Tuesday, 6 August 2019

Serikali Yajipanga Kuongeza Rasilimali Watu TRA

Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imejipanga kuongeza ufanisi wa kiutendaji na  ukusanyaji wa Mapato wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA kwa kuongeza wafanyakazi na kuboresha makazi ya watumishi, ikiwa ni sehemu ya kutatua changamoto za utekelezaji wa Bajeti ya Mamlaka hiyo kwa mwaka wa Fedha 2018/19.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam  na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, wakati wa ziara ya kikazi ya kufuatilia mafanikio na changamoto za utekelezaji wa bajeti  ya mwaka 2018/19 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Dkt. Kazungu alisema kuwa, amebaini upungufu wa takribani wafanyakazi 2000 wa kada mbalimbali katika mamlaka hiyo, hivyo kufifisha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa kiwango toshelevu ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Kama Wizara ya Fedha na Mipango tumeona kuna umuhimu wa kuiwezesha TRA katika rasilimali watu na fedha ili kuongeza mapato ya Serikali katika muda mfupi ujao ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla”, alieleza Dkt. Kazungu.

Alisema  kuwa changamoto nyingine ni pamoja na upungufu wa vitendea kazi yakiwemo magari, ambapo ameahidi kulifanyia kazi suala hilo ili kurahisisha utendaji kazi wa Mamlaka hiyo muhimu katika mstakabali wa ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Dkt. Kazungu alisema ziara yake katika Mamlaka ya Mapato Tanzania ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara yake hususani katika eneo la changamoto zilizojitokeza kwa mwaka uliopita  na kuangalia ni njia zipi zinaweza kutumika kuzitatua  ili kuleta ufanisi kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu TRA, Dkt. Edwin Mhede, alimpongeza Dkt. Kazungu  kwa kufanya ziara katika Taasisi yake na akamhakikishia kuwa amejipanga kimkakati kuhakikisha mapato yanaongezeka na pia iwapo suala la upungufu wa wafanyakazi litatatuliwa, ongezeko la makusanyo litakuwa sio jambo gumu kwa mamlaka yake.

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatibu Kazungu, anafanya ziara katika Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha kubaini changamoto za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 na kuangalia utatuzi wake kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Mwisho.


Share:

Yesu FEKI Aliyeitembelea Kenya Wiki Iliyopita Afariki Dunia

Michael Job raia wa Marekani ambaye ni Mhubiri na Muigizaji anayeidaiwa kuwa Yesu feki, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini.
 
Hospitali ya Heyn imethibitisha kifo hicho na wamesema alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na amefariki wakati akipatiwa matibabu hospitalini hapo.

Yesu  huyo feki alikaribishwa na Wachungaji wawili kutembelea nchini Kenya wiki iliyopita na alikuwa mgeni katika siku ya tamasha la dini ya wakristo nchini humo na kudanganya watu kuwa yeye ni Yesu amerudi kama alivyoahidi.

Wiki iliyopita Serikali ya nchini Kenya ilimuondoa Michael Job na kuwakamata wachungaji hao wawili  kwa kosa la kumualika Yesu huyo wa uongo.

Picha na Video zilimuonyesha Michael Job akiwa amevalia mavazi kama ya Yesu wa ukweli zilienea kwa wingi katika mitandao ya kijamii


Share:

Chanjo Kuzuia Ugonjwa Wa Mapafu Ya Ng’ombe Yaingia Sokoni, Ya Kichaa Cha Mbwa Mbioni Kuzalishwa Nchini.

Na. Edward Kondela
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa wito kwa wananchi hususan wafugaji kuchanja ng’ombe wao dhidi ya ugonjwa wa mapafu ya ng’ombe (CBPP) ambao husababisha vifo kwa mifugo hiyo.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mifugo nchini Dkt. Hezron Nonga akizungumza katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kwenye viwanja vya Nyakabindi katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu amesema chanjo hiyo iliyoanza kutumika nchini Mwezi Julai mwaka huu inapatikana kwa Shilingi 200 hadi 250 pekee.

“Ugonjwa wa mapafu ya ng’ombe unasababisha kifo usipomkinga ng’ombe wako kwa kutumia chanjo hii utaingia gharama kubwa kwa kuwa ng’ombe huyo atakufa pia utatumia gharama kubwa kuwalinda ng’ombe wengine ulionao.” Amesema Dkt. Nonga

Akizungumzia zaidi kuhusu chanjo hiyo Dkt. Nonga amesema chanjo tayari ipo sokoni nchi nzima na kwamba vipo vituo 11 kila kanda na inapatikana kwa Shilingi 200 hadi 250 pekee na kuwataka wafugaji kuhakikisha ng’ombe wanachanjwa dhidi ya ugonjwa huo.

Aidha amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Kituo cha Kuzalisha Chanjo Kibaha (TVI) kilichopo Mkoani Pwani inatarajia katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili kuanza kuzalisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambazo kwa sasa zinanunuliwa kutoka nchi za nje.

Kutokana na watu wengi kuwa na utaratibu wa kumiliki mbwa katika makazi yao katika kipindi cha siku za hivi karibuni, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mifugo nchini Dkt. Hezron Nonga amewataka watu wanaomiliki mbwa kuhakikisha wanyama hao wanachanjwa kwa kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa hauna tiba endapo binadamu atang’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huo.

“Tunataka hii chanjo iwe inapatikana kila mahali pamoja na kufanya msako nchi nzima kwa watu wanaomiliki mbwa lakini hawapeleki mbwa hao kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.” Amesema Dkt. Nonga

Amefafanua kuwa kwa kawaida chanjo hiyo hupatiwa mbwa mara moja kwa mwaka ambapo kwa sasa inapatikana kwa Shilingi Elfu Moja pekee ili kuhakikisha wamiliki wa mbwa na wananchi wanakuwa salama.

Mwisho.


Share:

Wizara Ya Afya Kudhibiti Kifua Kikuu Magareza 15 Nchini

Na. Catherine Sungura, WAMJW-DSM
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti kifua kikuu na Ukoma kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza nchini wanaanza afua ya ufuatiliaji wa kutathimini hali ya huduma za kutokomeza kifua kikuu katika magereza nchini.
 
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Jeshi la Magereza (CP) Owesu Ngalama wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa maofisa wa jeshi hilo yanayofanyika kwenye bwalo la magereza ukonga jijini hapa.

CP Ngalama alisema kuwa afua hiyo itasaidia jeshi la magereza kuweza kubaini hali ya TB kwenye magereza kwani wanaoingia kwenye magereza ni wana jamii hivyo itasaidia kubaini ugonjwa huo kwa wafungwa na kwa jamii kwa ujumla

“Ugonjwa huu unaambukizwa kwa hewa hivyo kwa tathimini hii itasaidia kuleta utaalam mkubwa kwa wataalam wetu wa tiba waliopo kwenye jeshi kwani hali ya TB sio kubwa kwenye magereza ila lengo ni kuhakikisha hakuna maambukizi makubwa kwani wafungwa wanaingia na kutoka”.Alisema CP Ngalama

Aidha,ameishukuru wizara ya afya kwa kuendelea kushirikiana nao kwa muda mrefu hususan kwenye utoaji huduma za afya ikiwemo utoaji wa dawa,vifaa na vifaa tiba pamoja na masuala ya lishe kwenye vituo vya afya vilivyopo kwenye magereza nchini.

Naye Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP) kutoka Wizara ya Afya Dkt. Beatrice Mutayoba alisema ugonjwa wa Kifua Kikuu bado ni jangwa kwani bado kuna takribani watu laki moja na elfu hamsini na nne wanakadiriwa kuugua kifua kikuu kila mwaka na inakadiriwa vifo elfu ishirini na saba kila mwaka nchini.
 
Dkt. Mutayoba alisema kifua kikuu kinaweza kumpata mtu yeyote kwani maambukizi yake ni ya njia ya hewa hivyo yapo makundi hatarishi zaidi ikiwemo magereza hivyo wanaweka jitihada zaidi kuyafikia makundi hayo ili kutokomeza kifua kikuu ifikapo 2030.

“kama nchi tumepiga hatua kubwa sana kutokomeza ugonjwa huu hivyo tunaongeza juhudi zaidi kwenye makundi hatarishi ikiwemo magereza,migodini,wavuvi ili kuwafikia kwa karibu na kuhakikisha tunapunguza maambukizi ndani ya magereza na maeneo haya”.Alisisitiza

Hata hivyo alisema mkakati wa kudhibiti kifua kikuu upo kwa wananchi wote hivyo kama mpango wanaendelea kutoa elimu kwa watanzania wote mara waonapo dalili waende kwenye vituo vya afya kwani wizara ya afya inatoa dawa,vipimo na huduma za kifua kikuu bila malipo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya “Magerezani tunaweza utaratibu kwa wanaoingia kuwe na taratibu za uchunguzi ili anapokutwa na kifua kikuu waanze matibabu kwani unapoanza matibabu ndani ya wiki mbili huwezi kuambukiza wengine”.Alisema Dkt. Mutayoba

Mikoa kumi na tano itakayoanza na utekelezaji huo ni pamoja na Dar es salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Kilimanjaro, lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.


Share:

Watumishi wa umma na sekta binafsi wakumbushwa swala la maadili

Na Amiri kilagalila-Njombe
Serikali imewataka watumishi wa umma na sekta ninafsi kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa Umma kwa lengo la kuleta ustawi kwa jamii katika utoaji wa huduma bora na stahiki kwa wahitaji.

Agizo hilo linakuja wakati kukiwa na malalamiko kadha wa kadha kutoka kwa baadhi ya wananchi juu ya utendaji na uwajibikaji mbovu kwa baadhi ya watumishi wa umma ambapo imedaiwa kuwepo kwa anguko la maadili ya utumishi wa umma hatua ambayo imeleta athari kwa umma na kuhitaji hatua za haraka kuchukuliwa kuanzia vyuoni.

Akizungumza katika mahafali ya 4 ya chuo cha afya cha Mgao mkoani Njombe kaimu mganga mkuu wa mkoni Njombe Dr Manyanza Mponeja amewataka wahitimu wa kozi mbalimbali za afya chuo hapo kuzingatia miiko na mdaadili ya kazi pindi watakapo kuwa kazi kwa madai ya kwamba katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na madai ya kuporomoka kwa maadili ya utumishi wa umma hususani katika kada ya afya watu kutumia lugha chafu kwa wagonjwa ,mavazi yasiyo na staha pamoja na ulevi kupindukia hatua ambayo si njema.

Mbali na changamoto ya maadili Dr Mponeja ametolea ufafanuzi ombi la kuondolewa kwa gharama ya shilingi elfu 50 wanayotakiwa kulipa wanafunzi katika hospitali,vituo vya afya na zahanati ambazo wanaenda kujifunza elimu kwa vitendo ambapo amesema serikali imeipokea changamoto hiyo na kwenda kuangalia namna ya kuiondoa ili kutoa nafasi kwa wanafunzi hata wenye hali duni kupata mafunzo hayo muhimu.

“Sitegemei muuguzi ambaye anaandaliwa kukutana na mteja anayemweleza siri zake zote aweze kumtatulia akawa anavaa nguo fupi kiasi ambacho hata mteja anaanza kujiuliza”alisema Mponeja

Licha ya serikali kuahidi kutafuta ufumbuzi wa gharama elimu kwa vitendo inayotolewa na wanafunzi wa vyuo binafsi vya afya lakini afisa utumishi wa chuo cha afya cha mgao Deus Kuba anafafanua jinsi tozo hiyo inavyokwamisha jitihada za wanafunzi wanaotoka familia duni huku pia akionyesha kuwa tofauti na mitazamo ya ukosefu wa ajira katika sekta ya afya kwa kuwa watu wazaliwa na kuumwa kila uchwao hivyo wahitimu wanauwezo wa kufungua maduka ya dawa na phamasi binafsi na mkono kwenda kinywani.

“Wanafunzi wetu wanavyoenda kufanya mazoezi ya vitendo mahospital hususani ya serikali,utakuta kila mwanafunzi huwa anatakiwa kuchangia  gharama ya shilingi elfu 50,unakuta wengine wanashindwa hivyo ningependekeza hizi gharama aidha zitolewa au zipunguzwe”alisema Deus Kuba

Kwa upande wao wahitimu wa kozi mbalimbali za afya akiwemo  Evancy Machea na Hapness Amon wakieleza jinsi walivyo iva kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii na kumudu ushindani katika soko la ajira wamesema wamejengewa uwezo hata wakujiajiri kwa kufungua maduka ya dawa na phamasi.

Jumla ya wahitimu 59 wamehitimu na kukabidhiwa vyeti katika mahafali ya nne ya chuo cha afya Mgao.


Share:

YESU FEKI ALIYEIBUKIA KENYA NA KUZUA GUMZO AFARIKI DUNIA

Michael Job raia wa Marekani ambaye ni mhubiri na muigizaji anayeidaiwa kuwa Yesu Feki, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini.
Michael Job akiwa anaongea nchini Kenya.

Hospitali ya Heyn imethibitisha kifo hicho na wamesema alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na amefariki wakati akipatiwa matibabu hospitalini hapo.

Yesu feki alikaribishwa na Wachungaji wawili kutembelea nchini Kenya wiki iliyopita na alikuwa mgeni katika siku ya tamasha la dini ya wakristo nchini humo na kudanganya watu kuwa yeye ni Yesu amerudi kama alivyoahidi.

Wiki iliyopita Serikali ya nchini Kenya ilimuondoa Michael Job na kuwakamata wachungaji hao wawili kwa kosa la kumualika Yesu huyo wa uongo.

Picha na Video zilimuonyesha Michael Job akiwa amevalia mavazi kama ya Yesu wa ukweli zilienea kwa wingi katika mitandao ya kijamii hasa barani Africa.
Share:

Waziri Simbachawene apongeza mradi wa upandaji mikoko Zanzibar

Na Ofisi ya Makamu wa Rais
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. George Boniface Simbachawene ameupongeza mradi wa utunzaji mazingira kupitia upandaji miti ya mikoko mjini Zanzibar.
 
Mhe. Simbachawene ametoa pongezi hizo Agosti 5, 2019 katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kujitambulisha na kukagua miradi ya Muungano na Mazingira visiwani hapa.
 
Akiwa katika eneo hilo lenye hekta nne lililopo Shehia ya Kilimani Wilaya ya Mjini Mkoa wa Magharibi alisema ameridhishwa kuona namna ambavyo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ilivyotekeleza mradi huo pamoja na ufadhili kutoka Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
 
“Niwapongeze sana kwa mradi huu mzuri na tunaona matokeo yake umesaidia mawimbi yasije kwa kasi katika eneo hili na kusababisha mmonyoko na tukiamua kufanya kazi kwa pamonja na jamii tunaweza kufanya vizuri,” alisema.
 
Aidha, Mhe. Simbachawene alitoa wito kwa wataalamu kuangalia namna ya kuibua miradi mingine katika fukwe za mikoa mingine kama Dar es Salaam, Tanga, Lindi na Mtwara ili kusaidia kutunza mazingira.
 
Katika hatua nyingine alikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kianga katika Wilaya ya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi aliwapongeza wananchi kwa kusimamia mradi huo.
 
Alisema kuwa kwa kiasi cha sh. milioni 174 inadhihrisha namna wanavyotumia fedha kwa uaminifu na kuwa tutapiga hatua katika kuendeleza sekta ya huduma ya afya kwa wananchi.
 
“Nawapongeza sana wananchi hasa kwa kamati hii mmefanya vizuri kusimamia mradi huu wa ujenzi wa kituo cha afya tunaamini udokozi haukuwepo kazi imefanyika fenicha (samani) zipo, vifaa tiba na utendaji kazi mzuri unaendelea kufanyika,” alisema.


Share:

MTOTO WA DEREVA WA MKUU WA MKOA WA MARA ALIYEPATA AJALI AKIENDESHA GARI LA RC AFARIKI DUNIA


Mtoto wa Dereva wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Kasobi Shida mwenye umri wa miaka 26, aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Musoma baada ya kupata ajali wakati akiendesha gari ya Mkuu wa Mkoa,Adam Malima amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Juma Ndaki amethibitisha kutokea kwa kifo hicho ambapo amesema,  kifo hicho kimetokea kwa sababu ajali aliyoipata ilikuwa ni mbaya hali iliyopelekea kijana huyo kupata majeraha ndani ya mwili wake.


''Ni kweli amefariki na sababu ya kifo chake, baada ya madaktari kumfanyia upasuaji waligundua utumbo wake umepasuka na damu imevujia ndani kwa ndani'' amesema RPC Ndaki.

Aidha Kamanda Ndaki akielezea hali ya Dereva wa Mkuu wa Mkoa (Baba wa Marehemu), amesema hali yake inaendelea vizuri na kwamba madaktari wanaendelea kumfanyia ushauri wa kisaikolojia ili arejee kwenye hali yake ya kawaida.

Kasobi Shida alipata ajali siku ya Agosti 4, baada ya kuchukua gari hilo bila ridhaa ya mzazi wake ambapo lilimshinda kuendesha na kutoka nje ya barabara kisha  kugonga daraja.


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne 06 August

























Share:

Monday, 5 August 2019

Mwanahabari Erick Kabendera Apandishwa Mahakamani na Kusomea Makosa Matatu ya Kuongoza Genge La Uhalifu,kukwepa Kodi Na Kutakatisha Fedha.

Mwanahabari Erick Kabendera amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka 3 ikiwemo kujihusisha na genge la uhalifu,kukwepa kodi na kutakatisha fedha  Tsh.173.2 Milioni.

Hati ya mashtaka dhidi ya mshtakiwa Kabendera imesomwa na mawakili wawili  wakuu wa serikali, na mmoja Mwandamizi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile.

Mshtakiwa Kabendera anatetewa na mawakili wa kujitegemea, Gebra Kambore, John Mallya na Benedict inshabakaki.

Akisoma shtaka la kwanza, wakili wa serikali Mkuu, Paul Kadushi amedai, mshtakiwa anadaiwa katika siku tofauti tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Kabendera alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Katika shtaka la pili lililosomwa na wakili Wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi imedaiwa, siku na mahali hapo mshtakiwa  bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya sh. 173, 247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Katika shtaka la utakatishaji fedha lililosomwa na wakili Wa serikali Mwandamizi, Wankyo Simon imedaiwa, kati ya Januari 2015 na Julai 2019 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha sh. Milioni 173.2 wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa Kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.

Hata hivyo, mshtakiwa Kabendera hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kwa kupata kibali kutoka kwa DPP.

Mawakili wa utetezi wakiongozwa na wakili Kambore, wameomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi haraka kwani kesi dhidi ya mteja wao haina dhamana. Hivyo katika terehe itakayokuja wangependa kujua upelelezi umefikia wapi.Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 19 Mwaka huu, mshtakiwa amepelekwa rumande.



Share:

Alichokisema Rais Magufuli Wakati Akifungua Maonyesho Ya 4 Wiki Ya Viwanda Kwa Nchi Za SADC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amefungua maonesho ya viwanda ya nchi za Jumuiya ya SADC, yaliyofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki hiyo, Rais Magufuli amezitaka nchi hizo kupeana fursa wenyewe kwa wenyewe hasa linapofikia suala la biashara, ambapo ameziomba nchi hizo, kuangalia namna ya kushirikiana kwa manufaa ya uchumi wa viwanda.

"Tuweke kipaumbele kwenye utumiaji wa teknolojia ya viwanda kwenye Jumuiya yetu kabla ya kwenda mbali, tuuziane bidhaa kabla ya kwenda kwingine, kama Namibia wanahitaji mahindi tuwapelekee mahindi, hili soko la watu Mil. 300 wa SADC litakuza uchumi wetu." amesema Magufuli.

"Sekta ya viwanda imeanza kuleta mafanikio kwa nchi za SADC, hamasa ya ujenzi wa viwanda umeongezeka, kwa sisi Tanzania tumeweka mkazo wa kutumia malighafi zinazozalishwa hapa, kwa miaka 3 zaidi ya viwanda 4000 vimeanzishwa." Amesema Rais Magufuli.

Maonesho hayo ya viwanda yanatarajia kufanyika kwa wiki nzima kuanzia leo, Julai 05, ambapo mara baada ya kukamilika kwa maonesho hayo, utaanza mkutano wa Marais 19 wa nchi za Jumuiya ya SADC ambapo Rais Magufuli ni Mwenyekiti.


Share:

Wananchi Wahimizwa Kuchangamkia Fursa Zilizopo SADC

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Stergomena Tax amewataka wafanyabiashara nchini Tanzania kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuanza kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika nchi wanachama.

Dk Stergomena  ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 5, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya bidhaa katika wiki ya Viwanda kwa Nchi 16 za SADC. Uzinduzi huo umefanywa na Rais John Magufuli katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) nchini Tanzania.

Katika hotuba yake, Dk Stergomena amewataka wafanyabiashara kutoa taarifa katika wizara ya viwanda pale wanapokutana na vikwazo wakati wa shughuli zao za kibiashara ndani ya jumuiya hiyo iliyoondoa vikwazo na baadhi ya tozo za kibiashara.


Share:

SIMBA CREAM TANGA WATOA MSAADA KITUO CHA KULEA WATOTO YATIMA RASKAZONE CHA CASAFAMILIA ROSSETE

 KATIBU Msaidizi wa Tawi la Simba Cream la Jijini Tanga Edgar Mdime ambaye pia ni Mweka Hazina kulia akimkabidhi biskuti mtoto Huchirachi Ally leo anayelelewa kwenye kituo cha Kulea watoto yatima cha Casafamilia Rosetta Centre kilichopo Raskazone Jijini Tanga wakati wapenzi na wanachama wa Simba Jijini Tanga walipokwenda kutoa misaada kwenye kituo hicho ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya simba
 KATIBU Msaidizi wa Tawi la Simba Cream la Jijini Tanga Edgar Mdime ambaye pia ni Mweka Hazina kulia akimkabidhi biskuti mtoto Huchirachi Ally leo anayelelewa kwenye kituo cha Kulea watoto yatima cha Casafamilia Rosetta Centre kilichopo Raskazone Jijini Tanga wakati wapenzi na wanachama wa Simba Jijini Tanga walipokwenda kutoa misaada kwenye kituo hicho ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya simba
 KATIBU Msaidizi wa Tawi la Simba Cream la Jijini Tanga Edgar Mdime ambaye pia ni Mweka Hazina kulia akimkabidhi msaada wa vitu mbalimbali Mkurugenzi wa MKURUGENZI wa Kituo hicho Irine Kaoneka

 Sehemu ya wana Simba
 Sehemu ya wana Simba wakiwa wamebabe vitu mbalimbali baada ya kufika kwenye kituo hicho
 KATIBU Msaidizi wa Tawi la Simba Cream la Jijini Tanga Edgar Mdime kushoto akiwa na Mwanachama mwenzie Bertha Mwambela wakiingia kwenye kituo hicho wakiwa na vitu mbalimbali
Sehemu ya viti ambavyo vimekabidhiwa leo vikiwa vimetolewa


TAWI la Simba Cream la Jijini Tanga leo wamekabidhi misaada ya viti mbalimbali kwenye kituo cha Kulea watoto yatima cha Casafamilia Rosseta ikiwa ni kuelekea kilele cha siku ya Simba maarufu kama Simba Day.

Hafla ya makabidhiano ya msaada wa vitu ulifanywa na katibu Msaidizi wa tawi la Simba Cream Edgar Mdime kwa Mkurugenzi wa Kituo hicho Irine Kaoneka

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo MKURUGENZI wa Kituo hicho Irine Kaoneka amesema kwamba wamekuwa wakiiombea kila mara klabu ya Simba iweze kufanya makubwa kwenye soka hapa nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.

Alisema kwamba wamefurahishwa na ugeni huo kutoka Simba Tanga kwani wamefanya jambo jema bibilia inasema ibada njema ni iliyosafi kusaidia jamii inayokuwa ikihitaji mahitaji mbalimbali

“Hivyo kwa hili Simba Cream hapa mmefanya ibada njema na sisi tutaendelea kuiombea Simba kila wakati ili iweze kupata mafanikio makubwa pamoja na kuendelea kuiwakilisha nchi kwenye mashindano makubwa “Alisema

Awali akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Katibu Msaidizi wa Tawi la Simba Cream la Jijini Tanga alisema kwamba wameamua kukabidhi msaada huo ili kurejesha shukrani kwa jamii

“Leo hii tumekabidhi msaada huu tunaamini kwamba utakuwa chachu kwenye kituo hiki lakini pia niwatumie salamu watani wetu wa Jadi Yanga wajipange kwani msimu ujao hawatasalimika na kipigo kutoka kwa Mnyama “Alisema

Mdime ambaye pia ni Mweka Hazina alisema pia utaratibu huu wa Simba Day umekuwa ukifanyika kwa kipindi cha miaka 10 sasa kwa kutoa misaada mbalimbali kwa watoto yatima na kuwafariji wagonjwa .

Alisema wameandaa Coaster na wanachama 33 wataondoka kuelekea dar kwa ajili ya kushuhudia Simba day wamejipanga wapo vizuri na hawana presha.

Hata hivyo alisema kutokana na uwepo kwa kikosi kipana ndani ya timu hiyo hakuna mtu ambaye wanaweza kumuogopa wala kushindana nao isipokuwa TP Mazembe.

Mwisho.
Share:

Lugola Aaapa Kuendelea Kupambana na Polisi Wasiotii Maagizo Yake

Na Felix Mwagara, MOHA.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola mara baada ya kuteuliwa na Rais Dk John Joseph Pombe Magufuli kuiongoza Wizara hiyo, kazi ya kwanza aliyoifanya ni kulivunja Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na mabaraza yote ya ngazi ya Mkoa nchini.


Waziri Lugola alitangaza uamuzi huo Julai 5, 2018 jijini Mbeya alipozungumza na Wajumbe wa Baraza la usalama barabarani mkoani humo kutokana na changamoto mbalimbali zilizokua zinalikabili Baraza hilo, ikiwemo ongezeko la ajali, na askari wa usalama barabarani kujihusisha na matukio ya kuchukua rushwa.

Kutokana na uboreshaji wa baraza hilo, Lugola anaendelea kuhakikisha matrafiki wanafanya kazi kwa weledi kuepuka rushwa na kutonyanyasa madereva ambao wanafuata taratibu za usalama barabarani.

Licha ya baadhi ya madereva kutii sheria bila kushurutishwa lakini wapo ambao wanavunja sheria za usalama barabarani, Waziri Lugola anawaagiza Polisi nchini kuendelea kuwakamata na kuwapiga faini pamoja na kuwapeleka mahakamani wanaovunja sheria.

Lugola alisema kuna baadhi ya askari wa usalama barabarani wanajua sheria lakini wanafanya makusudi kwa lengo la kupata fedha za rushwa kwa madereva wanaofanya makosa au wana vyombo vya moto ambavyo ni vibovu.

Kutokana na changamoto hizo, Lugola akiwa katika ziara zake za kikazi zilizoambatana na mikutano ya hadhara, alizozifanya kuanzia mwezi Julai, 2019 mara baada ya kuteuliwa kuingoza Wizara hiyo, katika Mikoa ya Kigoma, Kagera, Arusha na Morogoro, licha ya kuzungumza mengi ya Wizara yake, lakini alijikita zaidi kusambaratisha kero za bodaboda nchini.

Lugola anasema yeye hawezi kufanikiwa peke yake bila Jeshi la Polisi hasa Kikosi cha Usalama Barabarani kumpa nguvu anapotoa maagizo yake kwa viongozi wa Jeshi ambapo lengo lake kuu si kubomoa bali kuboresha na kuwafanya madereva wa bodaboda waweze kupambana na hali ngumu ya maisha kupitia biashara ya bodaboda wanaoifanya.

“Lengo langu kuu ni kuwasaidia waendesha bodaboda waweze kufanya kazi zao kwa amani, bila bughudha kama walivyoahidiwa na mheshimiwa Rais Magufuli, hivyo maelekezo ninayotayoa kwa Jeshi lazima yafuatwe,” anasema Lugola.

Lugola amesema baadhi ya Wakuu wa Vikosi vya Usalama Barabarani (MaRTO) wanapuuza maagizo yake wakisema kuwa ni maagizo ya kisiasa hivyo wao wanafuata sheria, hali inayomfanya Waziri huyo kuchukizwa na kauli hizo ambazo zinavunja sheria za nchi na pia yeye Waziri anamamlaka ya kutoa agizo lolote ambalo lipo sahihi kwa mujibu wa sheria.

“Mimi ni Mwanasiasa nikiwa jimboni kwangu Mwibara, nje ya jimbo langu, mimi ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, hivyo ninapotoa maelekezo au maagizo ni kutokana na nafasi yangu na lazima yafuatwe ili nchi iweze kusonga mbele,” anasema Lugola.

Akizungumza katika Mkutano wa hadhara, uliofanyika Uwanja wa Stendi, Wilayani Malinyi, Mkoani Morogoro, ambao ulihudhuriwa na mamia ya wananchi Wilayani humo, Waziri Lugola anatoa ya moyoni jinsi baadhi ya viongozi matrafiki mikoa kuyapuuza maagizo yake anayoyatoa.

Lugola anasema yeye anajua sheria ya usalama barabarani, na yupo Wizarani kwa lengo la kumsaidia Rais katika mapambano ya kuondoa umaskini na nchi kuwa na uchumi wa kati, hivyo sekta ya bodaboda ni muhimu katika mapambano ya kuondoa umaskini.

“Sijawahi kutamka katika mikutano yangu yote ya ndani au ya hadhara, kuwa bodaboda wasikamatwe, bali nasema bodaboda lazima wapewe mazingira mazuri ya kufanya kazi yao bila bugudha, na pia kuyakamata hovyo bodaboda na kuzilundika vituoni kwa makosa ambayo yanapaswa kutozwa faini hilo nimelikataza,” anasema Lugola.

Anasema wapo baadhi ya wakuu wa matrafiki mikoa wanayapuuza maagizo yake na mmojawapo ni RTO Mkoa wa Arusha ambaye anatumia mikutano anayoalikwa kunipinga na kuyaaita maagizo yangu ninayoyatoa kwa maunfaa ya nchi ni yakisiasa.

Lugola kutokana na kumfuatilia RTO huyo kwa muda mrefu, kupitia mkutano wa hadhara wa Mji wa Malinyi, alitamka hadhara kumuondoa madarakani Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani humo, Charles Bukombe na kumuagiza Katibu Mkuu, pia kumchukulia hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwa matrafiki hao wa mikoa nchini.

Lugola amesema RTO huyo ameshuhudia katika video ambayo ilikua inasambaa mitandaoni akiwa katika mkutano jijini Arusha, akipinga maagizo yake na kuyaita ya kisiasa na pia kutokuyatekeleza.

“Sitoi maagizo ya kisiasa bali anatoa maagizo yatakayomsaidia rais kazi zake kwa wananchi wanyonge wanaopambana na umaskini na ajira, kutokana na kutokuwa na nidhamu kwa RTO huyu namuagiza katibu Mkuu achukue hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kumuondoa u-RTO afanye shughuli zingine za kipolisi,” anasema Lugola.

Pia Lugola anatoa onyo kwa RTO wa Mikoa ya Morogoro na Mara, kujitathimini katika utendaji wao, na pia anawataka wakuu wa vikosi hao katika mikoa mbalimbali nchini kuyasimamia vema maagizo yake kwa kutowaonea wananchi, kuacha kuchukua rushwa barabarani.

Lugola anasema Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na haitaki kumnyanyasa mwananchi yeyote kupitia makosa ya trafiki wasiokuwa waaminifu.

Katika Mkutano huo, Lugola anaagiza kuwa, Jeshi katika vituo vya polisi nchini, bodaboda zinazotakiwa kuwepo vituoni ni zile zilizopo katika makundi matatu ambayo ni Bodaboda zilizohusika kwenye uhalifu, zilizotelekezwa au zilizookotwa na zilizohusika katika ajali.

“Ninasisitiza kwa mara nyingine, bodaboida hizo ndizo zinapaswa kuwepo vituoni, lakini kuziweka bodaboda ambazo hazipo katika makundi hayo, napiga marufuku na hii nataka Polisi nchi nzima munielewe,” anasema Lugola.

Katika kazi ya kuhakikisha madereva wa bodaboda na magari nchini wanafanya kazi zao kwa utulivu bila kunyanyaswa, Januari 2, 2019, akiwa mjini Bukoba, Mkoani Kagera, anatangaza kuwa, gari lolote litakalokamatwa na trafiki kwa kosa la bodi ya gari bovu, weipa haitoa maji, taa za breki haziwaki, mafuta yanavuja, hapo kosa ni moja tu, gari ni bovu na faini ni shilingi 30,000, na si sahihi kuwa kila tatizo la gari ni kosa linalojitegemea.

Huku wananchi wakimshangilia Waziri Lugola katika mkutano huo, aliendelea kusema kuwa, Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na haitaki kumnyanyasa mwananchi yeyote kupitia makosa ya trafiki wasiokuwa waaminifu.

“Kutokana na changamoto za barabarani, nawaagiza polisi wa usalama barabarani nchini, gari lolote litakalokamatwa kwa kosa la bodi ya gari bovu, weipa haitoa maji, taa za breki haziwaki, mafuta yanavuja, hapo kosa ni moja tu, gari ni bovu na faini ni shilingi 30,000, na si sahihi kuwa kila tatizo la gari ni kosa linalojitegemea,” anasema Lugola.

Akiwa Mkoani Arusha, mwezi Februari, 2019, katika Mkutano wake wa hadhara uliofanyika Jimbo la Arumeru, Waziri Lugola anapiga marufuku tabia ya baadhi ya askari Polisi hapa nchini kukamata pikipiki wakiwa hawana sare za Jeshi, anasema kwa kufanya hilo kunaleta kero kwa madereva na pia anayekamatwa anaweza akadhaniwa kuwa ni jambazi.

Lugola anaongeza hayo katika Mkutano huo wa hadhara uliofanyika uwanja wa Wilayani humo, akisisitiza kuwa, polisi wanapaswa kufuata utaratibu wa kijeshi hasa wanapokamata vyombo vya moto na siyo kuvunja utaratibu.

Lugola anafafanua kuwa, bodaboda zinazovunja sheria za usalama barabarani zinapaswa kukamatwa bila kuwaonea huruma, ila ni kosa Polisi kuwanyanyasa vijana hao ambao wanapata ridhiki kupitia biashara hiyo.

“Mnapaswa kukamata hizi bodaboda zinapofanya makosa, tabia ya kukurupuka huku mkitafuta fedha zisizo halali, huko ni kuwaonea waendesha bodaboda,” anasema Lugola.

Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda wa Wilaya ya Arumeru, jijini Arusha na Tanzania kwa ujumla wafuate sheria za usalama barabarani zikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha vyombo hivyo vya moto wanapaswa kuwasha taa.

WaziriI Lugola licha ya kuzungumza hayo katika mikutano yake ya hadhara, pia anazungumza maneno hayo katika Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa, Wilaya na pia Mikutano yake na askari na watumishi raia wa Wizara yake waliopo mikoani.

Pia Waziri Lugola, anatangaza dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi.

Waziri Lugola anaendelea na ziara ya aina hiyo nchi nzima, na anatarajia Agosti 10, 2019 kuanza ziara Mkoa wa Rukwa ambapo anatarajia kuzitembelea Wilaya zote za Mkoa huo kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi, na pia kutangaza kazi nzuri zinazofanywa na Rais John Magufuli nchini.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger