Wednesday, 3 September 2025
ABIRIA WA SAFARI ZA USIKU WAPEWA ELIMU HATARI YA KULALA CHINI YA BASI
.jpg)
Katika jitihada za kuimarisha usalama wa abiria wanaosafiri nyakati za usiku, Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga kimeanzisha kampeni ya kutoa elimu kwa abiria kuhusu hatari zinazoweza kuwapata wanapochukua hatua zisizo salama wakiwa safarini, ikiwemo tabia ya kulala chini ya basi badala ya kukaa kwenye viti walivyopangiwa.
Elimu hiyo imetolewa na Sajenti David Ndimila wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, ambaye amesisitiza kuwa kumekuwa na ongezeko la abiria wanaoamua kujilaza chini kwenye njia ya kupita ndani ya basi, hasa nyakati za usiku wanapopatwa na usingizi.
Sajenti Ndimila amefafanua kuwa kitendo hicho si tu kwamba ni kinyume na kanuni za usalama wa abiria, bali pia ni hatari kubwa kwa maisha yao.
“Kuna matukio ambapo basi linapata mtikisiko wa ghafla, iwe ni kutokana na hitilafu ya barabara au tukio la dharura la kuhitaji dereva kupunguza mwendo kwa haraka. Katika hali kama hiyo, abiria waliolala chini wako kwenye hatari kubwa ya kujeruhiwa, hasa kwa kugongwa na vitu vya ndani ya gari au kugonga sehemu ngumu kama viti au sakafu ya basi,” alieleza.
Katika kampeni hiyo, Sajenti Ndimila amezungumzia umuhimu wa abiria kufuata sheria ndogondogo za usalama barabarani ambazo mara nyingi hupuuziwa lakini zinaweza kuokoa maisha, na kusisitiza kuwa ni lazima abiria waketi kwenye viti vyao walivyowekewa na kufunga mikanda ya usalama wakati wote wa safari, bila kujali umbali au muda wa usafiri.
“Kufunga mkanda si kwa ajili ya kupendeza au kufuata mazoea, bali ni hatua ya msingi ya kujilinda dhidi ya ajali ambazo mara nyingine hutokea kwa ghafla.
Tunawaomba abiria wote wawe na uelewa na waache tabia ya kuchukulia poa masuala ya usalama barabarani,” ameongeza Sajenti Ndimila.
Aidha, ametoa wito kwa wamiliki na madereva wa mabasi kuhakikisha wanatoa elimu kwa abiria wao kabla ya kuanza safari, na kuwajibika kwa kuhakikisha kila abiria anakaa kwenye kiti na anafunga mkanda, Pia amesisitiza umuhimu wa madereva kuwakumbusha abiria kila wanapoanza safari ya usiku, kwani ni wakati ambao watu wengi hupatwa na usingizi na kufanya maamuzi yasiyo salama.
Kwa upande wao, baadhi ya abiria waliopokea elimu hiyo wamekiri kuwa hawakuwa wanatambua hatari ya kulala chini ya basi.
“Nilikuwa nafikiri kulala chini kunaongeza usingizi au kupunguza uchovu, lakini sasa nimeelewa kuwa ni hatari zaidi,” amesema mmoja wa abiria waliokuwa safarini kuelekea Mwanza.
Kampeni hiyo inaendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga na imepokelewa kwa mikono miwili na wadau wa usafiri, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa kupunguza ajali za barabarani na kulinda maisha ya watumiaji wa vyombo vya usafiri.

NAIBU WAZIRI CHUMI ASHIRIKI SHEREHE ZA KUADHIMISHA MIAKA 80 YA UHURU VIETNAM
MADEREVA WA SERIKALI WATAKIWA KUDUMISHA NIDHAMU NA WELEDI KAZINI
Tuesday, 2 September 2025
MIKAKATI UDHIBITI UPOTEVU WA MAJI CHALINZE YAWA DHAHIRI
TBS YAENDELEA KUWATAHADHARISHA WANANCHI KUHUSU BIDHAA HAFIFU
Monday, 1 September 2025
VITONGOJI 1,997 SAWA NA 88.4% VIMEPATIWA HUDUMA YA UMEME KILIMANJARO





























































