INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Tuesday, 16 February 2016
Majambazi Yaua Polisi Tanga
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Askari
wa jeshi la polisi Koplo George Braiton aliyepigwa risasi na majambazi
wakati akikabiliana nao katika tukio la ujambazi lililotokea barabara ya
sita na saba jijini Tanga amefariki dunia.
Koplo
Braiton amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya
Mkoa wa Tanga,Bombo, akiwa na watu wengine wawili waliopigwa risasi
katika tukio hilo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga ACP.Mihayo Msikhela amesema kuwa bastola
ilitumika kupoteza uhai wa Koplo George Braiton wa kituo cha polisi
Chumbageni na kujeruhi raia wengine wawili ambao bado wanaendelea na
matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga.
Polisi
wamesema walifanikiwa kuwakamata majambazi hao wakiwa na bastola
waliyoitumia kwenye tukio hilo pamoja na visu wanavyovitumia kwenye
matukio ya kihalifu.
Majirani
waliokuwa wakiishi na Koplo Braitoni wamesema tukio hilo
limewagusa,lakini wakaiomba jamii kuwafichua wahalifu kwa lengo la
kukabiliana na vitendo hivyo.
Kolpo Braitoni anatarajiwa kusafirishwa kupelekwa mkoani Mara Februari 16 kwa ajili ya mazishi.
MPYA:BODI YA MIKOPO WATUMBULIWA MAJIPU MKURUGENZI WA BODI YA MIKOPO ASIMAMISHWA KAZI
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako amewasitishia mikataba ya kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya
Mikopo (HESLB), George Nyatega na Wakurugenzi wengine watatu kutokana na
utendaji mbovu katika kuendesha bodi hiyo.
Wengine
ni Mkurugenzi Mkuu wa Mikopo ya wanafunzi asimamishwa kazi, wengine ni
Mkurugenzi wa Urejeshaji wa Mikopo, Mkurugenzi Upangaji na Utoaji wa
Mikopo.
Mkataba
wa Mkurugenzi Mtendaji HESLB umesitishwa. Ilikua uishe mwezi August
2016. Mhasibu Mkuu (Bw. Kisare), Mkurugenzi wa Utoaji Mikopo (Bw.
Laizer) na Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo (Bw. Chagonja) wamesimamishwa
kupisha uchunguzi.
Amewateua
wafuatao ku Kaimu nafasi; Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mteule ni Bw. Jerry
Sabi kutoka Mzumbe University na Kaimu Mhasibu Mkuu mteule ni Bw.
Daniel Mafie kutoka NECTA
SEKRETARIETI YA AJIRA:MATOKEO YA USAILI ULIOFANYIKA TAREHE 13-02-2016
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Wasailiwa waliochaguliwa kuendelea na usaili wanatakiwa kufika, tarehe na muda kama ilivyo oneshwa kwenye ratiba ya usaili. Wasailiwa wanakumbushwa kufika na vyeti halisi (Original certificates) KADA: ICT OFFICER GRADE II (APPLICATION DEVELOPMENT ICT MANAGEMENT) MWAJIRI: (e-Government Agency) SN EXAM NUMBER SCORES REMARKS 1 eGA ICT APPL DEV MGT - 0081 53 SELECTED 2 eGA ICT APPL DEV MGT - 0069 52 SELECTED 3 eGA ICT APPL DEV MGT - 0140 52 SELECTED 4 eGA ICT APPL DEV MGT - 0035 51 SELECTED |
|
| Read more... |
Serikali kutangaza ajira 40,000 za walimu
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Ili kupunguza ukosefu wa walimu katika shule za msingi na sekondari
nchini, serikali inatarajia kutoa ajira 40,000 kwa walimu mwaka huu ili
kuendana na kasi ya uandikishaji wa wanafunzi na utoaji wa elimu bure.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jaffo, amewaeleza wanahabari kuwa idadi hiyo inalenga kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu shuleni na utoaji wa elimu bora zaidi.
Jaffo alisema ajira hizo zitatangazwa mapema mwaka huu na zitaongeza nguvu kwenye shule zenye uhitaji wa walimu hasa mpya na zile zilizoandikisha wanafunzi wengi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza.
Sambamba na hilo, ameahidi kushirikiana na shule za msingi zilizoandikisha wanafunzi wengi zaidi wa darasa la kwanza ili shule hizo zipate miundombinu ya kutosha kuwahifadhi wanafunzi hao.
Amesema kwa kuanza, serikali imejipanga kuongeza majengo katika shule ya msingi Mbagala Majimatitu ambayo imeandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 1,022, idadi ambayo ni sawa na wanafunzi wa shule moja kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jaffo
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jaffo, amewaeleza wanahabari kuwa idadi hiyo inalenga kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu shuleni na utoaji wa elimu bora zaidi.
Jaffo alisema ajira hizo zitatangazwa mapema mwaka huu na zitaongeza nguvu kwenye shule zenye uhitaji wa walimu hasa mpya na zile zilizoandikisha wanafunzi wengi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza.
Sambamba na hilo, ameahidi kushirikiana na shule za msingi zilizoandikisha wanafunzi wengi zaidi wa darasa la kwanza ili shule hizo zipate miundombinu ya kutosha kuwahifadhi wanafunzi hao.
Amesema kwa kuanza, serikali imejipanga kuongeza majengo katika shule ya msingi Mbagala Majimatitu ambayo imeandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 1,022, idadi ambayo ni sawa na wanafunzi wa shule moja kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.
Rais Magufuli Amteua Dr. Asha Rose Migiro Na Mathias Chikawe Kuwa Mabalozi Wapya....Dr. Kipilimba Kateuliwa Kuwa Bosi Mpya Wa NIDA
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya
uteuzi wa mabalozi watatu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Rais
Magufuli pia amefanya uteuzi wa makamishna wanne wa Jeshi la Polisi na
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Taarifa
ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, imewataja mabalozi
walioteuliwa kuwa ni Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro, Mheshimiwa Mathias
Meinrad Chikawe na Dkt. Ramadhan Dau.
Vituo vya uwakilishi kwa mabalozi hawa vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia kukamilika.
Kwa upande wa Makamishna wa Polisi, Balozi Sefue amewataja walioteuliwa kuwa ni:
Naibu
Kamishna wa Polisi Simon Nyakoro Sirro ambaye amepandishwa cheo kuwa
Kamishna wa Polisi, na ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya
Dar es salaam. Kamishna Sirro anajaza nafasi iliyoachwa wazi na
Kamishna Mstaafu Suleiman Kova.
Naibu
Kamishna wa Polisi Albert Nyamuhanga ambaye amepandishwa cheo kuwa
Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Fedha, Utawala na
Lojistiki. Kamishna Nyamuhanga anajaza nafasi iliyoachwa wazi na
Kamishna wa Polisi Clodwing Mathew Mtweve aliyeteuliwa kuwa Katibu
Tawala wa Mkoa wa Mwanza.
Naibu
Kamishna wa Polisi Robert Boaz Mikomangwa ambaye amepandishwa cheo kuwa
Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Intelijensia.
Kamishna
Mikomangwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Valentino Mlowola
aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Nsato Marijani Mssanzya ambaye
amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara
ya Mafunzo na Operesheni.
Kamishna
Mssanzya anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Paul
Moses Chagonja aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.
Aidha,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemteua Dkt. Modestus Francis Kipilimba kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Kabla
ya Uteuzi huu Dkt. Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya
Udhibiti (Director of Risk Management) katika Benki Kuu ya Tanzania.
Dkt. Kipilimba anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Dikson Maimu ambaye
uteuzi wake ulitenguliwa.
Teuzi zote zinaanzia leo tarehe 15 Februari, 2016
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
15 Februari, 2016
Mchakato Wa Kura Ya Maoni Ya Katiba Mpya Waanza
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, amesema
mchakato wa Kura ya Maoni ya Katiba mpya umeanza baada ya kumalizika
kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Kauli
hiyo ya Jaji Lubuva imekuja wakati wadau wa siasa nchini wakimtaka Rais
Dk. John Magufuli, kutoendelea na Kura ya maoni badala yake mchakato wa
Katiba mpya urudi nyuma baadhi ya mambo yaliyo kwenye Katiba
iliyopendekezwa yarekebishwe.
Itakumbukwa
kuwa mchakato wa Katiba mpya uliingia dosari baada ya baadhi ya
viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupinga mfumo wa Serikali Tatu
uliokuwa umependekezwa na Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba,
iliyokusanya maoni nchi nzima na matokeo yake kuzaa kundi lililojiita
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Tulikuwa
tunangoja tumalize uchaguzi, kama vile ambavyo Mnyamwezi anavyobeba
mzigo, unamaliza mmoja unakwenda kwa mwingine. Sasa tumemaliza (uchaguzi
mkuu), tunakwenda kwa lingine (Kura ya Maoni),” alisema Jaji Lubuva.
Aliongeza: “Tunaliangalia
na kama Tume tutakuja kuwajulisha wananchi hali ikoje, tuliahirisha
(Kura ya Maoni) ili tumalize hili (uchaguzi mkuu).” alisema Jaji Lubuva na kuongeza.
“Hili
ni suala linalohitaji mambo ya bajeti kubwa na ndiyo tumetoka kwenye
uchaguzi na serikali ndiyo inaanza, kwa hiyo ni suala ambalo
tunaliangalia na baadaye wananchi watajulishwa,” alisema Jaji mstaafu Lubuva.
Alipoulizwa kuhusu makadirio ya bajeti ya kuendesha kura hiyo ya maoni, Lubuva alisema: “Hilo niulize siku nyingine, sina zaidi ya hapo kwa leo.”
Rais
Magufuli alipokuwa akihutubia Bunge la 11 siku ya kulizindua Novemba
20, mwaka jana, alisema serikali yake imepokea kiporo cha mchakato wa
Katiba ambao haukukamilika katika awamu iliyomtangulia kutokana na
kutokukamilika kwa wakati kwa uandikishaji wapiga kura.
“Napenda
kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo
iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa
maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la
Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu
kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba,” alisema Rais Magufuli.
Mbali
na muundo wa serikali tatu, baadhi ya mambo ambayo Ukawa walitaka yawe
kwenye Katiba mpya ni mamlaka ya Rais kupunguzwa, ushindi wa Rais uwe
zaidi ya asilimia 50, Tume huru ya Uchaguzi, matokeo ya Rais kupingwa
mahakamani, kuwe na mgombea binafsi, mawaziri wasitokane na wabunge, na
muundo mpya wa Bunge la Muungano.
Waziri Kairuki : "TAKUKURU Kuna Majipu Yanayohitaji Kutumbuliwa "
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
WAFANYAKAZI
wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), wametakiwa kuanza
kujisafisha huku wakiambiwa kwamba taasisi hiyo haitaepuka kutumbuliwa
majipu.
Aidha,
wameagizwa kuwasilisha upya taarifa za mali zao kwa Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, zifanyiwe uhakiki wa mali; moja baada ya
nyingine kubaini waliofanya udanganyifu wa umiliki wa mali zao.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki
alisema hayo jana Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa
viongozi wa taasisi hiyo.
Alisisitiza
kuwa tayari anazo taarifa zinazohitaji baadhi ya viongozi wa taasisi
hiyo kutumbuliwa majipu muda muafaka utakapowadia.
Kairuki
aliagiza taasisi hiyo kufanyia tathmini kesi zake zote, ilizowahi
kushindwa na kuja na majibu ya sababu za kushindwa na endapo itabainika
hazikushinda kutokana na mchezo mchafu wa wachunguzi, wahusika
wachukuliwe hatua haraka iwezekanavyo.
“Niliposikia
mnataja majina yenu wakati wa kujitambulisha, nilikuwa nafurahi sana
kwani wengi wenu nawajua na nina taarifa zenu. Haiwezekani wewe mtu
mmoja watu wengi wawe wanakuongelea vibaya. Msifikiri majipu humu
(Takukuru) hakuna, yapo na nawahakikishia tutayatumbua tu,” alisisitiza Waziri huyo.
Alisema
iwapo yupo mtumishi hasa viongozi wa taasisi hiyo, anayejitambua kuwa
ni ‘jipu’, ajisalimishe kwani akiendelea kusubiri na kutumbuliwa, mwisho
wake utakuwa mbaya.
“Tukiwatumbua
hali itakuwa mbaya kwani nyie mko chini ya Ofisi ya Rais, hata Rais (Dk
John Magufuli) hatasita kuwachukulia hatua si tu za kinidhamu bali hata
za kisheria,” alibainisha.
Alisema
katika taasisi hiyo, yapo maeneo mengi yanayohitaji kutumbuliwa majipu
kuanzia Uhasibu, Ukaguzi na Manunuzi zikiwemo ofisi za mikoani akitolea
mfano Mkoa wa Kilimanjaro na makao makuu, Upanga, Dar es Salaam.
“Tutasafisha
nawahakikishia hata ikibidi kuanza upya, ikitulazimu pia kufukuza wote
ikithibitika mnakwenda kinyume na maadili yenu tutawafukuza ila
hatutamwonea mtu, kwani wako watu wengi wenye sifa wanaotaka kufanya
kazi,” alisisitiza Kairuki.
Alisema
kuanzia sasa, ofisi hiyo itawekewa malengo ya utendaji wake na
kufanyiwa tathmini hasa kwa kesi zilizoshindwa ifahamike aliyezifanya,
sababu za kushindwa, iwapo imetokana na uzembe au kama upo mkono wa
mtu.
Alisema
imefikia wakati sasa watumishi wa taasisi hiyo wanapaswa sasa wale
kiapo cha ahadi ya uadilifu na kukisaini ili watakaoshindwa wachukuliwe
hatua za kinidhamu.
Taarifa za mali
Aliwataka
watumishi wote wa taasisi hiyo, kurejea upya kuwasilisha taarifa za
mali zao kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alisema
taarifa hizo zitapewa kipaumbele cha kuhakikiwa mali moja baada ya
nyingine na endapo mtumishi atabainika kufanya udanganyifu wa mali
anazomiliki, atachukuliwa hatua.
Alihadharisha
kuwa chombo hicho cha kupambana na rushwa hakipaswi kutuhumiwa kwa
rushwa. Alisema kikituhumiwa kwa sifa hiyo, ni sawa na kuigeuza Takukuru
kuwa jipu badala ya vidole vya kutumbulia majipu.
Takukuru mpya
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga kuhakikisha inazalisha chombo
kipya cha kuzuia na kupambana na rushwa chenye maadili.
Aliwataka
wanaoona hawawezi kwenda na kasi hiyo, wawasilisha barua zao za
kujiuzulu kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Kamishna wa Polisi
Valentino Mlowola.
Hata
hivyo, alisema Serikali inatambua kuwa kazi ya upelelezi na uchunguzi
ni ngumu kutokana na kukabiliwa na vishawishi vingi, jambo ambalo
wanahitaji ujasiri. Alisisitiza watumishi hao kutunza heshima yao na
chombo hicho.
“Faraja
ya uchunguzi ni kufanikisha majalada kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP) na baadaye watuhumiwa kufikishwa mahakamani. Sasa ili kufanikisha
faraja hii ni vyema kufanya kazi kwa weledi na tusiwe na pupa ili mradi
tupeleke kesi nyingi kwa DPP na kuziwasilisha mahakamani,” alisema Kairuki.
Aliendelea,
“Nasema haya kwa sababu nafahamu bado kwenye uchunguzi hapa Takukuru
kuna upungufu. Nafikiri mmemuona Mheshimiwa Rais anavyoshughulikia suala
la rushwa na ufisadi, ni wajibu wenu Takukuru kufanikisha azma hii kwa
kuja na matokeo ya utendaji chanya.”
Aidha,
waziri huyo aliitaka taasisi hiyo kutumia weledi, sifa yaa ukachero wa
kiupelelezi na kiuchunguzi kufuatilia matukio yenye shaka yanayoendelea
mitaani na si kusubiri taasisi kubwa kuyavumbua.
“Nyie
ndio makachero tumieni ukachero wenu kuibua ufisadi, kuna mtu mmoja
amebainishwa na Rais lakini jina lake kwa umaarufu na utajiri wake
linatumika kama kituo, alishajiuliza sababu na kuchunguza?” alihoji.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mlowola aliwataka wafanyakazi wa
taasisi hiyo kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Kasi ya Magufuli
Aliwataka
wahakikishe wanaendana na kasi ya Dk Magufuli na Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ya utendaji na utumbuaji wa majipu katika maeneo yenye
ubadhirifu wa fedha, rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
“Natarajia
tutafanya kazi kwa weledi na si nguvu, kwa mfano taarifa zilizotolewa
katika maeneo ya bandarini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), siye
ndio tulitakiwa tuziwasilishe juu (ngazi ya Rais). Naomba tusisubiri
kuletewa,” alisisitiza.
Aliwataka watumishi hao kujiepusha kuwa watuhumiwa wa rushwa. “Jamani
hii ni mbaya kwetu Polisi akituhumiwa ujambazi ni mbaya sana, lakini
ofisa wa Takukuru akituhumiwa rushwa ni dhambi kubwa. Sisi tuwe watu wa
mwisho kutuhumiwa kwa rushwa."
Aliwataka
watumishi hao kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha wanaisaidia
Serikali kwenye eneo la upotevu wa fedha kwa kufuatilia matumizi na
miradi ya maendeleo na fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri na kwenye
manunuzi ya umma.
Alisema
katika utekelezaji wa jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa nchini
kwa mwaka 2014/15 taasisi hiyo ilipokea malalamiko 4,675. Ilifanyia
uchunguzi na kukamilisha majalada 667, kupeleka kwa DPP majalada 278,
walirejeshewa majalada 172 yenye vibali vya kufungua mashtaka na
kufungua kesi mpya 314 nchini kote.
Aidha
alisema taasisi hiyo ilishinda kesi 132 mahakamani na washitakiwa
walihukumiwa vifungo mbalimbali ikiwemo faini. Ziliokolewa Sh bilioni
saba zilizokuwa ziingie kwenye mifuko ya wabadhirifu wachache.
Ndani
ya siku 100 za Rais Magufuli madarakani taasisi hiyo ilipokea
malalamiko 411 kutoka kwa wananchi, imefungua mafaili 146 ya uchunguzi.
Imepeleka kwa DPP mafaili 103, mafaili 65 yenye kibali cha DPP
yamerejeshwa kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka, jumla ya kesi 72 mpya
zimefunguliwa mahakamani na imeshinda kesi 40 na kushindwa kesi 52.
“Ndani
ya siku 100 tumefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 11 akiwemo
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Kipallo Kisamfu,” alisisitiza.
Tanzia: Msanii Wa Bongo Fleva John Woka Afariki Dunia
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Msanii
wa muziki wa kizazi kipya ambaye alijipatia umaarufu mkubwa kwa staili
yake ya kuimba kama mlevi, Joni Woka amefariki dunia alfajiri ya leo.
Woka amefariki baada ya juzi kupata ajali ya kulipukiwa na mtungi wa
gesi. Alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili jijini Dar
es Salaam.
Hii ni taarifa iliyotolewa na mtu wa karibu na rapper huyo kuelezea ajali hiyo:
"Walikuwa wanahangaika kurekebisha usafiri kwenye garage hapo Sinza,
sasa katika kuhangaikia upande wa AC mtungi wa gas ukalipuka,moja ya
vipande vya chuma chenye ncha kali kikamchoma kichwani. Madaktari
wanahofia imefika mbali kiasi kwamba damu inamwagikia kwenye ubongo."
Msanii John Woka ambaye alikuwa kwenye kundi la Watukutu Family, alijipatia umaarufu kwa nyimbo zake za Sophia, baby gal na nyinginezo, ambazo aliziimba kwa mtindo wa ulevi.
Msanii John Woka ambaye alikuwa kwenye kundi la Watukutu Family, alijipatia umaarufu kwa nyimbo zake za Sophia, baby gal na nyinginezo, ambazo aliziimba kwa mtindo wa ulevi.
Kwa yeyote aliyeguswa na angependa kutoa rambi rambi anaweza kuwasiliana na kaka yake kwa namba +255767007005.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.





Wasailiwa waliochaguliwa kuendelea na usaili wanatakiwa kufika, tarehe na muda kama ilivyo oneshwa kwenye ratiba ya usaili. 


