Share:

Sunday, 29 January 2023

MGODI WA BARRICK BULYANHULU WAZIDI KUBORESHA MAISHA YA WANANCHI WA NYANG'HWALE


Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare (Kushoto) akibadilishana nyaraka za makubaliano na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale, Bw.John Isaac John muda mfupi baada ya kusaini mkataba wa makubaliano katika hafla iliyofanyika katika Mgodi wa Bulyanhulu.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare (Kulia) akibadilishana nyaraka za mkataba wa makubaliano na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw.Majagi Maiga ambapo mgodi huo utatoa kiasi cha shilingi milioni 989 kwa ajili ya kufankisha miradi ya kijamii kupitia fedha za mfuko wa uwajibikaji kwa jamii katika kipindi cha mwaka huu.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare, akiongea wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nywang’hwale ya kutekeleza miradi ya kijamii katika wilaya hiyo kupitia fedha za uwajibikaji wa jamii katika hafla iliyofanyika mgodi hapo mwishoni mwa wiki, kushoto ni Meneja wa Meneja uhusiano wa jamii wa mgodi huo Agapiti Paul.
Kaimu Mwenyekiti wa mfuko wa maendeleo wa halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw.Patrick Athanas akiongea katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika mgodi wa Bulyanhulu.
Diwani wa kata ya Kharumwa iliyopo katika halmashauri ya Nyang’hwale akiongea wakati wa hafla hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw. Majagi Maiga (kushoto) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale, Bw.John Isaac John wakisaini mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya kijamii kutumia fedha za uwajibikaji kwa jamii zitakazotolewa na Barrick Bulyanhulu mwaka huu.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw. Majagi Maiga (kulia) wakisaini mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya kijamii kutumia fedha za uwajibikaji kwa jamii zitakazotolewa na Barrick Bulyanhulu mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw.Majagi Maiga akiongea wakati wa hafla hiyo
Wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu na wageni waalikwa katika hafla hiyo fupi wakifuatilia matukio ya kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano baina ya Mgodi na Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Picha ya pamoja ya Wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu na viongozi wa Serikali wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale iliyopo mkoani Geita baada ya kusaini mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya kijamii kutumia fedha za uwajibikaji kwa jamii zitakazotolewa na Barrick Bulyanhulu mwaka huu.

 ***
Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, uliopo wilayani Msalala mkoani Geita unazidi kuboresha maisha ya Wananchi wanaoishi katika Halmashauri ya Nyang’hwale kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii ambapo mwishoni mwa wiki viongozi wa Mgodi huo na halmashauri hiyo walisaini mkataba wa makubaliano wa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya milioni 989,000,000/- katika kipindi cha mwaka 2023.

Akiongea katika hafla hiyo iliyofanyika katika Mgodi wa Bulyanhulu na kuhudhuriwa na viongozi wa Halmashauri ya Nyang’hwale na wafanyakazi wa Barrick, Meneja wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare, alisema kampuni itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha inafanikisha miradi ya kuboresha jamii zinazozunguka katika maeneo ya migodi yake kwa mujibu wa sera za nchi kupitia fedha za Uwajibikaji kwa jamii (CSR).

Sangare, alisema Mgodi wa Bulyanhulu mwaka huu unatarajia kuzalisha karibia wakia 215,000 za dhahabu,ambapo kutokana na uzalishaji huu utatenga shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya miradi ya uwajibikaji kwa jamii iliyopendekezwa na wilaya husika ambapo kati ya fedha hizi zitaenda kwa halmashauri za wilaya za Msalala na Nyang’wale.

“Nawapongeza Kamati ya Maendeleo ya Halmashauri ya Nyang’hwale kwa kuchagua miradi yenye kugusa mahitaji ya Wananchi ikiwemo ya afya, maji na elimu sambamba na miradi mingine ya maendeleo, natumaini miradi hii itatekelezwa kama ilivyopangwa na kukamilika kwa wakati mwafaka uliopangwa na nawashauri katika siku za usoni mwendelee kupendekeza miradi endeelvu ambayo itaacha alama hata muda wa mgodi ukiisha” alisema Sangare.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Bw .John Isack John, aliipongeza Barrick Bulyanhulu kwa mapinduzi makubwa ya maendeleo inayoendelea kufanya katika maeneo yanayozunguka mgodi kupitia fedha za uwajibikaji wa jamii (CSR) ambayo yanazidi kuboresha maisha ya wananchi na kuwafanya wajivunie kuwepo migodi katika eneo lao.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Bw.Majagi Maiga, alishukuru Barrick Bulyanhulu, kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika manispaa hiyo na aliahidi kuwa Serikali itahakikisha fedha zote zinatumika kwa lengo lililokusudiwa la kufanikisha miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Baadhi ya miradi itakayotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii za Barrick Bulyanhulu katika halmashauri ya Nyang’hwale katika kipindi cha mwaka huu ni kumalizia ujenzi wa wodi maalum katika hospitali ya Nyang’hwale (97,860,500/-),kumalizia ujenzi wa gereji katika kijiji cha Kharumwa (40,000,000),kumalizia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Ikangala (11,625,000),kumalizia ujenzi wa vyumba bitatu katika shule ya msingi Samia Suluhu (18,833,000),ujenzi wa choo na sehemu maalum ya kuchoma taka katika zahanati ya Iyenze (14,279,250),kukamilisha ujenzi wa jingo la maabara katika sekondari ya Mwingiro (16,000,000),kumalizia jengo la utawala katika sekondari ya Kaboha (67,602,000),kukamilisha ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya msingi ya Kharumwa (60,000,000) na kukamilisha ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa katika shule za msingi za Nyamikonze, Ngwasabuka,Iyenze na Kafita 62,500,000).


Miradi mingine ni kukamilisha jengo la utawala,maabara choo na mfumo wa maji katika shule ya sekondari ya Nyamtukuza (51,169,200),ujenzi wa kituo cha mabasi katika kijiji cha Ikangala (170,000,000),kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Mwingiro (74,178,450),kukamilisha ujenzi wa jengo la dharura hospitali ya Mwingiro (69,250,000),kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Nyijundu (45,885,000),mpango wa kuinua ufaulu wa wanafunzi mashuleni (25,000,000),matenki ya kuhifadhi maji na kujenga mfumo wa kuvuna maji ya mvua katia sekondari ya Mwingiro (6,000,000),ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya msingi ya Kharumwa (60,086,225),kukamilisha ujenzi wa kituo cha polisi cha Kharumwa (17,931,375) na kununua jenereta kubwa na kuimarisha miundombinu ya hospitali ya wilaya ya Nyang’hwale (50,000,000).

Share:

WANAFUNZI WAHUNI WALIOMDHALILISHA MTANDAONI MWANAFUNZI WA CHUO CHA CDTI WAKAMATWA


Na. Abel Paul wa Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limesema kuwa limefanikiwa kuwakamata wanafunzi wawili wa chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia kwa mwanafunzi wa chuo hicho kwa njia ya mtandao na wanafunzi wenzake.


Akitoa taarifa hiyo leo Januari 29,2023 Kamanda wa Polisi mkoani Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amewataja waliokamtwa kuwa ni EFRON ISAYA (32) na COSMAS ROBERT (26) wote wakiwa ni wanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.


Kamanda Masejo amesema kuwa Januari 21 mwaka huu muda wa saa 11:00 jioni huko katika Chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (CDTI)  kilichopo wilaya ya Arumeru na Mkoa wa Arusha kuliripotiwa tukio la unyanyasaji wa kijinsia mwanafunzi wa chuo hicho  (jina tumelihifadhiwa) kwa njia ya mtandao na wanafunzi wenzake.


ACP Masejo amesema baada ya kupata taarifa hiyo jeshi hilo lilianza uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata wanafunzi hao wawili.

Masejo amesema bado Jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na mara utakapokamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.


Sambamba na hilo Polisi mkoani humo wametoa onyo kwa watu wachache ambao wana matumizi mabaya ya mitandao inayodhalilisha utu na heshima ya jamii yetu ya Kitanzania ambapo amewataka kuacha mara moja tabia hiyo kwani Jeshi hilo litawachukuliwa hatua kali za kisheria.

Share:

WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WAHIMIZWA KUSIMAMIA MIRADI YA TASAF KIKAMILIFU

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati) akizungumza na Watendaji wa Halmashauri ya Mji Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita.
Sehemu ya Watendaji wa Halmashauri ya Mji Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati meza kuu) mara baada ya Naibu Waziri huyo kukagua miradi ya TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Geita.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Msangi Tsetonga akifafanua jambo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri Ndejembi, iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Mji Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wapili kutoka kulia) akielekea kukagua madarasa ya shule ya Msingi Kivukoni yaliyopo katika Halmashauri ya Mji Geita wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita, wengine ni watendaji wa mkoa huo.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (aliyenyanyua mikono) akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Nyanza mara baada ya kukagua madarasa na vyoo vya shule ya Kivukoni vilivyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Geita.

Mwonekano wa darasa lililopo shule ya Msingi Kivukoni katika Halmashauri ya Mji Geita, lililojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

*********************************

Na. Veronica Mwafisi - Geita Tarehe 29 Januari, 2023


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kama wanavyosimamia miradi mingine ya maendeleo.

Mhe. Ndejembi amewahimiza wakurugenzi hao, wakati akizungumza na Watendaji wa Halmashauri ya Mji Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita.

Mhe. Ndejembi amehimiza miradi ya TASAF kusimamiwa vizuri kama inavyosimamiwa miradi mingine ya maendeleo kwani miradi yote inatekelezwa na Serikali chini ya uongozi makini wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuliletea taifa maendeleo.

Mhe. Ndejembi amesema, katika utekelezaji wa miradi ya TASAF inaonyesha kuwa wakurugenzi na watendaji wa halmashauri hawashiriki kikamilifu katika usimamizi na badala yake huwaachia waratibu na watendaji wa TASAF.

“Usimamizi wa miradi ya TASAF unapaswa kupewa kipaumbele, hivyo wakurugenzi ni lazima waisimamie miradi hii kikamilifu kwa sababu fedha inayotumika upatikanaji wake unatokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, miradi ya TASAF ikisimamiwa kikamilifu kama ambavyo inavyosimamiwa miradi mingine ikiwemo ya elimu, afya na miundombinu ni dhahiri kuwa, watanzania watanufaika na taifa litapiga hatua katika mendeleo.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mji Geita, Mhe. Joseph Lugaila amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo katika Mkoa wa Geita.

Aidha, Mhe. Lugaila amemshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Geita yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger