Friday, 17 January 2025

TUME YA RAIS YA MABORESHO YA KODI YAKUTANA NA WADAU WA KODI MKOA WA SHINYANGA KUKUSANYA MAONI

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi  imefanya mkutano na wadau wa masuala ya kodi Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kukusanya maoni kuhusu uzoefu, changamoto na mapendekezo ya namna ya kuboresha mifumo ya kodi nchini.

Mkutano huo umefanyika leo, Ijumaa, Januari 17, 2025, katika ukumbi wa Lyakale Mjini Shinyanga, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi.

Akifungua mkutano huo, Wakili Mtatiro amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau katika michakato ya kuboresha mifumo ya kodi, akisema kuwa michango na maoni yao ni muhimu na yatatumika kama sehemu ya mikakati ya kuleta mageuzi ya kimsingi katika sekta hiyo.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mwanamapinduzi wa kweli, anayehamasisha na kusikiliza maoni ya wananchi. Anachukua hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa maoni ya wananchi yanatekelezwa kwa manufaa ya wengi. Tume hii ya Rais haiachi jambo lolote nyuma, inazingatia taaluma na weledi wa hali ya juu katika kufanya tathmini ya mifumo ya kodi. Hivyo, michango yenu leo itachukuliwa kama maoni muhimu kwa kuboresha mifumo ya kodi na itafanyiwa kazi,” amesema Wakili Mtatiro.

Wakili Mtatiro amesema changamoto za kodi ni changamoto za kitaifa na kuahidi kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kujitahidi kuboresha mifumo ili kuhakikisha kuwa masuala ya kodi yanakuwa endelevu na yanahusisha pande zote kwa faida ya nchi nzima.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, CPA Leonard Mususa, ameeleza kuwa tume hiyo inaendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu mifumo ya kodi, mapato, na tozo mbalimbali zinazohusiana na sekta ya kodi.

Amesema kazi hii inaimarisha juhudi za Serikali katika kuhakikisha kuwa mfumo wa kodi unakuwa rafiki kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, na kwamba tume inashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa kodi zinakusanywa kwa njia bora na yenye haki, huku ikifanya mabadiliko ili kutoa kero na malalamiko ambayo yamekuwa yakichochea malumbano.

“Tume ya Rais inatekeleza majukumu yake kwa umakini mkubwa ili kuondoa kero za kodi na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Tumelenga kuvutia mitaji ya ndani na nje ya nchi na kwa upande mwingine, tunafanya tathmini ya kina ili kuona ni hatua zipi zinapaswa kuchukuliwa ili kuboresha mifumo ya kodi nchini,” ameeleza CPA Mususa.

Mkutano huo umetoa fursa kwa wadau muhimu wa masuala ya kodi kutoka Mkoa wa Shinyanga kutoa maoni yao kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika masuala ya kodi.

Wadau hao pia wamependekeza njia mbalimbali za kutatua changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu katika ukusanyaji wa kodi, kuboresha mawasiliano kati ya serikali na wafanyabiashara na kuongeza ufanisi katika utendaji wa mifumo ya kodi.

Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi kukusanya maoni ya wadau kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ili kuwezesha mabadiliko ya mifumo ya kodi kwa namna itakayowafaidi wananchi na nchi kwa ujumla.

Share:

CCM SONGEA MJINI YAIOMBA SERIKALI KUHARAKISHA FEDHA ZA MRADI WA MAJI WA MIJI 28

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea Mwinyi Msolomoni(katikati) )kulia kwake ni James Mgego Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea mjini na kushoto kwake ni Mhandisi Vincent Bahemana ambaye ni msimamizi wa mradi wa maji na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma

 



Na Regina Ndumbaro Ruvuma 


Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mjini kimempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Shilingi bilioni 145.77 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma. 


Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Mwinyi Msolomi, wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati ya siasa waliotembelea mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).


Msolomi amesema mradi huo ni muhimu kwani unatarajiwa kumaliza changamoto ya uhaba wa maji kwa wakazi wa maeneo mbalimbali, hususan mtaa wa Sokoine na kata ya Making’inda.


 Ameongeza kuwa mradi huo utaimarisha maisha ya wananchi kwa kuwaondolea adha ya kutafuta maji kwa muda mrefu na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.


Katibu wa CCM wilaya ya Songea, James Mgego, ameitaka Serikali kutoa fedha zilizobaki ili kuhakikisha mkandarasi anaendelea na ujenzi wa mradi huo ambao ulisimama kutokana na ukosefu wa fedha.


 Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutahakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika kwa zaidi ya miaka 20.


 Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Vicent Bahemana, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Januari 2024 na unatarajiwa kukamilika Septemba 2026. 


Amefafanua kuwa Serikali tayari imelipa Shilingi bilioni 21.87 kama malipo ya awali kwa mkandarasi, huku kazi mbalimbali zikiendelea kufanyika, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa matenki na ulazaji wa mabomba.


Mradi huo unahusisha ujenzi wa kidaka maji katika Mto Njuga chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 17 kwa siku, mtambo wa kuchuja na kutibu maji lita milioni 16, na matenki matatu yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 9.


 Pia, unahusisha upanuzi wa mtandao wa mabomba ya maji na ukarabati wa mtambo wa kuchuja maji wenye ufanisi wa chini ili kukidhi mahitaji ya Manispaa ya Songea.


Msolomi na wajumbe wengine wa kamati ya siasa wameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo lakini wameitaka Serikali kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati ili kuharakisha utekelezaji. 


Pascal Msigwa, mjumbe wa kamati hiyo, ameitaka Serikali kuharakisha mradi huo ili kuwasaidia wananchi kuondokana na mgao wa maji.


Kwa sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 4.8, huku matenki mawili yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 2 kila moja yakikamilika, na ujenzi wa tenki kubwa la lita milioni 5 ukiwa katika hatua za msingi. 


Serikali inatarajiwa kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa ufanisi ili kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Songea.
Share:

TGNP KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WAANDISHI WA HABARI KUTOA ELIMU KUHUSU AZIMIO LA BEIJING


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) imesema itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari nchini kutoa elimu kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 pamoja na azimio la Beijing wakati wa kuelekea miaka 30 ya Beijing.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni wakati akifungua warsha kwa waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji TGNP, Lilian Liundi amesema matarajio ya TGNP ni kuona wanahabari wanaueleza umma kuhusu azimio la Beijing pamoja na misingi ya usawa wa kijinsia.

Amesema kuelekea kumbukizi ya miaka 30 ya mkutano wa Beijing, ni muhimu kuimarisha juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu azimio hilo, kuelezea mafanikio pia kuelekea kwenye maadhimisho hayo.

"Vyombo vya habari vina jukumu kubwa katika kuelimisha jamii kuhusu masuala ya kijinsia na maendeleo, kuibua na kuripoti habari zinazohimiza usawa wa kijinsia, huku wakizingatia weledi na uchambuzi wa kina". Amesema Liundi.

Ameongeza kuwa jukumu la kupigania usawa wa kijinsia linapaswa kuwa la kila mtu, bila kujali itikadi za kisiasa, dini, au kabila.

Warsha hiyo iliwakutanisha wanahabari kutoka mikoa ya Manyara, mbeya, kilimajaro, Dar es Salaam, Kigoma, Katavi, Mtwara na Iringa.
Share:

Thursday, 16 January 2025

MISA-TAN YAWATEMBELEA WADAU WA HABARI KANDA YA ZIWA KUJADILI NAMNA YA KUFANYA KAZI KWA PAMOJA


Na Mwandishi wetu - Mwanza.

Mwenyekiti wa MISA Tanzania Bwana Edwin Soko amefanya ziara kwenye Taasisi za Kitaifa zenye Makao Makuu Kanda ya Ziwa zikiwemo Mamlaka ya Uthibiti wa Nishati na Maji(EWURA) Kanda ya Ziwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) Kanda ya Ziwa.

Ziara hiyo ameifana leo Januari 16,2025

Soko amekutana na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandishi Imelda Salumu na kujadilili nama ya kufanya kazi Kwa pamoja likiwemo eneo la kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu ili wafanye kazi Kwa weledi zaidi.

Kwa upande wake Mhandishi Imelda alieleza kuwa anaipongeza MISA Tan Kwa kuona umuhimu wa kuwa karibu na wadau mbalimbali wa habari na kusisitiza ataendelea kufanya kazi pamoja na wanachama wa MISA na waandishi wa habari wote nchini.

Wakati huo huo Soko alikutana pia na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa George Mhina ambapo walijadili juu ya umuhimu wa MISA Tan kwenye kusimamia weledi ndani ya taaluma ya habari.

Mhina alisema kuwa, EWURA wapo tayari kushirikiana na MISA Tan kwenye kufanya kazi kitaaluma ili kusaidia kupatikana kwa habari jengefu.


Ziara hizo zimekuwa ni mwendelezo wa Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika(MISA TAN) kujitambulisha Kwa wadau na kuongeza uwigo wa kufanya kazi Kwa pamoja.



Share:

Wimbo Mpya : NYANDA MALIGANYA - TAARIFA YA INAGA

 

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger