Tuesday, 17 August 2021

WAJUMBE BODI YA SHUWASA WATEMBELEA NA KUKAGUA UJENZI WA MRADI WA MAJI NGOGWA - KITWANA KAHAMA

Kaimu Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola  (kushoto) akielezea kuhusu Mradi wa ujenzi wa maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama unaosimamiwa na kutekelezwa na SHUWASA wakati wajumbe wa Bodi ya SHUWASA walipotembelea na kukagua mradi huo leo Jumanne Agosti 17,2021.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Bodi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imetembelea na kukagua utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama unaosimamiwa na kutekelezwa na SHUWASA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) na Wakala wa Usambazaji Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga na wilaya ya Kahama.

Wajumbe hao wa Bodi ya SHUWASA wametembelea mradi huo leo Jumanne Agosti 17,2021 na kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wenye gharama ya shilingi Bilioni 2.4 unaotarajiwa kukamilishwa ifikapo Mwezi Oktoba ,2021.

Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA, Bi. Mwamvua Jilumbi amesema maendeleo ya ujenzi huo yanaridhisha huku akibainisha kuwa mradi huo uliopaswa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2020 ulikwama kutokana changamoto ya upatikanaji wa mabomba.

“Tulikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa mabomba ambapo Mzabuni tuliyeingia naye mkataba badala ya kuleta mabomba tuliyokubaliana yeye alileta mengine tu yasiyohusika. Tulivunja mkataba naye tukatafuta mzabuni mwingine ambaye sasa analeta mabomba ya chuma na tunatarajia ifikapo Mwezi Oktoba 2021 wananchi wataanza kupata huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria”,amesema Jilumbi.

Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha inawatua ndoo vichwani akina mama hivyo pindi mradi huo utakapokamilika utasaidia wananchi kuondokana na kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama na kujikuta wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola amesema mradi huo unaojengwa kwa kutumia Wataalamu wa ndani ‘Force Account’ unajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.4 na unatarajiwa kunufaisha wananchi zaidi ya 27,000 pindi utakapokamilika mwezi Oktoba 2021.

“Mradi huu unahusisha ujenzi matanki mawili katika maeneo ya Ngogwa na Kitwana. Ujenzi tanki la Ngogwa lenye ujazo wa lita za ujazo 680,000 umekamilika na lile la Kitwana lenye ujazo wa lita 135,000 ujenzi wake uko mbioni kukamilika na tupo kwenye hatua za ukamilishaji ujenzi wa maghati 14 ya kuchotea maji”,amesema Mhandisi Katopola.

Ameeleza kuwa licha ya SHUWASA kuhudumia kata zote 17 za Manispaa ya Shinyanga kwa kuzipatia huduma ya maji safi na salama, Serikali iliiteua SHUWASA kusimamia ujenzi wa mradi wa maji wa Ngogwa - Kitwana kwa vile ndiyo Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Shinyanga ambapo baada ya kukamilika kwa mradi, Mamlaka ya Maji ya Mji wa Kahama (KUWASA) ndiyo itakayoendelea kusimamia mradi huo.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Kaimu Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola (kushoto) akielezea kuhusu Mradi wa ujenzi wa maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama unaosimamiwa na kutekelezwa na SHUWASA wakati wajumbe wa Bodi ya SHUWASA walipotembelea na kukagua mradi huo leo Jumanne Agosti 17,2021. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Muonekano wa ghati la maji katika Senta ya Kitwana kwenye Mradi wa ujenzi wa maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama unaosimamiwa na kutekelezwa na SHUWASA.
Kaimu Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola (wa pili kulia) akiwaonesha ghati la maji katika Senta ya Kitwana kwenye Mradi wa ujenzi wa maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama unaosimamiwa na kutekelezwa na SHUWASA wakati wajumbe wa Bodi ya SHUWASA wakitembelea na kukagua mradi huo.
Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi wa maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama, Mhandisi Hassan Kassim Fussi akielezea kuhusu ujenzi wa maghati 14 ya kuchotea maji wakati wajumbe wa Bodi ya SHUWASA walipotembelea na kukagua mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola (kulia) akiwaelezea wajumbe wa Bodi ya SHUWASA kuhusu ujenzi maghati la kuchotea maji unaoendelea katika Mradi wa maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Bi. Mwamvua Jilumbi.
Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Bi. Mwamvua Jilumbi (katikati) na wajumbe wa bodi ya SHUWASA wakiangalia shughuli ya ujenzi wa maghati ya kuchotea maji katika Mradi wa maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama.
Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Bi. Mwamvua Jilumbi (katikati) na wajumbe wa bodi ya SHUWASA wakiangalia shughuli ya ujenzi wa maghati ya kuchotea maji katika Mradi wa maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama.
Wajumbe wa bodi ya SHUWASA wakiangalia shughuli ya ujenzi wa tenki la juu kwenye mwinuko ‘riser’ wa mita 12 lenye ukubwa wa lita 135,000 katika kijiji cha Kitwana
Muonekano hatua ya ujenzi wa tenki la juu kwenye mwinuko ‘riser’ wa mita 12 lenye ukubwa wa lita 135,000 katika kijiji cha Kitwana.
Wajumbe wa bodi ya SHUWASA wakiangalia shughuli ya ujenzi wa tenki la juu kwenye mwinuko ‘riser’ wa mita 12 lenye ukubwa wa lita 135,000 katika kijiji cha Kitwana
Wajumbe wa bodi ya SHUWASA wakiangalia shughuli ya ujenzi wa tenki la juu kwenye mwinuko ‘riser’ wa mita 12 lenye ukubwa wa lita 135,000 katika kijiji cha Kitwana
Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Bi. Mwamvua Jilumbi (katikati) akizungumza katika Tenki la Maji la Kitwana lenye ujazo wa lita 135,000
Wajumbe wa bodi ya SHUWASA wakiwa katika kata ya Busoka ambapo bomba la maji ya Mradi wa Ngogwa - Kitwana litapita eneo la barabara.
Muonekano ujenzi wa ghati la kuchotea maji katika Shule ya Msingi Ngogwa kijiji cha Ngogwa kata ya Ngogwa.
Mhandisi wa Mipango na Ujenzi kutoka SHUWASA, Wilfred Julius akielezea kuhusu ujenzi wa tenki la kukusanyia maji la ardhini ‘Ground water tank’ lenye ukubwa wa lita 680,000 katika kijiji cha Ngogwa kata ya Ngogwa.
Kaimu Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola akiongoza wajumbe wa Bodi ya SHUWASA na wadau wengine kupanda Mlima Ngogwa wenye urefu wa mita 280 ili kwenda kuona tenki la kukusanyia maji la ardhini ‘Ground water tank’ lenye ukubwa wa lita 680,000 katika kijiji cha Ngogwa kata ya Ngogwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA , Bi. Mwamvua Jilumbi (kulia) akipanda Mlima Ngogwa wenye urefu wa mita 280 ili kwenda kuona tenki la kukusanyia maji la ardhini ‘Ground water tank’ lenye ukubwa wa lita 680,000 katika kijiji cha Ngogwa kata ya Ngogwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Bi. Mwamvua Jilumbi akipanda katika tenki la kukusanyia maji la ardhini ‘Ground water tank’ lenye ukubwa wa lita 680,000 katika kijiji cha Ngogwa kata ya Ngogwa.
Muonekano tenki la kukusanyia maji la ardhini ‘Ground water tank’ lenye ukubwa wa lita 680,000 katika kijiji cha Ngogwa kata ya Ngogwa.
Kaimu Mkurugenzi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola (mwenye suti ya bluu) akishuka katika tenki la kukusanyia maji la ardhini ‘Ground water tank’ lenye ukubwa wa lita 680,000 katika kijiji cha Ngogwa kata ya Ngogwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Bi. Mwamvua Jilumbi (mbele) na wajumbe wa Bodi ya SHUWASA wakiondoka katika tenki la kukusanyia maji la ardhini ‘Ground water tank’ lenye ukubwa wa lita 680,000 katika kijiji cha Ngogwa kata ya Ngogwa.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza wakati Wajumbe wa SHUWASA walipowasili katika ofisi za Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA).
Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Bi. Mwamvua Jilumbi (kushoto) akizungumza wakati Wajumbe wa SHUWASA walipowasili katika ofisi za Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA).
Awali Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi wa maji wa Ngogwa – Kitwana, Mhandisi Magige Marwa kutoka KUWASA akielezea kuhusu ujenzi wa mradi huo kwa Wajumbe wa Bodi ya SHUWASA.
Awali Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi wa maji wa Ngogwa – Kitwana, Mhandisi Magige Marwa kutoka KUWASA akielezea kuhusu ujenzi wa mradi huo kwa Wajumbe wa Bodi ya SHUWASA.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Share:

SERIKALI YAAGIZA ASKOFU GWAJIMA AKAMATWE


Kushoto ni Waziri wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima, na kulia ni Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima
 ***
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, ameliagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kumtafuta na kumkamata popote alipo mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima ili athibitishe kauli anazozitoa dhidi ya Serikali na viongozi kuhusu chanjo ya Covid-19.

