Sekretarieti ya Ajira
inapenda kutoa tahadhari kwa waombaji wote wa nafasi za kazi kupitia
chombo hiki kuwa kumezuka kundi la watu wanaojifanya ni watumishi wa
Sekretarieti ya Ajira ambao kwa makusudi wamekuwa wakiwapigia simu kwa
lengo la kuwalaghai baadhi ya waombaji wa nafasi za kazi Serikali
wakidai wapewe fedha ili waweze kuwasaidia kupata kazi Serikalini kwa
urahisi mara baada ya kufanya usaili.
Katibu wa Sekretarieti ya
Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amefikia hatua ya kutoa
tamko hili kutokana na baadhi ya waombaji wa nafasi za kazi Serikalini
kukumbwa na kadhia hiyo na kutoa taarifa. Amesema Ofisi yake haina
utaratibu wa kuwapigia simu waombaji wa fursa za ajira Serikalini na
kuwadai fedha ili kuweza kuwapatia nafasi ya ajira. Hivyo, endapo kuna
msailiwa yeyote atakayepigiwa simu ajue hao watu ni matapeli na ni vyema
akawapuuza kw akutokuwapa ushirikiano na badala yake kuwaripoti katika
vyombo vya dola ili waweze kuwachukulia hatua stahiki.











