Wednesday, 1 January 2025

WATENDAJI NGAZI YA MKOA WA RUVUMA WAPATIWA MAFUNZO YA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

Na Regina Ndumbaro, Ruvuma

Watendaji wa ngazi ya Mkoa wa Ruvuma kutoka Wilaya za Mbinga, Nyasa, na Songea wamepatiwa mafunzo ya jinsi ya kusimamia zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika maeneo yao.

Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Jeshi la Wananchi, Chandamali, na kuhudhuriwa na Hakimu Japhet Bwire Manyama, ambaye alitoa viapo kwa maafisa watendaji hao.

Mafunzo hayo yamefunguliwa na  Mkurugenzi wa Daftari la Wapiga Kura na TEHAMA Taifa, Stanslaus Mwita, kwa niaba ya Mheshimiwa Jaji Mstaafu Jacob Mwambegele, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. 

Akizungumzia mafunzo hayo,yaliyoanza rasmi leo, Tarehe 1 Januari 2025M kurugenzi wa Daftari la Wapiga Kura na TEHAMA Taifa, Stanslaus Mwita, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwafundisha watendaji jinsi ya kujaza fomu za uandikishaji na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voter Registration System - VRS) kwa ufanisi. 

"Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora. Mafanikio ya zoezi hili yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya watendaji wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa, na wadau wengine wa uchaguzi",amesema.

Pia, maafisa wa TEHAMA watapata mafunzo maalumu ya kushughulikia changamoto za kiufundi (troubleshooting) zitakazojitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wapiga kura katika vituo vya kujiandikisha.

Mwita ameongeza kuwa mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya uandikishaji wapiga kura, hatua itakayosaidia kuhakikisha uwazi na kupunguza vurugu zisizohitajika. 

Aidha, maafisa wa uandikishaji wamehimizwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa watendaji wa maeneo yao na kubainisha kuwa vitambulisho walivyopewa na Tume ni utambulisho wa kutosha katika maeneo waliopangiwa.


Share:

WAZIRI KOMBO AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA MAHAKAMA YA WILAYA YA MAGHARIBI B


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amesema kuimarika kwa miundombinu ya Mahakama ni hatua muhimu itakayowawezesha wananchi kupata huduma katika mazingira mazuri, salama na rafiki.

Ameyasema hayo leo Januari 1, 2025 wakati akiweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Magharibi B huko Kisakasaka, Zanzibar.

Balozi Kombo amesema, kwa miaka mingi mahakama zimekuwa na changamoto ya miundombinu ya majengo na Serikali inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kumaliza changamoto hizo kwa kujenga majengo mapya na ya kisasa.

"Kwa mfano jengo lililokuwa likitumiwa na Mahakama ya Magharibi B pale Mwanakwerekwe lilikuwa finyu mno kiasi cha kusababisha msongamano mkubwa na kuwapa usumbufu waliofuata huduma mahali pale," alisema Mhe. Kombo.

Waziri huyo ameongeza kuwa, pamoja na ufinyu huo, pia halikuwa rafiki kutokana na kukosekana nafasi kwa ajili ya maofisa wa Mahakama.

Vilevile, kukosekana kwa huduma za watu wenye mahitaji maalumu na maegesho kulisababisha muda mwingi wananchi walikuwa wanazagaa kwa kukosa sehemu tulivu ya kusubiri huduma.

Amesema, hali hiyo ndiyo iliyosababisha Serikali kuchukua hatua za makusudi kuja na mradi wa ujenzi wa majengo ya Mahakama ya mikoa na wilaya Unguja na Pemba.

Pia, amesema ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo saba ambao ulipangwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Kwa upande wa Unguja, Balozi Kombo amesema, mradi huo wa Loti Nambari 2 unajumuisha majengo manne ambayo ni: Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini, Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Mahakama ya Mkoa wa Kusini na Mahakama ya Wilaya ya Magharibi B.

Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya majengo ya ofisi, hivyo ni wajibu wa watumiaji wa miundombinu hii na wananchi kwa ujumla kuitunza ili iweze kudumu kwa miaka mingi ijayo.
Share:

BENKI YA CRDB YAFUNGUA MATAWI MAPYA MUGANGO, SIRARI MKOANI MARA

 

Katika kuufunga mwaka 2024 kwa huduma bora, Benki ya CRDB imefungua matawi mapya mawili mkoani Mara yaliyopo Mugango katika Wilaya ya Musoma Vijijini na Sirari wilayani Tarime.


Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema uzinduzi wa matawi hayo ni sehemu ya jitihada za Benki kuiishi kaulimbiu yake ya ‘ulipo, tupo’ kwa kuwafuata wananchi katika kila pembe ya nchi na kuwapa huduma bora za fedha kwa maendeleo yao binafsi na kuchangia uchumi wa taifa pia.
“Mkoa wa Mara una shughuli nyingi za kiuchumi kuanzia migodi mikubwa na machimbo ya madini, uvuvi, kilimo na biashara ya mpakani hivyo ni muhimu kuwa na huduma za uhakika za fedha ili kuwajumuisha wananchi kwengi katika uchumi. Ulikuwa ni mpango wa Benki yetu ya CRDB kuhakikisha tunafungua matawi haya mawili kabla mwaka 2024 haujaisha,” anasema Raballa.


Kabla ya ufunguzi wa matawi hayo mapya, Raballa amesema wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanapata huduma za benki kupitia kwa mawakala waliotapakaa maeneo tofauti. Kwa mkoa mzima wa Mara, amesema Benki ya CRDB inao zaidi ya mawakala 600 wakiwamo 195 wanaohudumia katika Wilaya Ya Tarime na 35 Musoma Vijijini.
“Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wateja wilayani Tarime na Musoma, Benki yetu iliona kuna umuhimu wa kuboresha huduma ili kuendana na mahitaji yaliyopo sasa na yatakayojitokeza baadaye. Tulifanya utafiti wa kina kabla ya kujenga matawi haya yatakayowahudumia wananchi wa Mugango na Sirari pamoja na maeneo jirani,” amesema Raballa.


Kutokana na uzinduzi wa matawi hayo mawili, Benki ya CRDB sasa imefikisha jumla ya matawi 10 mkoani Mara ambayo ni Musoma, Tarime, Bunda, Serengeti, Nyamongo, Rorya, Shirati, Mugango na Sirari hivyo kuifanya kuwa na mtandao mpana zaidi wa matawi nchini kuliko benki nyingine yoyote nchini.
Akifungua tawi la Sirari, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Meja Edward Flowin Gowele amesema huduma za fedha ndio msingi wa maendeleo ya mwananchi binafsi, kaya na taifa kwa ujumla hivyo kilichobaki ni umakini wa wananchi kubuni miradi itakayowainua kiuchumi kwa kuzikabili changamoto zilizopo kwenye maeneo yao ili kunufaika na fursa zinazojitokeza.

“Tawi hili ni sehemu salama kwa wananchi kuhifadhi akiba zenu za fedha. Ni mahali ambapo wafanyabiashara mtapata mikopo ya kuimarisha miradi yenu na wafanyakazi nao wataweza kutimiza malengo yao. Benki ni rafiki wa kila mwananchi anayewa na kupanga maendeleo yake, tulitumie tawi hili kujinufaisha kwa kujenga uchumi imara wa kila mmoja wetu,” amesema Mheshimiwa Gowele.

Licha ya kunufaika na mikopo inayotolewa, Mheshimiwa Gowele amewahimiza wananchi wa Sirari, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara na Tanzania nzima kwa ujumla kuwekeza kwenye Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond inayoendelea kuuzwa na Benki ya CRDB ili kupata fedha zitakazowezesha ujenzi wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
“Ukiwekeza katika hatifungani hii una uhakika wa kupata faida ya asilimia 12 inayotolewa kila mwaka kwa muda wote wa miaka mitano wa uhai wake. Lakini, kumiliki hatifungani hii ni sawa na kuwa na nyumba, unaweza kuitumia kama dhamana kuchukua mkopo kutoka taasisi yoyote ya fedha. Nawasihi kila mmoja wenu na Watanzania wote kwa ujumla, kuitumia fursa hii kuwekeza kwenye hatifungani hii,” amesisitiza Mheshimiwa Gowele.

Kwenye uzinduzi wa tawi la Mugango, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya amesema ni fursa kwa wananchi wa Musoma kunufaika na huduma zinazotolewa na Benki ya CRDB zikiwamo zilizo chini ya Programu ya Imbeju inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake.
“Ufunguzi wa tawi hili umesogeza kwa karibu fursa za Programu ya Imbeju. Nawaomba wajasiriamali mlitumie tawi hili kupata mitaji wezeshi itakayosaidia kuinua biashara zenu. Hapa, mtapata ushauri wa kitaalamu ia wa namna bora ya kukuza shughuli zenu kwa maendeleo binafsi na taifa pia,” amesema Kusaya.

Sambamba na ufunguzi wa tawi la Benki ya CRDB Sirari, Benki ya CRDB imekabidhi madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzi kwa wanafunzi wa Wilaya ya Tarime. Madawati hayo yamepokelewa na Mheshimiwa Gowele aliyesema yatasaidia kupunguza uhaba uliopo katika shule za msingi na sekondai wilayani Tarime.
Share:

MBUNGE WA TARIME MJINI ACHUKIZWA NA MBUNGE WA NCHINI KENYA KUHAMASISHA KATIBA MPYA AOMBA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KUCHUKUA HATUA

 

Na Helena Magabe - Tarime

MBUNGE wa Jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki amesema ulinzi na usalama Tarime uko vizuri licha ya kuwa amekerwa na Mbunge wa Kurya Magharibi Nchini Kenya Matias Rhobi kuhamasisha katiba mpya nchini katika Jimbo lake na kuleta uchochezi kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amesema kitendo cha mbunge huyo kuchocheo wananchi kudai katiba mpya  akiwa kwenye sherehe aliyoalikwa na moja ya mtia nia ,akihoji kwanini Mbunge hakufika na kudai kuwa hakuna maendeleo Tarime ,hakuna barabara za lami ni kitendo ambacho kimemkera na ni uvunjifu wa sheria za nchi.

Amesema Mbunge  huyo anatakiwa kufanya maendeleo Nchini kwake hasa kwenye Jimbo lake ambalo yeye si mgeni anazijua barabara za jimboni kwake zilivyo mbovu hasa njia ya Kehancha ambayo ilijengwa zaidi ya miaka ishirini iliyopita hakuna maendeleo aliyofanya na  Jimboni kwake ni Mbunge Bubu ambaye haongelei Jimbo lake na hayuko kwenye rekodi ya vyombo vya habari .

Akiendelea kuzungumza amesema Katiba mpya sio kipaumbele cha wananchi wa Tarime bali wananchi wanahitaji maendeleo kama vile ,maji,umeme elimi,afya barabara na mahitaji muhimu hiyo katiba mpya anayowahamasisha wadai haitawasaidia kwani hata huko jimboni kwake  katiba haijaleta majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi wake hivyo aache  kuzungumzia vitu ambavyo haviingii akilini.


Ameiomba Serikali ya Kenya kumchukulia hatua mbunge huyo kwa sababu nchi ya Kenya ni jirani na ndugu hivyo asingependa kuona anasababisha mgogoro wa kudai  katiba na kusababisha uvunjifu wa amani   baina ya nchi mbili ambazo zina mahusiano mazuri.


" Kwanza sisi utamaduni wetu ni tofauti na wa nchi yao sisi tuna  heshima si rahisi kutukana  Kiongozi Kila mtanzania ana wajibu wa kuilinda heshima ya Nchi yake  kule  kwao wanatukana viongozi kwanza kura wanapiga  kwa ukabila,huku sisi tunafata sifa  asilete mambo yake ya kisiasa every day nikutia kauli ambazo hazina tija "alisema Kembaki.


Aidha amesema hakuna mtia nia ayemnyima usingizi kwani maendeleo amefanya na wananchi wanamkubali na katika sekta zote amezitendea haki kwa upande wa barabara ambayo alisema Bomani hakuna lami amesema itapata lami karibia maeneo yote na kwamba mbali na kilometa 6 za lami zilizo kwenye mpango zimeongezwa nyingine 18 ambapo kata ya Nyamisangura na Bomani zitapewa kipaumbele.



Share:

Tuesday, 31 December 2024

MBUNGE RWEIKIZA ALIVYOLIPAMBA JIMBO LAKE

Abainisha miradi mikubwa ya maendeleo kupitia kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba yake mzazi

Na Lydia Lugakila - Bukoba

MBUNGE wa jimbo la Bukoba vijijini Dkt. Jasson Rweikiza amebainisha miradi mikubwa ya maendeleo iliyofanyika na inayoendelea kufanyika jimboni kwake huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo, kwa kuwapatia zaidi ya shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mawili ambayo ni lango la kutoka na kuingia ndani ya mkoa wa Kagera.

Mbunge Rweikiza ametoa ufafanuzi huo  wakati akiongea wananchi mbalimbali pamoja na viongozi wa Mkoa wa Kagera waliofika katika viwanja vya Rweikiza vya shule ya Rweikiza iliyopo  Kyetema Wilaya ya Bukoba  kwa ajili ya kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba yake mzazi aliyekuwa akiitwa Samsoni Rweikiza. 

Rweikiza amebainisha kuwa,Dkt. Samia Suluhu Hassan amelipendelea Sana Jimbo lake kwani ametoa Mabilioni ya fedha kwa ajili ya maendeleo jimboni humo.

Akieleza miradi hiyo Mbunge huyo amesema kuwa pamoja na Daraja la Karebe ambalo limetengewa kiasi cha shilingi bilioni 9.3 kwa ajili ya ukarabati mkubwa kutokana na daraja hilo kuchoka kwasababu limejengwa muda mrefu.

Amesema Daraja hilo ambalo lipo Barabara kuu inayounganisha kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba,Misenyi na Karagwe  Wananchi hulitumia katika kusafirisha mazao na bidhaa nyingine.

Akitaja Daraja lingine amesema ni la Chanyabasa ambapo wananchi hutumia kivuko kuvuka toka kata zaidi ya nane kuja hospitali ya Wilaya ya Bukoba Vijijini na wengime wanaovuka kwenda Bukoba mjini kwa shughuli za kujiingizia kipato jambo linalosababusha  watumie muda mrefu wakisubiri kivuko kwasababu kinavusha watu wachache na mizigo kidogo.

Aidha amesema ujenzi huo unaotarajiwa kuanza muda wowote kuanzia hivi sasa unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 kutokana na maagizo ya Serikali awamu ya sita.

 Ametaja daraja jingine ambalo limeingizwa kwenye mpango wa kufanyiwa ukarabati mkubwa na fedha yake italetwa wakati wowote kuwa ni Kyetema, linaunganisha

Barabara kuu kutoka Dar es Salaam na mikoa mingine kuingia Bukoba na nchi jirani ya Uganda.

"Nitumie fursa hii kwa niaba ya Wananchi wa jimbo la Bukoba vijijini nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake mkubwa kwetu ametoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo yetu"alisema Dokta Rweikiza.

Ameongeza kuwa kuna mradi mkubwa wa maji Kemondo ambao umekamilika na wananchi wanatarajia kupata maji mwezi mmoja ujao.

Naye askofu wa Dayosisi ya kaskazini magharibi (KKKT)  Abedinego Keshomshahara amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inafanya maendeleo makubwa kwa Wananchi pia mbunge Rweikiza amekuwa kiungo kizuri kati ya wananchi,Serikali na viongozi wa dini zote.

Kwa upande wa katibu mkuu mstaafu wa chama cha Mapinduzi (CCM),katibu mkuu kiongozi mstaafu,Balozi na mbunge Dkt .Bashir  amesema Mbunge huyo ameonyesha mfano mzuri kwa Wananchi wake na Taifa kwa ujumla.

"Maombi ya miradi hiyo ililetwa kwenye chama wakati wa Serikali ya awamu ya tano na mbunge Rweikiza ambapo tuliingiza kwenye Ilani ila kutokana na maono mema ya Rais Dokta Samia  ameamua kutoa fedha nyingi ili ikajengwe na kunufaisha Wananchi" alisema Dokta Bashir.

Share:

BONANZA LA MICHEZO DR. SAMIA - JUMBE HOLIDAY LA KUFUNGA MWAKA 2024 NA KUUKARIBISHA MWAKA 2025 LAPAMBA MOTO SHINYANGA


Na Marco Maduhu,SHINYANGA

BONANZA la Michezo Dr. Samia/Jumbe Holiday limeendelea kushika kasi katika viwanja vya CCM Kambarage Mjini Shinyanga, kwa kuchezwa michezo mbalimbali.
Jackline Isaro (kulia) akicheza bao mara baada ya kuzindua bonanza hilo.

Mratibu wa bonanza hilo Jackline Isaro akizungumza juu ya bonanza hilo amesema linafanyika leo Desemba 31,2024 na kutamatika Januari Mosi 2025 majira ya saa 7 usiku katika viwanja vya mpira wa kikapu Risasi huku washindi wakipewa zawadi zao.
Jackline akizungumza kwa niaba ya James Jumbe ambaye ndiyo muandaaji wa bonanza hilo, amewataka majaji watende haki ili washindi wapatikane kwa uhalali.

Aidha, michezo ambayo inachezwa kwenye bonanza hilo ni mbio za baiskeli, mchezo wa bao,drafti,karata,ususi,Ps Game,Mpira wa pete,kikapu,kufukuza kuku kwa jinsia zote,kushindana kula,Polltable,kucheza mziki.
Michezo mingine ni mpira wa miguu, ambapo itakuwa kati ya bodaboda dhidi bajaji,bingwa wilaya ‘Ranges’ dhidi ya ngokolo, pamoja na DERBY ya upongoji.

Zawadi za washindi ni kwamba katika mbio za baiskeli mshindi katika makundi manne zawadi ni sh.milioni 2.1,mchezo wa bao mshindi wa kwanza sh.100,000,drafti mshindi wa kwanza sh.100,000, karat ash.100,000,msusi sh.100,000, Ps game mshindi wa kwanza sh.200,000 wapili sh.100,000, watatu sh.50,000.
Mpira wa pete, washindi wa kwanza watapewa sh.500,000, kleti za soda 7, mchele kilo 50, washindi wa pili sh.300,000, mchele kilo 50 na soda kleti 7.

Mpira wa kikapu kwa njinsia zote, mshindi wa kwanza atapa sh.500,000 na wapili sh.300,000.
Mchezo wa kufukuza kuku kwa jinsia zote washindi wa kwanza watapa kuku na sh.20,000, na mchezo wa kushinda kula washinda wakwanza watapata sh.20,000, huku mchezo wa polltable mshindi wa kwanza ataibuka na kitita cha sh.100,000, wapili sh.50,000.

Kwa upande wa mpira wa miguu timu ya bodaboda dhidi ya bajaji, mshindi wa kwanza atapata sh.500,000, Ng’ombe mmoja,kleti 7 za soda na mchele kilo 100, wapili sh.300,000, ng’ombe mmoja na mchele kilo 100.
Zawadi zingine bingwa wa wilaya Rangers dhidi ya Ngokolo, mshindi wa kwanza atapata 500,000,Ng’ombe mmoja, mchele kilo 100 na kleti 10 za soda, wapili atapata sh.300,000,Ng’ombe mmoja na soda kleti 10.

DERBY ya upongoji kwamba mshindi wa kwanza atapata sh.1,000,000, Ng’ombe mmoja,mchele kilo 100 na kleti 10 za soda, huku mshindi wa pili akipata sh.500,000,Ng’ombe mmoja, mchele kilo 100 na soda kleti 10.

TAZAMA PICHA👇👇
Mratibu wa bonanza la michezo Dr.Samia/ Jumbe Holiday Jackline Isaro akizindua bonanza hilo.
Mratibu wa bonanza la michezo Dr.Samia/jumbe Holiday Jackline Isaro akicheza bao.
Michezo mbalimbali ikiendelea kuchezwa kwenye bonanza hilo.
Share:

RAIS SAMIA AMLILIA JAJI WEREMA

 

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa familia ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Frederick Werema, huku akiwataka kuwa na subira na imani kufuatia kifo cha nguli huyo wa sheria nchini.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha

Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, mheshimiwa Jaji mstaafu Frederick Werema. 

Ninatoa pole kwa familia, mheshimiwa Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Majaji, ndugu, jamaa na marafiki”

“Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra na imani katika kipindi hiki cha kuomboleza msiba huu, na ailaze roho ya mpendwa wetu huyu mahali pema peponi,”- amesema.

Rais Samia ametuma salamu hizo kupitia mitandao yake ya kijamii leo Jumatatu, Disemba 30, 2024, muda mchache tangu kutolewa kwa  taarifa za kifo cha Jaji mstaafu  Werema zilipoanza kusambaa mitandaoni.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger