Thursday, 16 May 2024

ForumCC YAWANOA WAATHIRIKA WA MAFURIKO MOROGORO

 
Mshauri wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi kutoka ForumCC Tanzania, Rebecca Muna 

Na Christina Cosmas, Morogoro

WITO umetolewa kwa wananchi kuongeza uelewa na utayari kabla na baada ya majanga huku wakijua namna ya kujikinga nayo ikiwemo mafuriko kwa kupunguza au kuondokana na athari za kijamii na kiuchumi.

 Wito huo umetolewa jana na Mshauri wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi kutoka Asasi ya kitaifa inayohusika na masuala ya mabadiliko ya tabianchi (ForumCC Tanzania) Rebecca Muna wakati akizungumza na waathirika wa mafuriko wa kata za Lukobe na Kihonda Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kuwapatia elimu ya namna ya kujikinga na majanga ya mafuriko na hatua za kuchukua.


 “Mabadiliko ya tabia nchi ni athari moja iliyoleta athari nyingine ya mvua za Elnino na hatimaye mafuriko katika maeneo ya Manispaa ya Morogoro na maeneo mengine ya nchi na dunia kwa ujumla, mafuriko yametokea zaidi ya mara moja na kusababisha hasara kubwa ya kuharibika kwa mali sambamba na vifo”,alisema Muna.

Muna aliongeza kuwa, moja ya njia ya kujikinga na majanga ya mafuriko ni wananchi kusikiliza na kuzichukulia hatua taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini ikiwemo mvua kubwa, upepo na vimbunga.

Alisema kwa kushirikiana na ActionAid, Plan International, CAN Tanzania kwa ufadhili Start Fund wameweza kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo mablanketi na vyakula na kuwaondoa kwenye maeneo yaliyoathirika hasa kwa waathirika wa maeneo mengine ya manispaa ya Morogoro, Malinyi, Ifakara, Lindi na Rufiji.

Afisa Tarafa Manispaa ya Morogoro Winfred Kipako aliwataka wananchi waliokumbwa na mafuriko kwenye maeneo hayo kuwa watulivu wakati serikali ikijipanga kujenga mitaro itakayotoa maji kwenye njia za reli ya SGR na kuyapeleka kwenye mto Ngerengere ili mafuriko yasijirudie tena kwenye maeneo yao.


Share:

BIL 97.178 KUTUMIKA UJENZI BARABARA YA IFAKARA-MBINGU



Na Mathius Canal, Morogoro

Imeelezwa kuwa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Ifakara hadi Mbingu yenye urefu wa kilomita 62.5 utatumia Bilioni 97.178

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imebainisha kuwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/s Henan Highway Engineering Group Co. Ltd ya kichina imepewa zabuni ya kujenga barabara ya Ifakara-Kihansi yenye urefu wa kilometa 124 sehemu ya kwanza Ifakara-Mbingu ya kilometa 62.5 kwa kiwango cha lami.

Akizungumza mara baada ya kukagua hatua zinazoendelea za kuanza ujenzi wa barabara hiyo mara baada ya mvua kubwa za El-Nino kuanza kupungua Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema kuwa kilio kikubwa cha wananachi ni kupata barabara ya lami ambapo kwa sasa kimepatiwa majawabu kwa serikali ambapo tayari imetoa fedha na mkandarasi yupo eneo la mradi kwa ajiili ya ujenzi huo.

Mhandisi Kyamba amesema kuwa mradi huo utasimamiwa na kitengo cha usimamizi wa miradi cha TANROADS (TECU) na kwa sasa mkandarasi ameanza kufanya matengenezo ili barabara inayotumika sasa ianze kupitika kwani hilo ni jukumu lake kwa mujibu wa mkataba.

Ameeleza kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa wananchi kusafirisha bidhaa mbalimbali ikiwemo za kilimo kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo mkoa wa Morogoro pamoja na mkoa wa Njombe kupitia Ifakara, Mlimba, Kihansi hadi Makambako Mkoani Njombe.

Mhandisi Kyamba amesema kuwa Mradi huo wa ujenzi wa barabara ya Ifakara-Mbingu ni wa miezi 30 ambao umeanza tarehe 8 Disemba 2023 na unatarajiwa kumalizika ifikapo tarehe 8 juni 2026.

Naye Mhandisi Ntwale Lukas ambaye ni Fundi Sanifu Mkuu wa TANROADS Mkoa wa Morogoro amesema kuwa baada ya mvua za El-Nino kupungua tayari kwa sasa magari yameanza kusomba vifusi ili kurekebisha maeneo yote korofi ili kurudisha mawasiliano ya barabara.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Igima, kijiji cha Lufufu wameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuanza kujenga barabara hiyo kwakuwa itaharakikisha maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi hasa usafirishaji wa uhakika wa mazao hususani mpunga (mchele) na ndizi.

Wamesema kukamilika kwa ujenzi wake kutapunguza gharama za usafiri na usafirishaji wa mazao hayo kwenda kwenye masoko ya mjini na kuongeza kwa thamani ya mazao ya wakulima fofauti na sasa kutokana na kuwepo changamoto za miundombinu ya barabara.




Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO ALHAMISI MEI 16, 2024

Share:

Wednesday, 15 May 2024

ELIMU INAYOTOLEWA NA TAWA YAMWOKOA MWANANCHI KUTOKA MDOMONI MWA MAMBA







Na Beatus Maganja, TAWA

Mkazi wa Kijiji cha Kasenyi kilichopo wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza Bw. Obeid Francis (44) amenusurika kuliwa na mnyamapori aina ya mamba baada ya kuikumbuka na kuitumia elimu ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu inayoendelea kutolewa na Maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA maeneo mbalimbali nchini.

Akisimulia kisa hicho Obeid amesema tukio la kukamatwa na mamba huyo lilitokea oktoba 25, 2023 Kijiji cha Kasenyi majira ya jioni (saa 1 usiku) akiwa anaoga pembezoni mwa ziwa Victoria ambapo ghafla alishtukia amekamatwa mkono wa kushoto na mamba na kutupiwa ndani ya maji yenye kina kirefu na baadae kuibuliwa.

Kwa maelezo yake kitendo cha mnyama huyo kumuibua na kumrudisha majini kilirudiwa na mnyama huyo mara kadhaa na wakati anatafuta namna ya kujiokoa alikumbuka elimu iliyokuwa ikitolewa na Maofisa wa TAWA inayoelekeza kumchoma jichoni mnyama huyo kwa kutumia kidole pale ambapo mtu anapokuwa amekamatwa na mamba, na mara baada ya kufanya hivyo mamba huyo aliruka na kupotelea majini na yeye alijikokota kutoka majini akiwa amejaa majeraha.

"Nikiwa naoga majini, wakati ninageuka kwenda kuvaa nguo zangu ghafla nilishtukia upande wa mkono wa kushoto niliona kitu kikali kimenirukia, nilishtuka kikaanza kunizamisha ndani ya maji, kitu kizito na kinene, roho iliruka na kupata hofu kubwa, fikra zilinituma kwamba hapa tayari nimekamatwa na mamba" anaeleza Obeid Francis

"Liliponiibua likaanza kunipeleka kama umbali wa hatua tano kwenye maji marefu roho ikaniambia Sasa nimekufa, sasa nifanyeje? na usiku umeanza kuingia, lakini roho nyingine ikaniambia huwa wanasema mamba ukimkamata macho atakuachia, nilifanya hivyo na ndipo aliponiachia" ameongeza

Matukio ya wananchi kupata madhara yatokonayo na wanyamapori wakali na waharibifu hasa wale waishio pembezoni mwa maziwa na mito yamekuwa yakitokana na vitendo vya wananchi hao kufanya shughuli zao karibu na maji kama vile kuogelea/kuoga, kufua na kufanya uvuvi usio rafiki mambo ambayo yamekuwa yakihatarisha maisha yao.

TAWA imekuwa ikifanya jitahada endelevu za kutoa elimu ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko maeneo mbalimbali nchini kwa wananchi ili kuwapatia mbinu za kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na wanyamapori hao na inasisitiza wananchi kuzingatia elimu hiyo ili waendelee kuwa salama.



Share:

FCS NA TRADEMARK AFRIKA WASAINI KUTEKELEZA MRADI WA BIL. 2.3

 

 

Dar Es Salaam Tanzania, 14 Mei 2024 

Foundation for Civil Society (FCS) na TradeMark Africa wamesaini makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha mazingira wezeshi na jumuishi ya kibiashara kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanajumuishwa kikamilifu katika uendeshaji wa biashara, kukabiliana na changamoto kubwa za kimfumo katika biashara na changamoto ya tabia nchi kama sehemu ya kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi Tanzania.

FCS imepokea ruzuku ya bilioni 2.3 kutoka Trademark Africa kutekeleza mradi huo ambao umefadhiliwa na Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), Ireland, na Norway, wenye thamani ya dola za kimarekani 900,000, unaolenga kuunganisha nguvu za Sekta Binafsi na Mashirika ya kiraia ili kukuza ukuaji wa uchumi wa kijani.

Makubaliano hayo yamefanyika leo Mei 14, 2024, katika Ofisi za FCS Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo  Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Justice Rutenge amesema kuwa Ulinzi wa mlaji ni muhimu katika soko la biashara la kitaifa na kimataifa, na kwamba ushirikiano wao na Trademark Africa ni hatua kubwa ya kulinda haki za mlaji na kuhakikisha faida za Biashara ni shirikishi.

"FCS inajukumu la kipekee kama AZAKI na ina uwezo wa kutumia vema ubobezi wake kushirikiana na  Sekta Binafsi kushughulikia masuala muhimu ya uharibifu wa mazingira na ukosefu wa usawa wa kijamii" amesema Rutenge.

Aidha, ameongeza kuwa mradi huo pia unalenga kuweka mazingira jumuishi na endelevu ya Biashara kwa kuongeza fursa za kibiashara kwa makundi ya pembezoni, kushirikiana na Asasi za kiraia katika kushughulikia mahitaji yao, kukuza mazingira ya biashara rafiki, na kuimarisha ulinzi wa walaji.

"Mradi huu unalenga kuboresha ustahimilivu wa Biashara dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na hivyo kuchangia katika uendelevu wa muda mrefu wa uchumi wa Tanzania na uendelevu wa mazingira.

"Ushirikiano huu unawakilisha kielelezo cha jinsi ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi unavyoweza kushughulikia kwa ufanisi changamoto za kimfumo katika masoko, na kuunda njia za mazoea ya biashara jumuishi na endelevu" ameongeza Rutenge.

Amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi kumi na minane ijayo, FCS itatekeleza mkakati katika sekta nyingi za biashara, ikilenga kupunguza athari za matumizi ya mazingira na kukuza ushirikishwaji katika manufaa ya kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Trademark Africa Elibariki Shammy amesema, Mradi huo ni muhimu kwa malengo ya kimkakati ya kuchochea ukuaji wa biashara ambao ni endelevu na shirikishi.

"Tunaamini kwamba kupitia ushirikiano huu wa kimkakati baina yetu na FCS, tunaweza kuleta matokeo chanya na makubwa katika kuboresha mazingira ya biashara jumuisha nchini.

"kuwawezesha wanawake ni jambo la maendeleo na kuwajumuisha katika biashara kunakuza uchumi na kuinua jamii nzima" amesema Shammy.

Kupitia ushirikiano huo wa Trademark Africa na FCS kwenye mradi huo kunaendeleza mfumo bora jumuishi wa biashara utakaokabiliana na changamoto za biashara za kimataifa.

Share:

Tuesday, 14 May 2024

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO MEI 15, 2024

Share:

MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI NI KIKWAZO- MTATURU




MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ameishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukaa na wizara za kisekta ili kusaidia wakulima na wafugaji kuondokana na migogoro.

Amesema migogoro mingi ya wakulima na wafugaji hutokana na kutotengwa maeneo halisi ya wafugaji na hali hiyo imepelekea malalamiko katika maeneo mbalimbali nchini .

Hayo ameyasema bungeni leo wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambapo amesema suala hilo likifanyika litafanya mfugaji asionekane ni yatima.

“Kwa sababu kuwa na mifugo mingi kama ulivyosikia wengine wakisema si laana ni rasilimali kila mmoja anajivunia alichonacho

Hivyo naomba migogoro hii iweze kutatuliwa kwa amani ili wananchi wote waweze kufurahia mifugo yao.”

“Mheshimiwa Waziri kaa na wizara zingine zinazohusiana na wizara hii ziweze kusaidia wakulima na wafugaji kuondokana na migogoro hii,lakini mfugaji wa nchi hii asionekane ni yatima, kwa sababu kuwa na mifugo mingi, kama ulivyosikia wengine si laana ni rasilimali kila mmoja anajivunia alichonacho,la pili, naomba migogoro hii iweze kutatuliwa kwa amani ili wananchi wote waweze kufurahia mifugo yao, “ameongeza.

Aidha, Mtaturu ameshauri wataalam wa uvuvi wawepo wa kutosha watakaofanya tathimini ya mifugio kwenye maeneo yao ili kuwaondolea mzigo wataalam wa kata na vijiji wanaofanya kazi kubwa kwa niaba ya wizara.

“Kwenye eneo la wataalam unaweza kuwa na mipango mizuri kwenye level ya wizara lakini kule chini kwenye halmashauri hatuna wataalam huko, wa uvuvi, leo tunalia kule kwa sababu watalaam wa kata na vijiji ndio wanafanya kazi kubwa, kwa niaba ya wizara, Niombe sana tuongeze watalaam, waende wakafanye tathimini ya mifugo kwenye maeneo yetu, “amesema Mtaturu.

Kuhusu ujenzi wa majosho, amebainisha kuwa kwenye eneo hili kuna deni kwakuwa aliomba majosho manne hata hivyo hadi sasa lipo moja tuu hivyo kushauri yaongezwe.

“Nilikuomba majosho manne, umenipa moja katika kata ya Ntuntu lakini kuna josho muhimu lipo katika kata ya Siuyu, lile josho linatakiwa liondolewe katika maeneo ya kanisa niombe sana lile josho mnijengee ili wananchi wale waendelee kupata huduma za kuogeshea mifugo yao na kuweza kusaidia inenepe vizuri.”

Pia, ameomba kujengwa majosho ya kuogeshea na kulishia mifugo katika maeneo ya Issuna, Mang’onyi, Unyahati na Siuyu kwakuwa uhitaji ni mkubwa.

PONGEZI WA RAIS SAMIA.

Mtaturu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya katika kusimamia maendeleo ya nchi ambapo kupitia sekta zote kazi kubwa imefanyika hata kwenye sekta ya mifugo na uvuvi.

Aidha, amempongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Naibu Waziri Alexander Mnyeti, Katibu Mkuu Profesa Riziki Shemdoe kwa kazi kubwa wanazofanya.

“Sekta hii ni muhimu kwa uchumi wa nchi lakini chakula kama ambavyo tumekuwa tukielezwa kama siku ya protini ambayo ipo kwenye viwanja vya bunge, tumeambiwa kitakwimu tuna ng’ombe milioni 37.6 lakini tuna mbuzi na kondoo wa kutosha.”

Amesema kuwa maana yake ikitumika vizuri rasilimali hii inaweza kubadilisha uchumi wa nchi yetu na kuongeza pato la taifa kama mipango ikiwekwa vizuri.

“Ninamaani kabisa tukitumia rasilimali hii vizuri tukajipanga vizuri kulingana na mipango ambayo umetuambia, lakini tumpongeze Rais ametuongezea bajeti kutoka bilioni 169 hadi bilioni 460 ni zaidi ya asilimia 63 imeongezeka,”amesema Mtaturu.

Amebainisha kuwa maana yake ni kwamba kuna dhamira ya dhati kwa serikali kuhakikisha kwamba yale ambayo ni matamanio ya wizara hii kuwekeza rasilimali watu kupitia mipango mbalimbali ikifanyiwa kazi vizuri itaongeza uchumi wa wizara hii kwa kiasi kikubwa.

Aidha, ameipongeza wizara kwa bandari ya uvuvi kilwa masoko huku akieleza kuwa uwekezaji huo wa zaidi ya sh. bilioni 286 utawezesha meli zinazopaki eneo hilo kupeleka samaki inapotakiwa jambo ambalo litaongeza uchumi mkubwa katika sekta ya uvuvi.

Share:

MAENEO YALIOATHIRIWA NA MVUA BARABARA YA DAR-LINDI-MTWARA YOTE NI SHWARI


Barabara ya Dar es salam-Lindi-Mtwara sasa imerejea katika hali ya kupitika baada ya kukamilika urejeshaji wa mawasiliano katika maeneo yote yaliyokuwa yamekatika.

Mvua kubwa zilizoambata na Kimbunga Hidaya ziliharibu miundombinu ya barabara hiyo katika eneo la Mikereng’ende, Songas, Somanga na Matandu-Nangurukuru ambayo yalikatika kutokana na mvua zilizonyesha na kuambatana na Kimbunga Hidaya.

Juzi tarehe 9 Mei 2024 Magari ya Mizigo, Mabasi na magari mengine madogo yaliyokwama yalianza kuruhusiwa kuendelea na safari jambo ambalo liliamsha hisisa mseto kwa wananchi kuwapongeza wataalamu wa Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) kwa kazi waliyoifanya usiku na mchana katika kurejesha miundombinu hiyo.

Wakati huu wa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali, wananchi, wasafiri, wasafirishaji na watumiaji wengine wa barabara wanapaswa kusafiri kwa tahadhari kwani maeneo mengine yanaendelea na matengenezo.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger