Friday, 7 June 2024
Thursday, 6 June 2024
KIKOSI KAZI KUUNDWA KUDHIBITI UTOROSHAJI WA MADINI MKOANI SONGWE
Na Mwanahamisi Msangi, Songwe
TUME ya Madini Mkoa wa Songwe imeunda kikosi kazi maalum cha kupambana na kudhibiti utoroshaji wa madini na kusababisha serikali kukosa mapato.
Hayo yamesemwa na Afisa Madini Mkazi - Songwe, Chone Malembo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwatembelea wachimbaji wadogo katika eneo la Mbangala lililopo mkoani humo.
“Kwa sasa kuna mawasiliano ambayo yanaendelea tunataka kutengeneza kikosi kazi madini Mkoa ambacho kazi yake itakuwa ni kufanya uchunguzi na kutoa taarifa kuhusu utoroshaji madini mahali husika ili kuchukua hatua stahiki lengo ni kudhibiti utoroshaji ambao husababisha Serikali kukosa mapato,”amesema Chone.
Katika hatua nyingine, Afisa huyo amesema wamegundua madini mapya aina ya Solidite ambayo yanapatikana Wilaya ya Momba.
SERIKALI YAAJIRI WATU WENYE ULEMAVU 1098
NA MWANDISHI WETU- KILIMANJARO
SERIKALI imeendelea kuwathamini watu wenye ulemavu nchini ambapo imeendelea kuwapa ajira watu hao huku takwimu zikionyesha toka mwaka 2022 mpaka sasa jumla ya watu wenye ulemavu 1098 wameweza kuajiriwa.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Utaribu, Ummy Nderiananga wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Balozi Emmanuel Nchimbi wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Naibu Waziri huyo alisema kuwa, alipoingia serikalini walitengeneza utaratibu wa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata ajira ambapo matokeo yake yanaoneka sasa ambapo watu hao wameweza kupata fursa za ajira.
Alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kundi la watu wenye ulemavu ambapo fedha hizo wamekuwa wakikopeshwa bila riba na kujinufaisha kiuchumi na kujiletea maendeleo.
Aidha Naibu Waziri huyo alisema kuwa, kundi hilo pia waliweza kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi ambapo kwa sasa serikali inatambua idadi ya watu hao.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo alisema kuwa, kazi kubwa imefanywa na Chama cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwaomba wananchi wa Moshi kuendelea kukiamini Chama hicho pamoja na kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika maboresho ya Daftari la kudumu la wapiga kura na kuwachagua wagombea wanaotokana na CCM.