Sunday, 9 March 2025

HABARI KUBWA KWENYE MAGAZETI YA LEO JUMATATU MACHI 10, 2025

Share:

KATAMBI ATOA KIBUNDA KINGINE MASHINDANO U-17 CUP, VIPAJI VYAANZA KUONEKANA!




Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, ametoa pesa shilingi milioni 1 kwa ajili ya kuendeleza mashindano ya “Katambi U-17 Cup” ambayo yanaendelea katika viwanja mbalimbali.
Mashindano haya yalizinduliwa rasmi Februari 18, 2025, katika Uwanja wa CCM Kambarage na Mwenyekiti wa Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga, John Siagi, ambayo yanashirikisha timu 16.


Katibu wa Mbunge, Samweli Jackson, amekabidhi kiasi hicho cha pesa leo, Februari 9, 2025, kwa Kamati ya Utendaji ya Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Shinyanga (SHIDIFA) kwa niaba ya Mbunge Katambi.
Amesema kuwa Mbunge Katambi alishatoa awali Shilingi milioni 4, na sasa ameongeza milioni 1 ili kuendeleza mashindano haya, akiwa na dhamira ya kuibua na kukuza vipaji vya vijana.


Ameongeza kuwa, kwa sasa mpira wa miguu ni ajira, akitaja mfano wa kijana James Nhungo ambaye alisajiliwa na Timu ya Simba “B” Under 20 kupitia mashindano ya Dr. Samia/Katambi Cup.

Samweli amekishukuru Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Shinyanga (SHIDIFA) kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha mashindano hayo yanaenda vizuri,huku akiwasihi pia marefa wachezeshe kwa haki bila upendeleo wa timu yoyote.


"Mbunge Katambi anapenda sana michezo na amekuwa akianzisha mashindano mbalimbali ili kuibua vipaji vya vijana. natoa wito kwa wadau wa michezo kuhudhuria mashindano haya ya U-17 ili kuona vipaji vya vijana," amesema Samweli.


Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu wilaya ya Shinyanga (SHIDIFA)Joseph Assey, amempongeza Mbunge Katambi kwa kuthamini michezo,amesema kwa mashindano ambayo yanaendelea hivi sasa ya Katambi U-17 Cup, tayari wameshaanza kuona vipaji vya vijana.
Katibu wa Mbunge Katambi, Samweli Jackson wapili (kutoka kulia)akikabidhi sh.milioni 1 kwa SHIDIFA kwa ajili ya kuendeleza mashindano ya Katambi U-17 CUP.

Share:

RAIS SAMIA : TANZANIA NI MSIMAMIZI MPANGO WA NISHATI SAFI AFRIKA




 📌Asema Ajenda ya Nishati Safi ni ajenda ya Nchi hivyo  tunaisimamia Afrika.

📌Nishati ni Mpango wa Maendeleo endelevu

📌Umeme umesambazwa Vijiji vyote nchini

📍Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  amesema kuwa Tanzania ni Msimamizi wa Mpango Maalum wa Nishati Safi Afrika.

Amesema hayo wakati akizungumza  katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo Kitaifa kwa  Tanzania yamefanyika Jijini Arusha, Tarehe 8 Machi, 2025 katika Uwanja wa Shekhe Amri Abeid Karuta.

Amefafanua kuwa Mpango wa Nishati Safi kuwepo nchini, kumeifanya Tanzania kuwa Msimamizi wa Mpango huo Maalum kwa Afrika.

" Katika Nishati Safi hii tunampango maalumu kama Tanzania, na kwa kuwa Tanzania ni msimamizi wa mpango huu kwa Afrika, hivyo nishati safi ya kupikia ni ajenda yetu kama nchi na tunaisimania Afrika", Alisema Dkt. Samia

Alisisitiza kuwa suala la nishati lipo katika mpango wa saba wa maendeleo endelevu katika nchi ya Tanzania hivyo Tanzania imefanya kazi nzuri katika kuhakikisha nishati safi inatumika.

"Sio nishati tu bali ni nishati safi tumefanya kazi nzuri ya kujenga bwawa la Mwalimu Nyerere na linatoa Megawati 2115 pamoja na bwawa hilo kuna mabwawa mengine madogo  sita ambayo yanatoa umeme katika maeneo mengine" 

Kuhusu usambazaji wa Umeme nchini, Dkt Samia  amesendelea kusema kuwa umeme kwa sasa Vijiji vyote 12,300 nchini tayari vimesambaziwa umeme na kazi hiyo inaendelea  katika Vitongoji.

" Suala la nishati tumepiga hatua kubwa tulikuwa tunafaidi umeme katika baadhi ya Vijiji na Minim sasa Serikali imeweza kusambaza umeme katika vijiji vyote 12300, Na tunavyoongea sasa Vitongoji  kadhaa tayari vimeunganishwa na kazi inaendelea," Alisisitiza Mhe. Rais.


Vilevile Dkt. Samia Suluhu Hassan alieleza namna Tanzania ilivyobarikiwa kwa uwepo wa Gesi Asilia ambayo kama Taifa inaendelea kuichakata huku akieleza kuwa sasa  nchi  imetoka katika Umeme wa kutumia mafuta na kuelekeza nguvu Gesi Asilia na Maji ili kupata  nishati safi.

 Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na baadhi ya  watumishi kutoka Wizara ya Nishati.







Share:

WAFANYAKAZI WANAWAKE BARRICK WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA KUSAIDIA JAMII

Wafanyakazi wanawake wa kampuni ya Barrick nchini na wakandarasi wake wameshiriki maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa kujikita kutoa msaada kwenye jamii sambamba na kujitolea muda wao kusaidia shughuli za kijamii ambapo baadhi yao wameshiriki maadhimisho ya kitaifa yaliyofanyika katika jiji la Arusha.

Wanawake kutoka mgodi wa Barrick Bulyanhulu wametembelea hospitali ya rufaa ya ya wilaya Nyang'hwale na Kituo cha afya cha Khalumwa Mkoani Geita na kukabidhi vifaa mbalimbali vya usafi na vya kusaidia wagonjwa wanaopata huduma za kiafya katika sehemu hizo.

Akiongea wakati wa kukabidhi msaada wa vifaa hivyo, Afisa Uhusiano wa Jamii Mwandamizi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo amesema katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu 2025, pamoja na kampuni kuwa na programu mbalimbali za ndani pia imeandaa programu za kusaidia jamii.

Akiongea na uongozi wa Hospitali hiyo, Afisa Uhusiano kutoka Mgodi wa Barrick Bulaynhulu Zuwena Senkondo, amesema katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu 2025, pamoja na kampuni kuwa na programu mbalimbali za ndani pia imeandaa programu za kusaidia jamii.

Amesema Barrick imekuwa ikitoa kipaumbele kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini ambapo kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii imeweza kujenga vituo vya afya katika maeneo yanaozunguka migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyang'wale Dkt. Zakhia Abdallah , ameishukuru Barrick kwa msaada huo sambamba na baadhi ya wafanyakazi wake kujitolea muda wao kutembelea hospitali na kutembelea wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo ikiwemo Wanawake waliolazwa katika wodi ya wazazi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang'wale Octavianus Rweyendera, amewapongeza Wanawake wa Barrick kwa kutumia maadhimisho ya siku yao kusaidia wenye mahitaji katika jamii sambamba na kutenga muda wao kuwatembelea na kuwapatia faraja.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Barrick walioshiriki maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na wenye mahitaji maalum Dkt. Dorothy Gwajima katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake dunia kitaifa yaliyofanyika katika jiji la Arusha.
Wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu na wakandarasi wake katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo wamekabidhi vifaa mbalimbali hospitali ya hospitali ya rufaa ya wilaya Nyang'hwale na Kituo cha afya cha Khalumwa Mkoani Geita

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI MACHI 9, 2025

Share:

Saturday, 8 March 2025

MENEJIMENTI VETA, YATEMBELEA EMIRATE ALLUMINIUM PROFILE KUPATA UZOEFU WA UFUNDI WA ALUMINIAMU





Menejimenti ya VETA ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, leo, tarehe 7 Machi 2025 imetembelea kiwanda cha Emirate Alluminium Profile kilichopo Tegeta jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu kuhusu namna ufundi wa Aluminiamu unavyofundishwa sehemu ya kazi.

Ziara ililenga pia kuona namna ya kuanzisha ushirikiano kati ya VETA na Emirate Alluminium Profile ili kuwezesha wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya VETA kupata ujuzi zaidi kuhusiana na ufundi wa Aluminiamu kupitia mafunzo ya mahala pa kazi. Akizungumza katika ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, amesema wamebaini shughuli za ufundi zinazofanywa katika kampuni hiyo zinaakisi Mitaala ya VETA, ambapo wanafunzi wa fani ya Useremala wanafundishwa masuala ya utengenezaji wa Aluminiamu.

CPA Kasore amesema kiwanda hicho kina mafundi waliobobea wenye uzoefu ambao VETA itawatumia kutufundisha na kufundisha katika vyuo vyake.

"Sisi VETA kwa kukutana na Emirates Alluminium Profile tunaenda kuwa na ushirikiano ambao utawezesha kutoa huduma na kuwezesha watu kwenda kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuajiriwa katika viwanda mbalimbali nchini," amesema CPA Kasore.

Aidha, CPA Kasore amesema kupitia ziara hiyo wameona kuna haja ya kutenganisha ufundi wa Aluminiamu na Useremala, ili kila moja iweze kujitegemea, hivyo kuzalisha vijana waliobobea kwenye ufundi wa Aluminiamu ambao una fursa nyingi kwa sasa.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Emirate Alluminium Profile, Ndugu Deogratius Marandu amewataka vijana kuwekeza katika kufanya kazi kwa kutumia mikono na sio kutumia ujanja ujanja ili kufanikiwa na hivyo kuiomba VETA kuendelea na kazi ya kuwaanda vijana ili waweze kuajirika na kujiajiri na kuchangia katika maendeleo ya jamii zao na Taifa. "Mimi nina imani sana na VETA hasa katika kuwanoa vijana naamini tunaenda kushuhudia mabadiliko mbalimbali katika masuala ya Ufundi stadi na tunaenda kuwapata wataalamu watakaoenda kufanya kazi kwa ufanisi," amesema. Kiwanda cha Emirate Alluminium Profile kinajihusisha na uagizaji na uuzaji wa Aluminiamu, vioo, pamoja na mipira kwa ajili ya kutengenezea madirisha na milango ya Aluminiamu.
Share:

VIJANA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA MAKUNDI HATARISHI

Mchungaji Peter Mayengo wa Kanisa la Moravian Jimbo la Ziwa Tanganyika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera
 

Na Lydia Lugakila-Bukoba

Vijana Katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wametakiwa kuachana na makundi mbali mbali yasiyofaa ikiwemo ikiwemo kujiingiza katika tamaa za kujipatia fedha za mkato bila kuwajibika, kukaa vijiweni, kujihusisha na madawa ya kulevya. 

Kauli hiyo imetolewa na Mchungaji Peter Mayengo wa Kanisa la Moravian Jimbo la Ziwa Tanganyika muda mfupi kabla ya semina ya ujasiliamali iliyolenga kuwanoa watu wa rika zote hasa vijana iliyofanyika kanisani hapo.

Mchungaji Mayengo amesema vijana wanatakiwa  wajifunze neno la Mungu na kufanya kazi huku akikili kuwepo kwa vijana wavivu ambao wamejikuta kutamani vitu vingi kwa wakati ambapo sio sahihi kwa namna yake.

"Vijana pia  wamejikuta wakitoa lugha za matusi, wapo pia wanaoingia kwenye madawa ya kulevya na wana makundi ya ajabu yasiyoleta mafanikio katika Taifa"amesema mchungaji Mayengo.

Mtumishi huyo wa Mungu ameongeza kuwa inaumiza kuona vijana wengi wa Bukoba wanakaa katika vijiwe vya Kahawa na Wazazi hawawakemei jambo linalosababisha kutengeneza vijana na Taifa ambalo linaenda kuharibika.

Amesema ni wakati sasa Wazazi na Watumishi wa Mungu kusimama vizuri katika kurekebisha vijana hao ki maadili ili kuwa naTaifa bora.

Aidha amesema malalamiko juu ya Vijana kukengeuka ki maadili ni mengi huku jamii ikishindwa kuelewa chanzo ni nini.

"Wazazi wanatakiwa kuwatengeneza vijana katika maadili pia Watumishi wa Mungu kuchukua nafasi ya pekee katika kutoa mafunzo ya neno la Mungu ili hofu iwe ndani yao"amesema Mayengo.

Hata hivyo amewahimiza vijana kujikita katika masuala ya ujasiriamali ili wapate ujuzi utakao wasaidia kwa maisha ya baadae huku akiiomba Serikali pia kuona namna ya kuwasaidia vijana wenye ujuzi ili kuwa na Taifa lenye wataalam wengi.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger