Saturday, 5 April 2025

MASHINDANO YA KATAMBI U-17 CUP YAHITIMISHWA KWA KISHINDO! KATUNDA FC MABINGWA



Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akikabidhi zawadi ya fedha kwa washindi wa mashindano hayo.

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MSHINDANO ya Katambi U-17 CUP yametamatika rasmi,huku Timu ya Katunda FC wakiibuka washindi wa michuano hiyo,baada ya kuifunga Busulwa Sec kwa mikwaju ya penati,na kisha kuondoka na Kombe pamoja na kitita cha pesa sh.milioni moja.
Fainali hiyo imechezwa Aprili 4,2025 katika Uwanja wa Chuo cha Ualimu Shinyanga SHYCOM,huku Mgeni Rasmi akiwa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro.


Mchezo huo umechezwa kwa kipindi cha dakika 90, na kuisha bila ya kufungana Magoli,na kisha kuchezwa mikwaju wa penati, na hatimaye Katunda FC kuibuka na ushindi wa Penati 4 kwa 3 dhidi ya Busulwa Secondari, huku mshindi wa tatu katika michuano hiyo akiibuka Ngokolo Secondari.
Mtatiro akitoa zawadi kwa washindi,amemtangaza mshindi wa Tatu ni Ngokolo Sekondari na wamepata Sh. Laki 5, Mshindi wa Pili Busulwa Sekondari sh.Laki 7, na mshindi wa kwanza Katunda FC sh,milioni 1.


Aidha, amempongeza Mbunge Katambi kwa kuendelea kuunga mkono michezo,kwamba kupitia mashindano hayo amekuwa akiibua vipaji vya vijana.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha, amesema michezo ipo kwenye Ilani ya uchaguzi wa CCM, na kwamba Mbunge Katambi amekuwa Mbunge wa mfano kuendelea kuitekeleza Ilani hiyo, sababu michezo ni sehemu ya kuimarisha afya,kuibua vipaji pamoja na ajira.


Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu wilaya ya Shinyanga (SHIDIFA) Sylevester Budete, amempongeza Mbunge Katambi kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo pamoja na kudhamini, huku akimuomba aendelee na jitihada hizo za kuinua michezo Shinyanga.
Nao baadhi ya vijana ambao wameshiriki mashindano hayo, wamemshukuru Katambi kwa kuonyesha vipaji vyao.


Mashindano hayo ya Katambi U-17 CUP yalizinduliwa Febuari 18,2025, na Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga John Siagi, katika Uwanja wa CCM Kambarage, na kushirikisha timu 16.


TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro (kulia)akimkabidhi Cheti cha Pongeza Katibu wa Mbunge Katambi,Samweli Jacksoni kwa niaba ya Mbunge kwa kuendesha mashindano ya Katambi U-17 CUP kutoka SHIDIFA.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akikabidhi Kombe kwa Washindi wa Mashindano ya Katambi U-17 CUP kwa Kampteni wa Timu ya Katunda FC.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akikabidhi zawadi ya fedha kwa washindi wa mashindano hayo.
Awali Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akisalimiana na wachezaji kabla ya mechi kuanza.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha akisalimiana na wachezaji.
Mechi ya Fainali ikiendelea kuchezwa.
Picha za pamoja na wachezaji.
Share:

Friday, 4 April 2025

MBINU SHIRIKISHI NI MUHIMU KUHAKIKISHA WATU WENYE ULEMAVU WANAJUMUISHWA KATIKA NYANJA ZOTE– MHE. NDERIANANGA



NA. MWANDISHI WETU BERLIN – UJERUMANI

Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, na Uratibu, Mheshimiwa Ummy Nderiananga amesema ni muhimu kuwa na mbinu shirikishi ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanajumuishwa kikamilifu katika juhudi za maendeleo kitaifa na kimataifa.

Mhe. Ummy amesema hayo aliposhiriki katika mjadala wa: Kuelekea Hatua Jumuishi za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Kutoka Berlin hadi Belèm na Zaidi : wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Watu Wenye Ulemavu uliofanyika Berlin Ujerumani tarehe 2-3 Aprili, 2025.

Amesema kuwa ingawa serikali, wadau, na mashirika ya kimataifa wanafanya kazi ya kujenga jamii jumuishi, bado watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi.

“Changamoto hizi zinahitaji suluhisho la pamoja na la muda mrefu ili kuhakikisha fursa sawa na upatikanaji wa rasilimali kwa wote, bila kumwacha mtu yeyote nyuma,” alisisitiza Mhe. Ummy.

Akizungumzia mifano ya mafanikio katika sera za ujumuishi wa watu wenye ulemavu kwenye masuala ya tabianchi, Mhe. Nderiananga alisema kuwa Serikali ya Tanzania imeweka sera, sheria, na mikakati mbalimbali kuhakikisha ujumuishi wa watu wenye ulemavu, hususan katika masuala ya menejimenti ya maafa na mabadiliko ya tabianchi.

Alitaja juhudi muhimu zilizofanywa na serikali kuwa ni pamoja na: Mifumo ya Usimamizi wa Maafa, ili kuhakikisha uwakilishi wa watu wenye ulemavu na kuzingatia mahitaji yao katika kukabiliana na majanga na urejeshaji wa hali baada ya maafa; Sera za Mabadiliko ya Tabianchi, zinazolenga kuimarisha ustahimilivu wa watu wenye ulemavu kwa hatua za kukabiliana na athari za tabianchi;

Mikakati Jumuishi ya Kukabiliana na Maafa, ikizingatia njia salama za uokoaji na mipango ya kuwahamisha watu wenye ulemavu; na Misaada ya Kijamii na Kisaikolojia, ili kusaidia watu wenye ulemavu wakati wa majanga

Aliziambia nchi nyingine kuwa zinaweza kujifunza kutoka Tanzania kwa kushirikiana na mashirika ya watu wenye ulemavu, kuunda sera jumuishi, kuhakikisha miundombinu inafikika, kufanya tathmini za athari, na kutenga fedha maalum kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Hatua hizi zinahakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawataachwa nyuma katika maandalizi ya kukabiliana na majanga na ustahimilivu wa tabianchi,” alisema, huku akialika mataifa mengine kuja Tanzania kujifunza juhudi zinazofanywa na serikali.

Kuhusu hatua mahsusi za ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika COP30 na sera za tabianchi, Mhe. Nderiananga alisema kuwa Tanzania imeweka mfumo madhubuti wa ujumuishaji watu wenye ulemavu katika mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa maafa kupitia sera, sheria, na miongozo mbalimbali.

Alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na COP na wadau wengine ili kuhakikisha ujumuishaji kamili wa watu wenye ulemavu katika hatua za kukabiliana na tabianchi na itaendelea kushirikiana na mataifa mengine na mashirika ya kimataifa kuhimiza ajenda ya ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika COP30.




Share:

BENKI YA DUNIA YAZITAKA TAASISI ZINAZOTEKELEZA MRADI WA HEET KUONGEZA KASI KATIKA UJENZI WA MIUNDOMBINU


Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bw. Nkahiga Kaboko, akizungumza wakati wa Kikao cha wadau watekelezaji wa Mradi wa HEET waliokutana Dar es Salaam.
........
Benki ya Dunia (WB), imetoa wito kwa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu Tanzania zinazotekeleza Mradi wa Elimu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kuongeza kasi katika eneo la ujenzi wa miundombinu na usimamizi, kutokana na kasi ndogo katika ujenzi wa Miundombinu inayoonekama kwa vyuo vingi kwa sasa.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi tarehe 03 Aprili 2025, siku ya pili ya kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu nchini, zinazotekeleza Mradi wa HEET na Benki ya Dunia, kinachoendelea katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumza wakati akichangia kwenye uwasilishaji wa moja ya taarifa za maendeleo ya Mradi; Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bw. Nkahiga Kaboko, amesema ni vizuri vyuo vikaongeza umakini katika kuwasimamia wakandarasi ili kumaliza kwa wakati shuguli za ujenzi kama yalivyo malengo ya mradi, badala ya kutegemea muda wa mradi kuongezwa.

Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Peter Msofe, ametilia msisitizo suala hilo na kutoa msimamo wa Wizara kuendelea kufuatia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo akiwataka wahusika wote wa Mradi kuhakikisha usimamizi wa kutosha unafanyika, ili wakandarasi waweze kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa mikataba.

“Jitahidini kuongeza usimamizi na umakini kwa wakandarasi ili wamalize kazi kwa muda uliokubalika, kasi ya ujenzi kwa vyuo vingi bado hairidhishi na muda tuliobaki nao kufika Juni 2026, ni mdogo” alisisitiza

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mratibu Msaidizi wa Mradi, Dkt. Happiness Nnko; amesema kwa upande wa Miradi ya Ujenzi, Chuo kinaendelea na Ujenzi wa Madarasa Ndaki ya Sayansi za Ardhi na Uhandisi CoESE, ambao umekamilika kwa asilimia 24.8, ujenzi wa Maabara Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati (CNMS) asilimia 9%, wakati ujenzi wa Kampasi mpya Njombe bado haujaanza; kutokana na taratibu za manunuzi za kumpata Mkandarasi wa Ujenzi kutokamilika.

Amesema changamoto kubwa katika ujenzi wa miundombinu zinatokana na mlolongo mrefu wa kuwapata wakandarasi wenye sifa huku baadhi ya wakandarasi kukosa vibali na hivyo kuchangia kwa sehemu kubwa ujenzi kuchekewa kuanza.

“Miradi yote hii imepangwa kukamilika mapema mwaka 2026, na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma, imejipanga kuhakikisha Miradi yote inakamilika kwa wakati uliopangwa pamoja na changamoto zilizopo” Alisisitiza Dkt. Nnko.

Aidha; ameyataja maeneo mengine ambayo UDOM imefanya vizuri kuwa ni pamoja na kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM) ambapo hadi kufikia kipindi cha taarifa hii, Chuo kimefanikiwa kwa asilimia 84.9% ya malengo, ambapo kati ya wanafunzi 44,567 waliokusudiwa kufikiwa nchi nzima, UDOM imewafikia wanafunzi 34,241; kati ya hao wanawake ni asilimia 32.3% na wanafunzi wenye mahitaji maalumu 214.

Kwa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mradi wa HEET unatekelezwa kwa tengeo la bajeti la jumla ya Dola za Kimarekani 23,000 na miradi yote inatazamiwa kukamilika mwezi Juni 2026.
Kiongozi kutoka Timu ya Benki ya Dunia, Prof. Roberta Malee, akichangia mada wakati wa majadiliano kuhusu utekelezaji wa Mradi wa HEET wakati wa Mkutano wa Wadau wa Mradi unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bw. Nkahiga Kaboko, akizungumza wakati wa Kikao cha wadau watekelezaji wa Mradi wa HEET waliokutana Dar es Salaam.
Mratibu Msaidizi, Mradi wa HEET Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Happiness Nnko, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi kwa Chuo Kikuu cha Dodoma, wakati wa kikao cha Wadau kinachoendelea jijini Dar es Salaam
Wawakilishi wa Vyuo Vikuu mbalimbali nchini wanufaika wa Mradi wa HEET, wakiwa kwenye mjadala wa pamoja baada ya kufanya mawasilisho.
Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Peter Msofe, akizungumza wakati wa kikao cha Wadau wa Mradi wa HEET waliokutana kujadili maendeleo ya Mradi, jijini Dar es Salaam.
Share:

Thursday, 3 April 2025

DKT. NCHIMBI AWAPOKEA WANACHAMA 200 WA ACT WAZALENDO WILAYANI TUNDURU




Na Regina Ndumbaro - Malunde 1 blog

Wanachama 200 wa Chama cha ACT Wazalendo, akiwemo Katibu wa Chama hicho Jimbo la Tunduru Kusini, Saidi Mponda, pamoja na Diwani wa Kata ya Mchoteka, Sefu Hassan Dauda, wamejiunga rasmi na Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Uamuzi wao wa kuhama ACT Wazalendo na kujiunga na CCM umetokana na kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

viongozi hao waliotoka ACT Wazalendo wamesema wamevutiwa na namna Serikali ya CCM inavyojitahidi kuboresha sekta za miundombinu, afya, elimu na uchumi kwa ujumla. 
Wameeleza kuwa maendeleo yanayoonekana katika wilaya ya Tunduru na maeneo mengine nchini ni kielelezo cha uongozi imara wa CCM, hivyo wakaona ni busara kujiunga na chama hicho ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo hayo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mlimgoti, wilayani Tunduru, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewapongeza wanachama hao kwa uamuzi wao wa kujiunga na CCM. 

Amesisitiza kuwa CCM ni chama chenye misingi ya maendeleo na akatoa wito kwa wanachama wa vyama vingine kujiunga na chama hicho ili kushirikiana katika kuleta maendeleo kwa Watanzania wote.

Aidha, Dkt. Nchimbi ametumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuhusu dhamira ya CCM kuendelea kusimamia maendeleo na kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na rasilimali za nchi. 

Amesema kuwa Serikali inayoongozwa na CCM itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa Watanzania wote kuilinda amani ya nchi kwa nguvu zote. 

Amesisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu kwa maendeleo na ustawi wa jamii, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na mshikamano na utulivu ili miradi ya maendeleo iweze kuwanufaisha wananchi wote.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger