Sunday, 7 September 2025
SALMA KIKWETE AONGOZA UZINDUZI WA KAMPENI JIMBO LA MCHINGA
Na Mwandishi wetu, Rutamba-Lindi
Katika tukio lililojaza shamrashamra na hamasa kubwa ya kisiasa, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Salma Rashid Kikwete, ameongoza uzinduzi mkubwa wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Salma, ambaye pia ni Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amepokelewa kwa shangwe na mamia ya wananchi katika viwanja vya Mahakama, Kata ya Rutamba.
Uzinduzi huo ulipambwa na uwepo wa viongozi wakuu wa kitaifa, akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Pia, tukio hilo lilishuhudia uwepo wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, aliyehudhuria kutoa baraka zake kwa mgombea na kuhakikisha mshikamano ndani ya chama unaimarishwa katika kuelekea uchaguzi huo muhimu.
Katika hatua ya kilele ya uzinduzi huo, Mhe. Salma Kikwete alipokea rasmi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 kutoka kwa Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, madiwani wote wa Jimbo la Mchinga walikabidhiwa nakala za Ilani hiyo huku wakihimizwa kuwa bega kwa bega na Mbunge ajaye katika utekelezaji wa miradi na sera zilizomo.
Akihutubia wananchi waliohudhuria, Waziri Mkuu Majaliwa aliwahakikishia kuwa Serikali ya CCM itaendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi wa Mchinga kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi inatekelezwa kwa ufanisi ili kuinua maisha yao na kuleta maendeleo endelevu kwa jimbo zima.
Uzinduzi huo unaashiria mwanzo wa kampeni zenye mvuto, mshikamano na matumaini makubwa kwa wananchi wa Mchinga, huku wakionesha imani kubwa kwa CCM na wagombea wake.
TANZANIA NA OMAN KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Hashil Abdalah amesema ujio wa ujumbe wa wafanyabishara kutoka nchini Oman utazidi kuitangaza Tanzania kimataifa hususani katika sekta ya viwanda na biashara hali itakayoongeza wawekezaji kutoka nje ya Tanzania Dkt Abdallah ameyasema Septemba 07, 2025 wakati wa Ziara ya Ujumbe huo katika Kiwanda cha Union Meat Group kinachojihusisha na uchakataji wa nyama ya mbuzi na kondoo pamoja na Kongani ya Viwanda ya Kasasa (KAMAKA ) vilivyopo Mkoani Pwani.
Naye, Mjumbe wa Baraza la Nchi na Mwenyekiti wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Oman Mkoa wa Al Wusta na Kiongozi wa Ujumbe huo Dkt. Salem bin Salim Al-Junaibi amesema ujumbe huo ulivutiwa na kufurahishwa na uwezo wa Kiwanda cha Union Meat kwa kuzingatia viwango vya juu kutoka kwenye usafi na weledi wa wafanyakazi hadi uzingatiaji wa viwango vya Halal.
"Ushirikiano huu unakuja kwa wakati unaofaa, tunapobadilisha uchumi wetu na kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji wa kimkakati katika vifaa, bandari, kilimo, utalii, nishati pamoja na usalama wa chakula." Bw. Al-Junaibi alisema
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe kutoka Oman Bw. Zahran Al Aras ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kuahidi kuendelea kununua nyama kutoka Tanzania kwa kuwa ina radha nzuri. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bi Mariam Gw'hwani ameuhakikishia ujumbe huo Kuwa Union Meat itaendelea kuzingatia viwango vya kimataifa vya afya, usafi, na utii wa Halal na kuwa Kiwanda chake kina uwezo wa kuchinja na nyama ya mbuzi na kondoo 3500 wanachinjwa kiwandani hapo kwa siku na
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa chemba ya wafanyabiashara wenye viwanda na wakulima nchini TCCIA Bw. Oscar Kissanga amesema faida ya ujio wa ujumbe huo nchini kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo na Kuwa taasisi yake iko tayari kutumia fursa zitakazotokana na uhusiano huo. Ujumbe huo wa wafanyabishara zaidi ya 15 umetembelea pia eneo la uwekezaji wa viwanda la KAMAKA lililopo Kibaha Pwani huku ukitarajiwa kuwepo nchini kwa siku tano na kutembelea miradi mbalimbali.












