Monday, 19 August 2024
MANALA AANDIKA BARUA YA WAZI KWA RAIS SAMIA , UJENZI WA UWANJA WA NDEGE KAHAMA

Barua ya Wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Kupitia Waziri wa Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi
Mhe. Rais,
YAH: OMBI LA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE KATIKA MANISPAA YA KAHAMA
Kwa heshima na taadhima, napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza Mhe. Rais kwa kazi kubwa na nzuri inayoendelea kufanyika chini ya uongozi wako thabiti. Nikiwa mwananchi na mdau wa maendeleo katika Manispaa ya Kahama, napenda kuwasilisha ombi langu la kujenga uwanja wa ndege ndani ya manispaa hii muhimu, ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii katika eneo hili na nchi kwa ujumla.
Manispaa ya Kahama, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, inakadiriwa kuwa na idadi ya watu takribani milioni 1. Hii inaashiria kwamba nusu ya wakazi wa Wilaya ya Kahama wanatoka ndani ya manispaa hii. Ukosefu wa uwanja wa ndege katika eneo hili umekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na usafirishaji wa haraka wa abiria na mizigo. Watu wengi wanakosa huduma hii muhimu, hali inayosababisha gharama kubwa za usafiri na muda mwingi kwa wakazi wa Kahama na maeneo jirani wanapotumia viwanja vya ndege vya Shinyanga au Mwanza.
Kahama ni miongoni mwa wilaya zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa kupitia vitega uchumi mbalimbali kama vile madini, kilimo, na biashara.
Uwepo wa uwanja wa ndege katika Manispaa ya Kahama utachochea zaidi ukuaji wa sekta hizi kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma, na kuongeza mapato ya serikali. Takwimu zinaonyesha kuwa uwepo wa uwanja wa ndege unaweza kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi kikubwa kupitia ada na kodi mbalimbali zinazohusiana na shughuli za usafiri wa anga.
Pamoja na faida hizo kwa serikali, wananchi, wafanyabiashara, na makundi mengine yatakayohusishwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na huduma hii, watapata fursa za ajira, kuongezeka kwa usafirishaji wa bidhaa za kilimo, madini, na biashara, pamoja na kuboresha hali ya maisha kwa ujumla. Manispaa ya Kahama ikiwa na vitega uchumi vingi, mabadiliko haya yatakuwa na athari chanya kwa uchumi wa eneo hili na taifa kwa ujumla.
Iwapo utekelezaji wa mradi huu muhimu utachelewa kutokana na sababu mbalimbali, napendekeza hatua mbadala kama ifuatavyo:
1. Kutathmini na kupanua uwanja wa ndege wa Buzwagi: Uwanja huu ambao sasa ni mali ya serikali, unaweza kufanyiwa tathmini na kupanuliwa ili kukidhi mahitaji ya usafiri wa anga kwa Kahama na maeneo jirani.
2. Kupitia upya ratiba za ndege: Kupitia na kuongeza idadi ya siku za safari za ndege zinazotumia uwanja huo kwa wiki, ili kupunguza gharama kwa wakazi wa Kahama na maeneo jirani wanapolazimika kusafiri hadi Shinyanga au Mwanza kwa huduma hiyo.
Napenda kumalizia kwa kutoa pongezi kwa serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuendelea kutekeleza ahadi kwa Watanzania, wakiwemo wananchi wa Kahama.
Naomba maombi yangu yaweze kupokelewa na kufanyiwa kazi kwa ajili ya maendeleo ya Manispaa ya Kahama na taifa kwa ujumla.
Nakutakia kazi njema na utekelezaji wa majukumu yenu kwa maslahi ya Watanzania wote.
Wako katika ujenzi wa taifa,
Mhandisi Dkt. Manala Tabu Mbumba
Mdau wa Maendeleo Kahama
TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA MAFUTA NA GESI MACHI 2025
Na Mwandishi wetu.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameshiriki katika kikao cha maandalizi ya Mkutano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE'25) unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 5 hadi 7 Machi, 2025 katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku tatu wa kimataifa utafanyika chini ya kauli mbiu “Unlocking Investment in Future Energy: The Role of Petroleum Resources in the Energy Mix for Sustainable Development in East Africa” ambapo utatanguliwa na kufuatiwa na safari za kutembelea maeneo ya kijiolojia na kujionea vivutio mbalimbali kitalii vilivyopo katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Aidha, watazungumzia masuala ya mabadiliko kuelekea katika matumizi ya nishati safi na kuwakutanisha wadau zaidi ya 1000 kutoka mataifa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Biteko alisema “Kama nchi tumepata fursa ya kuandaa mkutano huu wa kimataifa na Serikali imepanga kufanya hivyo kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuandaa mkutano wenye tija kwa nchi na kutoa nafasi kwa Watanzania kufaidika na uwepo wa mkutano huu”.
Dkt. Biteko alitoa rai kwa wahudhuriaji wa kikao hicho kutumia vema fursa ya uwepo wa mkutano wa EAPCE’25 kutangaza biashara, huduma na utaalamu wao pamoja na kujenga mitandao na washirika kutoka mataifa mbalimbali.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba alieleza kuwa mkutano wa EAPCE’25 pia utahusisha maonesho ya huduma na bidhaa mbalimbali na hivyo kutoa fursa kwa wadau kuchangamkia fursa hiyo.
“Sambamba na mkutano na maonesho eneo lingine ambalo wadau wanakaribishwa kuchangamkia ni udhamini wa mkutano ambao unatoa nafasi ya kujitangaza ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia ukubwa wa mkutano wenyewe” alisema Mha. Mramba.
Kikao hicho ni cha awali cha maandalizi kuelekea mkutano wa EAPCE'25. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti (www.eapce25.eac.int)
Sunday, 18 August 2024
WAKALA WA VIPIMO ZANZIBAR WAJIFUNZA KUTOKA WMA BARA
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai (katikati), akisikiliza maelezo kutoka kwa Mussa Kongola, Msimamizi wa Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Kampuni ya Maurel & Prom, Madimba Mtwara (kushoto). Kulia ni Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mtwara (WMA), Saad Haruna. Simai alitembelea Mtwara Agosti 16 na 17, 2024 kujifunza namna WMA mkoani humo inavyotekeleza majukumu yake.
********************
Veronica Simba – WMA
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai amefanya ziara ya siku mbili mkoani Mtwara kwa lengo la kujifunza majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) ambapo amekiri kunufaika zaidi ya alivyotarajia.
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake, Agosti 17, 2024 Simai amesema lengo hasa la ziara hiyo lilikuwa kutembelea eneo linalotumiwa na Wakala wa Vipimo Mtwara kwa ajili ya ukaguzi na uhakiki wa magari ya kusafirishia mafuta ili ZAWEMA ikatumie teknolojia hiyo na kuboresha zaidi huko Zanzibar.
“Hata hivyo, ziara hii imekuwa ya mafanikio makubwa kwetu kwa sababu tumepata zaidi ya kile tulichokusudia,” amesema.
Akifafanua, Simai ameeleza kwamba mbali na kujionea na kujifunza kuhusu uanzishaji wa mtambo wa ukaguzi na uhakiki wa magari ya kusafirishia mafuta, amepata fursa ya kutembelea maeneo mengine ambako WMA hutekeleza majukumu yake ikiwemo Bandari ya Mtwara na katika eneo ambalo gesi asilia huvunwa na kuchakatwa huko Madimba.
Amesema, matarajio yake ni kwenda kuibua miradi mbalimbali ukiwemo wa ujenzi wa eneo la ukaguzi wa magari ya mafuta ambao utaenda sanjari na ujenzi wa mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa dira za maji kwa njia ya kielektroniki. “Hata hivyo kwa nilichokiona huku WMA Mtwara, iko haja kutumia mtambo wa kawaida pia pamoja na uwepo wa huo wa kielektroniki,” ameeleza.
Simai amemshukuru Mtendaji Mkuu wa WMA Tanzania Bara, Alban Kihulla kwa ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwa ZAWEMA katika kuhakikisha wanatimiza matarajio yao ya kutekeleza majukumu ya uhakiki vipimo kwa ufanisi na tija kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar.
Awali, akieleza kuhusu majukumu yanayotekelezwa na WMA mkoani Mtwara, Meneja wa Mkoa wa Wakala hiyo, Saad Haruna amesema ni pamoja na uhakiki wa vipimo ambavyo hutumika katika sekta za kilimo, biashara, mazingira pamoja na usalama.
Katika sekta ya kilimo, Haruna amesema WMA huhakiki mizani zinazotumika wakati wa kununua mazao pamoja na wakati wa kuyasafirisha.
Aidha, kwa upande wa biashara amesema WMA inawajibika kuhakiki vipimo vinavyohusiana na sekta hiyo ambapo ametoa mfano wa mafuta yanayosafirishwa kutoka nchi za nje kuletwa nchini kupitia Bandari ya Mtwara.
“WMA hufanya uhakiki kuanzia Bandarini mafuta yanaposhushwa na kupita kwenye kipimo maalum kijulikanacho kama ‘flow meter’ kwa lugha ya kigeni, zoezi ambalo huendelea kufanyika katika matenki ya kuhifadhi mafuta, vituo vya mafuta na katika pampu zinazotumika kujaza mafuta katika magari.”
Vilevile, Haruna amesema jukumu lingine ambalo hutekelezwa na WMA mkoani humo ni kuhakiki dira mpya za maji ambazo hutumika kuwafungia wateja maji pamoja na zile ambazo zilikwishaanza kutumika.
Pia, katika sekta ndogo ya gesi asilia, amesema WMA huwajibika kuhakiki vipimo vyote vinavyotumika kupima kiwango cha nishati hiyo kuanzia inapovunwa hadi kiwango kinachopelekwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kiwango kinachopelekwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na hata kile kinachopelekwa kwa Kampuni kubwa ya kuzalisha saruji ya Dangote.
Akizungumzia malengo ya kuhakiki vipimo, Haruna amesema ni jukumu la Serikali kupitia Wakala wa Vipimo, kuhakikisha pande zote zinalindwa yaani mlaji apate bidhaa kadri alivyolipia bila kupunjwa ilhali muuzaji apate malipo stahiki kulingana na kiwango alichouza.
Kwa upande wake, mmoja wa Wasimamizi wa Mtambo wa kuchakata gesi asilia katika Kiwanda kilichoko Madimba, Mussa Kongola ameipongeza Serikali kwa kuanzisha Wakala wa Vipimo akisema inatekeleza majukumu muhimu sana yanayozinufaisha pande zote.
“Uwepo wa jicho la tatu ni muhimu sana ili kuhakikisha pande zote zinanufaika kwa kupata kilicho stahiki na kwakweli nimewafahamu WMA kwa muda mrefu, kazi yao ni njema sana,” amesisitiza.
Ikumbukwe kwamba, kwa mujibu wa takwimu kutoka TPDC, asilimia 60 ya umeme unaozalishwa nchini kupitia TANESCO hutokana na gesi asilia. Aidha, korosho ambazo huzalishwa kwa wingi mkoani Mtwara ni moja ya mazao ya kimkakati yanayolimwa nchini. Vilevile, uwepo wa Bandari ya Mtwara pamoja na maeneo mengine mbalimbali ambayo yanatumia vipimo, vyote vinadhihirisha umuhimu wa uwepo wa Wakala wa Vipimo kwa manufaa ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Utendaji mzuri wa wataalamu wa Wakala wa Vipimo Tanzania Bara umekuwa ukivutia nchi mbalimbali kuja kujifunza namna bora ya kuendesha sekta hiyo.
Ziara ya mafunzo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar imefanyika mkoani Mtwara badala ya Dar es Salaam au Mkoa mwingine kulingana na ukubwa wa kazi zinazotekelezwa na ZAWEMA ambao unaelezwa kuwiana na majukumu yanayotekelezwa na WMA Mtwara.
Mojawapo ya Mita zinazopima kiwango cha gesi asilia inayovunwa na kuchakatwa katika kiwanda kilichoko Madimba, Mtwara, ikiwa na nembo/alama ya Wakala wa Vipimo (WMA) kuthibitisha kwamba Mita hiyo imehakikiwa na Wakala hiyo. Taswira hii ilichukuliwa Agosti 17, 2024 wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai, ilyolenga kujifunza namna WMA Mtwara inavyotekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai (mwenye fulana nyeusi-kushoto), akiwa katika ziara ya mafunzo Bandari ya Mtwara. Agosti 17, 2024 kujionea na kujifunza namna majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) katika sekta mbalimbali.
Mojawapo ya Mita zinazopima uzito wa magari yenye makaa yam awe kutoka katika Bandari ya Mtwara, ikiwa na nembo/alama ya Wakala wa Vipimo (WMA) kuthibitisha kwamba Mita hiyo imehakikiwa na Wakala hiyo. Taswira hii ilichukuliwa Agosti 17, 2024 wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai, ilyolenga kujifunza namna WMA Mtwara inavyotekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali.
Gari lililobeba makaa ya mawe likipimwa uzito katika Bandari ya Mtwara kwa kutumia Mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA). Taswira hii ilichukuliwa Agosti 17, 2024 wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai, ilyolenga kujifunza namna WMA Mtwara inavyotekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai (katikati), akisisitiza jambo kwa Mussa Kongola, Msimamizi wa Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Kampuni ya Maurel & Prom, Madimba Mtwara (kushoto) na Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mtwara (WMA), Saad Haruna. Simai alitembelea kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia Agosti 17, 2024 kujifunza namna WMA mkoani humo inavyotekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai (kushoto), akiwa katika ziara ya mafunzo katika kiwanda cha kuchakata gesi asilia kilichoko Madimba, Mtwara, Agosti 17, 2024 kujionea na kujifunza majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) katika sekta mbalimbali.
Saturday, 17 August 2024
UMMY AMSHUKURU RAIS DKT SAMIA
Na Hadija Bagasha Tanga,
Aliyekuwa Waziri wa afya ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa heshima kubwa ya kuwa Waziri wake kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu akiitumikia nafasi ya waziri ofisi ya Rais Tamisemi na baadaye wizara ya afya huku akisema ameyapokea mabadiliko hayo kwa moyo mkunjufu na kwa moyo wa shukrani.
Ummy ametoa shukrani hizo wakati akizungumza kwenye mkutano wa ndani katika ziara ya Makamu wa pili wa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah ambaye ni mlezi wa kichama katika Mkoa wa Tanga.
Ummy amesema kuwa ameyapokea mabadiliko yaliyotokea kwa moyo mkunjufu na kwa moyo wa shukrani kwani Rais Samia ameonyesha Imani yake kwake Kwa kiwango kikubwa huku akiahidi sasa kuwatumikia wanatanga ipasavyo.
"Nimeyapokea mabadiliko haya kwa moyo mkunjufu lakini kwa moyo wa shukrani namshukuru Mwenyezi Mungu kwa yaliyotokea kubwa nikuahidi mheshimiwa Makamu wa Rais nitaendelea kuwa mwaminifu na mtiifu kwa Mwenyekiti wangu wa chama na chama kwaujumla lakini pia nikuahidi kwamba sasa nitafanya kazi kwa karibu sana na wananchi wangu ambao ndio walionipa heshima ya kuweka rekodi ya kuwa mbunge wa kwanza mwanamke katika jimbo la Tanga,"alisisitiza Ummy.
Aidha Ummy amesema kwamba kazi kubwa sasa iliyopo mbele yao ni kuendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi katika jimbo la Tanga kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa ccm Wilaya Tanga Meja Hamis Mkoba.
"Tunasimama kifua mbele watu wa Tanga kwa jinsi Rais Samia alivyorubeba ksa kuboresha bandari ya Tanga hili jambo nililisema kwa sauti kubwa na kwa nguvu kubwa wakati naomba kura tunamshukuru Rais kazi hii aliianza Rais Magufuli na sasa Rais Samia anaendeleza Bilioni 429 zimewekwa katika bandari ya Tanga, bandari ya Tanga imeboreshwa niliwaambia watu wa Tanga kwamba nataka Tanga iwe kama Singapore maana yake mameli makubwa yatie nanga katika bandari ya Tanga ndugu zangu wanatanga na sasa meli kubwa tunashuhudia zikitia nanga hapa, "alisema Ummy.
"Mheshimiwa Makamu wa Rais kwetu sisi hili moja tu tuna deni kubwa kwa Rais Samia kwani hatumdai lakini yeye anatudai ushindi wa kishindo kwa sababu mameli makubwa sasa yanatia nanga katika bandari yetu ya Tanga juzi imekuja meli ya magari 500 yamechochea ajira nimepokea vijana wa Tanga 200 na siku nyingine tutakuletea madereva wa kuendesha gari za IST wanasema kwanini wanaoendesha watoke Daresalaam wameanzisha umoja tunawafungulia ofisi ili sasa madereva wa IST watoke jiji la Tanga, "alisema Ummy.
"Nikuhakikishie Makamu wa, Rais tutakwenda nyumba kwa nyumba, shuka kwa shuka, kitanda kwa kitanda, kata kwa kata kutafuta ushindi wa chama cha mapinduzi katika mitaa yote 181 ya jiji la Tanga na kata zote 27,"alisema Ummy.
Aidha amewashukuru wanatanga Kwa kumuwezesha kutimiza historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kugombea Jimbo la Tanga na kushinda.
KIJANA AFARIKI WAKATI AKIHONDOMOLA TENDO LA NDOA NA BINTI GHETONI... CHANZO CHADAIWA DAWA ZA KUBOOST NGUVU

Kijana mwenye umri wa miaka 23 Raia wa Burundi amepoteza maisha wakati akifanya mapenzi.
Tukio hilo limeripotiwa kutokea Jumanne 12 August 2024 katika tarafa ya Kayogoro mkoani Makamba kusini mwa nchi ya Burundi.
Kijana huyo ajulikanae kwa jina la Eric(23) alipata mgeni ambaye pia alikuwa mpenzi wake aliyetambulika kwa jina la Grace (17) ndipo walipoanza kufanya mapenzi nyumbani kwa kijana huo baada ya mda Éric alipoteza maisha
Kwa mujibu wa mamlaka za vyombo vya dola na idara ya afya nchini Burundi chanzo cha kifo ni mshtuko wa moyo ambapo imedhibitishwa na daktari mkuu wa mkoa wa Makamba ambaye alifika eneo la tukio.
Majirani wa marehemu wakihisi kuwa kijana huo alitumia vidonge vya kuongeza nguvu kwenye tendo kitu ambacho hakijaweza kudhibitishwa.
Marehemu atazikwa jumamosi 17 August 2027 huku mwanamke aliyeshiriki naye mapenzi akishikiliwa na jeshi la polisi.
Kamishina wa jeshi la polisi mkoa wa makamba amefahamisha vyombo vya habari kuwa msichana huyo amewekwa kizuizini kwa ajili ya kulinda usalama wake.


















































