Monday, 4 November 2024

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAWASILI SHINYANGA, WANANCHI KUPATA FURSA YA MATIBABU BORA

...

Na Kadama Malunde  - Malunde 1 blog

Katika juhudi za kuboresha huduma za afya, kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imewasili mkoani Shinyanga leo, Novemba 4, 2024. 

Madaktari 47 kutoka sehemu mbalimbali nchini watatoa matibabu ya kibingwa kwa wananchi kwa muda wa siku sita, wakilenga kusaidia wale wasio na uwezo wa kupata huduma hizo.

Kambi hiyo imepokelewa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, ambapo madaktari hao sasa wamesambazwa katika halmashauri zote sita za mkoa. 

Mratibu wa Madaktari Bingwa, Everine Maziku kutoka Wizara ya Afya, ameeleza umuhimu wa kampeni hii akisema“Tunampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza mpango huu unaosaidia kuboresha afya za wananchi, hasa wale wanaokabiliwa na changamoto za kifedha.”

Mbali na kutoa matibabu, madaktari hao pia watajenga uwezo wa watoa huduma za afya katika hospitali za eneo hilo, na kuanzisha huduma ambazo awali hazikuwepo. 

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Faustine Mlyutu, amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi: “Nawaomba wananchi wa Shinyanga mjitokeze kwa wingi kupata matibabu ya kibingwa kutoka kwa madaktari hawa. Hii ni fursa ya pekee ya kuokoa afya zenu.”

Madaktari, akiwemo Missano Yango kutoka Hospitali ya Rufaa Dodoma, ambaye ni bingwa wa Magonjwa ya nje, ameeleza wamejipanga kutoa huduma bora na kuhamasisha wananchi kujitokeza. 

“Tumejizatiti kutoa huduma stahiki na tunawakaribisha wananchi kwa wingi,” amesema Yango.

Kambi hii ni mwendelezo wa juhudi za serikali kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini na ni nafasi muhimu kwa wananchi wa Shinyanga kuboresha afya zao kwa kupitia matibabu ya kitaalamu na ya kibingwa.

 

Picha ya Pamoja ikipigwa.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger