Tuesday, 30 September 2025

MILIONI 473 KUTEKELEZA MRADI WA KAMERA ZA USALAMA DODOMA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amefanya ziara ya kutembelea mradi wa kusimika kamera za usalama (CCTV) katika jiji la Dodoma, mradi unaolenga kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, mali zao pamoja na miundombinu ya umma.

Mradi huo unahusisha njia kuu nne zinazoingia na kutoka jijini pamoja na baadhi ya maeneo ya ndani ya jiji yenye mikusanyiko mikubwa ya watu, miundombinu ya serikali na maeneo yenye historia ya matukio ya kihalifu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri, amesema mradi huo unahusisha ufungaji wa nguzo 50 zitakazobeba jumla ya kamera 106 ambazo zina uwezo wa kusoma namba za magari, sura za watu, kuhesabu vyombo vya usafiri na watu, pamoja na kubaini matukio mbalimbali ikiwemo magari yaliyopaki sehemu zisizoruhusiwa .

Amesema Mradi huo utakapo kamilika utasaidia kudhibiti makosa ya barabarani, vitendo vya jinai na uharibifu wa miundombinu, huku ukitoa uhakika wa usalama kwa wadau wa maendeleo na wawekezaji.

Ameeleza kuwa Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 473 ambazo zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

"Halmashauri imeingia mkataba na Kampuni ya Wisjane Smart System, iliyopokea kazi rasmi tarehe 1 Juni mwaka huu, na inatarajiwa kukamilisha ndani ya siku 90 tangu kuanza kwake, " ameeleza Shekimweri.

Kwa upande wa Mtaalam wa mradi huo, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Wisjane Smart System, Wisley Ussiri, amesema Kamera zilizofungwa ni za aina tatu .

Amezitaja kuwa ni kamera zinazoweza kusoma namba za magari, kamera zenye uwezo wa kufuatilia matukio kwa umbali mrefu wa viwanja 45 vya mpira sawa na kilomita 4.5, na kamera za kufuatilia mienendo ya watu na kwamba Maeneo ya vipaumbele ya ufungaji ni Nala, Machinga Complex na maeneo ya katikati ya jiji la Dodoma.

Ussiri ameongeza kuwa Mfumo huu, unaoendeshwa kwa teknolojia ya kisasa, unatarajiwa kusaidia vyombo vya usalama kwa kiasi kikubwa ikizingatiwa changamoto ya uhaba wa nguvu kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema utekelezaji wa mradi huu utakuwa chachu ya kuongeza usalama na kudhibiti uhalifu jijini Dodoma, kwani kamera zitakuwa zikirekodi na kubaini matukio mbalimbali kwa haraka.

Amesisitiza kuwa uwepo wa Kamera hizo pia utaleta heshima kwa jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi na kurahisisha shughuli za kila siku za wananchi.

Senyamule amezitaka Taasisi mbalimbali kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwekeza katika mifumo ya ulinzi wa kisasa itakayosaidia kulinda rasilimali zao.

Aidha, ameahidi kuendelea kusimamia suala la amani na utulivu hususan katika kipindi cha uchaguzi, huku akiwataka wananchi kuhakikisha wanatimiza haki zao bila kuvunja sheria.





Share:

OFISI YA KANDA YA KATI YATOA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA MAABARA ZA KEMIA KWA WAKUU WA SHULE ZA SEKONDARI DODOMA

Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Kati, Magdalena Mtenga (aliyesimama), akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Usimamizi wa Maabara za Kemia kwa Wakuu wa Shule za Sekondari wa Jiji la Dodoma (TAHOSSA) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Bustani, Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma, Septemba 29, 2025.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Sechelela Dodoma, ambaye ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA), Grace Shilly, akimkaribisha Meneja wa Kanda yaKati, Magdalena Mtenga (hayupo pichani) kwa ajili ya kufungua mafunzo ya Usimamizi wa Maabara za Kemia kwa Wakuu wa Shule za Sekondari kutoka Jiji la Dodoma (TAHOSSA) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Bustani Wilaya ya Kondoa,mkoani Dodoma, Septemba 29, 2025.
Mtumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Kati, Revocatus Mwamba, akiwasilisha mada juu ya Mfumo wa Ubora ndani ya Maabara za Kemia, Usimamizi na uteketezaji wa Kemikali taka katika mafunzo ya Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) wa Jiji la Dodoma yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Bustani, Wilaya ya Kondoa, Septemba 29, 2025.
Mwakilishi wa Walimu Wakuu wa Kanda ya Kati (TAHOSSA), Peter Mlugu, akiishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutoa Mafunzo ya Usimamizi wa Maabara za Kemia kwa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) wa Jiji la Dodoma yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Bustani, Wilaya ya Kondoa, Septemba 29, 2025.
Baadhi ya Walimu Wakuu walioshiriki mafunzo wakiuliza maswali juu ya majukumu yaMamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika mafunzo ya Usimamizi wa Maabara za Kemia kwa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) kutoka Jiji la Dodoma yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Bustani kilichopo Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma Septemba 29, 2025.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Chinyika Wilaya ya Mpwapwa, Nerbert Msyenga, akiomba ufafanuzi juu ya usimamizi wa kemikali taka na uteketetezaji wake katika mafunzo kwa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) kutoka Jiji la Dodoma yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Bustani, Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma Septemba 29, 2025.
Wakuu wa Shule wakijaza Dodoso la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikalikuhusu taarifa za Usimamizi wa Maabara za Kemia katika mafunzo kwa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) wa Jiji la Dodoma yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Bustani, Wilaya ya Kondoa, Dodoma, Septemba 29, 2025.
Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) wakifuatilia mafunzo ya Usimamizi waMaabara za Kemia yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Bustani wilayani Kondoa,Mkoa wa Dodoma, Septemba 29, 2025.
Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Kati, Magdalena Mtenga (watatu kulia, Mstari wa Mbele), akiwa pamoja na viongozi waWakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) kutoka wilaya za Dodoma, Chemba, Bahi, Chamwino, Kondoa DC, Kondoa TC, Kongwa na Mpwapwa baada ya mafunzo ya Usimamizi wa Maabara za Kemia katika Mkoa wa Dodoma yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Bustani Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma, Septemba 29, 2025.


Share:

MAMBO 20 NILIYOYAONA KWA DK.SAMIA TUKIJIANDAA KWENDA KUTIKI OKTOBA 29


Na Said Mwishehe, 

01:KAMPENI zinaendelea kushika kasi na mgombea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anaendelea kuchanja mbuga,ameshakwenda mikoa karibia 16 mpaka sasa.

02:Tayari ameshapita katika mikoa ya Dar es Salaam ,Morogoro, Dodoma,Songwe,Mbeya,Njombe,Iringa, Singida,Tabora,Kigoma,Zanzibar,Ruvuma,Lindi,Mtwara,Pwani ,Tanga na leo Kilimanjaro.

03:Kote ambako mgombea Urais amefanya mikutano mikubwa na midogo,amefanya mikutano ya barabarani ambayo iliandaliwa kwa ajili ya kuzungumza na wananchi na kisha kueleza yaliyofanywa katika kipindi cha miaka mitano na mipango ya Serikali katika miaka mitano ijayo.

04:Pamoja na hayo kazi kubwa ambayo Dk.Samia Suluhu Hassan anayoifanya katika mikutano ya kampeni ni kuinadi Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030 pamoja na kuomba kura kwa watanzania ili apate ridhaa ya kuwatumikia katika miaka mitano ijayo.

05:Katika kampeni za mgombea Urais Dk.Samia moja ya jambo kubwa ambalo nimeliona ni jinsi ambavyo watanzania wanavyompenda,wanaonesha upendo wa kweli.Watanzania wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika mikutano yake na muda wote wanaona kuna na tabasabu usoni na moyoni.

06:Zipo sababu ambazo zinawafanya Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mikutano yake ya kampeni na moja ya sababu ni kwamba Dk.Samia Suluhu Hassan amegusa maisha ya wananchi ,amegusa makundi yote,amegusa sekta sekta zote. Kwa kifupi amegusa maisha ya Watanzajia wote na mimi ni miongoni kwao.

07: Katika miaka miaka minne na nusu ya Dk.Samia Suluhu Hassan kuwa madarakani amegusa maisha ya wakulima wa Taifa hili,kupitia mfumo wa ruzuku katika pembejeo za kilimo wakulima wanaona maisha yao yalivyobadillika.

08:Wakulima wameongeza uzalishaji katika mazao ya chakula na biashara.Kwa Afrika Tanzania inashika nafasi ya pili kwa uzalishaji mahindi na hayo ni matokeo ya mfumo wa ruzuku ambao umeenda kubadilisha maisha ya wakulima wa Taifa hili. Ukienda katika mazao kama mbaazi,korosho,kahawa,chai na mahindi wakulima wanalima kwa kujinafasi.

09:Dk.Samia katika miaka minne na nusu ya uongozi wake amegusa maisha ya watoto wa Taifa hili na hapa nazungumzia mpango wa Serikali wa kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita.

10:Serikali ya Rais Samia imebeba jukumu la kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyobora bila kulipa. Kwa elimu ya Vyuo Vikuu, Serikali imeendelea kutoa fedha za mkopo kwa wanafunzi elimu ya juu. Ndio maana wanasema Oktoba 29,2025 wanatiki kwa Samia

11:Ukitaka kujua mgombea Urais kwa tiketi ya CCM amegusa maisha ya watanzania wa makundi mbalimbali zungumza na wafugaji na wakulima ambao walikuwa na migogoro ya ardhi kwa ajili ya kulima na kufuga lakini Dk.Samia amemaliza, migogoro haisikiki tena na kama ipo ni ile inayozungumzika. Sio migogoro ya kushikiana mapanga.Ndio maana wafugaji wanasema watatiki kwa Samia ifikapo Oktoba 29.

12:Katika kipindi cha uongozi wake Dk Samia amefungua milango kwa wananchi kunufaika kupitia rasilimali zilizopo nchini kwa kutekeleza miradi ya kimkakati kama ujenzi wa reli ya kisasa, madaraja, barabara na upanuzi wa bandari za maziwa makuu na baharı.

13:Dk. Samia katika mikutano yake ya kampeni ameendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kutunza amani na utulivu nchini jambo ambalo ndivyo msingi wa maendeleo

14: Siyo hivyo tu kwakuwa ni kiongozi mwenye kuwajali wananchi, ameendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa matumizi ya kupikia ili kulinda afya za wananchi hususan wanawake.

15. Dk. Samia katika uongozi wake ameamua kumtua mama ndoo kichwani na mpango huo utekelezaji wake unafanyika kwa vitendo kupitia miradi mbalimbali ya maji, upatikanaji huduma hiyo kwa nchi nzima umefika zaidi ya asilimia 80

16: Pamoja na yote Dk.Samia Suluhu Hassan ni kiongozi ambaye Mungu amemjalaalia karama ya utu. Ni kiongozi anayeamini katika utu wa mtu ,heshima na kujali na ndio maana katika uongozi wake thamani ya utu wa mtu imepewa nafasi kubwa. Katika uongozi wake hata waliokuwa wamenyimwa haki zao kama kupanda madaraja na kupandishwa mishahara leo wanafufahia.Nao wanasema kwa kulipa Utu huo watatiki Oktoba 29.

17: Kuna mambo yanavutia kwa Dk.Samia pamoja na kuomba ridhaa lakini katika mambo ambayo amekuwa akiyazungumza kwa msisitizo ni mipango yake katika miaka mitano ijayo katika kuhakikisha watanzania wa hali ya kiuchumi nao wanapata hali bora za kiuchumi.Anasema yeye haongozi Wa tanzania wanyonge bali Watanzania wanaoweza kushiriki kikamilifu katika kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

18.Msisitizo wa Dk.Samia kuwa atahakikisha huduma muhimu za kijamii kama maji,umeme,afya,elimu, miundombinu ya barabara pamoja na huduma nyingine za kijamii zinakwenda maeneo ya vijijini yaani kule chini kabisa.Sote tunafahamu maisha ya vijijini kwetu na lengo la Dk.Samia ni kubadilisha kabisa maisha ya vijiji vyetu,ukiona umeme na maji vijijini ujue ndio kazi inaendelea.

19: Ni wakati wa Watanzania sasa kuanza kujiandaa kwenda kupiga kura ifikapo Oktoba 29 mwaka huu na hapa msisitizo wangu sote tuende kutiki kwa Dk.Samia mama mwenye upendo na kubwa zaidi Muumba wa mbinga na ardhi amempa hekima,busara na maarifa.Tusiipoteze nafasi hii,twendeni tukatiki kwa Samia.

20: Jambo kubwa na la mwisho kwa leo ninaloliona kwa Dk. Samia ni ujasiri wake wa kuendeleza diplomasia ya uchumi. Katika kipindi chake amefungua milango ya Tanzania kushirikiana na mataifa mbalimbali duniani, kuimarisha uwekezaji na kuongeza ajira kwa vijana kupitia viwanda na miradi mipya.

Ni Rais anayeamini kuwa Watanzania wana haki ya kunufaika na rasilimali zao kupitia ushirikiano wa kimataifa wa haki. Hivyo Oktoba 29 wananchi wanasema wanatiki kwa Samia ili diplomasia hii iendelee kuwanufaisha.

HITIMISHO

Kwa kuangalia mambo haya 20 niliyoyashuhudia kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka yake minne na nusu ya uongozi na sasa akiwa mgombea urais kupitia CCM, hakuna shaka Watanzania wameona matunda ya kazi yake.

Amegusa kila sekta, ameweka mbele utu wa mwanadamu, ameimarisha diplomasia, ameleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii, huku akisisitiza amani na mshikamano wa Taifa.

Ifikapo Oktoba 29, ni wakati wetu wa kuthibitisha shukrani hizi kwa vitendo kwa kwenda kutitiki kwa Dk. Samia, mama mwenye busara, upendo na dira ya kulipeleka Taifa letu mbele zaidi

KWA WALE WATAKAOTIKI KWA SAMIA OKTOBA 29,2025 BASI TUWASILIANE 0713833822
Share:

RAIS SAMIA ALETA MWANGA WA ELIMU KWENYE VIJIJI KAHAMA

 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu akimshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha Manispaa ya Kahama kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ya elimu

Muonekano wa madarasa ya shule ya sekondari ya Amali Lowa

Na Neema Nkumbi – Kahama


Ni sauti zilizobeba furaha na shukrani, Sauti za baraka baada ya wananchi wa Kahama kuhakikishiwa kesho yenye mwanga wa elimu bora na mafanikio.


Hii ni ishara ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuwaletea wananchi maendeleo.


Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, utekelezaji wa ilani umejidhihirisha katika sekta za Elimu, Afya, Maji, Barabara, Masoko, Nishati pamoja na utoaji wa mikopo kwa Vijana, Wanawake na Wenye Ulemavu.


Sekta ya Elimu: Ndoto zinazotimia


Moja ya mafanikio makubwa ni ujenzi wa shule mpya, zikiwemo Shule ya Sekondari Amali Lowa na Wendele, zilizopunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kufuata elimu.


Shija Butemi, mwanafunzi wa Amali Lowa, anakumbuka changamoto walizopitia kabla ya shule hiyo kujengwa:


“Mwanzoni tulisoma Sekondari ya Nyandekwa, Tulikuwa tunapata tabu kubwa, hasa sisi wasichana, Mara nyingi tulitembea kwa miguu, na wakati mwingine tulilazimika kuomba msaada kwa bodaboda ambao walituuliza ‘mnatupa nini?’ Hali hii ilisababisha baadhi ya wenzetu kushawishika vibaya na kuishia kupata mimba, Tunamshukuru Rais Samia kwa kutujengea shule ya karibu, sasa tunafika mapema na masomo yamekuwa rahisi.”


Kephline Ezekiel, mwanafunzi wa Sekondari ya Wendele, anaongeza:


“Awali tulikuwa tukisafiri kutoka kijiji cha Tumaini hadi Sekondari ya Ngogwa, umbali mrefu uliotusababisha uchovu na kushuka ufaulu, Shule hii mpya imetupunguzia changamoto hizo, Naomba wazazi waache kuwazuia watoto wao waende shule; elimu ndiyo urithi wa kweli.”


Shija Bundala, mwanafunzi mwingine wa Amali Lowa, pia anawataka wenzake walioacha shule kwa sababu ya umbali warejee sasa kwa kuwa shule ipo jirani.


Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Shule ya Amali Lowa, Mwalimu Ezekia Ngabo, anasema shule hiyo ilianza rasmi Julai 28, 2025 ikiwa na wanafunzi 47 (wavulana 13 na wasichana 34) na walimu 9 pamoja na mlinzi mmoja.




“Shule hii ina mikondo miwili: wa jumla na wa amali (elimu ya vitendo), Kupitia mkondo wa amali, hasa somo la kilimo, tunawajengea wanafunzi stadi za maisha zitakazowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.”




Mtazamo wa Viongozi


Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, anabainisha kuwa mafanikio haya ni matunda ya ushirikiano kati ya Serikali Kuu na Halmashauri:




“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuwekea mazingira bora ya ukusanyaji mapato na kutupatia fedha za maendeleo. Tulipokea zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za Wendele na Amali Lowa, zikiwa na madarasa, jengo la utawala, maabara na vyoo, Ujenzi umekamilika na wanafunzi wameanza kusoma, Huu ni ushahidi wa dhamira ya serikali kuwekeza kwenye elimu bora.”


Masudi ameongeza kuwa miradi mingine ya maendeleo katika sekta za afya, barabara na maji imeendelea kuipamba Manispaa ya Kahama, na kuimarisha ustawi wa wananchi.


Hitimisho


Wananchi wa Kahama sasa wananufaika moja kwa moja na miradi ya elimu, afya, na miundombinu, matunda ya Ilani ya CCM na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita.


Changamoto bado zipo, kama vile mahitaji ya walimu na vifaa vya kisasa vya kujifunzia, lakini matumaini yamejengeka, Ndoto za watoto wa vijijini kupata elimu bora sasa zinageuka kuwa uhalisia.


Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa amani na utulivu ili miradi ya maendeleo iendelee.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu akimshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha Manispaa ya Kahama kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ya elimu
Muonekano wa madarasa ya shule ya sekondari ya Amali Lowa
Muonekano wa madarasa ya shule ya sekondari Wendele
Wanafunzi shule ya sekondari Wendele wakiwa darasani
Shija Butemi mwanafunzi wa Amali Lowa, akiishukuru selikali ya Rais Samia kwa kuwajengea shule karibu na maeneo ya nyumbani kwao
Wanafunzi shule ya sekondari Wendele wakiwa darasani

Wanafunzi shule ya sekondari Wendele wakiwa darasani
Share:

Monday, 29 September 2025

MENEJA TRA WILAYA YA BAHI ASISITIZA USAJILI WA TIN NA MALIPO YA KODI AWAMU YA TATU




Na. Yahya Saleh-Bahi

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Bw. Emmanuel Nyeme amewataka Wafanyabiashara na Walipakodi kwa ujumla ambao hawajasajiliwa kufanya hivyo kwani ni kinyume cha sheria kufanya biashara bila kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).


Pia, amewakumbusha kulipa malipo ya kodi ya awamu ya tatu kabla ya tarehe 30 Septemba, 2025.

