Friday, 5 September 2025

KIKAO CHA 19 CHA KAMATI YA MIFUKO NA PROGRAMU ZA UWEZESHAJI WAFANYIKA ARUSHA


Kikao cha 19 cha Kamati ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kimefanyika Mkoani Arusha katika ukumbi wa VETA-Njiro kikihusisha wajumbe kutoka taasisi mbalimbali.

Kikao hicho kimekusudia kujadili maendeleo ya mifuko na programu za uwezeshaji hapa nchini ikiwemo mifuko inayotoa mikopo, dhamana, ruzuku pamoja na programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Washiriki wa kikao hiki ni wajumbe wote wa kamati hiyo, waratibu wa mifuko na programu za uwezeshaji pamoja na wataalam wa TEHAMA.

Katika kikao hicho, wajumbe walipata pia fursa ya kuona Mfumo Jumuishi wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji (National Empowerment Management Information System – NEMIS).
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA SEPTEMBA 5,2025






Magazeti








Share:

Thursday, 4 September 2025

MAVUNDE AWEKA WAZI MIKAKATI YA KUIPAISHA MTUMBA KIUCHUMI


Na Alex Sonna,Dodoma

Katika jitihada za kuboresha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo ya kweli, Mhe. Anthony Mavunde ameahidi kuibadilisha sura ya Jimbo la Mtumba endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.

Akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni Dodoma Mavunde alisema kuwa anahitaji ridhaa ya wananchi wa Jimbo hilo ili aweze kuwatumikia kwa ufanisi zaidi kwa sababu yeye ni mtumishi wa watu, na anaelewa kwa undani kero na changamoto zinazowakabili.

Amesema moja ya malengo yake makuu ni kuhakikisha Mtumba inageuka kuwa mji wa kisasa unaong'aa, hasa kwa kuzingatia kuwa Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 600.

Ameongeza kuwa Kupitia mpango huu, Mavunde anataka kuona Mtumba inakuwa kitovu cha maendeleo na huduma bora kwa wakazi wake.

Katika sekta ya elimu, Mavunde amekuwa mstari wa mbele. Tayari amejenga shule mbalimbali zikiwemo Shule ya Msingi Chiwondo, Mkoyo na Mahomanyika Sekondari.

Ameahidi kwamba endapo atapata nafasi ya kuwa mbunge, atahakikisha kila eneo lenye upungufu wa shule linapatiwa shule ili watoto wote wapate haki ya msingi ya elimu. Kwa sasa ujenzi wa Shule ya Chawha unaendelea, hatua inayodhihirisha dhamira yake ya kuboresha elimu.

Mavunde pia amegusia changamoto ya michango ya mitihani ya Jumamosi, akisema kuwa atahakikisha michango hiyo inaondolewa ili kupunguza mzigo kwa wazazi.

Aidha, amesema kuwa atahakikisha barabara ya Hombolo – Mayamaya pamoja na barabara nyingine za ndani katika mitaa mbalimbali ambazo ni korofi, zinatengenezwa. Ameahidi kununua greda maalum litakalotumika kuimarisha barabara hizo mara kwa mara.

Katika sekta ya maji, Mavunde amesema kuwa uwezo wa kuzalisha maji jijini Dodoma umefikia lita milioni 47 kwa siku na kueleza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kata zote ikiwemo Hombolo, Ihumwa, na Mahomanyika zinapata huduma ya maji safi na salama.

Ameahidi kuwa huduma hiyo itatolewa bure kwa baadhi ya maeneo yenye uhitaji mkubwa kama njia ya kupunguza gharama kwa wananchi.

Baadhi ya wananchi wa Jimbo la Mtumba wamezungumza na Mzalendo Blog kuwa Mavunde anaonekana kuwa na maono makubwa kwa Jimbo lake, akilenga kuboresha miundombinu, huduma za kijamii na uchumi wa wananchi.
Share:

KWAHERI KADALA KOMBA: MWANDISHI, MWALIMU NA MTETEZI WA JAMII






Taifa limepoteza nguzo muhimu ya mawasiliano na maendeleo ya jamii kufuatia kifo cha mwanahabari mashuhuri wa Dodoma, Kadala Komba, ambaye alikuwa akiishi wilayani Bahi, mkoa wa Dodoma.

Kadala amefariki dunia jana, tarehe 3 Septemba 2025, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Mwili wake unasafirishwa leo kuelekea mkoani Mbeya kwa ajili ya maziko yatakayofanyika nyumbani kwao, ikiwa ni heshima ya mwisho kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya habari na maendeleo kwenye jamii.

Kadala Komba alikuwa ni miongoni mwa waandishi waliotoa mchango mkubwa katika kuripoti taarifa zenye mwelekeo wa kuelimisha, kuhabarisha na kuhamasisha maendeleo, hasa katika maeneo ya vijijini.

Akiwa mwandishi huru aliyejikita zaidi katika wilaya ya Bahi, alifanya kazi na vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya mkoa, vikiwemo Dodoma FM, Shine News Blog, na miradi ya kijamii kama vile “TAKUKURU Rafiki”.

 Kupitia kazi yake, alijizolea heshima kama sauti ya wasio na sauti, akisimamia ukweli na uwajibikaji katika utumishi wa umma na maendeleo ya wananchi.

Zaidi ya kuwa mwandishi, Kadala alikuwa pia mhamasishaji kijamii na mtetezi wa uwazi, hasa katika usimamizi wa miradi ya jamii, elimu na afya.

Mojawapo ya makala zake zilizowahi kusambaa sana ilikuwa kuhusu matumizi ya teknolojia ndogo katika kilimo cha karanga na mtama, ambapo aliangazia mafanikio ya wakulima wa Bahi waliotumia zana za kisasa kuboresha mavuno.

Aliamini kuwa habari ni chombo cha mabadiliko, na alitumika vyema kuonesha matumaini ya Tanzania ya vijijini.

Katika mitandao ya kijamii, Kadala alikuwa na ushawishi mkubwa, hasa katika majukwaa ya Facebook na WhatsApp, alikokuwa mstari wa mbele kushirikisha taarifa za haraka kuhusu shughuli za kijamii, kampeni za afya, elimu na haki za wananchi.

Alitumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kuhamasisha watu kujitokeza katika mijadala ya maendeleo, na kuwashauri vijana kuhusu nafasi ya uandishi katika kujenga taifa.

Watu waliomfahamu wanamuelezea Kadala kama mtu mnyenyekevu, mwenye maono, aliyejitolea kwa hali na mali kwa ajili ya jamii yake.

Baadhi ya wana tasnia ya habari wanasema alikuwa kielelezo cha uandishi wa kiadili na wa maadili.

“Kadala alikuwa si tu mwandishi, bali mwalimu kwetu, kila taarifa yake ilikuwa na mafunzo,” alisema mwandishi mwenzake wa Dodoma FM.

Mwili wa marehemu unasafirishwa leo mchana kuelekea Mbeya, nyumbani kwao, ambako shughuli za maziko zinatarajiwa kufanyika kesho tarehe 5 Septemba 2025.

Familia, marafiki, wanahabari na wananchi kwa ujumla wanatarajiwa kujumuika kumpa heshima ya mwisho mtu aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kuwahabarisha, kuwaelimisha na kuwatetea wengine.



Imetayarishwa na Dotto Kwilasa
Tarehe: 4 Septemba 2025
Chanzo: Taarifa kutoka kwa familia, mitandao ya kijamii na kumbukumbu za vyombo vya habari.



Share:

MAVUNDE AZINDUA KAMPENI KWA KISHINDO, AAHIDI KUIGEUZA MTUMBA KUWA MJI WA KISASA



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Mwanasiasa na mtumishi wa watu, Anthony Mavunde, amezindua rasmi kampeni zake za kugombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kwa kishindo kikubwa, akiahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi, kijamii na kimazingira katika jimbo hilo endapo atachaguliwa kuwa Mbunge.

Akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi huo leo Sept. 3,2025 Mavunde amesema kuwa anaomba ridhaa ya wananchi ili aendelee kuwatumikia kwa moyo mmoja, kwa kuwa amekuwa akiishi nao, anazifahamu changamoto zao, na ana nia ya dhati ya kuzitatua.

Mavunde ameeleza kwamba Serikali inawekeza zaidi ya shilingi bilioni 600 katika ujenzi wa mji mpya wa Serikali eneo la Mtumba, jambo ambalo ni fursa ya kipekee ya kufanya Jimbo hilo kuwa la kisasa, wa kuvutia na wenye huduma bora.

Amesisitiza kuwa uongozi wake utalenga kuhakikisha maendeleo hayo yanawanufaisha wananchi wa kawaida kwa kuwawekea miundombinu na huduma bora karibu yao.

Ameeleza kuwa tayari amejenga shule kadhaa zikiwemo Shule ya Msingi Chiwondo, Mkoyo, na Mahomanyika Sekondari ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Chahwa unaendelea.

Mavunde ameahidi kuwa kila kata au mtaa usio na shule, atahakikisha unapata shule ili kuondoa changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kutafuta elimu.

Aidha, amesema atapambana kuhakikisha michango ya mitihani ya Jumamosi inaondolewa ili kuwapunguzia mzigo wazazi.

Katika kuboresha miundombinu, Mavunde ameeleza kuwa atahakikisha barabara ya Hombolo – Mayamaya pamoja na barabara nyingine za ndani zinazopitika kwa shida zinajengwa kwa kiwango bora.

Ameahidi kununua greda maalum litakalotumika kwa matengenezo ya mara kwa mara ya barabara hizo ndani ya jimbo.

Kwa upande wa huduma ya maji, Mavunde amesema kuwa uwezo wa kuzalisha maji jijini Dodoma kwa sasa umefikia lita milioni 47 kwa siku na lengo lake ni kuhakikisha kila kata ikiwemo Hombolo, Ihumwa, na Mahomanyika inapata maji safi na salama kwa urahisi.

Amesema baadhi ya maeneo yenye uhitaji mkubwa huduma hiyo itatolewa bure, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo muhimu.

Mavunde amesema kuwa ili yote hayo yatimizwe anahitaji ushindi ili aendelee kuwa mtumishi wa kweli wa watu wa Mtumba huku akiahidi utumishi wa haki, uwazi, na maendeleo kwa vitendo kwa kuweka mbele maslahi ya wananchi wake.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger