Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wamiliki wa ardhi wanaotaka kujenga kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu zote wakati wa kufanya ujenzi.
Waziri Lukuvi alisema hayo mwishoni mwa wiki hii katika ofisi yake ya ardhi ya mkoani Dar es salaam na Pwani. Alisema sheria inamtaka mmiliki wa ardhi anayetaka kufanya ujenzi kupata kibali kutoka halmashauri za miji, manispaa na majiji na kuongeza kuwa sheria hiyo inakataza kufanya ujenzi bila kibali kutoka mamlaka husika.
”Naelekeza watendaji wote wawe wa ardhi au mipango miji kuhakikisha sheria zinafuatwa kwa kudhibiti ujenzi holela na sheria inakataza kabisa kujenga bila kupata kibali kutoka katika mamlaka husika” alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, zoezi la urasimishaji linaloendelea sasa maeneo mbalimbali ni kwa majengo yaliyojengwa tu na kusisitiza kuwa zoezi la urasimishaji isiwe sehemu endelevu ya kuvunja sheria na kubainisha kuwa angetaka kuona maeneo yote ya miji hasa Dodoma yanajengwa kwa kupatiwa kibali.
Aliwataka wataalamu wote hasa waliopo halmashauri katika yale maeneo yaliyotangazwa kimji kwa mujibu wa sheria wananchi wake waelimishwe kujenga katika viwanja vilivyopangwa na kupimwa na wawe wamepatiwa vibali na mamlaka za halmashauri husika.
” Hatua zichukuliwe kuzuia jambo hili tunataka miji endelevu ambayo wananchi wanaishi na kujenga kwa mujibu wa sheria” alisema Lukuvi.