Msanii mkongwe wa muziki wa Hip Hop hapa Tanzania, Afande Sele ametoa ushauri na mtazamo wake juu ya sakata la Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) kuwafungia wasanii wenzake Diamond Platnumz na Rayvanny kutotumbuiza ndani na nje ya nchi.
Afande Sele ameanza kwa kushangazwa kwa nini BASATA wawafungie wasanii hao kutofanya show nje ya nchi ile hali wamefanya kosa hilo ndani ya nchi?
“Haijawahi kutokea….unacheza faulo kwenye ligi ya ndani lkn unapewa adhabu ya kutoshiriki hadi mechi za kimataifa…Basata ni mfano wa mtu aliyesifiwa kwa mbio hadi amepitiliza kwao.”ameandika Afande Sele kwenye ukurasa wake wa Instagram na kueleza namna adhabu hiyo ilivyokuwa kubwa na kumpongeza Diamond na Rayvanny kwa kuomba msamaha.
“BASATA kama wazazi wametimiza wajibu kwani bakora moja haimuui mtoto bali humnyoosha ktk njia sahihi ingawa ktk hili la sasa Baraza limetumia panga au rungu kumuadhibu mtoto kitu ambacho kiasi fulani kinaleta ukakasi hata kama mtoto ameonyesha ujeuri kiasi gani…ila ukweli utabakia palepale kwamba Basata ni Jiwe na wasanii ni Nazi hivyo busara ni wasanii nao kutimiza wajibu wao kwa kuomba Radhi…huo ndio uungwana.”
Wiki hii Diamond na Rayvanny wamefungiwa na BASATA kutofanya show za ndani na nje kwa muda usiojulikana.
Tayari wawili hao wameshaomba radhi kwa kutumia wimbo wa Mwanza jukwaani wakati wakijua wimbo huo umefungiwa.