Monday, 27 February 2023
Sunday, 26 February 2023
VIJANA WA ULINZI SHIRIKISHI WAONYWA KUJIHUSISHA NA VITENDO VYA KIHALIFU
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala liwewaonya baadhi ya vijana wa ulinzi shirikishi kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya kihalifu wakati wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi katika mitaa yao.
Rai hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala Dr. Debora Magiligimba ACP katika bwalo la Polisi Buguruni alipokutana na vijana wa ulinzi shirikishi katika Wilaya ya Kipolisi Buguruni kwa lengo la kuwapa maelekezo na mwongozo wa utakaosaidia kuboresha utendaji wa kazi za ulinzi shirikishi katika maeneo yao.
"Baadhi ya vijana wa ulinzi shirikishi mmekuwa mkishirikiana na wahalifu kwani mnatoa taarifa ya doria zenu kwa wahalifu mkiwajulisha sehemu mlipo jambo ambalo linawasaidia wahalifu hao kujipanga na kubadili sehemu ya kwenda kufanya matukio ya uhalifu",amesema.
Pia Kamanda Dr. Debora Magiligimba ametaka kila kikundi cha ulinzi shirikishi kuhakikisha kunakuwa na sare kwa ajili ya kuvaa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya ulinzi katika mitaa yao.
" Sare zinasaidia kuwatofautisha na vibaka pindi uhalifu unapotokea jambo ambalo litawasaidia wananchi kuwatofautisha na wahalifu", ameongeza.
Aidha Kamanda Dr. Debora Magiligimba amewataka vijana hao wa ulinzi shirikishi kuepuka vitendo vya ukatili katika familia zao na kutoa rai kwao kama kuna kijana wa ulinzi shirikishi ametendewa matendo ya ukatili wawezekufika katika madawati ya kijinsia na watoto yaliyopo katika vituo vya Polisi kutoa malalamiko yao.
Kikao hicho cha ulinzi shirikishi kiliudhuriwa Wakaguzi Kata 08 na vijana wa ulinzi shirikishi wapatao 139 kutoka katika Kata 08 zinazopatikana katika Wilaya ya Kipolisi Buguruni.
ASIYEJULIKANA AVAMIA KANISA KATOLIKI GEITA, AHARIBU VITU VITAKATIFU
Sehemu ya uharibifu uliofanywa
NA ROSE MWEKO, GEITA
MTU asiyefahamika amevamia na kuingia ndani ya kanisa Katoliki jimbo la Geita na kufanya uharibifu katika altare na sakrestia na kuvunja tabernakulo huku akimwaga ekaristi takatifu na kuchana kitabu kitakatifu Biblia huku akiharibu mfumo wa camera za ulinzi.
Taarifa iliyotolewa na Askofu wa Jimbo katoliki la Geita kwa njia ya simu Flavian Matindi Kasalla amesema mtu huyo alivunja kioo cha mlangoni na kuharibu madhabahu takatifu huku akiharibu sehemu mbalimbali za ibada na kuharibu vitabu vitakatifu.
“mpaka sasa hatujajua alikotokea na wala hatujui aliingia saa ngapi japo ilikua ni usiku wa kuamkia siku ya jumapili, kanisa letu linalindwa na kampuni ya ulinzi ila mpaka sasa ni kitendawili kuwa mlinzi alikuwa wapi, mtu aliyefanya tukio hilo amekamatwa na ameshafikishwa katika vyombo vya usalama pamoja na mlinzi aliyekuwa zamu siku hiyo” alisema Askofu Kasalla.
Watu wawili wanashilikiwa na jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi akithibithisha kukamatwa kwa watu hao Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita ACP Berthaneema Mlay alisema jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini nani kamtuma na sababu za kufanya uharibifu huo.
“mtu huyo anaonekana alikuwa mlinzi na ni mtu ambaye amekuwa akihudumu katika kanisani haswa huko alikotoka Bukoba hivyo jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi na itakapobainika tutatoa taarifa zaidi kwani mpaka sasa kuna mambo tunayafuatilia tatutayazungumza ili kutovuruga upelelezi.
Chanzo - The Profiletv blog
BABA AKAMATWA TUHUMA ZA KULAWITI WATOTO WAKE WA MIAKA 8 na 11 SHINYANGA MJINI
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linachunguza tukio linalomhusisha mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka zaidi ya 35 kwa tuhuma za kuwalawiti watoto wake wawili wenye umri wa miaka 8 na 11 wanafunzi wa shule ya msingi Mapinduzi B, iliyopo kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi amethibitisha mwanaume huyo kukamatwa kwa ajili ya uchunguzi.
Kamanda Magomi amesema upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Akizungumzia tukio hilo Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Kambi Butete amesema Februari 22 Mwaka huu majira ya saa tano asubuhi watoto hao walifikishwa katika Hospitali hiyo na kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari ambapo majibu ya vipimo vyao yamekabidhiwa kwa vyombo vya usalama kwa ajili ya hatua za kisheria.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mapinduzi B, Hassan Hemed ambaye ameeleza namna alivyopokea taarifa za tukio hilo, na kusema kuwa kushamiri kwa matukio hayo inachangiwa na wazazi na walezi kutowajibikia jukumu la malezi bora na makuzi kwa watoto.
‘Hizi taarifa za hawa watoto wawili nilizipokea kwa kuletewa na watu ambao wao wanasema ni wanaharakati ndiyo waliniletea hawa watoto saa sita usiku asubuhi nikaenda kwa hawa watoto mpaka wanapoishi mpaka ndani kwao ni kweli wanalala chumba kimoja na baba yao mzazi", amesema Mwalimu Hemed.
Taarifa za kulawitiwa kwa watoto hao ziliripotiwa kwa Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Mapinduzi B, usiku wa Februari 22, Mwaka huu 2023.
Via Misalaba blog
CHRISTINA MNDEME ATEULIWA KUWA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA, FRANCIS MICHAEL SONGWE, KINDAMBA TANGA
Mhe. Christina Mndeme
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi na uhamisho wa wakuu wa mikoa mitatu ya Shinyanga, Tanga na Songwe.
Wakuu wa mikoa wapya walioteuliwa ni Christina Mndeme ambaye anakwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga huku aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Francis Michael ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Christina Mndeme anachukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, ambae alichaguliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.
Aidha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba amehamishiwa Mkoa wa Tanga, huku aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Omary Mgumba uteuzi wake ukitenguliwa.
VIONGOZI NA WATUMISHI WA CHUO CHA MWEKA WAASWA KUWA WAADILIFU
Afisa Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini – Arusha Bw. Baraka Mgimba akitoa mada kuhusu Uadilifu katika mafunzo kwa viongozi na watumishi wa umma kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori –Mweka. Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 24 February, 2023 chuoni hapo mkoani Kilimanjaro
Afisa Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini – Arusha Bw. Musiba Magoma akitoa mada kuhusu Hati ya Ahadi ya Uadilifu katika mafunzo kwa viongozi na watumishi wa umma kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori –Mweka. Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 24 February, 2023 chuoni hapo mkoani Kilimanjaro.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini- Arusha imetoa mafunzo kuhusu Uadilifu kwa Viongozi na watumishi wa Umma kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori -Mweka mkoani Kilimanjaro na kuwaasa kuwa waadilifu katika Utumishi wa Umma.Mafunzo hayo yalifanyika chuoni hapo tarehe 24 February, 2023.
Akitoa mada kuhusu Uadilifu, Afisa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili kanda ya Kaskazini- Arusha Bw. Baraka Mgimba alieleza kuwa Viongozi na watumishi wote wa Umma wanapaswa kutenda kazi kwa uadilifu wa hali ya juu ikiwa ni moja ya misingi ya maadili katika utumishi wa Umma.
Bw. Mgimba alieleza kuwa uadilifu ni hali ya kufanya jambo sahihi katika wakati sahihi hata pale ambapo hakuna mtu anayekuona “uadilifu huanza nafsini mwa mtu mwenyewe ndipo unaanza kuonekana kwa wengine.”alisema.
Bw, Mgimba alielezea sifa za mtu muadilifu kuwa ni pamoja na; kujali wengine, kujitolea kusaidia watu wenye uhitaji, kuwa msikivu, kujizuia na tamaa, kuwa mnyenyekevu, kuwa mwaminifu katika hali zote pamoja sifa nyingine nyingi ambazo binadamu yeyote anapaswa kuwa nazo.
Aidha Bw. Mgimba aliendelea kusema kuwa kiongozi ama mtumishi wa Umma anapaswa kutenda kazi kwa kufuata kanuni misingi na miongozo mbalimbali iliyowekwa ili kuleta tija katika utendaji kazi wao ‘‘ Misingi hii pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa nchini ikifuatwa vizuri itakuza hali ya uadilifu kwa viongozi na watumishi wote nchini ”
Kwa mujibu wa Bw. Mgimba alieleza kuwa Serikali kupitia Sekretarieti ya Maadili imedhamiria kukuza hali ya uadilifu nchini kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa viongozi na watumishi wa umma nchini lengo likiwa ni kuwakumbusha jinsi wanavyotakiwa kuenenda katika utendaji kazi wao.
Pamoja na hayo Bw. Mgimba aliongeza kuwa kiongozi na mtumishi yeyote ni kioo cha jamii inayomzunguka hivyo anapaswa kuishi maisha yatakayoipa jamii imani juu serikali yao kwani kiongozi na mtumishi wa Umma anafanya kazi kwa niaba ya serikali ‘‘ Kiongozi na mtumishi wa umma anapokua muadilifu na kutenda kazi katika hali ya uadilifu anajenga imani ya wananchi kwa serikali yao’’
Aidha akitoa mada nyingine iliyohusu Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi na watumishi wa umma Bw. Musiba Magoma ambaye ni Afisa maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya kaskazini –Arusha alieleza kuwa kila kiongozi na mtumishi yeyote wa umma mara tuu anapoteuliwa ama kuajiriwa anapaswa kukiri Ahadi ya Uadilifu ambayo itampa dira ama mwongozo wa ni yapi anapaswa kufanya ama kutokufanya katika nafasi ama wadhifa wake .
Bw. Magoma alifafanua kuwa Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi na watumishi wa umma ina lengo la kuwahamasisha na kuwafanya kuwa na mwenendo unaofaa, inatoa nafasi kwa kiongozi na mtumishi wa Umma kujitathmini mwenyewe kutokana na kile alichoahidi na pia kuhamasisha viongozi na watumishi wa umma kuzingatia misingi ya maadili katika utendaji kazi wao.
Pamoja na hayo Bw. Magoma alieleza kuwa ipo misingi ya Ahadi ya Uadilifu inayomuongoza kiongozi kama vile Uwazi, uwajibikaji, uzingatiaji wa sheria kanuni na taratibu, kutoa huduma bora bila upendeleo, kuwa na matumizi sahihi ya taarifa pamoja na nyingine nyingi.
Katika hatua nyingine Bw. Magoma alifafanua kuwa zipo athari mbalimbali zinazotokana na kukiukwa kwa Ahadi ya Uadilifu kama vile wananchi kupoteza imani kwa serikali yao, kiongozi kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni sheria na taratibu,kiongozi ama mtumishi kusimamishwa kazi na nyingine nyingi ambazo zitaathiri hali ya kiongozi ama mtumishi wa umma, familia jamii na hata serikali kwa ujumla.
Akielezea umuhimu wa mafunzo hayo kwa watumishi hao, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Wahab Kimaro alisema kuwa mafunzo kama hayo ni muhimu kwa viongozi na watumishi wa Umma na ni vyema yakatolewa mara kwa mara kwani yanaongeza ufanishi katika utendaji kazi wao wa kila siku.
“Tumepata watumishi wapya, wapo waliohamia pia kwa hiyo ni vyema wakapata mafunzo haya ya uadilifu ili sote tuzungumze lugha moja katika kutekeleza majukumu yetu” alisema.
Pamoja na hayo Pro. Kimaro alifafanua kuwa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa viongozi na watumishi wa Umma ni moja ya silaha muhimu ya kuwafanya kuwa waadilifu kwani binadamu yeyote huwa muadilifu ikiwa kuna mahala atapaswa kujieleza ama kuchukuliwa hatua na pia kinamfanya awe na hamasa ya kutekeleza kile alichoapa.
Prof. Kimaro aliongeza kuwa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kinasaidia sana kukuza nidhamu kwa viongozi na watumishi wa umma “ Kiapo hiki ni muhimu sana kwani mtumishi wa umma anapokwenda kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa anachukuliwa hatua kwa kile alichosema kwamba atatekeleza katika kiapo chake” alisema.
Mafunzo hayo ya Siku moja yaliandaliwa na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori –Mweka mkoani Kilimanjaro.
Saturday, 25 February 2023
SIMBA SC YAONDOKA NA ALAMA TATU MBELE YA VIPERS, YAICHAPA 1-0
NA EMMANUEL MBATILO
KLABU ya Simba imefanikiwa kuondoka na alama tatu ugenini baada ya kufanikiwa kuichapa Vipers ya nchini Uganda 1-0, na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye kundi akiwa amecheza mechi tatu.
Katika mchezo huo muhimu ambao Simba Sc alihitaji kupata ushindi ili aweze kupata matumaini katika kuwania nafasi mbili za juu na kuweza kutinga robo fainali kwenye michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika inayoendelea.
Simba Sc ilifanikiwa kupata bao la mapema kipindi cha kwanza kupitia kwa beki wao kisiki Inonga Baka na kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
MADIWANI RUNGWE WATAKIWA KUSIMAMIA UTOAJI MIKOPO KWA WANAWAKE, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu ameshiriki katika Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Busokelo Wilayani Rungwe pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Akitoa salamu za Serikali katika baraza hilo, Haniu ameishukuru Halmashauri hiyo kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo kwa ufanisi na kuagiza Wakandarasi ambao hawajamaliza hiyo kufanya hivyo kwa wakati ili wananchi wapate huduma stahiki na Kwa wakati.
Wakati huohuo, Haniu ameagiza Watalamu mbalimbali katika Halmashauri hiyo kukusanya mapato ya Serikali kwa bidii huku akiomba Madiwani kuendelea kumulika vyanzo vya mapato katika maeneo yao ili kusaidia kutekeleza Miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Aidha, ameliomba baraza hilo kusimamia kwa ukaribu utoaji wa mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ikiwa ni 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Haniu ameongeza kuwa mikopo hiyo hutolewa na Serikali ili kuinua kiwango cha pato kwa wananchi, hivyo Halmashauri haina budi kutoa kwa wakati na kusimamia urejeshwaji wake ili iwanufaishe na wengine.
Katika hatua nyingine DC Haniu ameeleza Serikali imekuwa ikihamasisha wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wenye umri wa kujiunga na elimu ya Msingi sambamba na kidato cha kwanza hivyo kila mzazi na jamii kwa jumla ina wajibu wa watoto wote wanaenda shule.
Wanafunzi wawasili shuleni
Halmashauri ya Busokelo mpaka sasa wanafunzi wa kidato cha kwanza wameripoti kwa 92% na darasa la kwanza 103%.
Aidha, ameshukuru shule zote zinazotekeleza zoezi la chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari na kuagiza wazazi wote ambao hawajaanza kutekeleza zoezi hilo kuanza kufanya hivyo ili kuondoa udumavu na utapiamlo kwa wanafunzi na kuongeza ufaulu shuleni.
Migogoro ya Ardhi
Kuhusu migogoro ya Ardhi, Haniu amekemea migogoro inayoendelea katika ngazi ya kaya na Jamii na kuwa utatuzi uendelee kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa kuwashirikisha viongozi na Baraza la Ardhi.
Amesema "Migogoro mingi inatoka ngazi ya kaya ni vema suluhisho lake pia likaanzia ngazi ya kaya badala ya kugombana na kuhatarisha amani katika jamii."
Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu ameongoza zoezi la kukabidhi pikipiki kwa Watendaji wa Kata 06 na Maafisa Ugani 40 wa Halmashauri ya Busokelo Wilayani Rungwe zikiwa ni jitihada za Serikali kuongeza uzalishaji mali shambani, kukusanya mapato na uimarishaji wa utawala bora.
Akikabidhi pikipiki hizo, Haniu ameagiza Watendaji hao wa Serikali kuhakikisha wanazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuwaletea Maendeleo wananchi na kuwaondolea changamoto mbalimbali zinazowakabili hasa Vijijini."
SERIKALI ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI-MAJALIWA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa tuzo kwa washindi wa Mafunzo ya Uanagenzi kwenye kundi la Makampuni makubwa kwa mwaka 2023. Makabidhiano hayo yalifanyika katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uazalishaji rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira, kwenye hoteli ya Hyatt Kempisk jijini Dar es salaam, Februari 24, 2023.Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uazalishaji rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira, kwenye hoteli ya Hyatt Kempisk jijini Dar es salaam, Februari 24, 2023. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uazalishaji rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira, kwenye hoteli ya Hyatt Kempisk jijini Dar es salaam, Februari 24, 2023. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uazalishaji rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira, kwenye hoteli ya Hyatt Kempisk jijini Dar es salaam, Februari 24, 2023.Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTEVET) Dkt.Adolf Rutayuga akizungumza katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uazalishaji rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira, kwenye hoteli ya Hyatt Kempisk jijini Dar es salaam, Februari 24, 2023.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba-Doran akizungumza katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uazalishaji rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira, kwenye hoteli ya Hyatt Kempisk jijini Dar es salaam, Februari 24, 2023.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza jambo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uazalishaji rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira, kwenye hoteli ya Hyatt Kempisk jijini Dar es salaam, Februari 24, 2023.Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi viongozi wa makampuni makubwa walioshiriki katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uazalishaji rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira, kwenye hoteli ya Hyatt Kempisk jijini Dar es salaam, Februari 24, 2023. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi viongozi wa makampuni makubwa walioshiriki katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uazalishaji rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira, kwenye hoteli ya Hyatt Kempisk jijini Dar es salaam, Februari 24, 2023.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
**********************
NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na Sekta Binafsi katika utoaji elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutosha unaohitajika katika sekta mbalimbali.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa waajiri wote nchini waendelee kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha malengo ya kukuza ujuzi na kuongeza soko la ajira yanafanikiwa kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Februari 24, 2023) katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uzalishaji wa rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira. ”Maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote yanategemea sana ngazi ya ujuzi wa nguvukazi uliyokuwa nayo. Hivyo, mchango wa wadau ni muhimu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amewapongeza waajiri kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo (field practical), uanagenzi, utarajali pamoja na namna wanavyoshiriki wenu katika kuandaa mitaala inayotumika kwenye vyuo na taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu sana katika kuendeleza ujuzi kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda. “Nataka nitumie fursa hii kuwapongeza lakini Serikali inatambua na inathamini juhudi mnazozifanya katika utoaji wa ajira kwa wahitimu wetu, tunawapongeza sana.”
Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Uzalishaji wa Wafanyakazi Wenye Ujuzi Nchini Tanzania”, Waziri Mkuu amesema kauli hiyo ni thabiti kwani inaweka msisitizo katika ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi.
“Ni ukweli usiopingika bila ujuzi hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana. Ujuzi unahitajika kwenye nyanja mbalimbali za uzalishaji hapa nchini kwani mataifa yote yaliyopiga hatua kubwa za maendeleo yamefanikiwa kwa kuweka kipaumbele katika kuongeza rasilimali watu yenye ujuzi.”
Amesema maeneo yaliyowekewa msisitizo ni sekta za kipaumbele, kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na kati ili kuhakikisha vijana wanaohitimu wanapata maarifa na ujuzi wa kazi utakaowawezesha kujiajiri na kuajirika. “Hii ni pamoja na kuimarisha mifumo na kuongeza kasi ya kurasimisha ujuzi ili nguvukazi ya Taifa itumike ipasavyo katika soko la ajira la ndani na nje.”
Amesema kwa kutambua umuhimu wa kukuza na kuendeleza ujuzi, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan inatekeleza kwa vitendo dhamira yake ya dhati ya kuwasaidia vijana hapa nchini kupitia mipango na mikakati mbalimbali ukiwemo Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026), unaolenga kukuza ujuzi kwa Watanzania wapatao 681,000.
Waziri Mkuu amesema kulingana na utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2021, nguvu kazi ya vijana ni milioni 14.2 sawa na asilimia 55 ya nguvu kazi yote nchini, ambapo vijana milioni 12.5 sawa na asilimia 87.8 ya nguvu kazi ya vijana nchini wameajiriwa au kujiajiri.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kupitia utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ujuzi Nchini, vijana 22,899 wamepatiwa ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Kati ya hao, vijana 14,440 wakiwemo vijana wenye ulemavu 349 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi katika fani mbalimbali.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Makakati wa Taifa wa Uendelezaji wa Ujuzi wa Mwaka 2016/17-2025/26 ambao moja ya malengo yake ni kuwa na ushirikiano kati ya waajiri, wadau na vyuo au taasisi za elimu.
“Ushirikiano huu uteleta tija kubwa na kuondoa dhana ya kwamba wahitimu wetu hawana ujuzi unaohitajika katika ulimwengu wa kazi”
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTEVET) Dkt.Adolf Rutayuga amesema Mafunzo yanayotolewa kwenye Vyuo na Taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, yanaongozwa na mahitaji ya soko la ajira, hivyo, ushirikishwaji wa waajiri na wadau mbalimbali katika maandalizi ya mitaala ni muhimu sana.
"Baraza linatenga muda kama huu ili kukutana na waajiri hao na wadau wetu wa elimu va ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Kukutana huku, kunatufanya kuwa karibu na kuwa na mahusiano mazuri na wadau wetu ambapo tunakumbushana kuhusu nafasi yao katika kukuza ujuzi, na hivyo kuwaonesha kwamba wao ndio wanatakiwa kuamuru nini Kinatakiwa kufundishwa katika vyuo na taassi zetu". Amesema Dkt.Rutayuga.
Amesema ili kupata Waajiri Bora wa mwaka 2023, zoezi la uchakataji wa takwimu lilifanyika kwa kuwagawa katika makundi matatu; waajiri wakubwa (waajiriwa 100 na zaidi), Waajiri wa kati (waajiriwa 50-99) na Waajiri wadogo (waajiriwa 5-49).
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba-Doran amesema ili Tanzania iweze kushiriki kikamilifu katika soko shindani la Afrika Mashariki na dunia ni lazima hatua za maksudi zichukuliwe katika kukuza ujuzi hususani kwa vijana. “Katika kutimiza adhma hii, Chama Cha Waajiri tunaamini waajiri wana nafasi kubwa katika kufikia malengo tuliyojiwekea kama nchi.”
“Mfano, kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano, awamu ya tatu (“the National Five-Year Development Plan-Phase three), tumelenga kupunguza ukosefu wa ajira kutoka asilimia 9 (mwaka 2019) kufikia asilimia 8 ifikapo mwaka 2025/26. Kukuza ujuzi ni kati ya mipango iliyobainishwa na Serikali ili tufikie lengo na kuongeza idadi ya wahitimu waliopata mafunzo mahala pa kazi ni njia mojawapo ya kukuza ujuzi nchini kwa vijana wetu.”
Amesema wao wanatarajia kuongeza idadi ya wahitimu wenye mafunzo ya uanagenzi kufikia 231,000 ifikapo mwaka 2025/26 kutoka 46,000, mwaka 2019/20, vivyo hivyo na kwa mafunzo tarajari, lengo ni kufikia wahitimu 150,000 ifikapo mwaka 2025/26 kutoka 30,000, mwaka 2019/20.
WANANCHI KATAVI WAVUTIWA NA HATUA YA WIZARA YA AFYA KUELIMISHA SURUA KWA NJIA YA SINEMA
Na Elimu ya Afya kwa Umma.
Baadhi ya wananchi kutoka kata ya Majimoto Halmashauri ya Mpimbwe Wilayani Mlele Mkoa wa Katavi wamepongeza Wizara ya Afya kwa kuanza zoezi la uelimishaji na uhamasishaji wa chanjo ya Ugonjwa wa Surua kwa njia ya Sinema katika Mkoa wa Katavi.
Wakizungumza mara baada
kushuhudia uelimishaji kuhusu madhara ya ugonjwa wa Surua na umuhimu wa Chanjo ya Surua, baadhi ya wananchi hao wamesema hatua hiyo itawasaidia kuwajengea uelewa zaidi umuhimu wa Chanjo na madhara yatokanayo na ugonjwa wa Surua.
Kwa upande wake mratibu wa uelimishaji huo kutoka Wizara ya Afya Simon Nzilibili amesema hatua hiyo ya uelimishaji kuhusu Surua mkoa wa Katavi itarahisisha kufikia wananchi wengi kwani muda wa jioni asilimia kubwa ya wananchi ni rahisi kupatikana baada ya kutoka kwenye shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo .
Ikumbukwe kuwa Wizara ya Afya imekuja na mikakati mbalimbali ya uelimishaji Surua ikiwemo kutumia magari ya Matangazo, lugha mama ,wasanii wa nyimbo za asili, viongozi wa dini, wazee wa kimila na watu mashuhuri, njia ya Sinema,mabango na vyombo vya habari pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii.
Kutokana na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa shirikishi na kuwajali wananchi wake, Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu tayari ameshafanya ziara Mkoani Katavi ambapo Februari 24.2023 amezungumza na wananchi wa Majimoto katika Mkutano wa hadhara.
Hatua hii imekuja baada vifo 13 vitokanavyo na Surua kuripotiwa Mkoani Katavi ambapo Moja ya vyanzo ni wazazi kutokuwa na mwitikio wa kuwapeleka watoto vituo vya afya kupatiwa chanjo .
NAIBU WAZIRI MASANJA ATATUA MGOGORO WA MPAKA KATI YA KIJIJI CHA BUGER NA HIFADHI YA TAIFA ZIWA MANYARA
***************
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ametatua mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Ziwa Manyara Mkoani Arusha na wananchi wa kijiji cha Buger kilichopo katika wilaya ya Karatu, uliosababishwa na wananchi hao kuvuka vigingi vya hifadhi na kuendelea na shughuli za kilimo, ufugaji na makazi.
Ametatua mgogoro huo leo wakati wa ziara ya kikazi ya kusikiliza changamoto za wananchi kuhusu mipaka ya hifadhi Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Mhe. Masanja amefafanua kuwa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) baada ya kuweka vigingi katika eneo la kijiji cha Buger, kaya tatu zinaonekana zimo ndani ya hifadhi ambapo awali tathmini ya Kamati ya Mawaziri Nane ilionesha kaya 300 zimo ndani ya hifadhi hivyo kupendekeza kuangaliwa upya uwezekano wa kuziacha kaya hizo.
"Maamuzi ya Baraza la Mawaziri yaliamuliwa na yalitaka baadhi ya kaya ziondoke lakini ikatumwa kamati ya wataalamu uwandani kufanya tathmini upya” Mhe. Masanja amefafanua.
Amesema baada ya kamati hiyo kutoa mapendekezo Serikali iliamua kuweka vigingi kwa lengo la kuzuia wananchi wanaoendelea na shughuli za kibinadamu lakini bado wananchi waliendelea kuingia katika eneo la hifadhi.
Kufuatia uamuzi huo, Mhe. Masanja amesema Serikali italipa fidia kaya tatu zilizo ndani ya hifadhi ya ziwa Manyara baada ya TANAPA kufanya tathmini.
“Niwaombe kwa wale ambao wamevuka vigingi tulivyoweka na kuingia katika hifadhi, Serikali iwalipe fidia baada ya kufanyiwa tathmini”Mhe. Masanja amesisitiza.
Amewaasa wananchi wa kijiji cha Buger kutoendelea kuingia katika eneo la hifadhi ya Ziwa Manyara kwa sababu ndio eneo lenye chanzo cha maji kinachotegemewa na mji wa Karatu na pia husaidia kuhifadhi mazingira na kuchevusha mazao.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Dadi Kolimba amesema Serikali inalinda msitu huo kutokana na faida zake katika kuleta mvua na kutunza vyanzo vya maji.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Karatu, Mhe. Daniel Awack amesema ni vyema TANAPA ikaendelea kuimarisha ushirikiano baina yake na wananchi ili waone faida za uhifadhi .