Hayo ameyazungumza leo Jumatatu tarehe 29.09.2025 wakati wa zoezi la elimu ya kodi mlango kwa mlango katika Wilaya ya Bahi.

"Ni kinyume cha sheria kufanya biashara bila ya kuwa na Nambari ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN)", alisema Bw. Nyeme.

Aidha, amewasisitiza wafanyabiashara kutoa Risiti za kielektroniki kwa wateja wao pale wanapofanya manunuzi huku akiwahimiza wananchi nao kudai risiti pale wanaponunua bidhaa au huduma kutoka kwa Wafanyabiashara.

Kwa upande wao Wafanyabiashara Wilayani Bahi waliotembelewa katika zoezi hilo, wameipongeza TRA kwa kuja na kampeni hiyo huku wakiomba zoezi hilo liwe endelevu.
Share:

DKT.YONAZI :TUIMARISHE LISHE,TUPUNGUZE MAGONJWA SUGU




NA. MWANDISHI WETU - DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amewataka wadau kushirikiana na Serikali katika kuimarisha hali ya lishe nchini ili kupunguza kasi ya kuenea kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.


Amesema ulaji usio faa na mitindo mibaya ya maisha vimechangia kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza jambo linalohatarisha maendeleo ya Taifa.




Dkt. Yonazi ameyasema hayo jijini Dar es salaam leo 29 Septemba, 2025 katika Mkutano Mkuu wa 11 wa Wadau wa Lishe unaoendelea katika kituo cha mikutano cha APC Bunju.



Dkt. Yonazi amesema tafiti zinaonesha kuwa uzito uliozidi na uliokithiri ni chanzo kikuu cha magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yakiwemo kisukari, moyo, figo na baadhi ya saratani.


“Napenda kukumbusha wadau, taasisi na wataalam kushirikiana na serikali kufanya tafiti zitakazosaidia kuleta majibu ya changamoto za lishe, pamoja na kusaidia watu kubadili tabia za ulaji na mtindo wa maisha ili kuzuia magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yanayohusiana na ulaji usiofaa na ambayo ni tishio kwa Taifa letu,”alisema Dkt. Yonazi





Dkt.Yonazi ameongeza kuwa Takwimu zinaonesha licha ya hali ya lishe nchini kuendelea kuimarika bado kuna changamoto hususani kwenye uzito uliozidi na kiriba tumbo hii kutokana maendeleo tunayoyapata na mabadiliko ya mtindo wa maisha hususani ulaji usiofaa hivyo jitihada za pamoja kati ya wadau na serikali zinahitajika ili kukabiliana na tatizo hili.




Akizungumza kuhusu mkutano huo Dkt. Yonazi amesema lengo ni kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha Mwaka wa Tatu 2024/2025 katika maeneo mahsusi yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26).


Vilevile amesema mkutano huo unatoa fursa kwa wadau wote wa lishe kujadili namna utekelezaji ulivyofanyika, changamoto na mikakati ya kufanikisha utekelezaji katika kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa mpango huo hususan mwaka 2025/26.




Kwa mujibu wa Dkt. Yonazi mkutano huo unatazamiwa kuongeza msukumo mpya wa utekelezaji wa afua za lishe miongoni mwa wadau kama moja ya nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.




“Uwepo wenu hapa, ni uthibitisho tosha wa ushirikiano mlionao na utayari wenu katika kuhamasisha uboreshaji wa hali ya lishe kwa Watanzania, hususani makundi yanayoathirika zaidi ambayo ni watoto wadogo na wachanga, watu wenye mahitaji maalum, wanawake wajawazito na wale walio katika umri wa uzazi,”amesema Dkt. Yonazi.







Dkt. Yonazi amewashukuru wadau wote walitoa mchango wa fedha na ushauri wa kitaalamu katika kufanikisha maandalizi ya mkutano huo na amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau ili kuhakikisha Taifa linapata mafanikio dhidi ya mapambano ya tatizo la utapiamlo.







=MWISHO
=
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger