Monday, 16 August 2021
FHI 360 YATOA BAISKELI 242 KWA WAWEZESHAJI UCHUMI KUPAMBANA NA VVU SHINYANGA
MGOMBEA WA UPINZANI ASHINDA URAIS ZAMBIA

MWALIMU NA MWENZAKE MBARONI WAKITUHUMIWA KUMUUA MTOTO WA MIAKA MITANO KWA KIPIGO SINGIDA
Na Dotto Mwaibale, Singia
JESHI la Polisi Mkoa wa Singida linawashikilia Mwalimu Regina Laurent, (28) wa Shule ya Msingi Mang'onyi na Mathias Marmo (30) kwa tuhuma za kumuua kwa kipigo mtoto mwenye umri wa miaka 5 aitwaye Joyce John, mkazi wa Kijiji na Kata ya Mang’onyi, wilayani Ikungi mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi ( ACP) Stella Mutabihirwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa watuhumiwa hao walikuwa ni walezi wa mtoto huyo na kuwa uchunguzi zaidi ukikamilika wote wawiliwatafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalowakabili.
Mutabihirwa akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuhusu tukio hilo alisema Agosti 11/2021 majira ya saa 1:30 usiku katika Hospitali ya Malkia wa Ulimwengu iliyopo maeneo ya Puma, Wilayani Ikungi, Mkoa wa Singida mtoto huyo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu hospitalini hapo ambapo wauguzi wa hospitali hiyo walitilia mashaka kifo hicho kutokana na majeraha aliyokuwa nayo marehemu na ndipo waliamua kutoa tarifa kwa Jeshi la Polisi.
Alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida lilipata taarifa hizo siku hiyo majira ya saa 2:00 usiku ambapo lilifanya uchunguzi wa awali na kubaini kuwa majeraha aliyoyapata marehemu yalitokana na kupigwa na vitu vinavyodhaniwa kuwa ni fimbo na kitu butu sehemu mbalimbali za mwili wake na wazazi wake walezi ambao ni Mathias Marmo, (30), Mwalimu wa Shule ya Msingi Mang'onyi na Regina Laurent, (28), wote wairaq na wakazi wa mang'onyi.
Aidha Mutabihirwa alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo alikuwa akipigwa na kufanyiwa ukatili mara kwa mara na walezi wake hao na kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linaendelea kukemea vitendo vya kikatili vinavyofanywa na baadhi wazazi na walezi na linawaomba wananchi kuachana na vitendo hivyo vikiwemo kutoa adhabu zisizokuwa na mipaka kwa watoto na kusababisha unyanyasaji wa kijinsia na wazazi wameaswa kuwalea watoto wao katika maadili mema.
NAIBU WAZIRI DK.MABULA AKUTANA NA WADAIWA SUGU WA KODI ZA ARDHI MKOA WA SINGIDA
Na Dotto Mwaibale, Singida.
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amekutana na wadaiwa sugu wa kodi ya pango la Ardhi Mkoa wa Singida ili kutafuta njia bora za kulipa madeni hayo.
Mabula alikutana na wadaiwa hao katikati ya wiki hii baada ya kukutanishwa nao kwenye kikao chake na watumishi wa idara za ardhi na wadau mbalimbali wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani hapa.
Alisema kwenye Sheria ya ardhi kifungu cha (33) kifungu kidogo cha (3),kinasema mtu yeyote ambaye anamiliki ardhi anatakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi kama sheria inavyoelekeza.
Alisema lakini kuna baadhi ya watu baada ya kupimiwa maeneo yao hujificha na hawaendi kuomba kumilikishwa ili waanze kulipa kodi.
Alisema kutokana na hali hiyo Serikali iliona iweke utaratibu kwa mtu yeyote ambaye amepimiwa eneo lake apewa siku 90 za kuomba kumilikishwa na asipofanya hivyo baada ya siku hizo atatakiwa kulipa kodi, ambapo pia ilitoa msamaha kwa waliopimiwa kipindi cha nyuma wataanza kulipa kuanzia mwaka jana sheria ilipoanzishwa.
Mabula alisema wizara imeamua kutoa nafasi hiyo kwa wadaiwa hao kabla ya kuanza utekelezaji wa sheria ili waweze kujua wajibu wao kama raia, taasisi na watu binafsi wa kulipa kodi ambapo wizara itatoa nafasi ya mwaka mmoja waweze kulipa madeni yao.
"Niwatake watumishi wa wizara hii mkaanze kusimamia sheria, kwasababu hamsimamii sheria vizuri ndio maana mchakato huu wa kulipa kodi unakuwa mgumu,nniwaombe walipa kodi lipeni kodi zenu kila mwaka mkivusha zoezi la kulipa litakuwa zito kwasababu kiwango kitaongezeka kutokana na kulimbikiza." alisema Mabula.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida Shamim Hozza akisoma taarifa ya utekelezaji wa wizara hiyo mkoani hapa alisema mkoa ulipangiwa kukusanya maduhuri yatokanayo na ardhi Sh. Bilioni moja na milioni mia tisa lakini walikusanya Sh. Bilioni moja na milioni mia mbili sawa na 66%.
Alisema moja ya changamoto zilizosababisha ofisi yake kushindwa kufikia lengo ni madeni makubwa ya Serikali na baadhi ya taasisi za dini ambazo zimekuwa na ukakasi wa kulipa madeni hayo.
Hozza alisema ili kukabiliana na changamoto hizo ofisi yake inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhamasisha na kufanya mikutano ya wananchi pamoja na kutoa matangazo kwa njia mbalimbali, kutoa nyaraka za umilikishaji na madeni na kwa wale ambao walikaidi kulipa madeni walifikishwa kwenye mabaraza ya ardhi kwa hatua zaidi.
Dkt.Mabula kabla ya kufanya kikao hicho alishiriki katika zoezi la mradi wa upimaji mipaka ya vijiji na makazi katika Kijiji cha Mnang'ana wilayani Ikungi ambao unatekelezwa kwa pamoja na mashirika ya UN WOMEN, UNFPA na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa ufadhili wa KOICA.












