Tuesday, 4 June 2019

Makamba Aridhishwa Na Kasi Ya Uzalishaji Wa Mifuko Mbadala

Na Lulu Mussa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba amefanya ziara ya kikazi ya kukagua viwanda vinavyozalisha mifuko mbadala ikiwa ni siku ya nne tangu kuanza kwa utekelezaji wa Sheria ya Marufuku ya Mifuko ya Plastiki nchini.
 
Akiwa katika Kiwanda Cha African Paper Bag Ltd kilichopo katika eneo la Chango’mbe jijini Dar es Salaam Waziri Makamba amesema ameridhishwa na kasi ya kiwanda hicho ambacho kinazalisha mifuko ya karatasi laki tano kwa siku na mifuko ya ‘Non-Woven’ ipatayo laki moja kwa siku.
 
“Wajibu wa Serikali si kupiga marufuku na kuondoka, tunahakikisha tunaziba pengo la mifuko ya plastiki kwa kuweka mazingira wezeshi kwa uzalishaji wa mifuko mbadala yenye ubora na bei nzuri kwa watu. Lazima tuwasaidie wajasiriamali, wafanyabiashara na wenye viwanda kuzalisha mifuko ili kuziba pengo la mahitaji kwa kuwa na mifuko mbadala yenye ubora na viwango vinavyokidhi mahitaji” Makamba alisisitiza.
 
Amesema kuondoka kwa mifuko ya plastiki kumeibua fursa mpya za uchumi shirikishi, ajira mpya, mapato mapya na kusisitiza kuwa Shirika la Viwango Nchini (TBS) linaandaa viwango vipya vya ubora wa mifuko hiyo mbadala vitakavyobainisha malighafi na unene wa mifuko mbadala itakayozalishwa ili kuwalinda watumiaji ikiwa ni pamoja na taarifa zitakazoainisha mfuko husika una uwezo wa kubeba kilo ngapi.
 
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Kampuni ya African Paper Bag Ltd Bw. Hasnai Mawji amesema kuwa kwa sasa mahitaji ya mifuko kiwandani kwake ni makubwa sana na wameongeza uzalishaji kwa kuagiza mashine mpya mbili sambamba na kuongeza idadi ya watumishi kukidhi mahitaji kwa sasa.
 
“Kiwanda chetu kinazalisha mifuko tani 100 kwa mwezi na tumeagiza mashine nyingine ili kuongeza uzalishaji wa kufikia tani 200 kwa mwezi na sasa tunafanya kazi masaa 24, shifti zimeongezeka kutoka shifti 1 ya awali na sasa tuna shifti 3, tumeongeza ajira kutoka watu 30 awali na sasa tuna watumishi 60 na lengo ni kufika watumishi 100” Alilisitiza Bw. Mawji.
 
Katika hatua nyingine Waziri Makamba pia amepata fursa ya kutembelea Kiwanda cha Green Earth Paper Product Ltd kilichopo katika eneo la Mbezi Makonde chenye uwezo wa kuzalisha mifuko 22,000 kwa siku na kusisitiza kuwa katazo la mifuko ya Plastiki si kwa faida ya mazingira pekee bali pia ni muhimu katika kuinua uchumi na ustawi wa watanzania.
 
Aidha Mkurugenzi wa Kiwanda cha Green Earth Paper Product Bw. Robert Mosha amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya zuio kiwanda hicho kilipokea oda ya kiasi cha Shilingi Milioni 124 na katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya zuio la mifuko ya plastiki kiwanda hicho kimepokea mahitaji yenye thamani ya Shilingi 124 ikiwa ni kiwango cha juu ukilinganisha na mahitaji ya awali kwa kipindi kifupi.
 
Kuanzia tarehe 1 Juni Serikali imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya Plastiki nchini ikiwa ni pamoja na Utengenezaji, Uingizaji, Usambazaji, Usafirishaji na Matumizi ya Mifuko hiyo bila kujali unene wake.


Share:

Taarifa Kwa Umma Toka Jeshi La Polisi Makao Makuu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jeshi la Polisi Tanzania linapenda kuwashukuru wananchi wote kwa jinsi wanavyoendelea kutoa ushirikiano  kwa kutoa taarifa na ufadhili unaowezesha kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu nchini kwani uhalifu unaendelea kupungua na kuifanya nchi yetu  kuendelea kuwa shwari na salama.

Yapo  matukio mchache ambayo tunaomba ushirikiano zaidi kutoka kwa wananchi wote katika kupeana elimu ya kuyaepuka kuyatenda matukio kama vile mauaji yanayotokana  na vitendo vya wananchi kujikulia sheria mikononi, wivu wa mapenzi na  ulevi.   Pia matukio ya ubakaji na ajali zinazosababishwa na uzembe wa madereva. 

Jeshi la Polisi Tanzania lina amini kama kila mtu  kwa nafasi yake akishiriki katika kutoa elimu, kuonya na kufiwachua wanaotenda uhalifu huo, kuanzia ngazi ya familia matukio ya aina hiyo yatapungua kwa kiasi kikubwa.

Mtakumbuka pia tarehe 01/06/2019 serikali ilitoa maelekezo kuwa,  ndiyo mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini na utekelezaji ukaanza kwa ufanisi mkubwa.  Jeshi la Polisi linatoa wito agizo hilo liendelee kuzingatiwa na wenye mifuko ya aina hiyo waisalimishe kama ilivyoelekezwa na kama kuna mwenye taarifa za mtu mwenye kumiliki mifuko hiyo atoe taarifa Polisi au mamlaka zingine ili hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni ziweze kuchukuliwa.

Aidha,  kama mnavyofahamu tunaelekea kipindi cha sikukuu ya Eid El Fitri ambayo husheherekewa  duniani kote baada ya mfungo wa  Mwezi  Mtukufu wa Ramadhani.  Jeshi la Polisi linatoa wito kwa watanzania wote kuwa makini katika suala zima la ulinzi na usalama ili waweze kusheherekea kwa amani na utulivu sikukuu hiyo kubwa na muhimu.

Kila  mmoja ajiepushe na vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha  usalama wa maisha na mali zao kama vile kuacha nyumba bila waangalizi, ulevi wa kupindukia, kuruhusu vijana na watoto walio chini ya uangalizi wa wazazi kwenda katika nyumba za starehe au maeneo yanayoweza kuhatarisha usalama na utu wao. Kujiepusha kuendesha vyombo vya moto bila kufuata sheria za usalama  barabarani kama vile kuendesha chombo cha moto ukiwa umelewa , mwendo kasi, pamoja na kujaza abiria kupita kiasi.

Pamoja na kwamba,  Jeshi la Polisi katika Mikoa yote  limejipanga kikamilifu kuimarisha  ulinzi  katika maeneo yote ya ibada na  maeneo mengine ambayo yatakayokuwa na mikusanyiko  mikubwa  ya watu tunaelekeza kila mmoja  usalama uanzie kwake  na kwa wale wanaomiliki maeneo ya starehe wazingatie maelekezo ya kiusalama waliopewa na
Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi  na watakayoendelea kuwapa.  Pia tunatoa onyo kwa wale wanaodhani wanaweza kutumia sherehe hizi kufanya uhalifu watambue kuwa watashughulikiwa kwa nguvu zote kwa mujibu wa sheria za nchi.

Tunawaomba  wananchi wote pale watakapoona viashiria au kumtilia mtu mashaka kuwa huenda akawa  mhalifu watoe  taarifa kupitia  namba  za simu za bure  0787 668 306 au 111 au 112.
                   
Tunawatakia  Watanzania wote Sikukuu njema yenye amani na utulivu  ya Eid El  Fitri.
Imetolewa na:

……………………………..
DAVID A. MISIME - SACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi.


Share:

Waziri Biteko akutana na Kampuni ya uwekezaji ya Ngwena

Na Issa Mtuwa – Dodoma
Waziri wa Madini Doto Biteko amekutana na Mwekezaji wa Kampuni ya Ngwena Tanzania Ltd “Ngwena” na kufanya nao mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali, kubwa likiwa ni kutoa Ufafanuzi kuhusu Marekebisho ya Sheria ya Madini inavyotoa fursa na mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya madini hapa nchini.
 
 Hatua hiyo inafuatia ombi la kampuni hiyo kuomba kukutana na waziri Biteko ili kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kutoka kwake kuhusu mabadiliko hayo ya sheria.
 
Ombi la kutaka kuonana na waziri ni kutokana na kampuni ya Ngwena kupata taarifa za upotoshaji na zisizo sahihi kuhusu mabadiliko ya sheria ya madini yaliyofanywa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu taratibu mbalimbali za uwekezaji na shuguli nyingine zinazo husu sekta ya madini.
 
Upotoshaji unaofanywa kwa maksudi na baadhi ya watu ndani nan je ya nchi kwa lengo la kutaka kuifanya Tanzania kama sio mahali sahihi pa kuwekeza. 
 
Biteko ameuambia ujumbe wa kampuni ya Ngwena kuwa, mabadiliko ya sheria yamefanyika kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili mwekezaji na taifa kwa upande mwingine. 
 
Amefafanua kuwa, tangu mabadiliko hayo yapitishwe hakuna malalamiko ya kupingwa kwa marekebisho hayo kwakuwa yalizingatia maslahi mapana ya kila upande na kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki na ndio sababu mpaka sasa tangu marekebisho hayo yafanyike hakuna kampuni au muwekezaji alie acha wala kuonyesha nia ya kufunga shuguli zake kwa sababu ya marekebisho ya sheria.
 
Ameongeza kuwa, Tanzania inawahitaji sana wawekezaji na mara zote kila panapokuwa na jambo haliendi sawa mara moja hukaa na kujadili na mwekezaji na kutatua changamoto.
 
 Ameitaka kampuni ya Ngwena kwenda kuwa mabalozi ili kuwaeleza  wengine kuhusu ukweli ulivyo kuhusu marekebisho ya sheria yaliyofanywa na kuachana na upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu ambao hawana dhamana ya kuyazungumzia masuala hayo. 
 
Amewakaribisha watu na wawekezaji wote wanaotaka kupata ufafanuzi wa jambo lolote kutembelea ofisini kwake jijini Dodoma.
 
Aidha, kwa upande wa kampuni ya  Ngwena ukiongozwa na Meneja Mkuu H.E Kavishe amemshukuru Waziri kwa ufafanuzi mzuri alioutoa na kwamba walichokuwa wanakisikia na alichokisema waziri ni vitu tofauti na kuongeza kuwa, kuonana kwao kumewafungua masikio na kupata ukweli kutoka kwenye mtu sahihi na mwenye dhamana ya sekta ya madini.
 
Ameongeza kuwa, ni kweli upotoshaji waliokuwa wanaupata ungeweza hata kuwarudisha nyuma, hivyo watakwenda kufikisha ujumbe kwa wenzao.
 
Kikao hicho pia, kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Edwin Igenge, na Mkurugenzi wa Sera na Mipango  Wizara ya Madini, Augustine Ollal, Kamishna masaidizi anaeshuugulikia Migodi na Biashara Ali Ali na  Kamishna masaidizi anaeshugulikia Lesseni Maduh ….


Share:

Waziri Mkuu Kabidhiwa Kisima Cha Maji

*Wananchi washangilia, waishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma

CHANGAMOTO ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama iliyokuwa inawakabili wananchi wa vijiji vya Nandagala ‘B’ na Ingawali wilayani Ruangwa imekuwa historia baada ya Ubalozi wa Uturiki kupitia taasisi yake ya Diyanet kuwachimbia visima virefu.

Visima hivyo viwili vimekabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana (Jumatatu, Juni 3, 2019) na Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya jamii nchini, Muhammed Cicek. Hafla hiyo imefanyika katika kijiji cha Nandagala ‘B’.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania na Uturuki ni nchi rafiki na kwamba Serikali ya Uturuki imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Tanzania katika uboreshaji wa huduma za jamii zikiwemo za afya, elimu na maji.

Waziri Mkuu baada ya kuvipokea visima hivyo amewataka wananchi wa vijiji hivyo kupitia kamati zao za maji zihakikishe zinaisimamia vizuri miradi hiyo na pia wawe wanatoa taarifa za mapato na matumizi ya kila mwezi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Ruangwa, Samwel Pyuza ahakikishe huduma ya umeme inafikishwa katika mradi huo kwa ajili ya kusukuma maji badala ya kutumia jenereta.

Kwa upande wake, Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala za jamii nchini, Muhammed Cicek amesema Watanzania na Waturuki ni ndugu, hivyo amefurahi baada ya wananchi wa vijiji hivyo kupokea zawadi ya visima hivyo walivyowakabidhi.

Wakizungumza baada ya makabidhiano hayo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nandagala ‘B’ wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu na makazi yao.

Mmoja wa wakazi hao Safina Angulupele (63) amesema awali kabla ya kisima hicho walikuwa wanapata maji kutoka katika kijiji kingine na pia hayakuwa na uhakika, hivyo uwepo wa kisima kwenye kijiji chao ni mkombozi kwao.

Naye mkazi mwingine wa kijiji hicho Zainab Issa amesema huduma ya maji safi na salama ni muhimu kwa maendeleo ya jamii, hivyo anaipongeza Serikali kwa kuwafikishia huduma karibu na makazi. “Sasa hata sisi wazee tunaweza kwenda kisimani na kuchota maji.”

Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, imedhamiria kuwafikishia wananchi wote huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

WADUKUZI 'HACKERS' WATEKA TOVUTI ZA SERIKALI NA KUFUTA TAARIFA

Serikali ya Kenya imebaki imeduwaa baada ya ‘hackers’ kupenya kwenye tovuti zake kadhaa na kuchukua usukani.

 Hali ni mbaya hivi kwamba hata mtandao wa kulipia madeni ya serikali maarufu kama IFMIS ulikuwa pia umedukuliwa. 

Kulingana na gazeti la Standard, jumla ya tovuti 27 ya serikali ikiwemo ile ya Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), IFMIS na mingineyo ilikuwa imetwaliwa na wapenyezi hao kufikia Jumatatu Juni 3,2019. 

 Wale waliokuwa wakijaribu kuingia kwenye mtandao wa IFMIS walikuwa wanajikuta wameingia kwenye tovuti nyingine iliyojiita KURD Eletronic Team.

 Baada ya kundi hilo KURD kuteka tovuti hizo, liliweka logo zake huku likifuta habari za serikali.

 Licha ya kuwa ilikuwa vigumu kuingia kwenye IFMIS kufikia Jumatatu, Juni 3, baada ya shambulio hilo, wizara ya fedha ilisema kuwa mambo yalikuwa salama salmini. 

 “Mtambo wa IFMIS uko sawa. Hakujawa na shambulio lolote kwenye mtambo huu. Kile washambulizi walijaribu ni kuingia kwenye tovuti ya IFMIS, lakini tovuti na mtambo ziko tofauti,” Ujumbe ulisema. 

Tukio hilo ni changamoto kubwa kwa serikali ambayo hivi maajuzi imekuwa ikiokota /taarifa data za wananchi wote huku kukiwa na maswali chungu nzima wa iwapo habari hizo ziko salama.
Chanzo - TUKO
Share:

MAMA ALIYEJICHANA TUMBO KWA WEMBE KUTOA MTOTO AFUNGUKA

Na Petty Siyame- Habarileo
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kirando, Dk Gideon Msaki alisema iliwachukua zaidi ya saa sita kuokoa maisha ya Joyce kufuatia huduma ya dharura ya upasuaji waliyomfanyia ikiwa ni pamoja na kumuongezea uniti nne za damu.


"Naendelea vizuri....nampenda sana mtoto wangu,” anasema kwa taabu Joyce Kilinda (32) anayesadikiwa kurarua tumbo lake kwa ‘wembe’ na kumtoa mtoto wa kike akiwa hai, wakati alipoulizwa na mwandishi kuhusu hali yake juzi.

Mwanamke huyo amehamishiwa hospitali Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga kwa matibabu zaidi. Kuendelea kuimarika kwa hali ya mwanamke huyo kumetokana na juhudi kubwa za saa sita za kuokoa maisha yake zilizofanywa katika kituo cha afya Kirando baada ya kumpokea akiwa hajitambui na kupoteza kiasi kikubwa cha damu.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Boniface Kasululu, mzazi huyo alifikishwa katika Kituo cha Afya Kirando huku sehemu ya utumbo ukiwemo mfuko wa uzazi na kondo la nyuma vikiwa nje.

Aliongeza kuwa godoro alilobebewa mwanamke huyo kutoka nyumbani kwake hadi kituoni lilikuwa limelowa damu huku mwenyewe akiwa amezimia ambaye amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Rukwa mjini hapa na kupokewa Alhamisi saa tano usiku.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kirando, Dk Gideon Msaki zaidi ya saa sita kuokoa maisha ya Joyce kufuatia huduma ya dharura ya upasuaji waliyomfanyia ikiwa ni pamoja na kumuongezea uniti nne za damu kwa kuwa alikuwa amepoteza damu nyingi.

Joyce na mwanawe wamelazimika kusafirishwa umbali wa kilometa 160 kutoka Kituo cha Afya Kirando hadi Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Rukwa mjini hapa, huku hali yake na mwanawe vikielezwa kuimarika.

Dk Kasululu anakiri kuwa hadi sasa bado uchunguzi wa kitabibu haujabaini nini hasa kilichomsibu mwanamke huyo kujirarua tumbo lake na kumtoa mtoto akiwa hai. “Isitoshe swali jingine ambalo halijapatiwa majibu ni kwamba hajathibitishwa kama ni yeye mwenyewe aliyejirarua tumbo lake na kumtoa mtoto nje au kuna mtu mwingine aliyemfanyia hivyo,” alisisitiza.

Timu ya ufuatiliaji ya wataalamu wa afya ngazi ya mkoa na wilaya ikiongozwa na Dk Kasululu imejiridhisha kuwa huduma za dharura za upasuaji wa kuokoa maisha ya mwanamke huyo zimefanyika kwa mafanikio makubwa.

Kuonesha kuimarika kwa afya yake, Joyce ambaye amelazwa katika chumba maalumu cha uangalizi, mwandishi wa gazeti hili alipomtembelea aliweza kuinuka na kuketi kitandani kwa msaada wa muuguzi, Veronica Wambura.

Kituo cha Afya Kirando ambacho kiko umbali wa kilometa 160 kutoka Sumbawanga mjini ni miongoni mwa vituo vya afya tisa ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imevifanyia upanuzi na ukarabati kwa zaidi ya Sh bilioni 4 vikiwa na uwezo wa kukabiliana na huduma za upasuaji wa dharura.
Share:

Deni La Taifa Limeongezeka Kutoka Sh. Trilioni 49.86 Mwezi April,2018 Hadi Kufikia Sh.trilioni 51.03 Mwezi April ,mwaka 2019

NA Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mpango Dokta Philiph Mpango wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara  ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
 
Dokta Mpango amesema kati ya kiasi hicho,deni la ndani lilikuwa Sh.trilioni 13.25 na deni la nje ni Sh.Trilioni 37.78 ambapo ongezeko la deni la Serikali linatokana na kupokelewa kwa mikopo mipya  kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo  ikiwemo ujenzi wa jingo la tatu la kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere,Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa ,ujenzi wa miradi ya umeme ,ujenzi wa barabara na madaraja makubwa.
 
Aidha,Dokta Mpango amebainisha sambamba na ukopaji,Wizara imeendelea kufanya tathmini  ya deni la Taifa kila mwaka  ili kupima uhimilivu wake ambapo matokeo ya tathmini  iliyofanyika Mwezi Disemba ,2018 inaonesha kuwa deni la Taifa ni himilivu katika kipindi cha Muda mfupi ,wa kati na Mrefu.
 
Hivyo,thamani ya sasa ya deni la Taifa[Present Value of Total Public Debt]kwa pato la Taifa ni asilimia 27.2% ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70 na thamani ya sasa ya deni la nje kwa pato la taifa ni asilimia 22.2% ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55%  huku thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 157.3% ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 240% na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 15.2% ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 23%.
 
Hata hivyo,Dokta Mpango amesema ,serikali imeendelea kuhakikisha inalipa deni kwa wakati  kwa kadri linavyoiva ambapo katika mwaka 2018/2019 ,serikali ilitenga kiasi cha Sh.trilioni 1.41  kwa ajili ya kulipa riba ya deni la ndani na hadi kufikia  April,2019 Sh.trilioni  1.06 kimelipwa  sawa na asilimia 75.18% ya lengo.
 
Pia,Serikali ilitenga sh.bilioni 689.67 kwa ajili ya kulipa riba ya deni la nje  ambapo hadi kufikia April,2019  sh.bilioni 588.30 zimelipwa sawa na asilimia 85.30% ya lengo  ,vilevile ilitenga  Sh.Trilioni 1.66  kwa ajili ya kulipia mtaji  wa deni la nje ,ambapo hadi kufikia ,April,2019  sh.Trilioni 1.23  zimelipwa sawa na asilimia 74.10 ya lengo na Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kusimamia deni la Serikali  kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo ,dhamana  na Misaada  SURA 134 Pamoja na mkakati wa muda wa kati  wa kusimamia madeni.


Share:

WANAOSAFIRI NJE YA NCHI KUBADILI HATI ZA KUSAFIRIA KABLA YA JULAI 2019

Idara ya Uhamiaji Tanzania imewataka Watanzania wanaotaka kusafiri nje ya nchi hivi karibuni kubadilisha hati zao za kusafiria kabla ya Julai 2019.
Hatua hiyo itasaidia kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza wa kuzuiwa kusafiri kwenye viwanja vya ndege na vituo vya mipakani wakati wa kutoka nje ya nchi.
Taarifa iliyotolewa jana Juni 3, 2019 na kusainiwa na Msemaji wa Idara hiyo, Ally Mtanda imeeleza ni hitaji la kisheria kwa hati za kusafiria kuwa na uhai wa angalau miezi sita ili mwenye hati hiyo aweze kuomba visa ya kwenda nchi nyingine.
Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa kuhamia katika matumizi ya hati za kusafiria za kielektroniki zilizozinduliwa Februari 1 mwaka 2018 na Rais John Magufuli.
Mtanda ameeleza hati za zamani zitasitishwa matumizi yake Januari 31 mwaka 2020 hivyo ni muhimu kwa wahitaji wa hati mpya kuzipata kabla ya muda huo.
Kuhusu namna ya kupata hati mpya amesema idara hiyo imeshakamilisha ujenzi wa miundombinu katika mikoa 29, ofisi ya uhamiaji makao makuu, ofisi za uhamiaji Zanzibar na ofisi za balozi za Tanzania katika nchi 23.
Na Elizabeth Edward, Mwananchi
Share:

Waziri Hasunga Aiagiza Coasco Kukagua Vyama Vote Vya Ushirika

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Uongozi wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limetakiwa kukagua vyama vote vya Ushirika na kuwasilisha taarifa ya ukaguzi huo ofisi ya Waziri wa Kilimo kwa ajili ya hatua stahiki.

Mhe Japhet Hasunga (Mb), Waziri wa Kilimo ametoa agizo hilo jana tarehe 3 Juni 2019 wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa COASCO makao makuu sambamba na wakaguzi wa mikoa kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ofisi za COASCO makao makuu Jijini Dodoma.

Alisema kuwa lengo kuu la COASCO ni kuhakikisha kuwa vyama vya ushirika vinakidhi matakwa ya kisheria na misingi ya kuanzishwa kwake ili wanaushirika na vyombo vyao vinakuwa salama kulingana na makubaliano, katiba na sheria zilizopo vile vile kusimamia sheria za ushirika na sheria za biashara wanazofanya ikiwa ni pamoja na sheria na sera za nchi na utawala bora.

“Nakuagiza Kaimu Mtendaji Mkuu kuhakikisha kuwa unakagua vyama vyote vya ushirika, mimi nisingependa nikikuomba ripoti ya ukaguzi uniambie eti kuna vyama vingine hujakagua na taarifa ya ukaguzi iwasilishwe katika ofisi yangu” Alisisitiza Mhe Hasunga

Aliongeza kuwa huduma za ukaguzi zinazotolewa na Shirika zinasaidia kuimarisha utawala bora katika vyama vya ushirika, kuwajengea imani wanachama wa vyama vya ushirika juu ya shughuli zinazofanywa na vyama vyao na hivyo kuongeza uzalishaji na kuboresha huduma zinazotolewa na vyama vya Ushirika.

Mhe Hasunga pia alimuagiza kaimu Mtendaji mkuu huyo kuhakikisha kuwa anapeleka mapendekezo ya viongozi waliopo katika vyeo vyao ili kuweza kuthibitishwa kwa wale wanaostahili.

Kwa kutambua mchango wa ushirika katika mageuzi ya kiuchumi hasa kwa wakati huu ambao serikali ya awamu ya tano inakusudia kuingia katika uchumi wa kati (kupitia agenda ya Tanzania ya Viwanda), Hivyo ili kufanikisha agenda hiyo wametakiwa kutafuta vyanzo vipya vya mapato.

Aliongeza kuwa Vyama vya ushirika vina nafasi kubwa kuinua uchumi ikiwa tu usimamizi wa sheria na kanuni utaimarishwa kama inavyojidhihirisha katika serikali ya awamu ya tano.

Alibainisha pia kuwa, udhaifu katika usimamizi wa mifumo ya ufatiliaji ni moja ya changamoto zilizosababisha vyama vingi vya ushirika kutumbukia katika matatizo na kupelekea vyama vingi kufilisika.

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) ni Shirika la Umma lililoanzishwa kwa Sheria Na. 15 ya mwaka 1982 kwa lengo la kutoa huduma za ukaguzi na Usimamizi kwa Vyama vya Ushirika Tanzania.

Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2005 ili kupanua wigo wa huduma za Shirika za Ukaguzi na Ushauri kutolewa kwa vyama vya ushirika pamoja na taasisi za Umma, makampuni binafsi, mabenki na wateja wengine.

MWISHO



Share:

Makonda awajaza Mamilioni ya Pesa Wachezaji Simba, Samatta apewa mtaa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametimiza ahadi yake ya kuwazawadia wachezaji wa Simba waliotwaa tuzo za mwaka za klabu hiyo zilizopewa jina la ‘Mo Simba Awards’ zilizofanyika wiki iliyopita Hyatt Regency, Dar es Salaam.

Sambamba na wachezaji hao, wakiongozwa na kipa Aishi Manula, pia Makonda alimpa zawadi ya kipekee  nyota wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta kwa kuupa mtaa jina la mshambuliaji huyo.

Wachezaji wa Simba waliokabidhiwa zawadi hizo za fedha taslimu Dar es Salaam jana ni Manula aliyeondoka na sh milioni 10 kama kipa bora aliyeng’ara msimu huu, huku wengine wakiwa ni Meddie Kagere (mfungaji na mchezaji bora) na Erasto Nyoni (beki bora).

Wengine ni Clatous Chama (bao bora), James Kotei (kiungo bora), John Bocco (mshambuliaji bora), Rashid Juma (chipukizi bora) ambao kila mmoja alipata sh milioni moja.

Pia, Makonda alimzawadia sh milioni mbili mchezaji bora wa timu ya wanawake ya Simba, Simba Queens, Mwanahamisi Omari ‘Gaucho’, huku pia akimpa sh milioni tatu Msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara kwa kuthamini mchango wake katika uhamasishaji.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Makonda alisema: “Nimetaka kukamilisha ahadi nilioahidi siku ya Tuzo Mei 30 zilizoandaliwa na kupewa jina la MO Simba Awards 2019 ambazo hutolewa kwa wachezaji wa Simba Sport Club kila mwaka.

“Kubwa ni kutambua mchango na kujituma kwa mchezaji wa Simba aliyechaguliwa na wachezaji wenzake ni Erasto Nyoni aliyeshinda tuzo mbili na beki bora, wakati Meddie Kagere akiibuka mchezaji bora na mfungaji bora, pia namsifu Kagere kwa kuwaaminisha watu na staili yake ya kufumba jicho moja,” alisema Makonda.

Aidha, Makonda Alitumia nafasi hiyo kumpa Samatta zawadi ya mtaa kwa heshima aliyoipa Tanzania huko Ulaya, akiibuka mfungaji bora wa Genk, lakini pia kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ubelgiji.


Share:

Taarifa Kuhusu Uthibitishaji Wa Nyaraka

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuufahamisha Umma kwamba, kuanzia tarehe 20 Mei, 2019 malipo yoyote Kwa Wizara yanafanyika kwa njia ya Kielektroniki kupitia mfumo wa GOVERNMENT ELECTRONIC PAYMENT GATEWAY (GePG).

Hivyo, wateja wote watakao hitaji kufanya malipo ya uthibitisho wa nyaraka mbalimbali zikiwemo; vyeti vya talaka, ndoa, kuzaliwa, Kifo n.k wanapaswa kabla ya kufanya malipo yoyote kuwasiliana na ofisi za Wizara kupitia vituo vyake vilivyopo Dodoma, Dar es salaam na Zanzibar ili kupatiwa ‘Control Number’ ili kufanikisha malipo husika kupitia Akaunti ya Benki ya CRDB.

Wateja wanaoleta nyaraka hizo kwa uthibitisho, wanaendelea kukumbushwa pia kukamilisha hatua muhimu kabla ya kupatiwa ‘Control Number’ ikiwemo kupelekwa kwanza katika Mamlaka na Taasisi husika zilizotoa vyeti/nyaraka hizo ili vihakikiwe na kuthibitishwa.

UMMA WOTE UNAOMBWA KUZINGATIA RAI KWAMBA, MALIPO YOYOTE YATAKAYOFANYIKA KINYUME NA MAELEKEZO BAADA YA TANGAZO HILI, HAYATOPOKELEWA

Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,


Share:

MKURUGENZI RASILIMALI ZA MAJI WIZARA YA MAJI ARIDHISHWA NA JUHUDI ZINAZOFANYWA NA TANGA UWASA PAMOJA NA MRADI WA SLM

Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji George Mvomera katikati akitazama kikundi cha utunzaji wa mazingira cha Uwamakizi wakati ametembelea vikundi vya Uwamakizi na kuona namna wanavyotunza vyanzo vya maji katika eneo dogo la Bonde la Mto Zigi wilayani Muheza huku akiridhishwa na juhudu zilizofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafiri wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga UWASA) pamoja na mradi wa kunusuru vyanzo vya maji (SLM) kushoto ni Mkurugenzi wa Mazingira Wizara Maji Obadia Kibona. 
Mratibu wa mradi wa kunusuru vyanzo vya maji kupitia matumizi bora ya ardhi (SLM) Mhandisi Maximilian Sereka ambapo alisema mradi huo ulianza mwaka 2016 sasa wapo ndani ya mwaka wa nne kwenye utekelezaji wa mradi huo. 
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji George Mvomera kulia akiangalia miti aina ya mitiki iliyopandwa kwenye Kijiji cha Sembekeza wilayani Muheza wakati alipotembela vikundi vya uwamakizi na kuona namna wanavyotunza vyanzo vya maji katika eneo dogo la Bonde la Mto Zigi wilayani Muheza huku akiridhishwa na juhudu zilizofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafiri wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) pamoja na mradi wa kunusuru vyanzo vya maji (SLM).
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji George Mvomera katikati akionyeshwa namna miti ya mitiki inavyopandwa wakati alipotembela vikundi vya uwamakizi na kuona namna wanavyotunza vyanzo vya maji katika eneo dogo la Bonde la Mto Zigi wilayani Muheza huku akiridhishwa na juhudu zilizofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafiri wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) pamoja na mradi wa kunusuru vyanzo vya maji (SLM).
Mtaalamu wa Mazingiwa Tanga Uwasa Ramadhani Nyambuka kushoto akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji George Mvomera
Mhandisi Rashid kutoka Tanga Uwasa kushoto akiwaongoza wataalamu mbalimbali
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji George Mvomera akitazama namna miche ya matikiti inavyopandwa
Wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kufika kwenye ofisi za Umoja wa Wakulima Wahifadhi wa Mazingira Kihuhwi Zigi 
Kikundi cha Uwamakizi kikitoa burudani
Sehemu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali wakifuatilia matukio mbalimbali
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji George Mvomera kwenye shuti nyeusi katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na kikundi cha Uwamakizi
**
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji George Mvomera ametembelea vikundi vya uwamakizi na kuona namna wanavyotunza vyanzo vya maji katika eneo dogo la Bonde la Mto Zigi wilayani Muheza huku akiridhishwa na juhudu zilizofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafiri wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) pamoja na mradi wa kunusuru vyanzo vya maji (SLM). 

Mradi huo unasimamiwa na Wizara ya Maji chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambao umeweza kusaidia utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwemo upandaji wa miti kwenye maeneo husika na hivyo kufanya maeneo hayo maji kutiririka mwaka mzima. 

Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo ikiwa ni wiki ya mazingira, Mvomera alioneshwa kuridhishwa na utunzaji wa mazingira unaofanywa na Uwamakizi huku akiwataka wananchi kote nchi kujiunga kwenye vikundi vinavyojihusisha na namna ya kutunza mazingira kwenye vyanzo vya maji ikiwemo kupanda miti rafiki inayotunza maji katika kipindi cha kiangazi. 

Alisema wameona kazi kubwa na nzuri inayofanyika kwenye eneo hilo kwani miaka ya nyuma mito hiyo ilikuwa haititirishi maji lakini sasa hivi kutokana na uwepo wa utunzaji wa mazingira maji yameanza kurudi kwenye hali yake ya kawaida na hilo ndio lengo lao nchi nzima wananchi wajiunge kwenye vikundi na kujihusisha na namna ya kutunza mazingira leo. 

“Lakini katika kusheherekea wiki ya mazingira lengo la mwaka huu ni kuhamasisha wananchi kmuacha kutumia mifuko ya plastic lakini pia tumejifunza mengi zaidi miti inayopandwa lazima iweze rafiki kwenye utunzani wa vyanzo vya maji kwani inachangia uwepo wa maji kwenye mito kipindi cha kiangazi”Alisema. 

Mkurugenzi huyo alisema miti hiyo inasaidia kufanya mito kutiririsha maji mwaka mzima kwenye maeneo ya vyanzo hizyo huku akikipongeza kikundi cha Uwamakizi kwa kuhifadhi mazingira na Mto Zigi na mito mingine midogo inayoingiza maji kwenye mto huo. 

Aidha alisema pia wanategemea kuanzisha mfuko wa maji (Water Fund) kwenye eneo la Uwamakizi kwa kushirikiana na Tanga Uwasa na wadau wengine kuunda mfuko huo ili mradi huo uwe endelevu uhifadhi wa mazingira uendelea kwenye maeneo mengi zaidi ya bonde dogo la mto Zigi ambayo ni sehemu ya bonde la Mto Pangani. 

“Niwapongeza uwamakizi kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini nitoe wito maeneo mengine Tanzania waende kujifunza uwamakizi namna ya kutunza vyan zo vya maji namna inavyoileta faida kwa wananchi wanalima kokoa mitiki inayowezesha kujiongeza kipato na kutunza maji kwa kupanda mazao mbadala ya mahindi na maharage ambayo yangewezea kuharibu vyanzo hivyo”Alisema. 

Hata hivyo alisema Wizara ya Maji imekuwa ikisaidia maeneo mengi kuanzisha vyama vya watumiaji wa maji kwa nguvu ya wizara maeneo mengine wa usafiri na ofisi faida za jumuiya za watumiaji maji zinasaidia kutatua changamoto za utunzaji wa maji na mazingiea eneo la uwamakizi watafanya kila njia kuwatafutua usafiri wa pikipiki kwa sababu ni eneo kubwa kupitia mradi wa kunusuru. 

Naye kwa upande wake Mratibu wa mradi wa kunusuru vyanzo vya maji kupitia matumizi bora ya ardhi (SLM) Mhandisi Maximilian Sereka alisema mradi huo ulianza mwaka 2016 sasa wapo ndani ya mwaka wanne kwenye utekelezaji wa mradi huo. 

Alisema mradi huo unatekelezwa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na shirika la Maendeleo Dunia (UNDP) pamoja na Mfuko wa Mazingira (GF) kwa kipindi cha miaka minne ya utekelezaji kwa kushirikiana na sekta mbalimbali wamepata mafanikio mengi ikiwemo utoaji wa elimu kwenye maeneo yote mawili Ruvu na Zigi hivyo kuwafanya wananchi kuwa na uelewa mkubwa ukilinganisha na kipindi wanaanza mradi. 

Mratibu huyo alisema pia kumekuwepo na ushirikianao kwenye sekta mbalimbali wakati wa utekelezaji wa mradi huo ambao unaratibiwa na sekta ya maji kwa kushirikiana ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Wizara ya Kilimo,Mifugo, 


“Lakini pia sekta za serikali mbalimbali ikiwemo mamlaka za maji ya Tanga Uwasa,Moruwasa na Dawasa lakini pia wilaya mbalimbali wanazoshirikiana nazo kwa ukaribu zaidi wilaya za Tanga na Morogoro”Alisema
Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya June 4




Share:

Monday, 3 June 2019

Mlinzi Ahukumiwa Kunyongwa Hadi Kufa Kesi ya Mwanafunzi wa Shule ya Scolastica

Mahakama Kuu ya Tanzania imemhukumu kunyongwa hadi kufa aliyekuwa mlinzi wa shule ya Scolastica mkoani Kilimanjaro, Hamis Chacha kwa kosa la kumuua aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Humprey Makundi.

Pia, Mahakama hiyo imemuhukumu mmiliki wa shule hiyo, Edward  Shayo na aliyekuwa mwalimu wa nidhamu, Labani Nabiswa kifungo cha miaka minne jela kila mmoja wa kosa la kuficha ukweli wa  mauaji ya mwanafunzi huyo.

Hukumu hiyo imetoelewa leo Jumatatu Juni 3, 2019 na Jaji Firmin Matogolo baada ya kumtia hatiani Chacha kwa kumuua kwa makusudi mwanafunzi huyo wa kidato cha pili, Makundi.

Mwanafunzi huyo aliuawa Novemba 6,2017 na baadaye mwili wake kutupwa mto Ghona, mita takribani 300 kutoka shuleni na baadae kuzikwa na Manispaa kabla ya kufukuliwa kwa amri ya mahakama.


Share:

Taarifa Ya Kusitishwa Kwa Matumizi Ya Pasipoti Za Zamani Zinazosomeka Kwa Mashine (MRP) Ifikapo Tarehe 31 Januari 2020

Kufuatia kuzinduliwa na kuanza kutumika  kwa Pasipoti Mpya za Kielektoniki  (e Passport), Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji inapenda kuufahamisha umma kuwa, tayari imekamilisha  ujenzi wa miundo mbinu ya utoaji wa huduma ya pasipoti hizo katika Mikoa ishirini na tisa (29), Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu, Afisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar na Ofisi za balozi za Tanzania  Ishirini  na tatu (23) zilizopo nje ya Nchi;

ambazo ni Uingereza (London), Ufaransa (Paris), Marekani (Washington DC na  New York), Canada (Ottawa), Israel (Telaviv), Saudi Arabia (Jeddah na Riyadh), Comoro (Moron), Kenya (Nairobi na  Mombasa), Ujerumani (Berlin), Algeria (Algiers), Italia (Rome), Nigeria (Abuja), Misri (Cairo), Uholanzi (The Hague), Ubelgiji (Brussels), Zambia (Lusaka), India (New Delhi), Malawi (Lilongwe), China (Beijing), Malaysia (Kuala Lumpur).

Nchi ambazo zitafunguwa Mfumo huo hivi karibuni ni Afrika Kusini, Msumbiji na Zimbabwe. Aidha, kwa Balozi zilizosalia, kazi ya ufungaji mitambo ya huduma hiyo inaendelea na itakamilika hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu.

Kwa Msingi huo, Idara ya Uhamiaji inawakumbusha  Watanzania wote Ndani na Nje ya Nchi kuwa matumizi ya Pasipoti za zamani yatasitishwa ifikapo tarehe 31 Januari, 2020.

Aidha, idara inawasisitiza wale wote wenye Pasipoti za zamani (MRP) na wanaokusudia kusafiri nje ya Nchi hivi karibuni, kuhakikisha wanabadilisha Pasipoti zao mapema kabla ya mwezi Julai mwaka huu ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wa kurejeshwa katika Viwanja vya Ndege na Vituo vya Mipakani wakati wa kutoka Nchini. Ni hitajio la Kisheria kwa Pasipoti kuwa na angalau uhai wa kuanzia miezi sita ili mwenye pasipoti hiyo aweze kuomba Visa ya Nchi anayokwenda na kuruhusiwa kuondoka Nchini kupitia Vituo vya kuingia na kutoka nchini.

Imetolewa na
Ally M. Mtanda (SI)
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji
Makao Makuu, Dar es Salaam


Share:

Rais Magufuli awapongeza Watanzania kwa kuitikia wito wa kuachana na mifuko ya plastiki......Afanya ziara ya kushtukiza Feri Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza Watanzania kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuacha kutumia mifuko ya plastiki ambayo ina madhara makubwa katika mazingira na viumbe hai wakiwemo binadamu.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo June 3,2019 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la samaki la Feri Jijini DSM baada ya kufanya ziara ya kushtukiza sokoni hapo na kujionea wafanyabiashara na wanunuzi wa samaki wakitumia mifuko mbadala.

Rais Magufuli amempongeza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wote ambao wamesimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa tangu mwaka 2016 kuhusu kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara kutotumia mwanya huo kuuza mifuko na vifungashio  mbadala kwa bei kubwa na badala yake amewataka wafanyabiashara hao pamoja na wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vya kutengeneza mifuko na vifungashio kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini.

Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuwa na vifaa vya kubebea bidhaa wanazozinunua madukani na masokoni ili kuepuka gharama kununua vifungashio ama mifuko mbadala.

Rais Magufuli ameziagiza mamlaka zinazohusika, kuhamasisha utengenezaji wa mifuko na vifungashio mbadala hapahapa nchini ili kuongeza ajira katika viwanda vya kutengenezea bidhaa hizo badala ya kuacha wafanyabiashara wakigeuza nchi kuwa mahali pakuingiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

Akiwa katika soko hilo la Feri, Rais Magufuli amenunua samaki kutoka kwa wafanyabiashara wadogo wanaotumia vitambulisho vya wajasiriamali na amewapongeza kwa juhudi zao za kujitafutia kipato halali.

Ameiagiza Manispaa ya Ilala kupunguza tozo ya pango kwa wapaa samaki kutoka shilingi 1,000 hadi shilingi 500 kwa siku na ameitaka manispaa hiyo kutenga shilingi Milioni 10 kutoka kwenye makusanyo ya soko hilo kujenga jengo jingine la wafanyabiashara wasiouza samaki kama vile Mama Lishe, Baba Lishe na wauza bidhaa zingine ambao hawanufaiki na jengo la wauza samaki ambalo mwaka jana alichangia shilingi Milioni 20.

Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la wauza samaki ambalo alilichangia shilingi Milioni 20 mwaka jana ambapo ameagiza Manispaa ya Ilala ifanye ukaguzi wa gharama zilizotumika kutokana na kuwepo wasiwasi wa matumizi mabaya ya fedha.

Ameiagiza Manispaa ya Ilala na Menejimenti ya soko la Feri kuweka utaratibu wa kuwapokea wafanyabiashara wanaoingiza samaki sokoni hapo kwa muda wote wa saa 24, kuweka umeme na maji katika jengo mojawapo la wafanyabiashara wa samaki ndani ya siku 5 na kuingiza umeme katika jengo la huduma ya Msalaba Mwekundu (Red Cross) lililopo sokoni hapo.

Huku wakimshangilia Wafanyabiashara wa soko la Feri wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa jinsi anavyowapigania Watanzania wanyonge wakiwemo wafanyabiashara wadogo na wamemhakikishia kuwa watatekeleza maagizo yake ya kutotumia mifuko ya plastiki kama inavyoelekezwa katika sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.



Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger