Friday, 26 May 2023

WADAU SEKTA YA WANYAMAPORI NA MISITU WAONA MWANGA UTENDAJI WIZARA YA MALIASILI, WAMPONGEZA MHE. RAIS



Na John Mapepele

Wadau wa Sekta za Wanyamapori na Misitu nchini wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayofanywa hivi sasa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii hususan kasi ya utendaji wa viongozi wa wizara, ushirikishwaji wa wadau na kutangaza utalii kimataifa.

Wadau hao wametoa kauli hizo kwenye mkutano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa sekta za Wanyamapori na Misitu uliofanyika leo Mei 25, 2023 jijini Arusha.

Wamefafanua kuwa katika kipindi kifupi baada ya Rais Samia kuteua viongozi wapya wa Wizara, mwanga wa matumaini ya maendeleo na mapinduzi makubwa umeanza kuonekana.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji na Wauzaji wa Nyamapori Tanzania, Fransis Nade amesema katika kipindi hiki cha takribani miezi mitatu kumekuwa na ushirikishwaji mkubwa kwa wadau ambapo kumekuwa na mapitio makubwa ya maeneo mbalimbali ambayo yatasaidia kuboresha uhifadhi wa raslimali nchini.

Amesema njia pekee ya kuimarisha sekta hizo ni kuwashirikisha wadau kwa kufanya majadiliano ili waweze kutoa changamoto wanazokabiliana nazo hatimaye sekta iweze kutoa mchango mkubwa katika taifa ambapo mkutano wa leo umeshirikisha wadau wote.

“Ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa kutuletea mabadiliko haya katika kipindi hiki kwenye Wizara yetu, Mungu ambariki sana kwani kazi kubwa imefanywa na viongozi wa wizara tunaamini sekta zetu zinakwenda kuchangia kiasi kikubwa kwenye uchumi wetu." amefafanua mdau wa Wanyamapori Jackson Msome.

Mdau wa asali mwenye uzoefu wa miaka 53 katika sekta hiyo, Kimishua Yona amesema kiwango ambacho Waziri Mchengerwa alielekeza katika kilele cha siku ya Misitu na Asali cha kuzalisha tani 138000 kutoka tani 35000 kwa mwaka za sasa kinaweza kwenda mara mbili zaidi kama wananchi watatumia utaalam.

Akiongea na wadau hao, Mchengerwa amesema katika kipindi hiki kifupi amebaini changamoto kadhaa ambazo amesema zinakwenda kutatuliwa.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na Kampuni za Uwindaji wa Kitalii kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani, (Value Added Tax) kwa huduma zisizotozwa kodi (Non - taxable services).

Kumekuwa na ucheleweshaji wa migawo ya fedha kwa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Jamii kutokana na kubadilishwa kwa mfumo wa ukusanyaji wa fedha na uhakiki wa viwango vinavyopaswa kutumwa.

Aidha, amesema kuwepo kwa tozo nyingi katika biashara ya mazao ya misitu na amefafanua kuwa Wizara imechukuwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na mamlaka zinazohusika ili kuona uwezekano kupunguza viwango vya tozo.

Mathalani Tozo ya CESS imepunguzwa hadi asilimia 3. Wizara inaendelea kulifanyia kazi suala hili.Pia kukosekana kwa wataalam wa kada ya misitu na ufugaji nyuki katika Halmashauri za Wilaya nyingi nchini hali inayosababisha mwitikio mdogo wa wananchi kushiriki katika shughuli za sekta za misitu pamoja ufugaji nyuki na kukosekana kwa soko la pamoja la mazao ya nyuki.

Amewataka watendaji wa Wizara kubadilika na kuwa na uchungu wa nchi yao.
Share:

Thursday, 25 May 2023

MIDAHALO YA KUPINGA UKATILI KWA WANAFUNZI MSALALA YAIBUA HOJA YA UANZISHWAJI WA KLABU ZA UKATILI


Mwezeshaji katika Mdahalo wa kupinga Ukatili wa Kijinsia Jackson Malangila kutoka Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) akizungumza na wanafunzi wa shule ya Msingi na Sekondari Lunguya hawapo pichani
Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Lunguya wakiandika ujumbe wa kupinga ukatili kwenye Bango wakati wa Mdahalo wa kupinga ukatili
Mwanafunzi kidato cha Tatu katika shule ya sekondari Lunguya Lameck John akichangia Mada kwenye mdahalo wa kupinga ukatili wa kijinsia

Na Salvatory Ntandu - Msalala

Uanzishwaji wa midahalo ya kupinga ukatili wa kijinsia katika Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga kupitia mradi wa Ushirikishwaji wa Jamii kwa njia ya Midahalo wenye dhima ya kutokomeza ukatili na mila na desturi hasi kwenye jamii imetajwa kuleta tija kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuzitambua haki zao za msingi.

Hayo yamebainishwa leo na baadhi ya washiriki wa Mdahalo huo akiwemo Godfrey Tinya, Mwanafunzi wa Darasa la sita Shule ya Msingi Lunguya wakati akichangia hoja hiyo amesema ipo haja ya kuundwa kwa klabu za kupinga ukatili zitakazowawezesha kupaza sauti uliofanyika katika shule ya Msingi Lunguya.

Amesema kuwa wapo baadhi ya wanafunzi pindi wanapofika darasa la Saba hushawishiwa na wazazi wao wafanye vibaya katika mtihani wa mwisho ili wakaozeshwe,au kuozeshwa hali ambayo husababisha kukosa haki zao za msingi za kielimu na endapo Klabu zitakuwepo zitasaidia kuibua ukatili huo.

Naye Patrick Magembe Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Lunguya amesema Klabu hizo zitasaidia kukemea vitendo vya ukatili kwa wanafunzi wa kike katika jamii kwani wengi wao watakuwa wanazitambua haki zao za msingi.

“Midahalo hii ina tija tuomba Serikali na Wadau tuendelee kujengewa uwezo pindi zitakazoanzishwa Klabu hizi zitasaidia kuleta matokeo chanya kwetu na ni msaada kwa wanafunzi wa kike ambao hawana sehemu pa kupazia sauti,”amesema Magembe.

Kwa upande wake Tumain Makemba mwalimu wa Malezi katika shule ya sekondari Lunguya amesema kuwa watahakikisha wanasimamia zoezi la uanzishwaji wa klabu hizo na kutoa rai kwa serikali na wadau wengine kuzijengea uwezo pindi zitakapoanzishwa ili ziwezekuwa na uwezo wa kujiendesha.

Akizungumza katika Mdahalo huo Jackson Malangila kutoka Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) Wakuu wa Shule hizo wanaweza kuanzisha Klabu hizo ili kuleta matokeo Chanya kutokana na mradi huo kujumuisha makundi mbalimbali katika jamii ili kuwa sehemu ya kupaza sauti kwa wenzao wenye jinsi ya Kike.
“Mradi huu unatekelezwa kwa Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) na Shirika la Misaada la Korea Kusini (KOICA) ,”amesema Malangila.

Amefafanua kuwa TGNP inasimamia midahalo hii ili kuwajengea uwezo wanafunzi kujua namna bora ya kupinga vitendo vya ukatili ambavyo husababisha madhara kama halitapatiwa suluhiso,ukatili bado upon a unafanyika kwa kificho wakipata elimu kupitia Klabu watakuwa mabalozi wazuri.

Kwa mujibu wa Takwimu za hali ya ukatili nchini zilizotolewa jana Katika Halmashauri ya Msalala na Kamishina wa Polisi Jamii, CP Faustine Shilogile amesema idadi ya Matukio ya ukatili yameongezeka na kufikia 30,566 kwa mwaka 2022 ikilinganishwa na matukio 1193 kwa mwaka 2021.

Amesema mwaka 2022 matukio ya ukatili kwa watoto yalikuwa 12163 ikilinganishwa na matukio 11419 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la matukio 670.
Share:

NAIBU WAZIRI KATAMBI AZINDUA MRADI WA KIJANA NAHODHA


 
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa Kijana Nahodha unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID), Jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (hayupo pichani) katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bi. Kate Somvongsiri akieleza jambo wakati wa hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Mradi Kijana Nahodha kutoka T- MARC Tanzania, Dkt.Tuhuma Tulli, akifafanua jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (kushoto) akizungusha mfano wa uskani wa meli kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bi. Kate Somvongsiri (kulia) kuashiria uzinduzi wa mradi wa Kijana Nahodha, hafla iliyofanyika jijini Dodoma ambapo viongozi mbalimbali wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Taasisi ya T-MARC wakishuhudia uzinduzi huo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kutoka kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Meneja Masoko wa T- MARC Tanzania Bw. Alpha Joseph (kulia) alipotembelea maonesho katika uzinduzi wa Mradi wa Kijana Nahodha unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID). Kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bi. Kate Somvongsiri.


PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

Na: Mwandishi Wetu - DODOMA

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amezindua mradi wa Kijana Nahodha unaolenga kuwafikia vijana 45,000 watakaonufaika na masuala ya elimu ya uongozi, ujasiriamali, afya na ujuzi.

Akizungumza Mei 24, 2023 kwenye uzinduzi huo wa mradi huo unaotekelezwa na Shirika la T-MARC Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID), Mhe. Katambi amesema mradi huo ni muhimu katika kuwezesha maendeleo ya kiuchumi hasa katika kuwajengea vijana uwezo wa kutumia vizuri rasilimali zilizopo ili kuleta maendeleo katika jamii.


“Aidha, miradi ya aina hii ni uthibitisho wa ushirikiano thabiti na dhati uliopo baina ya serikali ya Tanzania na Marekani, tunatambua mradi huu wa kijana nahodha utasaidia kufikia malengo tuliyokusudia ya kukwamua kijana wa kitanzania azione fursa na kuwa na mchango kwa Taifa lake,”amesema.

Naibu Waziri Katambi amewataka vijana wa mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na mikoa yote mitano ya Zanzibar kuchangamkia fursa ya mradi huo.


“Niwaombe pia viongozi na maafisa mliopo wa Wizara zote zinazohusika na utekelezaji wa mradi huu kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa ipasavyo kwa kuzingatia Sera na Miongozo ya Nchi iliyopo ili kuweza kuleta toja kwa maslahi mapana ya Taifa letu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana nchini,”amesema.


Naye, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri, amepongeza serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa jitihada za kuwainua vijana.


“Mradi huu utaleta manufaa kwa Tanzania na ni muhimu vijana wakatumia fursa ya mradi huu, nchi inayowekeza kwa vijana inapiga hatua kimaendeleo,”amesema.


Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la T-MARC Tanzania, Charles Singili, amesema mradi utainua vijana kufikia ndoto zao na unatekelezwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya nchi.


Akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi wa mradi huo, Dkt.Tuhuma Tulli, amesema utatekelezwa kwa miaka minne (2022-2026) na unalenga kusaidia vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 25 hususan vijana ambao hawana elimu ya shuleni, vijana wasio na ajira, vijana wenye ulemavu, wasichana waliozaa katika umri mdogo na wenye maambukizi ya VVU.


Amesema mradi huo unafadhiliwa na USAID kwa Dola za Marekani Milioni 10.6 na utaenda kuboresha upatikanaji wa elimu ikiwa ni pamoja na elimu ya ufundi stadi, afya, uraia, ujasirimali na uongozi.
Share:

MAHABUSU WALALAMIKIA VITENDO VYA RUSHWA MANYARA


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akifuatilia kwa makini taarifa inayotolewa na Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Nkonge Edwin alipofika gerezani hapo na timu ya wataalam wa Mama Samia Legal Aid Campaign.

*****************

-Gekul aagiza watuhumiwa kuchunguzwa.

Na Lusajo Mwakabuku – WKS MANYARA

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul ameuagiza Uongozi wa Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Manyara pamoja na viongozi wa Jeshi la Polisi Mkoani humo kufanya uchunguzi juu ya tuhuma zilizotolewa na mahabusu na Wafungwa wa gereza la Babati Mjini dhidi ya askari na watumishi wa vyombo hivyo vya haki ambapo katika nyakati tofauti wameonekana kutumia nafasi zao kudai rushwa kwa malengo ya kukwepesha haki.

Tuhuma hizo zimetolewa tarehe 24/05/2023 wakati timu ya wataalam wanaoendesha Mama Samia Legal Aid Campaign ikiongozwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul ilipofika gerezani hapo kwa lengo la kutoa elimu pamoja na msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo kubwa iliyozinduliwa mwanzoni mwa mwaka huu ambayo itadumu kwa miaka mitatu mpaka 2026.

Akiambatana na wataalamu kutoka Ofisi ya Mashtaka, Tume ya haki za binadamu, Mrakibu wa Polisi wa Mkoa, Dawati la jinsia la polisi, Wanasheria na watumishi wengine kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Naibu Waziri Gekul alifika katika gereza la Babati na kufanikiwa kuongea na uongozi lakini pia na wafungwa na mahabusu waliokuwepo katika gereza hilo lengo likiwa ni kubaini changamoto za kisheria zikiwemo upatikanaji wa dhamana kwa wafungwa wanaostahili pamoja na namna kesi zao zinavyoendeshwa.

Timu ya wataalam wa Mama Samia Legal Aid Campaign ilipokewa na uongozi wa Gereza hilo ambapo pamoja na mambo mengine, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Nkonge Edwin alimweleza Naibu Waziri kuwa moja kati ya vitu ambavyo gereza hilo limefanikiwa kuvitekeleza ni pamoja na kesi kusikilizwa kwa wakati kitu ambacho ni kilio kwa watu wengi walio vizuizini katika maeneo mengine huku akiainisha kasoro ndogondogo zikiwemo uchakavu wa vyombo vya usafiri katika kutoa huduma za wafungwa pamoja na kukataliwa kwa rufani zilizo nje ya muda.

Timu hiyo ya Mama Samia Legal Aid Campaign baada ya kuongea na uongozi wa Gereza iliingia ndani ya gereza na kuongeza na mahabusu pamoja na wafungwa ambapo elimu ya sheria ilitolewa jinsi mtu anavyokamatwa kituoni mpaka anapelekwa gerezani vitu vinavyotakiwa kufuatwa, Lakini pia mtaalam kutoka haki za binadamu alielezea haki za msingi za wafungwa wakiwemo gerezani ikiwemo haki ya dhamana kwa makosa yenye dhamana na pia Ofisa kutoka Ofisi ya Mashtaka akaongelea wajibu wa Ofisa wa mashtaka wa wilaya na muda uliopangwa kisheria wa kushughulikia kesi za watu walio vizuizini ambapo kwa kwa mkoa huu hali imeonekana kuwa shwari kwani hakuna mfungwa au maabusu aliyelalamika kupitilizwa muda wa siku 90 wa kusomewa shitaka lake mara wanapowekwa vizuizini kwa mujibu wa sheria.

Ilipofika wakati wa maswali, wafungwa na mahabusu walianza kwa kubainisha changamoto zao wanazokumbana nazo kupitia risala iliyosomwa na Mahabusu Michael Marko ambayo pamoja na mengine ilielezea changamoto ya ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi unakopelekea mrudikano wa mahabusu gerezani, Ucheleweshwaji wan akala za hukumu kwa watu ambao wameshahukumiwa, Kuporwa fedha wakati wakikamatwa na polisi na pia wakasema kumekuwa na kawaida ya mahabusu kukamatwa na kuachiwa huku pia wakiituhumu Ofisi ya Mashtaka kutokuleta mashahidi kwa wakati.

Hali ikazidi kubadilika mara baada ya wafungwa na mahabusu hao kupewa nafasi ambapo bila kusita wala uoga waliwataja maaskali na maofisa upelelezi pamoja na makarani wa mahakama kwa majina ambao waliwapora fedha wakati wakikamatwa na wengine kuwataka walipe ili kesi zao zisiendelee. Na pia mahabusu na wafungwa hao walieleza kuwa walitakiwa kutoa hela zilizoanzia milioni mbili na kuendelea ili waachiwe wakati mahabusu mwingine akidai askari alimwambia mke wake atoke Singida aje alale Manyara na siku ya pili mumewe ataachiwa (Akiashiria rushwa ya ngono)

Baada ya kupokea malalamiko hayo, Naibu Waziri aliwaagiza viongozi wa polisi pamoja na wa Ofisi ya Mashtaka alioambatana nao kuhakikisha kuwa wale wote waliotajwa katika tuhuma hizo uchunguzi wa kina unafanyika na wale wote watakaobainika kuwa wametumia mamlaka yaka yao vibaya basi hatua kali za sheria zichukuliwe dhidi yao na pia akawaagiza viongozi ha kuhakikisha wana jitihada za upatikanaji wa haki kwa mahabusu na wafungwa hao unapatika kwa wakati na bila usumbufu.
Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Nkonge Edwin akisoma taarifa ya Gereza la Babati mara baada ya Mhe. Gekul na timu yake kuwasili katika gereza hilo kwa lengo la kutoa elimu na msaada wa kisheria.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akisikiliza kesi ya mahabusu Mwajuma Mada aliyefika gerezani hapo ikiwa ni sehemu ya msaada unaotolewa na timu hiyo kwa watu walio vizuizini
.Timu ya wataalamu na uongozi wa gereza wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kazi hiyo ya kutoa msaada wa kisheria kwa watu walio vizuizini.
Share:

Wednesday, 24 May 2023

CHUO CHA TAIFA CHA UTALII (NCT) CHAHITIMISHA MAFUNZO YA UANAGENZI JIJINI DAR


Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Jesca William, Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa wanafunzi wa Kozi fupi ya Uanagenzi iliyofanyika Mei 24,2023 Jijini Dar es Salaam 

DAR ES SALAAM.

Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kimehitimisha rasmi mafunzo ya muda mfupi ya Uanagenzi yaliyodhaminiwa na Shirika la giZ kupitia mradi wa E4D.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) yamelenga kutoa ujuzi kwa vijana katika fani mbalimbali yatakayo wawezesha kuingia katika soko la ajira kwenye Sekta ya Utalii na kujiajiri wenyewe.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho Jesca William, amesema mafunzo hayo yamelenga kuongeza msukumo katika kuchangamkia fursa za ajira katika sekta hiyo kwa kuzingatia kwamba Sekta ya Utalii inazidi kukua, na watalii kuongezeka kutokana na filamu maarufu ya 'The Royal Tour' iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Afisa utumishi Halmashahuri ya Jiji la Dar es Salaam William Matto, akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji hilo, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wa maendeleo katika kuhakikisha wanawafikia vijana wengi zaidi.

Aidha amewataka wahitimu hao kutumia vyema mafunzo waliyoyapata Chuoni hapo kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi.

Nao baadhi ya wanufaika wa program hiyo wamesema kuwa, mafunzo hayo yamewasaidia kuongeza maarifa hasa katika kutekeleza majukumu yao pamoja na kuanzisha miradi binafsi.

Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kimefanikiwa kutoa wahitimu zaidi 400 tangu kuanzishwa kwa programu ya Uanagenzi Chuoni hapo, kuanzia mwaka 2014 hadi 2022 katika ngazi ya Stashahada.

(PICHA ZOTE NA: HUGHES DUGILO)

Afisa utumishi Halmashahuri ya Jiji la Dar es Salaam William Matto, akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji hilo.

Meneja Miradi wa giZ Costantine Shirati, akizungumza katika hafla hiyo.

Baadhi ya Wahitimu wakipokea vyeti..

Baadhi ya Wakufunzi wa NCT wakiwa na wanafunzi tayari kwa kukata keki maalum katika hafla hiyo.

Mkufunzi kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Mary Maduhu akizungumza alipokuwa akitoa neno la shukrani kwenye hafla hiyo.


Picha za pamoja.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger