Sunday, 26 May 2024

KASEKENYA AIPA TANROADS WIKI MOJA MALINYI KUFIKIKA

...



Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wiki moja kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro kuhakikisha anarudisha Mawasiliano ya barabara kati ya wilaya ya Ifakara na Malinyi katika kijiji cha Misegese, mkoani humo ili kuruhusu magari kupita mara baada ya daraja la Mto Fulua kuharibika kutokana na mafuriko.

Kasekenya ametoa agizo hilo Mei 25, 2024 wakati alipowasili wilayani Malinyi mkoani humo kukagua miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa na mvua za El-Nino ambapo amesisitiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka kurekebisha miundombinu hiyo ambayo ni kiungo muhimu kwa wilaya hizo mbili.

"Nakupa wiki moja, hakikisha hadi kufikia Jumamosi ijayo magari yawe yanapita hapa, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga daraja la kudumu katika eneo hili pamoja na kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami", amesema Kasekenya.

Aidha, Kasekenya amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha za matengenezo ya dharura katika miundombinu iliyoathiriwa na mafuriko ili kurejesha mawasiliano katika maeneo hayo.

Kadhalika, Kasekenya ametoa rai kwa wananchi kutokufanya shughuli za kibinaadamu ikiwemo kilimo karibu na mito kwani hali hiyo huathiri mabadiliko ya tabia nchi na kusabisha mito kuhama na hivyo kuharibu miundombinu ambayo hujengwa kwa gharama kubwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba, ameipongeza TANRAODS Mkoa wa Morogoro kwa kuendelea kukarabati na kuweka Makalvati katika daraja la mto Fulua ili kurejesha mawasiliano katika eneo hilo ambalo liliathiriwa na mvua za El-Nino zilizonyesha mwaka huu.

Ameeleza kuwa kwa sasa magari hayawezi kupita kutoka Njia panda kwenda Malinyi Mjini kutokana na maji kukata barabara kwa mita 100 hivyo uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na wananchi wamejenga daraja la muda ambalo linaruhusu kupitisha watumiaji wa njia ya miguu, baiskeli na pikipiki tu.

Naye, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Morogoro, Mhandisi, Alinanuswe Kyamba amemhakishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa tayari wamejipanga na wameanza kurejesha mawasiliano kuanzia eneo la Lupilo na kusisitiza kuwa wataendelea na kasi zaidi ili kurejesha mawasiliano eneo hilo ndani ya muda walioagizwa.

*Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi*

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger