INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
MAUAJI
ya Watanzania kwa njia ya kuchinjwa yanaendelea kushika kasi baada ya
usiku wa kuamkia jana wakazi wanane wa kitongoji cha Kibatini, kata ya
Mzizima jijini Tanga kukusanywa kwa mwenyekiti wa kitongoji na kisha
kuuawa kwa kuchinjwa shingo na watu wasiojulikana.
Watu
hao ambao inadaiwa kuwa ni majambazi walivamia usiku wa kuamkia jana
kwa kuvunja milango ya nyumba tatu ambazo wakazi hao walikuwa wamelala
na kuwachinja kisha kuiba biskuti, mchele na sukari na kutokomea navyo
kusikojulikana.
Wauaji
hao inadaiwa wana uhusiano na wahalifu ambao wamekuwa wakijificha ndani
ya mapango ya Majimoto na kujihusisha na matukio kadhaa ya uvamizi ili
kupora vyakula na kusababisha mauaji ya wakazi wa Jiji la Tanga, ikiwamo
katika duka kuu la Central Bakery mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Mmoja
wa shuhuda wa mauaji hayo, Kea Leonard (70) ambaye pia ni mkazi wa
Kibatini, katika mahojiano jana alisema wanaamini kwamba chanzo cha
mauaji ya wenzao ni kulipiza kisasi.
“Wiki
iliyopita majira ya saa tano asubuhi hapa tulikamata vijana saba kati
ya wanane wenye umri wa kama miaka 13 ambao walikuwa wakiranda randa
hapa kitongojini ili kutafuta namna ya kuvuka mto kwenda ng’ambo ya pili
na ndipo mmoja wao alipotutoroka,” alieleza Leonard na kuongeza:
“Watoto
hao tulipowaweka chini ya ulinzi na kuwahoji tukaanza kuwatilia shaka
hivyo mwenyekiti aliamua kuripoti Polisi na ndipo hao wakawachukua kwa
ajili ya mahojiano na hatukufuatilia tena kujua kwamba waliachiwa au la
kwa sababu hao watoto sio wenyeji wala wakazi wa eneo hili.”
Aliongeza
kwamba wakati wahalifu hao wanavamia nyumba ya mjumbe wa serikali ya
kitongoji kabla ya kumtoa nje walisikia mmoja wa watu hao akimhoji
kuhusu mahali walipopelekwa watoto saba.
Diwani
wa Kata ya Mzizima, Fredrick Charles alizungumza na waandishi wa habari
na kuthibitisha kwamba kati ya watu waliokufa mmoja ni Mjumbe wa
Serikali ya Mtaa wa Mleni uliopo kwenye kata hiyo.
“Hali
ya usalama hapa kwetu Mzizima si shwari kwa sababu wananchi wangu wa
Kibatini wamevamiwa na kuchinjwa usiku wa kuamkia jana majira ya saa
sita usiku,” alisema Chiluba.
Naye
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mleni kilichopo kitongoji hicho,
Shabani Amani alisema wamepatwa na hofu kubwa kuhusu matukio hayo.
“Tunadhani
kuna mapungufu katika suala la ulinzi hapa kwa sababu baada ya kutokea
matukio kadhaa eneo letu hasa baada ya kudaiwa kwamba mapango
waliyojificha wahalifu yako hapa jirani na kwetu kikosikazi cha
mchanganyiko wa askari polisi na wa JWTZ wanafanya doria kwa saa 24
lakini tunashangaa kwa nini matukio yanaendelea,” alisema Amani.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul alithibitisha mauaji hayo. “Mei 30, mwaka huu majambazi waliokuwa na visu na mapanga walivamia kaya tatu na kuua wananchi majira ya saa saba usiku,” alisema Kamanda Paul.
Aliwataja
waliouawa ni Issa Hussein (50) ambaye ni mmiliki wa kaya hiyo pamoja na
kuibwa biskuti, mchele na sukari katika duka dogo. Wa kaya nyingine ni
Mkola Hussein (40) na Hamis Issa (20), Hamis Issa (20) na aliyemtaja kwa
jina la Mikidadi (70).
Kamanda
aliwataja marehemu wengine ni Mahamud (35) ambaye ni mkwe wa Mikidadi,
Issa Ramadhani (25), Kadir (25) na Salum ambao ni wachunga ng’ombe
kijijini humo.
Hata
hivyo, mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mke wa marehemu Mkola aitwaye
Aisha Saidi, alisema walipofika nyumbani hapo waligonga mlango na kumtoa
nje Mkola na kuondoka naye.
“Nimeachwa
mjane na watoto sita... Baada ya hao watu kuingia walimkamata Mkola na
kumdai aeleze kwamba watoto wao saba wamepelekwa wapi na alipojibu sijui
wakamtoa nje na kumkusanya pamoja na wanakijiji hao wengine na
kuwachinja eti tu kwa sababu hawakutaja mahali walipopelekwa watoto,” alisema Aisha.
Katika
hatua nyingine, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
imesikitishwa kupokea taarifa za vitendo vya mauaji ya kikatili
vinavyoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini.
“Wimbi
hili la matukio ya vitendo vya mauaji na ukatili uliojitokeza kwa
kufuatana mwezi Mei 2016 yanavunja haki ya kuishi ambayo ndio msingi wa
haki zote za binadamu kwa ujumla wake.
"Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali mauaji haya yote na
matendo yote ya kikatili dhidi ya mwanadamu yanapotokea popote nchini,” ilieleza taarifa ya Mwenyekiti wa Tume, Bahame Nyanduga.
Tume
iliishauri serikali kupitia Jeshi la Polisi ichukue hatua mahsusi
kuhakikisha ulinzi wa wananchi dhidi ya mauaji na vitendo hivi, kwani
jukumu la kwanza la kuhakikisha usalama wa wananchi ni jukumu la
serikali.
Jeshi la Polisi lihakikishe watu wote waliohusika kutekeleza mauaji haya wanakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake, ilieleza.