TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania
(TCU), imetoa ufafanuzi juu ya taarifa za kutoka kwa matokeo ya
waombaji wa nafasi za kujiunga na vyuo vikuu hapa nchini, kwa mwaka wa
masomo 2016/2017, anaandika Charles William.
Kwa siku tatu sasa, kumekuwepo na taarifa za TCU
kutoa matokeo ya nafasi hizo huku wanafunzi wengi wakilalamikia
kushindwa kuyaona matokeo hayo katika tovuti ya tume hiyo.
Akizungumza kwa njia
ya simu jioni ya leo, Edward Mkaku, afisa habari mwandamizi wa TCU
amesema, TCU tayari imeweka matokeo ya awali ya nafasi hizo lakini
matokeo hayo ni awali tu na siyo rasmi mpaka pale yatakapothibitishwa. “Tumetoa matokeo ya awali (provisional results), ambayo mwanafunzi
anatakiwa kuingia katika akaunti yake ya TCU na kuona kama amepangiwa
Chuo au la, lakini matokeo hayo siyo rasmi mpaka pale yatakapokuwa
yamethibitishwa (approved),” amesema Mkaku na kufafanua zaidi kuwa; “Katika matokeo ya sasa tuliyotoa, mwanafunzi hawezi kuona amepangiwa
chuo gani wala kitivo au taaluma aliyopangiwa kusoma, ila tu
anajulishwa kuwa amepangiwa kusomea kitu kimoja kati ya vile vitano
alivyoomba.” Akitolea ufafanuzi juu ya wanafunzi ambao wamekosa nafasi za
kuchaguliwa katika hatua ya sasa, Mkaku amesema wanafunzi hao wanayo
fursa ya kuomba tena nafasi hizo. “Tayari zoezi la kuomba vyuo kwa awamu ya pili limeanza tangu jana
(Jumatatu), wanafunzi waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza wanaweza
kuomba tena katika awamu hii ya pili,” amesema. Uombaji wa nafasi kujiunga na vyuo vikuu unaofanyika mwaka huu,
utakuwa chini ya vigezo vipya vya kujiunga na elimu ya ngazi hiyo
tofauti na miaka iliyopita. Hii ni kufuatia mabadiliko yaliyotangazwa na
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Profesa Joyce
Ndalichako. Lakini pia uombaji wa mwaka huu, unafanyika wakati serikali ikiwa
katika mchakato wa kuwasaka wanafunzi waliopo vyuoni pamoja na
waliohitimu vyuo bila kuwa na vigezo. Vyuo vikuu mbalimbali visivyokidhi
matakwa ya kitaaluma pia vimechukuliwa hatua.
BUNGENI DODOMA: Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jaffo asema
wahitimu shahada za sayansi ambao si walimu kupatiwa mafunzo maalum
wakafundishe na wale wa sanaa ambao hawatapata nafasi sekondari
watafundisha shule za msingi.