Saturday, 5 July 2025
Friday, 4 July 2025
SINGIDA YAANDIKA HISTORIA:TRILIONI 1 7 ZAFUNGUA MILANGO YA MAENDELEO
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Mkoa wa Singida umeandika historia mpya ya maendeleo kwa kutumia zaidi ya shilingi trilioni 1.72 katika kipindi cha miaka mitano (2020/21–2024/25), fedha ambazo zimetumika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, elimu, afya, miundombinu na utawala bora.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 4, 2025 jijini Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa kupitia fedha kutoka Serikali Kuu, mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na michango ya wadau wa maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 1.055 zilitolewa na Serikali Kuu moja kwa moja, huku utekelezaji wa bajeti kwa kipindi hicho ukiwa wastani wa asilimia 95.
“Kuongezeka kwa rasilimali fedha kumewezesha Singida kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia ajira, kipato na upatikanaji wa huduma bora, hususan katika sekta ya kilimo ambacho kinategemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa mkoa wetu,” ameeleza Dendego.
Amebainisha kuwa katika kipindi hicho pato la ndani la mkoa (Regional GDP) limeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.709 mwaka 2020/21 hadi trilioni 3.398 mwaka 2024/25, hali ambayo imeongeza pia pato la mtu mmoja kutoka shilingi 1,588,604 hadi 1,710,562. Aidha, mapato ya ndani ya Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoani humo yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 150, kutoka shilingi bilioni 11.9 hadi bilioni 30, huku mapato ya halmashauri yakipanda kutoka bilioni 14.6 hadi 24.8.
Katika sekta ya kilimo na ufugaji, mkoa umefanikiwa kujitosheleza kwa chakula kwa kuongeza uzalishaji kutoka tani 649,850 hadi tani 1,325,201 kwa mwaka, huku usajili wa wakulima kupitia mfumo wa M-Kilimo ukiongezeka kwa asilimia 289, kutoka wakulima 75,398 hadi 293,385.
Pia matumizi ya pembejeo bora yameimarika ambapo matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 1,772 hadi tani 7,948, sawa na asilimia 348.4, na matumizi ya mbegu bora yakiongezeka kwa zaidi ya asilimia 123. Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 81 kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji, ambapo hekta 17,437 kati ya hekta 48,619 zinazofaa tayari zinatumika kupitia skimu rasmi 24.
MAZINGIRA WEZESHI YAFUNGUA FURSA MPYA ZA UWEKEZAJI TAWA
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta mbalimbali, hususan sekta ya utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa TAWA, Bw. Beatus Maganja, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.
“Tunawaambia Watanzania na wawekezaji wote kwa ujumla kuwa TAWA ni mahali sahihi kwa uwekezaji, unapotaka kuwekeza unakaribishwa sana. Ikumbukwe kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa mazingira wezeshi Kwa wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi yetu ” alisema Maganja.
"Kama alivyofanya Mhe. Rais na sisi tunamuunga mkono Kwa kuhakikisha kwamba fursa hizi zinakuwa wazi Kwa wawekezaji wote na ndio maana tuko hapa kuwatangazia waje kuwekeza katika hii taasisi" amesisitiza Afisa Habari huyo.
Aidha Maganja ameongeza kuwa TAWA inasimamia maeneo yenye rasilimali adimu, vivutio vya kipekee, na mandhari ya kuvutia ambayo yanatoa fursa kubwa ya uwekezaji endelevu kwa maslahi ya taifa na uhifadhi wa maliasili.
Bw. Maganja alitaja baadhi ya maeneo yaliyo tayari kwa uwekezaji kuwa ni Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park (Arusha), Wami-Mbiki (Morogoro), Mpanga/Kipengere (Mbeya na Njombe), Tabora ZOO, Ruhila ZOO na maeneo mengine mengi yenye fursa mbalimbali.
Kwa upande wake, Afisa Mhifadhi Mkuu kutoka TAWA, Dkt. Gladson Mlay, aliwahamasisha wananchi kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho hayo, ambapo wanaweza kujionea wanyamapori hai wakiwemo simba, chui, fisi, mamba na spishi mbalimbali za ndege.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaalika wananchi kuonja na kununua kitoweo cha nyamapori choma kilichoandaliwa kwa umahiri, akisema kuwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha matumizi ya rasilimali za maliasili kwa njia endelevu.
“Kwa wale ambao wanasema hawajawahi Kula nyamapori choma, nyama hiyo ipo hapa, mishikaki pia ipo na nyama ya kupeleka nyumbani nyumbani, "alisema Dkt. Mlay
NGOs ZACHANGIA MIRADI YA MAENDELEO JUMUISHI ILIYOGHARIMU BILIONI 30 MOROGORO
Wawakilishi wa Asasi za Kirai wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufanyika mkutano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Morogoro.Mkutano uliandaliwa na NaCongo kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Morogoro.Picha na Peter Kimath
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Mh.Adam Malima akiongea na asasi za kiraia katika Mkutano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Morogoro.
**
MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali mkoani Morogoro kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa huo yametekeleza miradi ya maendeleo jumuishi iliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 30 kwa kipindi cha miaka mitano hadi kufikia 2024/2025.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Mkoa wa Morogoro, Otanamusu Nicholaus alisema hayo katika mkutano wa tathmini ya mchango wa Mashirika hayo katika maendeleo ya taifa mkoani humo.
Nicholaus alisema mkutano mwaka huu ulibeba mada kuu ni “Tathmini ya mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya Taifa 2020/2021- 2024/25, mafanikio, changamoto,fursa na matarajio”.
Nicholaus alisema fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi ya maendeleo jumuishi, kwa kuzingatia sheria, miongozo na taratibu za nchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya hususani kampeni za chanjo.
Pia elimu ya afya ya uzazi na mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, elimu ikiwemo uboreshaji wa madarasa ya awali, mafunzo kwa walimu na uandaaji wa vifaa vya kujifunzia.
Alitaja miradi mingine ni uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji miti , uhifadhi wa vyanzo vya maji, uwezeshaji wa vijana na wanawake kiuchumi, kupinga ukatili wa kijinsia, utekelezaji wa haki za binadamu, na miradi ya maji safi ikiwemo ya uchimbaji wa visima katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Mwenyekiti wa Mashirika hayo mkoa wa Morogoro alisema katika kipindi cha miaka hii mitano, zaidi ya mashirika 150 yameweza kufanya kazi na kuwasilisha taarifa kwa vipindi tofauti vya kuanzia miezi sita hadi miaka sita ya mikataba ambapo mikataba huombwa upya kila baada ya mwaka.
“Mashirika haya yameendelea kushirikiana kwa karibu na Halmashauri zetu katika kutekeleza mikakati ya maendeleo kwa kushirikisha jamii, huku yakitoa mchango mkubwa katika kuinua maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa mkoa wetu” alisema Nicholaus.
Alisema mafanikio hayo yanadhihirisha kuwa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali ni mshirika wa kweli wa Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Nicholaus alisema mkoa huo una jumla ya NGOs 571 zilizosajiliwa na kutambuliwa na Serikali, pia mashirika 11 yamesajiliwa kimataifa, 457 kitaifa, 16 kimkoa na 24 katika ngazi ya Wilaya.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa huyo Malima,aliwataka wadau wa wote wa mashirika hayo kushiriki kikamilifu katika kuchochea maendeleo ya mkoa huo kiuchumi, kijamii, kielimu na kisiasa badala ya kushiriki kwenye shughuli zinazochochea mgawanyiko na uvunjifu wa amani.
Hivyo aliyatahadharisha mashirika yanayojihusisha na vitendo vinavyohatarisha amani na utulivu ndani ya mkoa huo, hasa kipindi kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 na yanayokwenda kinyume na maadili, mila, na desturi za wananchi wa mkoa huo hazitavumiliwa kamwe.
Naye Mkurugenzi wa Agriwezesha, Deogracia Ignas, alisema shirika lake linaendelea kushirikiana na Serikali kwa kugawa miche ya mazao ya mikakati ikiwemo ya parachichi kwa wakulima hatua ambayo inayochochea maendeleo ya sekta ya kilimo na kuhakikisha amani inaendelea kudumu.
FCC YATOA ELIMU KWA WANANCHI KATIKA MAONESHO YA 49 YA SABASABA

Tume ya Ushindani (FCC), imeendelea kutumia fursa ya Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) kwa kutoa elimu kwa Umma ambao ndio walaji au watumiaji wa bidhaa na huduma.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu "Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania", yameanza tarehe 28 Juni na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 13 Julai, 2025.
Wananchi mbalimbali wameendelea kujitokeza na kutembelea banda la FCC ambapo wamenufaika kwa kupata elimu zaidi inayohusu masuala ya Ushindani, Udhibiti wa Bidhaa Bandia na Kumlinda Mlaji kutoka kwa watumishi wa FCC.
Thursday, 3 July 2025
MKUU WA SOKO KUU ARUSHA AJITOSA UBUNGE JIMBO LA LUDEWA

Katika hatua za mwisho za mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkuu wa Soko Kuu la Arusha, Ndugu John Haule, amejitokeza kuchukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea Ubunge wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe.
Haule amefika katika Ofisi za CCM Wilaya ya Ludewa Julai 2,2025 ambapo amesema amepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Katibu wa CCM Wilaya pamoja na viongozi wengine wa chama.
"Ushirikiano nilioupata umenipa moyo zaidi, na ninayo nia ya dhati kulitumikia Jimbo la Ludewa kwa weledi na uzalendo," amesema Haule.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2022, Ndugu John Haule aliwahi pia kuonesha nia ya kugombea Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Wednesday, 2 July 2025
SAKALA AINGIA KWENYE KINYANG'ANYIRO UDIWANI KATA YA MJINI - SHINYANGA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana UVCCM wilaya ya Shinyanga Mjini Abdulaziz Said Sakala (kulia)akikabidhi Fomu ya Udiwani Kata ya Mjini,kwa Katibu wa CCM Kaya hiyo Rashid Abdalla.
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) wilaya ya Shinyanga Mjini Abdulaziz Said Sakala,amerejesha Fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea Udiwani Kata ya Mjini kwenye uchaguzi Mkuu 2025.
Amerudisha Fomu hiyo leo Julai 3,2025, kwenye Ofisi za Chama Cha Mapinduzi CCM Kata ya Mjini.
Akizungumza mara baada ya kurudisha Fomu hiyo,amesema akipata ridhaa ya kuwa Diwani atawaletea maendeleo wananchi,na kwamba mengi atayazungumza pale jina lake litakapoteuliwa.
"Katika uchaguzi huu,nafarijika kuona vijana wengi wamejitokeza Kugombea nafasi ya Udiwani na Ubunge, na pia nakishukuru Chama changu kwa kudumisha demokrasia," amesema Sakala.
MC MAMA SABUNI ACHUKUA FOMU KUGOMBEA UDIWANI VITI MAALUM KATA YA IBADAKULI

Na Mwandishi wetu Malunde 1 Blog
Mshereheshaji Maarufu wa matukio mbalimbali na Mshindi wa tuzo ya MC Bora Mwanamke kinara Kanda ya ziwa Anascholastica Mathew Ndagiwe maarufu kama MC Mama Sabuni amechukua fomu kuwania nafasi ya Udiwani wa Viti Maalum kupitia chama cha Mapinduzi katika kata ya Ibadakuli manispaa ya Shinyanga kwenye uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mc Mama Sabuni amechukua fomu hiyo mapema leo Julai 02, 2025 katika ofisi za Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini.
DKT. YONAZI ATOA WITO KWA WATUMISHI KUJENGA TABIA YA KUJIFUNZA ILI KUIMARISHA UWAJIBIKAJI SERIKALINI
Na mwandishi wetu, Dodoma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, amewataka watumishi wa umma kujenga tabia ya kujifunza kwa bidii ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Dkt. Yonazi ametoa wito huo leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa PEPMIS yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Ngome.
Akihimiza dhana ya kujifunza kwa kushiriki kikamilifu, Dkt. Yonazi alinukuu kauli maarufu ya Benjamin Franklin isemayo: “Niambie nisahau, nifundishe nitakumbuka, nishirikishe nijifunze.”
Alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa kila mmoja akisema: “Tuchukue sehemu ya tatu ya kauli hiyo kwa sababu tunachohitaji ni kujihusisha ili tuweze kujifunza zaidi na kuimarisha utendaji wetu.”
Aidha, Dkt. Yonazi aliwataka watendaji wote kuchangamkia fursa hiyo ya mafunzo ya PEPMIS ili kupata maarifa mapya yatakayosaidia katika kutathmini na kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku.
Kwa upande wake, Bw. Mutani Josephat Manyama – Mkufunzi wa Kitaifa wa Mfumo huo kutoka Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuwajengea uwezo watumishi wa umma kuhusu utekelezaji na tathmini ya utendaji kazi wao.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha viongozi na wasimamizi kufanya tathmini sahihi ya watendaji, jambo litakalosaidia maamuzi bora ya kiutumishi na kuongeza tija katika utumishi wa umma.
Tuesday, 1 July 2025
MIRADI SABA YA BILIONI 2.4 YAZINDULIWA TANGA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA AJIRA KWA VIJANA NA WATOTO
Na Hadija Bagasha Tanga,
Changamoto ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ulawiti na ajira kwa vijana Mkoani Tanga inakwenda kupatiwa ufumbuzi baada ya ujio wa miradi mikubwa saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.4.
Shirika la Botner Foundation la Nchini Uswis limetoa zaidi ya shilingi bilioni 2.4 kwajili ya ufadhili wa miradi saba ikiwemo mradi wa kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana na mradi wa malezi na makuzi ya watoto ukilenga kumaliza vitendo vya ulawiti kwenye kundi hilo
Akizunguza wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Tanga Dadi Kolimba ametaka fedha zilizotolewa na wafadhili kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa kuwafikia walengwa.
"Tunafanya uzinduzi wa miradi saba ambayo imakwenda kusaidia vijana na watoto kama mnavyofajamu nchi yetu kwa upande wa vijana kumekuwa na shida kubwa ya ajira soko la ajira katika nchi yetu ni changamoto na hivyo kupitia miradi hii ya Tanga yetu ambayo inapata ufadhili kutoka kwa Botnar foundation na wenzetu tumezindua leo miradi hii saba, "alisema Kolimba.
"Miradi hii inakwenda kusaidia vijana katika upande wa miradi ya afya lakini pia na elimu na tumeona fedha zinazokwenda kutekeleza miradi hii ni karibu bilioni 2.4 na sisi tutahakikisha kwamba tunasimamia vizuri miradi hii ili iweze kuwakomboa vijana katika jiji letu la Tanga waweze kujikwamua na kusimamia miradi yao na kuhakikisha wanaiendesha vizuri, "alisisitiza Kolimba.
Mwenyekiti wa Kamati ya uendeshaji mradi wa Tanga Yetu Juma Rashid ametaka vijana kushiriki kwenye miradi hiyo ili iweze kuwanufaisha na kuleta mabadiliko kwenye maisha ya watoto na kulifanya jiji la Tanga kuwa mahali pazuri pa kuishi.
"Awamu hii tuna miradi 7 na kati ya hii mitatu ipo kwenye sekta ya afya na mmoja eneo la ujasiriamalli, michezo ambayo sasa no ajira rasmi kwa vijana lakini linawaahughulisha vijana pamoja na watu wazima, "
"Eneo jingine ni la elimu , malezi na makuzi ya watoto ambapo miradi yote itakapotekelezwa vizuri na kazi yetu kubwa kama kamati ya uendeshaji ni kusimamia utekelezaji wa uendeshaji wa miradii hii iteekelezwevile imepangwa na itoe matokeo ambayo tunayafikiria yataleta mabadilikp katika maisha ya watoto na vijana,
Kwa upande wake mratibu wa asasi ya kiraia ya Gift of hope Said Bandawe amesema mtadi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa waraibu wa dawa za kulevya huku Mkurugenzi wa Taasisi ya Tayota George Bwire akisema mradi huo utasaidia kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimekuwa vikiongezeka mara kwa mara.
Miradi hiyo ambayo inalenga maeneo mbalimbali ikiwemo afya, ujasiriamali, michezo, elimu na makuzi ya watoto ikotekelezwa ipasavyo inatarajiwa kuwa na matokeo chanya katika jiji la Tanga.
BALOZI CHANA AONGOZA UVISHAJI VYEO NCAA, ATAKA UADILIFU NA WELEDI
Na Woinde Shizza , Arusha
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, amewavisha vyeo Manaibu Kamishna wawili wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) huku pia akishuhudia zoezi la uvishaji wa vyeo kwa Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Uhifadhi watano, waliovishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA, Jenerali mstaafu Venance Mabeyo.
Waliopewa vyeo na Waziri Chana ni Joas John Makwati, aliyepandishwa kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na kuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii, pamoja na Aidan Paul Makalla, aliyepandishwa kuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Huduma za Shirika NCAA.
Kwa upande mwingine, makamishna waliovishwa vyeo na Jenerali Mabeyo ni Gasper Stanley Lyimo (Mipango na Uwekezaji), Paul Geofrey Shaidi (Huduma za Sheria), Charles Marwa Wangwe (Idara ya Uhasibu na Fedha), Godwin Felician Kashaga (Ukaguzi wa Ndani) pamoja na Mariam Kobelo, aliyepandishwa kutoka Afisa Uhifadhi Mkuu Daraja la Kwanza na kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia Huduma za Utalii na Masoko.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Balozi Dk. Chana aliwataka maafisa hao waliopandishwa vyeo kuwajibika kwa bidii na kuonyesha uadilifu katika utendaji wao, akisisitiza kuwa cheo ni dhamana inayokuja na wajibu mkubwa.
“Nina imani kuwa viongozi mliovishwa vyeo leo mtakuwa chachu ya utendaji bora, mtatoa mfano kwa maafisa na askari mnaowaongoza. Juhudi zenu zitachangia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi na kulinda eneo la Ngorongoro pamoja na kulitangaza kama kivutio cha utalii,” alisema Dk. Chana.
Naye Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Abdul-Razak Badru, alisema watumishi wote wa mamlaka hiyo wamekamilisha mafunzo ya kijeshi, hatua iliyochukuliwa kutoka mfumo wa awali wa kiraia, na kwamba sasa rasilimali watu iliyopo itatumika kwa ufanisi zaidi kulinda rasilimali za taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Jenerali mstaafu Mabeyo, aliwataka viongozi hao kutumia nafasi walizopewa kwa uadilifu mkubwa, akisisitiza kuwa mafanikio ya hifadhi hiyo yanatokana na uwajibikaji wa viongozi wake.
“Natumaini kuwa viongozi waliovishwa vyeo watabeba matumaini mapya ya kuboresha sekta ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii. Nawapongeza pia wadau wote waliounga mkono juhudi za kuendeleza Ngorongoro hadi kutangazwa kuwa Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika kwa mwaka 2025,” alisema Mabeyo.

































