Saturday, 21 March 2026

KIJANA SERIKALI HAIHITAJI KELELE INAHITAJI USHIRIKA WAKO

...

 

Katika ulimwengu wa sasa unaoendeshwa na matokeo, dhana ya kijana kukaa pembeni na kupiga kelele kuishtumu serikali inazidi kupitwa na wakati, badala yake nafasi iliyo wazi na yenye tija ni ile ya kuwa mshirika (partner) wa maendeleo. 

Serikali, kama msimamizi wa rasilimali, inahitaji watu wenye masuluhisho ya ndani yanayotatua changamoto za kijamii, na mshirika namba moja ambaye taifa linamtafuta ni wewe kijana uliyejaa nguvu, ubunifu na maarifa.

Mfano bora na hai wa namna ushirika huu unavyoweza kuleta mageuzi makubwa ni kupitia kazi zilizotukuka za Doris Mollel na taasisi yake ya Doris Mollel Foundation. 

Kiukweli Doris hajaishia tu kulalamika kuhusu changamoto za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) au afya ya uzazi nchini, bali amekuwa mshirika mkuu wa serikali katika kuboresha huduma za afya, kiasi cha kuandika historia inayotambulika kimataifa.

Hivi karibuni, katika Makao Makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) mjini Geneva, Uswisi, Doris Mollel amepokea tuzo ya utambuzi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus. 

Tuzo hiyo ni kielelezo cha uongozi wake thabiti na ahadi yake isiyoyumba katika kuendeleza afya ya mama na mtoto nchini Tanzania, jambo ambalo limethibitisha kuwa masuluhisho yanayoongozwa na wazalendo wa ndani yana nguvu kubwa ya kubadili mfumo wa afya.

Utambuzi huu wa kimataifa kwa Doris Mollel si tu sifa kwake, bali ni ujumbe kwa kila kijana wa Kitanzania kuwa inawezekana kufanya makubwa ukiwa hapa nchini kwako. 

Badala ya kupoteza muda mwingi kwenye mijadala isiyo na tija mitandaoni , Doris amewekeza nguvu zake katika "locally-led solutions"—masuluhisho yanayotokana na jamii yenyewe—ambayo ndiyo mwelekeo wa sasa wa maendeleo duniani.

Serikali inapopata washirika kama Doris, mzigo wa huduma za kijamii unapungua na ufanisi unaongezeka, jambo ambalo linajenga taifa imara na lenye heshima kimataifa. Huu ni wakati wa vijana kuacha kulalamika kuwa hakuna fursa, na badala yake kuanza kutengeneza fursa kwa kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazotuzunguka, iwe katika elimu, afya, kilimo au teknolojia.

Mafanikio ya Doris Mollel kule Geneva ni kielelezo kuwa ulimwengu unatazama, na unathamini wale wanaojitofautisha kwa vitendo kuliko maneno. Ni mwito kwa kila kijana kujitathmini: Je, wewe ni mpiga kelele au ni mshirika wa maendeleo? 

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger