SINGIDA-Mpasuko ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umeendelea kutamalaki huku chanzo kikuu kikitajwa kuwa ni viongozi wakuu wa chama hicho kuyapa kisogo majukumu na vipaumbele vya chama huku wakiangalia fursa za kushibisha matumbo yao.
Hali hiyo, inatajwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho kuwa chanzo kikuu cha wao kukosa mwelekeo na kupoteza matumaini kuanzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa hadi Uchaguzi Mkuu ujao.
Miongoni mwa viongozi ambao wanatajwa kutotabirika ni Makamu Mwenyekiti wa chama Bara, Tundu Lissu ambaye imedaiwa ni hodari wa kulalamika, lakini uwezo wa kutenda ni sufuri.
"Wakati Taifa linajiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, Tundu Lissu alikuwa Ulaya.
"Wakati wa kampeni, alikuwa bize kutuambia ukweli kwamba chama chake hakikujipanga.
"Leo, siku ya uchaguzi, hayupo.Hodari wa kulalamika, lakini bingwa wa kutotenda. Huu ndio udhaifu wa uongozi wa CHADEMA.
"Wameshindwa kutekeleza ahadi zao, lakini wanaendelea kutoa maneno tupu, tunahitaji viongozi wanaotenda, si walalamikaji," amesisitiza mmoja wa wanachama.
Aidha, kwa nyakati tofauti mkoani Singida ambako ni nyumbani kwa Tundu Lissu baadhi ya wanachama wa chama hicho wamesema,hawana imani na Lissu katika siasa.
"Lissu siasa imemshinda na hata chama chetu bila uongozi mpya hakuna mwelekeo tena.
"Ni vema, Lissu akarejea kwenye taaluma yake, huku kwenye siasa hakumfai, siasa ya kisasa inahitaji umakini na utafiti, si uropokaji.
"Kama vipi Lissu na kina Mbowe watuachie chama chetu tukijenge upya, chama kimechoshwa hadi kimetuchosha wanachama wenyewe.
"Kwa mwelekeo wa sasa, hatuna matarajio ya kufanya vema tena, pengine tumewapa njia ya ushindi wa kishindo CCM katika chaguzi zote,"amesema Said ambaye ni mwanachama wa chama hicho na mkazi wa Ikungi.
0 comments:
Post a Comment