Wednesday, 3 April 2019

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA UNESCO KUHAKIKISHA USALAMA WA WAANDISHI WA HABARI


Msimamizi wa Usalama wa Waandishi wa Habari wa Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Patrick Kipangula akitoa neno la ufunguzi wakati wa kongamano la uandazi wa taarifa ya serikali kuhusu usalama wa waandishi wa habari lililofanyika mwishoni mwa juma katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Unesco jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Tirso Dos Santos akizungumza wakati wa kongamano la uandazi wa taarifa ya serikali kuhusu usalama wa waandishi wa habari lililofanyika mwishoni mwa juma katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Unesco jijini Dar es Salaam.
Ofisa programu wa Unesco kitengo cha Habari na Mawasiliano, Nancy Kaizilege akifafanua jambo wakati wa kongamano la uandazi wa taarifa ya serikali kuhusu usalama wa waandishi wa habari lililofanyika mwishoni mwa juma katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Unesco jijini Dar es Salaam.
Wadau wa tasnia ya habari wakitoa maoni wakati wa kongamano la uandazi wa taarifa ya serikali kuhusu usalama wa waandishi wa habari lililofanyika mwishoni mwa juma katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Unesco jijini Dar es Salaam.
Ofisa programu wa Unesco kitengo cha Habari na Mawasiliano, Nancy Kaizilege akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na wadau wakati wa kongamano la uandazi wa taarifa ya serikali kuhusu usalama wa waandishi wa habari lililofanyika mwishoni mwa juma katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Unesco jijini Dar es Salaam.
Wadau wa tasnia ya habari walioshiriki kongamano la uandazi wa taarifa ya serikali kuhusu usalama wa waandishi wa habari lililofanyika mwishoni mwa juma katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Unesco jijini Dar es Salaam. 
Wadau wa tasnia ya habari wakiendelea kujadiliana wakati wa kongamano la uandazi wa taarifa ya serikali kuhusu usalama wa waandishi wa habari lililofanyika mwishoni mwa juma katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Unesco jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Tirso Dos Santos akifafanua jambo wakati wa kongamano la uandazi wa taarifa ya serikali kuhusu usalama wa waandishi wa habari lililofanyika mwishoni mwa juma katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Unesco jijini Dar es Salaam.

***
SERIKALI imesema kwamba iko tayari kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na wadau wengine kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari wakati wakitekeleza kazi zao.

Kauli hiyo imetolewa Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo wakati wa kongamano la uandazi wa taarifa ya serikali kuhusu usalama wa waandishi wa habari.

Akizungumza kwa niaba ya wizara Msimamizi wa Usalama wa Waandishi wa Habari, Patrick Kipangula alisema kwamba serikali imeweka mazingira sawa ya kumlinda mwandishi wa habari ili kuiwezesha nchi na wananchi kuwa na taarifa za uhakika zinazogusa maisha na maendeleo yao.

Alisema kwamba katika kongamano hilo ni vyema washiriki wake wote wakatazama rasimu hiyo ambayo itakuja kuwasilishwa katika kikao kikubwa cha kitaifa kuzungumzia usalama wa waandishi.

Akizungumzia masuala ya sasa ambapo kukitokea tatizo kuhusu waandishi kunakuwa na malalamiko mengi, alisema kwamba ni vyema ikatambulika kwamba sehemu nyingi duniani na hapa nchini matatizo mengi dhidi ya waandishi wa habari hayasababishwi na serikali bali na watu binafsi.

Alisema waandishi wanapaswa kuelewa sheria wanazofanyia kazi ili kujua haki zao na pia kujua misingi ya usalama wao.

Alisema ni matumaini yake kwamba taarifa hiyo inayopikwa itasaidia kutambua mazingira ya waandishi hapa nchini na kuwezesha kuwa na usalama zaidi kama Umoja wa Mataifa unavyotaka katika kuzingatia vipengele vyake vya maendeleo endelevu hasa kipengele cha 16 na 10 hasa kifungu cha kwanza na cha pili kinachogusa usalama waandishi wa habari na wafanyakazi wa habari.

Alisema kwa sasa serikali imepania kuhakikisha kwamba waandishi wa habari wanakuwa salama na kwamba uhuru wa habari hautishiwi kwa kuwanyima uhuru waandishi wa habari.

Alisema sheria ya vyombo vya habari imetengenezwa kumlinda mwandishi wa habari hasa kwa kuzingatia kwamba waandishi pia wanatakiwa kupelekwa mafunzo na kuwekewa bima.

Katika mkutano huo ambao wawakilishi wa UNESCO walikuwepo, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Tirso Dos Santos aliwataka washiriki kuchangia ripoti hiyo ili iweze kuwa msingi wa usalama kwa waandishi wa habari.

Alisema taarifa hiyo ambayo pia imetengenezwa kwa taarifa kutoka katika mashirika ya kiraia ni muhimu sana katika utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia.

Alisema amefurahishwa sana na juhudi za serikali za kuandika taarifa hiyo, huku akisema mchango wa wadau ni muhimu ili kuwa na ripoti iliyokamilika.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali kuandaa ripoti kwa kusaidiwa na UNESCO kuhusu usalama wa waandishi wa habari ingawa mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakifanya.

Ripoti hiyo ya serikali inatarajiwa kuwasilishwa kwa mamlaka za juu na kujadiliwa Juni mwaka huu, huku taarifa hiyo ikitakiwa kukamilika Mei.

Naye Ofisa programu wa Unesco kitengo cha Habari na Mawasiliano, Nancy Kaizilege alisema katika mkutano huo kwamba ripoti hiyo ni mchanganyiko wa ripoti mbalimbali ikiwamo maswali yaliyoulizwa kwa kupitia mitandao.

Alisema kwamba taarifa hiyo inatarajiwa kufikishwa Wizara ya Fedha kabla ya kwenda kwenye mkutano mkubwa wa wadau.

Alisema kimataifa shauri hilo litakuwa wazi Julai mwaka huu wakati kwa Afrika itakuwa ni juni nchini Morocco.

Katika mkutano huo uliofanyika katika ofisi za UNESCO, wadau walikuwa wanaangalia rasimu ya serikali na usahihi wake kabla ya kwenda kwenye majadiliano katika jukwaa kubwa la kisiasa baadae mwaka huu.

Kwa mujibu wa vipengele vya SDG mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa wanatakiwa kutoa taarifa za hiari kuhusu usalama wa waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari.

Share:

CAG AJIBU UAMUZI WA BUNGE ..."NI JAMBO ZITO SANA...HUENDA LIKAJA TATIZO KUBWA ZAIDI"


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad amesema suala la Bunge kufikia uamuzi wa kutofanya naye kazi ni jambo zito ambalo linahitaji tathimini na kutazama athari zake.

Amesema kuwa maamuzi yakifanyika bila kuangalia athari zake yanaweza kuleta tatizo kubwa siku za baadaye.

Profesa Assad amesema hayo leo Jumatano Aprili 03, 2019 wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa njia ya simu.

“Nafikiri ni jambo zito sana hilo na kama nilivyosema tunahitaji tathimini kali kutazama athari zake ni zipi,” amesema na kuongeza “tukifanya maamuzi ambayo hatujatazama athari zake linaweza kuwa tatizo kubwa zaidi badala ya kupata solution,”

“Mi nafikiri tukae chini tutazame, halafu tuone athari ni zipi ili kuepuka matatizo ambayo tunaweza kuyasababisha… wasiwasi wangu ni kwamba huenda linaweza likaja kuwa tatizo kubwa zaidi kuliko linavyoonekana sasa hivi.”

Profesa Assad ametoa rai kuwa hansadi ya maswali na majibu kutoka katika mahojiano yake pamoja na Kamati ya Bunge ya Maadili iwekwe wazi ili kila Mtanzania ajue nini kilichozungumzwa baada ya kuitwa na kamati hiyo.

“Rai yangu ni kwamba ile hansadi ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iwekwe wazi kwa kila mtu ili kila mtu ajue nimeulizwa kitu gani na nimejibu kitu gani,” amesema nakuongeza “ili kila Mtanzania aweze kuweka tathimini yake, halafu aweze kupima kuwa hili lilipofikiwa ni sawa au sio sawa.”
Na Emmanuel Mtengwa, Mwananchi
Share:

TIBA MPYA YA SARATANI YA MATITI YAANZISHWA NCHINI


Mfano wa mwanamke akipima saratani ya matiti.

Wanawake wanaougua saratani ya matiti sasa wamepata ahueni baada ya njia mpya ya tiba ya ugonjwa huo kufanyika pasipo kukata kiungo hicho, baada ya serikali kununua mashine ya tiba za saratani za mionzi inayotumia teknolojia ya kisasa yaani ‘3D’ aina ya Linear Accelerators (LINAC).

Akizungumza na katika hospitali ya Mloganzila leo Aprili 2, 2019 Daktari bingwa wa upasuaji wa matiti kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili , Gasper Haule amesema wanatarajia kufanya upasuaji kwa wagonjwa wanne wanaougua saratani hiyo mapema wiki hii. 

“Tiba hii inafanywa kwa wale ambao wamegundulika kuwa saratani ipo katika hatua ya kwanza na ya pili, tutawafanyia upasuaji, tutatoa vivimbe na kisha watapewa tiba ya mionzi kwa kutumia mashine za kisasa zilizopo Ocean Road,” amesema Dkt. Haule. 

Awali matibabu ya saratani ya matiti yalitolewa nchini kwa njia ya kuondoa kabisa titi katika hatua yoyote ya ugonjwa.
Share:

LIVE: Rais Magufuli Akiendelea na ziara ya kikazi Mtwara

LIVE: Rais Magufuli Akiendelea na ziara ya kikazi Mtwara


Share:

Pierre Liquid atua Bungeni Dodoma

Peter Mollel maarufu Pierre Konki Liquid leo Jumatano April 3, 2019  yuko ndani ya ukumbi wa Bunge tayari kwa kushuhudia wabunge wakiendelea na kikao cha pili cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo.

Tazama hapo chini alivyopokelewa na Spika wa Bunge Job Ndugai na Naibu Spika Dr Tulia Ackson


Share:

Afikishwa Mahakamani Kwa Makosa Ya Kughushi Vyeti Vya Taaluma

Na Amiri kilagalila
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Njombe,imemfikisha katika mahakama ya hakimu mfawidhi wilaya ya Makete Bi.HONORATHA MWINUKA katibu muhtasi halmashauri ya wilaya ya Makete na kumfungulia kesi na CC.11/2019 kwa makosa ya kughushi vyeti vya taaluma chini ya sheria ya kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kaimu mkuu wa Takukuru mkoa wa Njombe CHARLES MULEBYA  amesema kuwa mshtakiwa kwa lengo la kujipatia ajira kama katibu muhtasi alighushi vyeti vya taaluma akionyesha kuwa alisoma kozi ya ukatibu muhtasi katika chuo cha utumishi wa umma (TPSC) Dar es salaam.

Ambapo alihitimu na kupewa cheti cha kumaliza kozi hiyo na kile cha matokeo huku akijua hajawahi kujiunga na chuo hicho wala kuhitimu kozi ya ukatibu muhtasi.

Mulebya amesema kitendo cha mshtakiwa  kughushi vyeti ni kinyume na K/F cha 333,335(a)337 na 342 vyote vya sheria ya kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Aidha amesema kesi dhidi ya mshtakiwa ipo mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Makete Mh.Jonathan Mpitanjia.


Share:

Serikali Kuendelea Kuimarisha Upatikanaji Wa Maji Safi Na Salama Nchini

Na; OWM (KVAU) - SONGWE
Serikali imedhamiria kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio mijini kufikia asilimia 95 na vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Hassan Suluhu wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Aprili 2, 2019 zilizofanyika uwanja wa Kimondo – Forest Mlowo, Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe.

Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 isemayo “Maji ni Haki ya kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”

Makamu wa Rais amesema kuwa dhamira ya Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni  kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu, afya, barabara,  umeme vijijini, usafiri wa anga, uvuvi, kilimo, viwanda na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wote.

“Sera yetu ya Maji ya mwaka 2002 inasisitiza upatikanaji wa maji safi na salama ambayo ni muhimu kwa maisha ya kila mtu, shughuli za kiuchumi na ustawi wa mazingira,” alisema Makamu wa Rais.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maji safi, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji nchini ikiwemo mabwawa ya kimkakati na kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji maji safi.

Aidha, Makamu wa Rais alitoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji kwa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kando ya vyanzo hivyo.

Kupitia hadhara ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Makamu wa Rais, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao ni muhimu katika kuleta maendeleo ya watu na huduma za kijamii.

Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ndio msingi mkubwa wa amani, Mshikamano, Uzalendo na Umoja tulionao katika Taifa.

“Tunu hii imekuwa ni kichocheo cha maendeleo kwa wananchi na wamekuwa wakihamasika kushiriki katika kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ya kijamii na kiuchumi iliyopo katika maeneo yao,” alisema Mhagama.

Waziri Mhagama aliongeza kwa kuwashukuru wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha tukio hilo muhimu la Kitaifa.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali (Mst.), Nicodemus Mwangela alishukuru Serikali kwa kuchagua Mkoa wa Songwe kuwa wenyeji wa Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2019.


Share:

Waziri Wa Madini Uganda Afurahishwa Na Usimamizi Wa Sekta Ya Madini Nchini

Na Greyson Mwase, Geita
Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris ames    ema kuwa amefurahishwa na usimamizi wa sekta ya madini nchini Tanzania na kusisitiza kuwa Uganda bado itaendelea kutuma wataalam wake pamoja na wachimbaji wadogo wa madini nchini Tanzania kwa ajili ya kujifunza namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Lokeris aliyasema hayo jana tarehe 02 Aprili, 2019 mara baada ya kutembelea migodi ya wachimbaji wadogo na wa kati ya madini iliyopo Wilayani Geita Mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne nchini Tanzania yenye lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika Sekta ya Madini kupitia Wizara ya Madini hususan katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini.

Akiwa ameongozana na  ujumbe wa maafisa waandamizi kutoka Serikali ya Uganda pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo aliwasili mkoani Geita na kupokelewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita pamoja na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo.

Ziara hiyo pia ilihusisha wataalam kutoka Wizara ya Madini. Tume ya Madini, vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa pamoja na waandishi wa habari.

Akielezea hali iliyopelekea nchi ya Uganda kuichagua nchi ya Tanzania kama sehemu ya kujifunza kuhusu Sekta ya Madini, Lokeris alisema kuwa, baada ya kutanya  utafiti katika nchi za Aftika Mashariki, walibaini kuwa nchi ya Tanzania ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwenye usimamizi wa sheria na kanuni za madini hali iliyopelekea wananchi wengi kunufaika nayo hususan wachimbaji wadogo wa madini.

Aliendelea kusema kuwa, Sekta ya Madini Nchini Uganda ndio inaanza kukua, hivyo wameona ni vyema kuja Tanzania  kwa ajili ya kujifunza na kwenda kuimarisha Sekta ya Madini ili baada ya miaka kadhaa angalau iwe inakaribiana na nchi ya Tanzania.

Akielezea mikakati ya matumizi ya uzoefu mkubwa ujumbe huo ilioupata kutoka kwa nchi ya Tanzania, Waziri Lokeris alisema hatua ya kwanza itakayofanywa na Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya  Madini ni kuhamasisha wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi na kuwapatia leseni.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kuwapatia leseni hatua itakayofuata itakuwa ni kuwaleta Tanzania kwa ajili ya mafunzo ambapo watajifunza kupitia wachimbaji wadogo wa madini wa Tanzania waliofanikiwa kwenye shugfhuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Aliendelea kueleza kuwa, nia ya Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya Madini ni kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa kasi na kuanza kuzalisha dhahabu na kuuza nyingine nje ya nchi na kujipatia mapato makubwa.

“Tumefurahishwa na usimamizi mzuri kwenye sekta ya madini hususan kwenye eneo la uwezeshaji wa wachimbaji wadogo, tumeona namna wanavyochenjua madini huku wakizingatia sheria na kanuni za mazingira,”alisisitiza Waziri Lokeris.

Naye Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo akielezea mafanikio ya sekta ya madini nchini alieleza kuwa, mafaniko yaliyopatikana ni pamoja na uboreshaji wa sheria mpya ya madini pamoja na kanuni zake inayotambua madini kama mali ya watanzania na kusisitiza kuwa wachimbaji wadogo wamekuwa wanufaika kwa kiasi kikubwa.

Aliongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeondoa tozo mbalimbali zisizo za lazima hali iliyopelekea wachimbaji wadogo kuzalisha madini kwa gharama nafuu na kulipa kodi na tozo mbalimbali serikalini.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko nchini kama njia mojawapo ya kudhibiti utoroshwaji wa madini kwa kuhakikisha wachimbaji wa madini wanakuwa na soko la uhakika la kuuzia madini yao kwa bei yenye faida.

Naye mmiliki wa mgodi wa  dhahabu wa Blue Reef uliopo katika eneo la Rwamgaza Wilayani Geita mkoani Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita (GEREMA), Christopher Kadeo akizungumza na  ujumbe huo uliofanya ziara kwenye mgodi wake akielezea mchango wa mgodi wake katika jamii iliyopo jirani alisema mgodi wake tangu ulipoanzishwa mwaka 1991 mpaka sasa umefanikiwa kuajiri watumishi 160 na vibarua takribani  200.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu, ulinzi kupitia ujenzi wa vituo vya polisi na kusisitiza kuwa mgodi umekuwa ukishirikiana kwa karibu zaidi na Tasisi nyingine za Serikali kama vile Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Chuo Cha Ufundi Dar es Salaam (DIT), Wizara ya Madini, Tume ya Madini na mashirika mengine ya kimataifa.

Aidha, aliongeza kuwa mgodi wake umewahi kupewa tuzo ya utunzaji bora wa mazingira na Rais wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Akielezea mikakati ya mgodi wake kwenye shughuli za uchimbaji wa madini  alisema mgodi wake unatarajia kufanya utafiti zaidi ili kugundua madini zaidi na kuunganisha leseni zake tano unazomiliki na kutoka kwenye uchimbaji wa kati hadi mkubwa.


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya April 3


























Share:

Tuesday, 2 April 2019

Picha : MAKAMU WA RAIS AZINDUA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2019 MKOANI SONGWE



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasha Mwenge kuashiria kuzinduliwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Mlowo mkoani Songwe.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasha Mwenge kuashiria kuzinduliwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Mlowo mkoani Songwe. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mwenge kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa mwaka 2019 Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi kuashiria kuanza kwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mwenge kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa mwaka 2019 Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi kuashiria kuanza kwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019. 
Share:

RAPA NIPSEY HUSSLE ALIUAWA AKIJARIBU KUIBUA UKWELI KUHUSU TIBA YA UKIMWI


Haikuwa sikukuu ya wajinga kama ambavyo mashabiki wa rapa Nipsey Hussle walitamani iwe ili taarifa za kifo chake zibaki kuwa za uongo. Lakini ilikuwa kweli, rapa huyo alipoteza uhai baada ya risasi mbili kutua kichwani na tumboni mwake.

Kwa mashabiki wa kazi zake, hakuwa rapa tu bali mwanaharakati aliyepambana kuhakikisha usawa hasa kwa Wamarekani wenye asili ya Afrika unakuwapo.

Jana akiwa nje ya duka lake la mavazi Marathon Clothing rapa huyo alivamiwa na kushambuliwa kwa risasi nyingi na mbili zilimpata kichwani na tumboni na kukatisha safari yake ya maisha ya miaka 33 aliyoitumikia hapa duniani.

Rapa huyo baba wa watoto wawili amefariki wakati akiendelea kuandaa jarida la Dk Sebi inayedaiwa kuwa aligundua dawa ya Ukimwi na kutibu wagonjwa watatu lakini alifariki katika mazingira ya kutatanisha.

Daktari huyo ambaye jina lake halisi ni Alfredo Darrington Bowman alikuwa raia wa Honduras lakini mara zote alipenda kutambuliwa kama Mwafrika anayeishi nchini Marekani.

Hussle aliyekuwa mchumba wa mwigizaji Lauren London alikuwa akiandaa jarida kuhusu kifo cha Dk Sebi akihusisha na tiba zake hasa ile inayotibu Ukimwi.

Inadaiwa kuwa Hussle aliamini kuwa kifo chake kilifanywa na wazalishaji wa dawa hasa zinazohusiana na magonjwa ya Ukimwi, kisukari na sikoseli ambayo alikuwa akiyatibu.

Dk Sebi ambaye alitumia mitishamba kutibu wagonjwa hayo, mara kadhaa alikamatwa nchini Marekani na mwaka 1987 alishtakiwa kwa kutengeneza dawa bila kuwa na kibali.

Alikamatwa zaidi ya mara mbili akiwa nchini Marekani akituhumiwa kutakatisha fedha.

Rapa Nick Cannon amesema ataendelea na utengenezaji wa jarida la Dk Sebi aliyefariki Agosti 26, 2016 akiwa katika mahabusu nchini Honduras.

Watu wengine maarufu akiwamo mbunifu wa mavazi Russel Simmons amejitolea kumsaidia Cannon katika kukamilisha kazi hiyo.
Share:

MKAZI WA MTWARA ALAMBA PESA ZA VODACOM TUZO POINTS


Meneja wa Vodacom Tanzania (PLC), mkoani Mtwara, Charles Minungu (kushoto) akiwa na meneja wa vodashop Mtwara, Frank Daud wakimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi 500,000/- mmoja wa washiriki wa kampeni ya Vodacom M-Pesa Tuzo Points, Eladius Lutha mkazi wa Naliendele katika hafla iliyofanyika Mtwara. Kupitia kampeni hii wateja 140 wa Vodacom walizawadiwa shilingi 25,000/-kila mmoja na baada ya kampeni kumalizika wateja 10 wa Vodacom nchi nzima watazawadiwa shilingi 500,000/-kila mmoja.

Share:

DC BURA AWAONYA WANA CCM KUHUSU RUSHWA KWENYE UCHAGUZI

Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilayani Kibondo mkoani Kigoma wametakiwa kuacha kupokea rushwa kwa baadhi ya viongozi wanaotaka kuja kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na serikali kuu.


Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Louis Bura wakati wa ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwezo Watendaji wa Chama Cha Mapinduzi ngazi ya tawi hadi kata na jumuiya zake na kuwajengea weredi na uelewa wa namna gani ya kuongoza ambapo  aliwataka kuwaacha wananchi kuchagua kiongozi aliye bora na sio kumpendekeza kiongozi ambaye amepita na kuwagawia rushwa katika kata zao.

Alisema kuelekea uchaguzi mwaka huu na mwaka 2020 ni lazima viongozi wa chama wawe makini na viongozi wanaotaka kugombea kwa kuwa watapita mitaani kuwashawishi kwa kuwa wao ndio wapiga kura wa kwanza na kuwataka viongozi hao kuacha kuchochea kiongozi flani apitishwe kwa kuwa katoa pesa.

Bura alisema kiongozi mtoa rushwa hafai katika uchaguzi huu kwa kuwa anakuwa ana lengo la kujitengenezea masilahi yake binafsi.

"Tunafahamu wapo baadhi ya watu wanaotaka kugombea wanapita wanawashawishi muwachague, niseme tu kwa yeyote tutakaemkamata hatutasita kumuadhibu na ikiwezekana tutashirikiana na viongozi wa chama kumfuta kabisa katika watu wanaogombea, hatutaki viongozi wanaotoa rushwa, kiongozi apite kwa kujiamini mwenyewe na kuaminiwa na wananchi", alisema Bura.

Akiwakaribisha watoa mada walioandaliwa katibu wa CCM Wilaya ya Kibondo Stanley Mkandawile aliwataka viongozi wa matawi na kata kuwa wa kweli kutoa tathmini za kweli ni mgombea gani anakubalika na  Wananchi ilikuhakikisha  wanakipatia ushindi wa kutosha chama.

Alisema viongozi wanaotoa fedha kuwashawishi wapiga kura kuwachagua hawafai na viongozi ambao hawakubaliki kwa wananchi hawafai, lazima viongozi wa chama wa kata na matawi, kupita kwa wananchi kujua ni kata gani chama kina mgombea ambaye anakubalika na kata gani ambako kuna changamoto kiongozi aliyepo hakubaliki.

Aidha Mkandawile alisema lengo la chama ni kuhakikisha kata 19 na vijiji vyote vya kata hizo wanapata ushindi pamoja ili kufanikisha hilo ni lazima  viongozi kupata idadi ya wanachama waliopo katika kata zao na kutatua kero zote ambazo zinaweza kusababusha chama kukosa ushindi.

Katibu kata ya Misezero,Benjamini  Mlinjie  alisema semina ya kuwajengea uwezo imewafungua fikra za uongozi na mpaka sasa wamejipanga kushirikiana na TAKUKURU  kuwafichua wale wote wasiojiamini na wanataka kutoa rushwa ili wapitishwe.

Alisema wapo baadhi wanatabia hizo na kwa sasa watahakikisha viongozi wote wanaopita wana uwezo wa kuongoza na wanapita kutokana na wananchi wanavyowakubali na sio kwa sababu ya kutoa rushwa.


Alisema wako tayari kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa,Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha chama kinapata viongozi waadilifu na wanaokubalika na wananchi kwa kuwa chama kina hazina ya kutosha.
Na Rhoda Ezekiel Kigoma - Malunde1 blog
Share:

CCM KIBONDO YAAGIZA MRADI WA MAJI ULIOKWAMA TANGU 2014 KAGEZI NA MLANGE UKAMILIKE NDANI YA MWEZI MMOJA

Wananchi wa vijiji vya Kagezi na Mlange Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma, wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita mbili kufuata maji katika chanzo cha maji kutokana na mradi wa maji uliogharimu zaidi ya bilioni moja kutokamilika tangu mwaka 2014 hadi sasa.

Wakizungumza jana kijijini hapo wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani kwa baadhi ya miradi ya serikali uliofanya na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali ya wilaya hiyo, baadhi ya wananchi hao waliokuwa wakigombania maji katika chanzo cha mto Kagezi, walisema wanapata shida sana ya kuchota maji na hasa ukizingatia Mlima uliopo katika chanzo hicho unawachosha.

Mmoja wa wananchi hao,Agnes Kunjira alisema wanalazimika kuamka asubuhi sana kuwahi kuchota maji ndipo waende mashambani, kutokana na kero hiyo wanashindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa wakati kwa kuwa maji ni uhai na wanahitaji maji.

Aidha aliiomba serikali kufuatilia kwanini mradi huo hautoi maji kwa kuwa kero waliyonayo inawatesa sana na endapo mradi huo ukikamilika na wakaanza kuchota maji vijijini itawasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya shughuli zao za maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Kagezi mwenyekiti wa kijiji hicho,Zabroni Ntimba, alisema tangu mradi huo uanze kujengwa ni muda mrefu na mpaka sasa ulitakiwa uwe umekamilika lakini mwaka 2018 wananchi walipata maji kwa muda wa miezi mitatu tu na baada ya hapo maji hayakutoka tena.

Alisema wananchi wanalalamika sana na hasa kwa kuwa walichangia asilimia 20% ya mradi hali hiyo inasababisha wananchi kushindwa kuchangia hata shughuli zingine za maendeleo, kwa kuwa wamechangia mradi wa maji lakini hawaoni mradi ukifanya kazi.

Akitoa ufafanuzi juu ya mradi huo Mhandisi wa maji wilaya ya Kibondo Michael Nguruwe alisema mkandarasi wa mradi huo aliingia mkataba ,wa shilingi bilioni moja na milioni (244,629,764/=)  mradi ulitakiwa kuwa umekamilika 2014 lakini kutokana na changamoto ya fedha kulipa kwa wakati kwa mkandarasi mradi uliongezewa muda hadi 2018 lakini mpaka sasa haujakabidhiwa kwa wananchi.

Alisema tatizo kubwa lililopelekea mpaka sasa mradi huo kutokamilika kwa wakati, ni changamoto ya mfumo wa umeme, ambalo mkandarasi alishindwa kulikamilisha na kama halmashauri wamezuia kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya umaliziaji wa mradi huo.

Alisema mpaka sasa wanaendelea kutafuta mkandarasi wa mfumo wa umeme katika mradi huo kwa ajili ya kuweka kifaa kitakachosaidia kuongoza mfumo wa umeme katika mradi huo na mradi ukabidhiwe kwa wananchi kwa ajili ya kutumika.

Kutokana na changamoto zilizopo katika mradi huo na kero wanayoipata wananchi, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Kibondo Hamisi Tahilo alisema chama kinaagiza mradi huo kukamilika kwa kipindi cha mwezi mmoja na baada ya mwezi mmoja watafika katika mradi huo kuangalia kama kweli wananchi wameanza kupata maji.

Alisema serikali imetoa zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya mradi wa Wananchi lakini hadi sasa mradi huo haujakamilika, serikali iliahidi kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani ni lazima watendaji kuhakikisha wanasimamia miradi ya serikali inafanyiwa kazi.

"Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM na fedha zinatolewa kwa ajili ya kukamilisha miradi wananchi wataiamini serikali baada ya kuona miradi hii inakamilika niombe ndani ya mwezi huo mmoja mradi huu uwe umekamilika", alisema Tahilo.

Hata hivyo aliwaomba wananchi kuwa na subira na kuendelea kujenga imani na CCM kwa kuwa imejipanga kuhakikisha wananchi wote wa vijijini na mijini wanapata huduma sawa sawa na wanaondokana na changamoto zote.

Na Rhoda Ezekiel Kigoma - Malunde1 blog

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Kibondo wakiwasaidia wananchi kubeba maji.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kagezi wakichota maji katika chanzo cha mto Kagezi baada ya kero kubwa ya maji kijijini humo.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger