Friday, 2 September 2022

DARAJA LA ESURI LALETA UKOMBOZI KWA WANANCHI OLORESHO




Wananchi wa Oloesho katika kata ya Olasiti na Olmoti, Halmashauri ya Jiji la Arusha wamepata faraja na kufurahia ujenzi wa daraja la Esuri lenye urefu wa meta 17 na upana wa meta nane (8) lililojengwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwa takribani shilingi 335,092,557.00.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa daraja hilo kwa Bodi ya Ushauri ya TARURA wakati wa ziara ya ukaguzi, meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha Mhandisi Laynas Sanya alisema kuwa daraja hilo lenye uwezo wa kuhimili uzito wa tani 30, litarahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi kutoka kata ya Olasiti na Olmoti na maeneo mengine ya jirani na kuondoa adha ya kutopitika kwa barabara kipindi cha mvua.

Inoti Shedrack, mkazi wa Oloresho alisema kuwa walikuwa wanateseka sana kabla ya daraja halijajegwa, hasa wakina mama na watoto lakini kwa sasa wanamshukuru Mugu daraja limekua ni mkombozi kwao.

“Tumejengewa daraja ambalo sasa hivi hatusumbuki kabisa na watoto wanaenda shule bila shida yoyote. Sisi wananchi wa Oloresho tunaishukuru sana Serikali na TARURA kwa kutengeneza daraja na barabara hii,” alisema Inoti.

Naye Mhe. Alex Martin diwani wa kata ya Olasiti alisema wanaishukuru sana TARURA kwa kutengeneza daraja hilo kwasababu walikuwa wakipata shida sana wakati wa mvua, na wakinamama wengi walikuwa wakijifungua watoto wao eneo hilo kwa wakunga wa kienyeji kutokana na kushindwa kuvuka kwenda hospitali.

“Kwa kweli tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu tumejengewa daraja hili ambalo limekuwa ni ukombozi kwetu kwa kutupunguzia adha tulizokuwa tunazipata,” alisema Alex.

Naye Mhe. Mrisho Gambo mbunge wa Arusha mjini alisema kuwa kwao imekuwa kama ndoto kwasababu walizoea kuona TANROAD ndiyo wanaweza kujenga madaraja yenye viwango bora kama hilo. 
“Tumeona kuwa kumbe TARURA ikiwezeshwa inaweza kufanya mambo makubwa zaidi na kuwafikia wananchi wengi zaidi. Tunaishukuru sana bodi yako mwenyekiti; mtendaji mkuu pamoja na watumishi wa TARURA ambao wametoa ushirikiano mkubwa sana kukamilika kwa daraja hili. Niwasihi madiwani wangu tuendelee kuiamini TARURA na wataendelea kufanya mambo makubwa tukiwaunga mkono,” alisema Mhe. Gambo.

Kwa upande wake Mhandisi Florian Kabaka, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA aliwashukuru wananchi pamoja na mbunge kwa kutambua na kuona kazi ambayo TARURA inafanya ya kuwahudumia wananchi na kurahisisha utoaji huduma kupitia barabara.

“Nimefarijika sana kuona daraja hili limewanufaisha sana sasa watu hawachukui muda mrefu sana kama zamani, wanaweza kukatisha hapa na kufika wanapotaka kwenda kwa urahisi na kupata huduma zao, na hili ndilo lengo la TARURA,”alisema Mhandisi Kabaka.

Aidha aliwashukuru wananchi kwa kutambua kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda na kuwajali kwa kuwawezesha TARURA kuwafikia na akaahidi kuwa TARURA itaendelea kuboresha zaidi kadiri inavyowezeshwa.

Mhandisi Victor Seff, Mtendaji Mkuu wa TARURA aliwaasa viongozi na wananchi wa eneo hilo kuilinda miundo mbinu hiyo na hasa alama za usalama zilizowekwa ili ziwanufaishe wao pamoja na vizazi vijavyo.





















Share:

BODABODA AKATWA SHINGO, APORWA PIKIPIKI BUNDA



Na Adelinus Banenwa - Bunda
Mtu mmoja ambaye ni dereva bodaboda aliyetambulika kwa jina la ISSA SAGUDA (22) mkazi wa Rubana kata ya Balili, Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara amekutwa amepoteza Maisha kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na tumboni maeneo ya shule ya msingi Rubana.



Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia tarehe 29/8/2022.


Mashuhuda wa tukio hilo wakizungumza na radio Mazingira Fm katika eneo la tukio wamesema wanafunzi waliokuwa wanaenda shule ndo waliogundua kuwepo kwa mwili huo.


“Ilikuwa asubuhi kwenye muda wa saa Moja wanafunzi walikuja kutuita kwamba kuna mtu amekatwa shingo amelala karibu na choo tukaamka haraka na tulipofika tukamuangalia alivyovaa mbele kidogo tukaona alama za break ya pikipiki na pembeni kuna damu na funguo za pikipiki ndipo tulipogundua kwamba huyu ni dereva bodaboda”, amesema shuhuda.



Kwa upande wake mwenyekiti wa waendesha pikipiki maalufu (bodaboda) Wilaya ya Bunda Dickson Joseph amesema tayari wamemtambua.




“Ni bodaboda mwenzetu alikuwa anapaki kwenye kituo Cha NM Bunda Mjini nimepigiwa simu asubuhi kwamba mwenzetu amekutwa amepoteza Maisha na pikipiki imeibiwa ndo nimefika hapa”



Dickson ameongeza kuwa suala ulinzi kwa bodaboda juu ya wateja hasa nyakati za usiku wameshaambizana kutokubali kubeba abiria bila wenzao kuwa na taarifa za mteja unayembeba anatoka wapi na anakwenda wapi.





Kwa upande wake Diwani wa kata ya Balili Mhe Thomas Tamka amesema mauaji yaliyotokea katika kata yake yanaumiza sana na hayakubariki amesema yeye kama mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata ataitisha kikao ili suala la ulinzi shirikishi uanze mara Moja



Baada ya mauji ya kijana Issa Saguda na kuporwa pikipiki katika mtaa wa Rubana Kata ya Balili Halmashauri ya mji wa Bunda, jeshi la Polisi limesema pikipiki hiyo imepatika eneo la Nyamikoma Wilayani Busega Mkoani Simiyu



Akizungumza na Radio Mazingira Fm Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi Dismas Kisusi amesema pikipiki hiyo yenye namba za usajili MC 499 CDH aina King lion ilikamatwa na walinzi shirikishi usiku wa tarehe 29 Agosti 2022 masaa machache baada ya kutendeka tukio hilo huku mtuhumiwa akifanikiwa kutoroka.



Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka waliohusika na mauaji hayo huku likitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kukomesha vitendo hivyo.




CHANZO - RADIO MAZINGIRA FM
Share:

WAWEKEZAJI ARUSHA WAMWAGIA SIFA RAIS SAMIA UJENZI WA BARABARA ZA TARURA



Wawekezaji na wananchi wa kata ya Themi, Halmashauri ya Jiji la Arusha wamemsifu na wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwajengea kwa kiwango cha lami barabara za Themi -Viwandani zenye urefu wa kilometa 1.4 kwagharama ya shiligi 1,175,141,850.00.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja jijini Arusha iliyofaywa na bodi ya ushauri ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA).

Akitoa pongezi hizo mkurugenzi wa “Spanish Tiles” Bobby Chadha alisema kuwa anamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwapatia barabara nzuri na bora za lami maeneo ya viwandani. 

“Ninamshukuru sana rais kwa sababu kwa mara ya kwanza tumepata barabara hizi za lami kwa zaidi ya miaka 40 niliyokuwa hapa. Barabara hizi zitasaidia sana kupungza gharama za usafiri, kukuza biashara 
na pia kupendezesha mji,” alisema Bobby.

Naye ndugu Satbir Hanspaul mkurugezi mtendaji wa “Hanspaul Group” alisema kuwa anamshukuru na kumpongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu walikuwa wanapata changamoto kubwa sana kwa magari kufika viwandani na magari mengi yalikuwa yanaharibika lakini sasa barabara imewaondolea kero hizo.

“Wageni walikuwa wakija eneo la Kiwanda na kuona miundombinu mibovu walikuwa wanapata wasiwasi na kiwanda pia, lakini tumeona Serikali yetu imeona changamoto na kuifanyia kazi haraka, sasa tunaaminika kwa sababu mazigira yameboreshwa,” alisema Hanspaul.

Mama Veronica Saimon mfanyabiashara wa eneo la viwandani alisema kuwa kabala ya barabara haijajengwa walikuwa wakipata shida sana kutokana na vumbi jingi pamoja na matope wakati wa mvua hali iliyokuwa inaathiri biashara yao.

Alieleza kuwa kwa sasa anamshukuru sana Rais Samia kwa kuwajali, sababu kwa sasa wanafanyabishara bila shida na wateja wengi wanawapata baada ya barabara kujengwa.

Kwa upande wake Mhe. Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini aliwashukuru watendaji na wataalamu wa TARURA kwa kazi kubwa wanayofanya na ameona tofauti kubwa sana baada ya TARURA kuanzishwa.

“Huko nyuma kaba ya kuanzishwa TARURA ilikuwa ngumu kupeleka mradi sehemu inayoeleweka na ukaleta tija kwa sababu kila diwani alikuwa akivutia upandewa wake. Leo mmewasikia hapa wawekezaji wamesubiri barabara kwa takribani miaka 40 lakini baada ya TARURA kuanzishwa barabara imejengwa,’alisema Mhe. Gambo.

Aidha alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa Kuendelea kuenzi falsafa ya Serikali ya “Tanzania ya Viwanda” kwa kuboresha miundombinu katika maeneo hayo ya viwandani yenye viwanda zaidi ya 20, ambapo ajira zinaogezeka na uchumi wa wanachi wa maeneo ya viwandani wanaofikia takribani 11,000 unaboreka.

Mtendaji mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff kwa upande wake alisema kuwa wamejipanga kuwafikia wannachi katika sehemu ambazo hazifikiki na pia katika maeneo ya kimkakati.

“TARURA tunakufikisha kusikofika lakini nasema pia Penye nia pana njia na pasipo na njia TARURA tupo, “alisema Mhandisi Seff.
Share:

Thursday, 1 September 2022

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA SEPTEMBA 2,2022
























Share:

WATOA HUDUMA ZA AFYA, WANACHAMA WACHANGIA KUHATARISHA UHAI WA MFUKO WA NHIF

 

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

Na Dotto Kwilasa,DODOMA


SERIKALI kupitia Wizara ya Afya nchini imesema inafanya jitihada kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma na wanachama wa Mfuko wa Taifa wa bima ya afya ( NHIF) vinavyolenga kujipatia manufaa kinyume na utaratibu.


Kutokana na hayo imesema ipo katika hatua za mwisho kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo itaweka mazingira kwa kila mtanzania kuwa na bima ya afya ili kuwezesha dhana ya kuchangiana gharama za matibabu hali itakayo saidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi. 


Hayo yameelezwa leo Jijini hapa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu hali ya mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) na kueleza kuwa Serikali haitakubali kuona Mfuko huo unatetereka hivyo kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wananchi wote kuwa na uhakika wa kupata huduma bora za afya.


Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya wataaluma 65 wamefikishwa katika mabaraza yao kutokana na kukiuka taratibu na miongozo ya taaluma za afya hivyo kuitaka NHIF kuimarisha mikakati yake ya kupambana na vitendo vya udanganyifu pamoja na kuimarisha matumizi ya Mifumo ya TEHAMA.


Hata hivyo Waziri huyo amewatoa hofu wanachama  wa NHIF na wananchi kwa ujumla kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuuimarisha Mfuko huo ili kuwa endelevu na kuwanufaisha wananchi walio wengi zaidi.


Pamoja na kuimarisha huduma za afya,Waziri huyo amekiri kuwa bado kuna changamoto ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya wananchi wenye magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ambayo gharama zake ni kubwa hali inayohatarisha uhai na uendelevu wa Mfuko wa NHIF.

 

Vilevile, changamoto nyingine iliyopo ni uwepo wa kundi kubwa la wananchi wanaojiunga na NHIF kwa hiari ambao, takribani asilimia 99 ni wagonjwa hatua inayotokana na kutokuwepo kwa Sheria ya ulazima kwa wananchi kujiunga na Bima ya Afya na kuondokana na kuelemewa kwa mfuko huo kunakotokana na gharama za matibabu  kuongezeka kwa idadi ya wanufaika wenye magonjwa yasiyoambukizwa na gharama zake, hali inayoweza kuathiri uhai na uendelevu wa Mfuko.