Waziri Gwajima ametoa agizo hilo leo Jumanne, Agosti 17, 2021 akiwa katika kijiji cha Kyatunge Wilaya ya Butiama mkoani Mara na kueleza kuwa Askofu Gwajima amekuwa akitoa taarifa za upotoshaji kwa makusudi kuhusu chanjo ya Corona jambo ambalo linaivuruga wizara yake na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari duniani.

Maagizo hayo ya Waziri Gwajima yanakuja ikiwa ni saa chache tangu Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel kumtaka Askofu Gwajima kujitafakari juu ya madhara yatakayowakuta wananchi kutokana na upotoshaji anaoendelea kuufanya na kuongeza kuwa hawezi kupingana na Serikali na hana uthibitisho wa kisayansi kuhusu chanjo ya corona.

“Gwajima amevuka mipaka, anapotosha Taifa, hawezi kupingana na serikali na hana uthibitisho wa kisayansi, anasema mtu akichanjwa kuna vitu vinaingizwa mwilini ili mtu afe baada ya miaka miwili ama kumi, tutamuita athibitishe hili, akishindwa tutamshughulikia.

“Nimekuja kumuonya nikiwa kama mwana sayansi, ili ajue kwamba ametukanyaga sehemu, Gwajima anajua ukweli lakini ameamua kucheza ligi, tunamuonya tunataka awe na uthibitisho wa Kisayansi kwa kile anachosema kuhusu Chanjo ya Corona.

“Tumetumia nguvu nyingi sana kumuelimisha (Askofu Gwajima), tunataka tuthibitishiane kwamba sisi na yeye nani anataka kuiangamiza nchi, tujue nani anataka kuilinda nchi,” alisema Dk. Mollel.

Askofu Gwajima na waumini wake amejipambanua kukataa chanjo ya corona iliyoletwa nchini kwa madai kuwa haijathibitishwa mamlaka husika za afya huku akiongeza kuwa zina madhara na zinaweza kuwaletea matatizo makubwa wananchi wa Tanzania huku akiitaka Serikali kujiridhisha na usalama wa chanjo hizo.

“Mimi namtaka daktari atakayeshadadia nitakula naye meza moja. Utakufa daktari, utaona,” alisema Askofu Gwajima huku akishangiliwa na waumini wake.

Aliendelea: “Daktari yoyote wa Kitanzania atakayeanza kushadadia watu wachanjwe na yeye mwenyewe hajafanya utafiti wa kuna nini ndani ya chanjo, madhara ya muda mfupi, madhara ya muda mrefu kwetu na watoto wetu na nchi yetu. Nasema hivi kufa na ufe kwa jina la Yesu.”

Aidha, Askofu Gwajima alidai kwamba janga la virusi vya corona lina uhusiano na juhudi za kusambaza teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya 5G huku akiongeza pia kuwa watakaochanjwa huenda vizazi vyao vikabadilika miaka kadhaa ijayo na kuwa mazombi.

Share:

MAAFISA BIASHARA WATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO YA MSINGI



Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA ) Bw. Godfrey Nyaisa akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa Mafunzo kwa Maafisa Biashara wa mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida yanayofanyika kwa wa siku tano jijini Dodoma.


Maafisa biashara kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro na Singida wakifuatilia mafunzo ya sheria ya leseni za biashara yanayotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) yanayofanyika katika ukumbi wa JK convetion Centre jijini Dodoma.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Biashara wa mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro mara baada ufunguzi wa mafunzo ya Sheria ya Leseni za Biashara yanayofanyika kwa siku tano katika ukumbi wa JK Convetion Centre Jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi wa Leseni wa BRELA Bw. Andrew Mkapa na kutosho kwake ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Leseni wa BRELA, Bw. Tawi Kilumile

**************************

Na mwandishi Wetu, Dodoma





Maafisa biashara nchini wametakiwa kutambua kuwa jukumu lao kuu ni kuwezesha ufanyaji wa biashara badala ya kuwa wakusanya mapatato shughuli ambayo ni sehemu tu ya kazi ambayo wanatakiwa kuifanya.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya sheria za leseni za biashara kwa maafisa biashara wa mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro, yanayofanyika jijni Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa amesema Maafisa Biashara wanapaswa kutumia sheria pia kutumia busara wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kwamba ikiwa watazifunga biashara wasitarajie mfanyabiashara huyo kufanya biashara na badala yake watachangia kuua uchumi wa nchi.

“Muepuke sana kufunga biashara, afisa biashara kazi yako kubwa ni kusimamia wafanyabiashara, ikiwa utaifunga biashara utasimamia watu gani, hii ina maana huwataki wafanyabiashara “, alisema Bw. Nyaisa na kuongeza kuwa anatarajia kuwa mafunzo hayo yatasaidia kubadili fikra na mitizamo ya maafisa biashara na watendaji wengine wa serikali na kuwa watoa huduma na msaada kwa wafanyabiashara, hivyo ni vema wakafuatilia mafunzo hayo vizuri ili watakaporudi katika vituo vyao vya kazi watumike kama chachu ya uwekezaji, ukuaji na uanzishwaji wa biashara.

Bw. Nyaisa amesema, kila mmoja awe kipimo kwa kuwezesha watu kuanzisha na kufanya biashara ili ifikapo mwisho wa mwaka kila mmoja ajipime na kujihoji ni watu wangapi aliowawezesha kuanzisha biashara, wawafuate watu na kuwawezesha kuanzisha biashara na sio watu wawafuate wao kutaka kuanzisha biashara na wasiwe watu wanaokimbiwa na wafanyabiashara.

Sambamba na hilo maafisa biashara hao wametakiwa kutoa huduma bora na kwa weledi jambo ambalo litawezesha wafanyabiashara walio wengi kurasimisha biashara kupata fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ama taasisi mbalimbali za kifedha.



Amesisitiza kuwa maafisa biashara wana jukumu la kuwaelimisha wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kusajili biashara zao na kupata leseni pamoja na kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa wafanyabiashara hao ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.

Amewataka wafanyabiashara kuondokana na dhana kwamba gharama ya usajili wa majina ya biashara na makampuni kubwa jambo ambali si kweli kwani BRELA ni taasisi ya huduma na gharama zinazotozwa ni ndogo.
Share:

RAIS SAMIA SULUHU AFANYA UTEUZI WA VIONGOZI MBALIMBALI

 



Share:

Tanzia : WAZIRI WA ZAMANI BASILI MRAMBA AFARIKI DUNIA


ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Fedha wa Tanzania, Basil Pesambili Mramba amefariki dunia leo Jumanne, Agosti 17, 2021 katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu.

Mramba aliwahi kuwa Waziri wa Fedha katika utawala wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambapo aliiongoza Wizara hiyo mwaka 2001-2005, baadaye Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko mwaka 2006 hadi 2008.

Familia ya Mramba imethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kuwa ni wanafamilia wachache wataruhusiwa kufika kutoa pole nyumbani kwa marehemu, Mawenzi Road, Oysterbay jijini Dar.
Share:

WAZIRI NDUMBARO AZINDUA ZOEZI LA UWEKAJI ALAMA KWA FARU ENEO LA HIFADHI YA NGORONGORO.


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro (wa sita kutoka kushoto) akishuhudia uzinduzi wa zoezi la uwekaji wa alama za utambuzi wa faru katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas ndumbaro akiongea na menejimenti na wadau wa uhifadhi wa Faru katika eneo la Kreta ya Ngorongoro wakati wa uzinduzi wa zoezi la uwekaji alama za utambuzi kwa mnyama faru.


Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Maurus Msuha akielezea zoezi la kuweka alama kwa Faru kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopatikana faru yanalindwa kwa kuwekewa alama za utambuzi.


Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi akielezea upekee wa Hifadhi ya Ngorongoro kwa eneo pekee unaloweza kuona faru weusi wakiwa katika maeneo yao ya asili.


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro (kulia) akimkabidhi cheti Kiongozi wa mradi wa Frankfurt zoological Society Bw. Rian Labuschagne kama ishara ya kutambua mchango wao katika mradi wa uhifadhi wa Faru Nchini.

*****************************

Na Kassim Nyaki-NCAA

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro amezindua zoezi la uwekaji wa alama kwa faru katika hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa Wanyama hao ambao ni zao kubwa la Utalii nchini



Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa Wanyama aina ya faru ni adimu na muhimu sana katika utalii na Uhifadhi hivyo ulinzi wao kwa kutumia teknolojia ya kisasa ni kipaumbele kuwezesha ufuatiliaji wa mienendo yao hasa wanapozunguka maeneo mbalimbali ndani ya Hifadhi.

“Faru ni zao muhimu katika Utalii na Uhifadhi, katika kuimarisha zao hili nawapongeza NCAA kwa hatua hii ya kushirikiana na wadau kubuni mfumo wa teknolojia ya kisasa unaosaidia kulinda na kufuatilia mienendo ya Faru hasa wanapotoka nje ya Hifadhi na kuingia kwenye mashamba ya watu” alisema Dkt. Ndumbaro.

Waziri Dkt. Ndumaro ameongeza kuwa Utalii wa Faru ni zao muhimu katika kuongeza pato la Nchi na idadi kubwa ya wageni wanaokuja Ngorongoro moja ya kivutio kikubwa kwao ni Faru hivyo teknolojia ya kuwalinda faru inasaidia kuongeza idadi yao kwa haraka zaidi.

Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Maurus Msuha ameeleza kuwa zoezi la kuweka alama kwa Faru ni utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopatikana faru yanalindwa kwa mbinu za kisasa na faru hao kuwekewa alama za utambuzi ili kuwafuatilia mienendo yao kwa urahisi zaidi.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi amebainisha kuwa Hifadhi ya Ngorongoro ndio eneo pekee Tanzania na duniani kote ambako mtalii anaweza kuwaona faru weusi wakiwa katika maeneo yao ya asili.

Ameahidi kuwa NCAA itaendelea kuhakikisha kuwa wanatumia mbinu zote za kisasa kuwalinda na kuwahifadhi faru hao ili waweze kuishi kwa mda mrefu zaidi kama ilivyokuwa kwa faru mkongwe zaidi ambaye alikufa katika hifadhi ya Ngorongoro mwaka 2019 akiwa na umri wa miaka 57.

Kiongozi wa mradi wa wa Frankfurt zoological Society Bw. Riam Labuschagne ambao ni wadau muhimu katika Miradi ya uhifadhi wa mnyama Faru nchini ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwezesha teknolojia za kidijitali na mafunzo kwa askari wanyamapori ili kuendeleza juhudi za muda mrefu za uhifadhi ambazo matunda yake yanaonekana kutokana na ongezeko la Faru nchini kila mwaka.

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE AGOSTI 17,2021
























Share:

Monday, 16 August 2021

WAZIRI MHANGAMA AZINDUA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA URATIBU NA UFUATILIAJI WA SHUGHULI ZA SERIKALI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akitoa hotuba fupi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) iliyofanyika leo Agosti 16, 2021 Jijini Dodoma.


Sehemu ya Viongozi wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia maswala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard), Jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akizindua rasmi Mfumo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) Kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Masauni. Kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Tixon Nzunda hafla iliyofanyika leo Agosti 16,2021 jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akiangalia Mfumo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) mara baada ya kuuzindua rasmi hafla iliyofanyika leo Agosti 16 ,2021, Jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Masauni. Kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Tixon Nzunda.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Tixon Nzunda akieleza jambo wakati wa hafla ya kuzindua rasmi Mfumo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) hafla iliyofanyika leo Agosti 16, 2021, Jijini Dodoma.


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) akieleza jambo wakati wa hafla hiyo.


Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Masauni akieleza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard), Jijini Dodoma. Katikati ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Tixon Nzunda.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Mawaziri walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard), Jijini Dodoma. Kushoto aliyekaa ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Tixon Nzunda.



PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU

(SERA, URATIBU, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

..............................................................................

Na: Mwandishi Wetu – Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia maswala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amezindua rasmi mfumo wa kielekroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za serikali ambao utawezesha kuimarisha uratibu wa shughuli za Serikali ikiwemo upatikanaji wa taarifa za utekelezaji kwa wakati.

Akizungumza wakati wa tukio la uzinduzi wa Mfumo huo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) hii leo Agosti 16, 2021 alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ina jukumu kubwa la kuratibu shughuli zote za Serikali ikiwa ni pamoja na kuratibu usimamizi wa utekelezaji wa Ilani Chama Cha Mapinduzi. Katika uratibu huo, Ofisi hiyo ina wajibu wa kuratibu taarifa kutoka wizara zote na taasisi za Serikali, hivyo kuzijumuisha na kuandaa ripoti ya Serikali ambayo huwasilishwa kwa mwezi, robo mwaka, nusu mwaka na mwaka kulingana na taarifa husika.

Waziri Mhagama alibainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikikabiliana na changamoto ya upatikanaji wa taarifa za utekelezaji na za uhakika kwa wakati, hali hiyo imechangiwa na kutotumia mifumo ya kielektroniki ambayo inarahisisha upatikanaji na uandaaji wa taarifa. Pia, changamoto nyingine ambayo ofisi hiyo au Serikali kwa ujumla inakumbana nayo ni uainishaji wa vigezo vya kupima ufanisi wa utekelezaji katika baadhi ya maeneo hivyo kwa kuzingatia changamoto hizo Ofisi ya Waziri Mkuu iliamua kuboresha Mfumo wa Dashboard ili kuongeza ufanisi na kurahisisha uratibu wa shughuli za Serikali.

“Mfumo huu wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) utaimarisha uwezo wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuratibu utekelezaji wa shughuli za Serikali pamoja na kuwezesha kupima ufanisi wa utekelezaji. Kwa sasa mfumo utawezesha upimaji wa utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kutumia viashiria vya utendaji,” alieleza Waziri Mhagama

“Kiu ya Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona serikali anayoiongoza inafanya kazi kwa pamoja na kujiratibu. Ni matumaini yangu tukiutumia vyema mfumo huu wa DashBoard utatuletea matokeo chanya na tutaifanya serikali yetu kuweza kutekeleza wajibu wake wa kila siku kwa wananchi” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa pamoja na mfumo huu kurahisisha uratibu na upatikanaji wa taarifa za utekelezaji wa shughuli za Serikali, pia mfumo huo una faida nyingine nyingi ikiwemo; kuwezesha upatikanaji wa taarifa za utekelezaji na kwa wakati; kuwa na sehemu moja ya kupata taarifa na takwimu sahihi kuhusu utendaji wa Serikali; kuwezesha ufanyaji tathmini na upimaji wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa kutumia viashiria na malengo tuliyojiwekea; kupunguza gharama na muda wa uandaaji na uwasilishaji wa taarifa; na kupata nyaraka muhimu ambazo ni dira katika kupanga na kutekeleza shughuli za Serikali.

Sambamba na hayo Waziri Mhagama amezitaka Wizara zenye sera za muda mrefu ambazo hazijafanyiwa tathmini zinafanyiwa tathmini haraka ili kubaini mahitaji ya kisera yaliyopo na kuandaa mikakati ya kuimarisha utekelezaji wa sera husika kabla ya kuwekwa kwenye mfumo huo mpya. Pamoja na hayo amewahimiza Viongozi wa Wizara mbalimbali kutekeleza maagizo na maelekezo ya Viongozi wa Kitaifa na wahakikishe wanatoa taarifa za utekelezaji wa maagizo hayo kwa wakati.

Aidha, Waziri Mhagama alitoa rai kwa wizara zote na taasisi za Serikali kuhakikisha wanawasimamia wataalam wanaohusika katika uwekaji wa taarifa kwenye mfumo huo ili waweze kuweka taarifa zote muhimu kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) alisema kuwa mabadiliko haya ya kidigitali yanasaidia kuisongeza Serikali karibu kwa wananchi badala ya wananchi kufuata huduma za serikali kwenye maofisi.

“Uwepo wa mfumo huu ni jambo ambapo tunapaswa kujivunia nalo kwa kuwa Miaka mitano iliyopita zaidi ya asilimia 80 ya mifumo tulikuwa tunanunua kutoka nje ya nje na tulikuwa tukilipia gharama kubwa sana lakini hii leo zaidi ya asilimia 70 ya mifumo yetu inatengenezwa na wataalam wetu wazalendo na hatutumii gharama kubwa kama hapo awali,” alisema Ndugulile

Naye, Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Masauni alieleza kuwa kuzinduliwa kwa mfumo huo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) utaongeza ufanisi wa kazi na uwazi.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Tixon Nzunda alisema kuwa katika mfumo huo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) moduli zimeongezwa kutoka mbili (2) za awali hadi moduli tano (5) ikiwa ni pamoja na Taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala kutoka kwenye Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; Moduli ya pili ni taarifa zote kuhusu sera zinazotekelezwa nchini, mikakati ya utekelezaji wa sera na taarifa za tathmini za sera; Moduli ya tatu ni Utendaji wa Wizara kwa kujumuisha muhtasari wa bajeti, kazi za kipaumbele na viashiria vya msingi na namna vinavyotekelezwa; Moduli ya nne ni taarifa ya utekelezaji wa maagiza yanayotolewa na Viongozi wa Kitaifa; na Moduli ya mwisho ni taarifa za utekelezaji wa ahadi za Rais kipindi cha Kampeni ya Uchaguzi Mkuu.
Share:

ISRAEL YAKOSHWA NA VIVUTIO VYA UTALII TANZANIA




Baadhi ya watalii kutoka Israel wakipita kuangalia kikundi cha utamaduni kutoka kabila la Wamasai katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kabla ya kuondoka kurejea Israel

Baadhi ya watalii kutoka Israel wakiwa katika eneo la kuondokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kabla ya kuondoka kurejea Israel


Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemedi Mgaza akiongea na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada ya watalii kuondoka kuelekea Israel

Kaimu Meneja Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi. Christina Kamuzola akiongea na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada ya watalii kuondoka kuelekea Israel


Afisa Masoko Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Bw. Michael Makombe akiongea na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada ya watalii kuondoka kuelekea Israel

*****************************

Na Waandishi wetu, Arusha

Mamia ya watalii kutoka Israel waendelea kuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii licha ya changamoto ya Ugonjwa wa UVIKO-19 ambao umeikumba dunia hivi sasa.

Kuja kwa watalii hao kunatokana na sio tu Tanzania kubarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, bali pia hatua za tahadhali zinachokuliwa na Serikali dhidi ya maambukizi ya virusi vya UVIKO-19.

Hatua hizo ambazo zimewejengea imani watalii kuendelea kuja nchini zimetambuliwa na Baraza la Wasafiri na Utalii Duniani (World Travels and Tourism Council-WTTC) ambapo Mwezi Agosti 2020 baraza hilo liliitangaza Tanzania kuwa nchi salama ya kuitembelea.

Akizungumza Jijini Arusha, wakati wa hafla ya kuwapokea watalii takribani 100 kutoka Israel na wengine 150 waliokuwa wanaagwa, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemedi Mgaza amesema ujio wa watalii hao umetokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nje, kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Israel na wadau wengine wa utalii za kutangaza vivutio vya utalii nchini humo.

Juhudi hizo ni pamoja na kushiriki maonesho ya utalii yanayofanyika kila mwaka nchini Israel ambapo kwa mwaka huu yamepangwa kufanyika mwezi Oktoba, kushiriki katika vyombo vya habari mbalimbali nchini humo pamoja na kuwatumia mawakala wa utalii, kampuni za kuongoza watalii na waandishi wa habari.

Mmoja wa watalii waliokuwa wanaagwa leo, Bw. Lior Ziegler aliwahakikishia Watanzania kuwa Watalii kutoka Israel wataendelea kuja nchini kwa sababu Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, huduma bora ikiwemo na mapokezi mazuri ya kuridhisha.

“Nimefurahia kutalii katika vivutio mbalimbali vya utalii hapa Tanzania kwa kweli ni vizuri sana…..nitaendelea kuhamasisha Waisrael kuja kutembea hapa na kujionea wenyewe vivutio hivyo adhimu,” Amesema Bw. Ziegler

Kauli hiyo imeungwa mkono na Afisa Masoko Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Bw. Michael Makombe ambapo alieleza kuwa watalii hao wamevutiwa na Bonde la Ngorongoro kutokana na mazingira yake ya upekee, wanyama kuonekana kwa urahisi pamoja na historia ya Olduvai Gorge ambapo ni eneo linaloaminika kuwa fuvu la mtu wa kale zaidi duniani limegunduliwa.

Kwa upande wa Kaimu Meneja Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi. Christina Kamuzola amesema TTB kwa kushirikiana na Serikali na wadau kutoka sekta binafsi itaongeza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii ili kufikia malengo ya Serikali ya kuleta watalii milioni tano na mapato ya Dola za Marekani bilioni 600 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa katika Ilani ya CCM ya 2020-2025.

Juhudi hizi ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Tarehe 27 Julai, 2021 akiwaapisha mabalozi wapya 13 na kuwaagiza pamoja na mambo mengine, kutangaza vivutio vya utalii, fursa za kiuchumi pamoja na uwekezaji zinazopatikana nchini.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger