Chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa shinyanga kimeziagiza kamati za siasa ngazi za vijiji,mitaa, kata na wilaya zote mkoani humo kuhakikisha wanajenga ofisi za matawi, vijiji, mitaa na kata ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama wake.
Agizo hilo limetolewa febuari 28 mwaka huu na Mwenyekiti wa (CCM) mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa katika maadhimisho ya miaka 43 ya (CCM) yaliyofanyika katika kijiji cha Bukindwasali katika halmashauri ya Ushetu wilayani kahama yaliyoenda sambamba na ukaguzi majengo ya chama hicho.
Mabala alisema kuwa kata ya Idahina imeongoza kimkoa katika ujenzi wa majengo ya chama ambapo mpaka sasa wamejenga ofisi za kata,kijiji na matawi 38 ya chama hicho ambayo yote yako katika hatua za kukamilika.
“Katika mkoa wa Shinyanga, kata ya Idahina mmeongoza kwa kujenga ofisi nzuri ya kisasa ya tawi la CCM Bukindwasali,niwaagize viongozi wangu CCM wa ngazi za wilaya zote kuhakikisha wanawahamashisha wanachama wetu kujenga ofisi ili kurahisisha utendaji kazi”alisema Mabala.
Sambamba na hilo Mabala aliwataka wanachama wa CCM kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ofisi za chama kwa ngazi zote ili kuwawezesha viongozi wapya waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa wanafanya kazi katika mazingira bora.
Kwa upande wake Naibu waziri wa ujenzi, na Mbunge wa jimbo la Ushetu,Elias Kwandikwa awamu ya Tano ya uongozi wa Dk John Pombe Magufuli imedhamiria kukijenga chama upya kwa kuhakikisha kila tawi,kijiji na kata vinakuwa na ofisi za kisasa za CCM.
“Niwaombe wanachama wenzangu jengeni ofisi za chama chetu mimi kama mbunge ninayetokana na CCM nitahakikisha nimalizia ujenzi wa majengo haya lengo letu ni kuwasaidia wanachama wetu kuhudumiwa kwa urahisi”alisema kwandikwa.
Naye Mwenyekiti wa CCM kata ya Idahina Masalu Walwa alisema kuwa katika eneo lake kumekuwa na mwamko mkubwa wa wanachama kushiriki katika ujenzi wa ofisi za CCM pamoja na majengo mengine ya Umma.
Aliongeza kuwa mbali na ofisi za CCM katika kata ya Idahina waliweza kujenga jengo la serikali ya kijiji,bweni la wasichana katika shule ya sekondari pamoja miradi mingine ya chama.
Mwisho.