Wizara ya Kilimo ipo katika hatua za mwisho kupeleka Bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Maendeleo ya Ushirika yatakayoendana na mahitaji ya sasa ambayo yatahusisha mabadiliko ya mfumo na muundo wa uongozi ili kuendana na mahitaji ya teknolojia na kuleta ushindani wa kibiashara.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe (Mb) ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma tarehe 6 Februari 2020 wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini Mhe Martini Mtonda Msuha aliyetaka kufahamu serikali ina mpango gani wa kurekebisha Sheria ya Vyama vya ushirika ili kuondoa mapungufu yaliyopo, hususani kwa upande wa uanachama na kuipa serikali nguvu za kisheria juu ya Vyama vya ushirika.
Bashe amesema kuwa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2015 – 2020 (Ibara ya 22 (g)(iv) na 86 (a) inaelekeza “Kuifanyia mapitio Sera ya Vyama vya Ushirika na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Ushirika na upatikanaji wa takwimu zitakazosaidia kuandaa mipango na kuleta mageuzi katika Sekta ya Ushirika na kuimarisha uchumi wa Taifa na Kuviimarisha vyama vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ya ndani na nje kwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji, uchambuzi na uenezaji wa taarifa za masoko na kutoa elimu juu ya uongezaji thamani na biashara“
Amesema kuwa Ushirika ni dhana ya hiari, lakini Serikali ni msimamizi mkuu wa vyama vya ushirika pale ambapo viongozi wake au vyama vyenyewe havitekelezi malengo yaliyokusudiwa na dhamira ya kuanzishwa kwa sekta ya ushirika.
Serikali inakiri vyama vinakabiliwa na changamoto za kiutendaji, usimamizi, viongozi kutokuwa waadilifu na mapungufu ya kimfumo ya uendeshaji wa vyama vya Ushirika hapa nchini.
Hata hivyo, Bashe amesema vipo baadhi ya vyama vya ushirika ambavyo vinafanya vizuri. Mfano, Chama cha Ushirika cha Chai Mkonge, Mafinga na Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU).
Kadhalika Mhe Bashe ameongeza kuwa Ushirika ndicho chombo cha kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi kwa kuwaunganisha wakulima ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kutoa huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo na kutafuta masoko ya mazao.