MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan leo
atawasha Mwenge wa Uhuru na kuzindua rasmi mbio zake ili kukimbizwa
katika halmashauri za wilaya na Manispaa zipatazo 179 za mikoa ya
Tanzania Bara na Visiwani.
Uzinduzi huo utakaofanyika kwenye
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambao utatanguliwa na shamrashamra za
halaiki kutoka kwa vijana zaidi ya 1,000 na vikundi vya utamaduni kutoka
wilaya za Morogoro na nje ya mkoa huo.Katika
uzinduzi huo, viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na vyama vya siasa
wamealikwa kushiriki wakiwemo pia mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pamoja na Waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Miongoni mwa mawaziri ambao hadi jana
walikuwa tayari wamewasili mkoani hapa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, Sera, Vijana, Ajira na Walemavu,
Jenista Mhagama na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mouldine Castico.
Mawaziri hao jana waliungana na Makamu
wa Rais kutembelea mradi wa vijana wajasiriamali wa mafundi seremala
eneo la Mtaa wa Betero, Kata ya Sabasaba, Manispaa ya Morogoro.
Kaulimbiu za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni “Vijana ni Nguvu kazi ya
Taifa, Washirikishwe na Kuwezeshwa.”
Baada ya kuwashwa leo, Mwenge wa Uhuru
utakimbizwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kuhitimishwa
wilayani Gairo ambako Aprili 25, mwaka huu utakabidhiwa mpakani mwa
wilaya hiyo na Kilindi ya Mkoa wa Tanga ili kuendelea na mbio zake.
Kwa mujibu wa ratiba ya mbio za Mwenge
wa Uhuru za mwaka huu, utakimbizwa katika Halmashauri na Manispaa
zipatazo 179 na kilele cha mbio hizo ni Oktoba 14, mwaka huu katika Mkoa
wa Simiyu.