"Kama mnakumbuka tarehe 29/08/2022 wakati nikifungua Mkutano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika kuhusu Ugonjwa wa Kipindupindu jijini Dar es Salaam, niliweka msisitizo wa kuweka nguvu na jitihada katika kuzuia magonjwa badala ya kusubiri kutibu;


Katika muktadha huo nilitoa angalizo kuwa hivi sasa nchini kwetu tunashudia ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo matibabu yake ni gharama kubwa na hivyo kama tutachelewa kuchukua hatua stahiki katika kudhibiti magonjwa hayo, basi kuna hatari pia kwa Mfuko wetu wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuelemewa na gharama za matibabu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanufaika wenye magonjwa yasiyoambukizwa na gharama zake, hali inayoweza kuathiri uhai na uendelevu wa Mfuko,"Amesema.


Kulingana na takwimu zilizopo, amesema gharama za magonjwa yasiyo ya kuambukizwa zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 35.65 mwaka 2016/17 hadi shilingi bilioni 99.09 mwaka 2021/22 na kwamba Gharama za kuhudumia wagonjwa wa saratani wanaopata tiba za mionzi na chemotherapia (chemotherapy services), kupitia Mfuko ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 22.5 mwaka 2021/22,"amesema


Kwa upande wa huduma za matibabu ya figo kwa wanachama wanaopata huduma ya kuchuja damu (hemodialysis services) Waziri Ummy amesema gharama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9.5 mwaka 2015/16 kufikia shilingi bilioni 35.44 mwaka 2021/22 huku idadi ya wagonjwa  wa figo imeongezeka kutoka 280 mwaka 2014/15 hadi kufikia 2,099 mwaka 2021/22.


"Gharama za matibabu ya moyo kwa wanachama wa Mfuko wanaopata matibabu ya upasuaji wa moyo (minimal and invasive cardiac procedures), ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 0.5 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 4.33 mwaka 2021/22,gharama za vipimo vya CT scan na MRI ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 5.43 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 10.87 mwaka 2021/22,"amefafanua 


Sambamba na hayo ameeleza kuwa ni wazi hali ya ustahimilivu na uendelevu wa Mfuko ipo mashakani endapo hatua stahiki hazitachukuliwa ambazo ni pamoja na kuimarisha afua za kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza  katika hatua za awali ikiwemo kuyatambua mapema kabla ya kuwa na athari kubwa,kuongeza idadi ya wanachama na kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma za afya.


Ametaja hatua nyingine ni kudhibiti matumizi ya huduma yasiyo na tija,kupunguza gharama za matibabu nchini,kuwa na Mfumo endelevu wa kuhakikisha Mfuko unakuwa na fedha wakati wote kutoka katika vyanzo vyake vya mapato na katika hatua hii tunaishukuru serikali kwa kuwasilisha michango ya watumishi kwa wakati. 


"Niwatoe wasiwasi wadau wa NHIF wakiwemo wanachama, watoa huduma pamoja na watanzania wote kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa Mfuko huu unakuwa imara, endelevu na stahimilivu kwani kwa sasa, ni moja kati ya mfumo unaotumika katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa nchini,"amesema


Amesema mfuko wa NHIF ndio umekuwa tegemeo la watanzania wengi hususani wa kipato cha chini pia  umekuwa tegemeo la vituo vya kutoa huduma za afya nchini pamoja na kuwa na wanachama asilimia nane (8) tu ya Watanzania wote, vituo vingi vya kutolea huduma vinategemea mapato kutoka katika Mfuko kwa zaidi ya asilimia 70.


"Katika kuhakikisha kuwa maamuzi yote yahusuyo Mfuko huu yanazingatia taratibu na miongozo ya kuendesha chombo hiki, tumefanya tathmini ya uhai na uendelevu wa mfuko kwa mujibu wa sheria na, hivyo tunatambua ni yapi yanapaswa kufanyika ili kuhakikisha mfuko wetu unakuwa endelevu na imara zaidi na matokeo ya awali yanaonesha uendelevu wa Mfuko huu unategemea sana ongezeko la wanachama watakaoandikishwa katika Mfuko huu,"amesema. 


Akizungumza uzoefu kutoka katika nchi nyingine ,Waziri huyo alisema unaonesha kuwa, kadri idadi ya wanachama inavyokuwa kubwa katika Mifuko hii ya bima za afya za umma kama NHIF, ndipo uwezo wake katika kugharamia matibabu unaongezeka na hivyo kuwa stahimilivu na endelevu kwa muda mrefu.

Share:

MWANZA HOTEL NI SALAMA... HAIJAUNGUA

 

MMILIKI wa New Mwanza Hotel Mwita Gachuma amekanusha uvumi ulikuwa umesambazwa wa kuungua kwa eneo hilo lililoko katika mwa Jiji kwa kusema ni sehemu ya eneo hilo ndiyo ilipata tatizo hilo.


Amesema hayo leo jijini Mwanza kuwa ni sehemu ya eneo la nyuma ya hotel hiyo iliyokuwa inatumiwa kama ukumbi wa harusi na kasino ambayo yameungua kwa moto unaohisiwa kutokana na hitilafu ya umeme.


Moto huo ulitokea usiku saa 1.30 siku ya tarehe 31 mwezi wa Nane kwa kile kinachohisiwa kuwa hitilafu ya umeme.


Gachuma ametoa shukurani kwa serikali ya mkoa huo, watendaji wa idara mbalimbali na wananchi kwa kuwezesha kuzimwa kwa moto huo kabla ya kuleta madhara makubwa kwa nyumba zilizopo karibu na sehemu hiyo.


Alisema madhara yaliyotokana na moto huo ni makubwa na watalaamu wa vyombo mbalimbali wamefika kufanya tathimini ya hasra hiyo kwani eneo hilo limeharibiwa vibaya na hivyo kuhitajika ujenzi upya.


"Watu wa Mamlaka Bima wamefika kwa ajili ya kufanya tathimini kuweza kujua ni kiasi gani cha hasara kimepatikana kutokana na moto huo hivyo  siwezi kusema kiwango halisi cha hasara kilichopatikana" alisema Gachuma.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima aliyefika tena kufatilia athari iliyotokana na moto huo alisema kuwa anashukuru vyombo vyote vya ulizi kwa kazi yao nzuri waliyofanya usiku wa tarehe 31 Agosti ilipoungua jengo hilo.


Alisema kutokana na jengo hilo kuwa katikati mwa majengo mengine madhara yake yangeweza kuwa makubwa zaidi endapo moto huo usingezibitiwa haraka.


'Nilikuwepo jana usiku kwenye tukio la moto huo hata hivyo nimeona nipite tena leo asubuhi kuona hali hiyo ambayo ingeweza kuleta madhara kwa moto huo kusambaa kwenye nyumba zingine' alisema Malima


Malima alitoa wito kwa watu wote kujenga majengo yao kwa kuweka tahadhari ya vitu vinavyozuia moto katika maeneo yao ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.

Share:

DC MBONEKO AZINDUA CHANJO YA POLIO AWAMU YA TATU SHINYANGA...ATINGA NYUMBA KWA NYUMBA

Share:

KINANA ATUA KIGOMA KWA ZIARA YA KUIMARISHA CHAMA

 

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Ndugu Abdulrahman Omari Kinana amewasili leo Alhamisi tarehe 01 Septemba, 2022 mkoani Kigoma kwa ziara ya siku moja mkoani humo ya kukagua uhai wa chama, utekelezaji wa ilani pamoja na kusikiliza kero za wananchi.

Kinana amewasili uwanja wa ndege wa Kigoma na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma Ndg Amandus Dismas Nzamba, Mkuu wa mkoa wa Kigoma Ndg Thobias Andengenye, wanachama na viongozi  wa chama na serikali.

Kinana ameanza leo ziara ya siku moja mkoani Kigoma ambapo ataendelea katika mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza. Katika ziara yake ameambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Ndg Shaka Hamdu Shaka.

#CCMImara
#KaziIendelee



 

Share:

KASINO NDANI YA MWANZA HOTEL YATEKETEA KWA MOTO


Kasino iliyopo Mwanza Hotel jijini Mwanza imeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijafahamika

Inaelezwa kuwa hakuna mtu aliyedhurika na moto huo japo umesababisha hasara katika kasino hiyo kwa kuteketeza vitu vyote vilivyokuwa ndani

Jeshi la zimamoto na uokoaji lilifika kwa wakati na kuanza kuuzima moto huo ili usiendelee kuleta madhara kufuatia hoteli hiyo kuwa katikati ya jiji la Mwanza na kuzungukwa na majengo mengine.

Miongoni mwa waliofika katika tukio hilo ni Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima

Kaimu kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji Kamila Labani amesema wamefanikiwa kuudhibiti moto huo usisambae katika hoteli hiyo huku bado wanaendelea kuchunguza chanzo cha moto huo.

Chanzo - EATV
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger